Herminie aapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Shelisheli
Dk. Mathew Antonio Patrick Herminie ameapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Shelisheli katika hafla iliyofanyika jioni ya leo katika uwanja wa Stad Linite, Roche Caïman.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, wageni mashuhuri pamoja na wananchi.
Dk. Herminie, ambaye ni kiongozi wa chama cha United Seychelles, alishinda uchaguzi wa urais uliomalizika hivi karibuni baada ya kumbwaga Rais aliyekuwa madarakani, Wavel Ramkalawan, katika duru ya pili ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa. Alipata asilimia 52.7 ya kura, huku Bw. Ramkalawan akipata asilimia 47.3.
Uchaguzi huo uliingia raundi ya pili baada ya wagombea wote wawili kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura katika duru ya kwanza.
Ushindi wa Dk. Herminie unaashiria kurudi madarakani kwa chama cha United Seychelles baada ya miaka mitano ya kuwa upinzani. Chama hicho kiliongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1977 hadi 2020.
Dk. Herminie, ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa kati ya mwaka 2007 na 2016, ameanza rasmi muhula wake kwa kuahidi kukuza haki za kijamii na kulinda mazingira tete ya taifa hilo la visiwa. Pia ametangaza kuwa serikali yake itasitisha ujenzi wa hoteli ya kifahari inayofadhiliwa na Qatar kwenye kisiwa chenye umuhimu mkubwa wa ikolojia.
Shelisheli, inayojulikana kwa fukwe zake safi na msimamo wake wa maendeleo endelevu, inaendelea kuwa moja ya vituo vinavyoongoza duniani vya utalii wa kifahari na wa kimazingira. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Shelisheli pia ni taifa tajiri zaidi barani Afrika kwa kipato cha mtu mmoja mmoja (per capita).