Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyozikumba Indonesia na Timor Mashariki yawaua watu zaidi ya 100
Watu takriban 101 wamefariki kufuatia mafuriko na maporomoko ya udongo kuzikumba nchi za Indonesia na Timor Mashariki siku ya Jumapili.
Mvua kubwa ziliyonyesha katika nchi hizo jirani zimesababisha maafa makubwa huku maji ya mafuriko yakivunja kingo za mabwawa na kusomba maelfu ya makazi ya watu.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni kuanzia kisiwa cha Flores mashariki mwa Indonesia hadi nchi jirani ya Timor Mashariki.
Nchini Indonesia pekee, watu 80 wamefariki na huku makumi wakiwa hawajulikani walipo. Mamlaka zinatahadharisha kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
"Matope, hali mbaya ya hewa pamoja na kifusi kikubwa kinachoendeea kujikusanya vimekuwa vikwazo vikubwa kwa shughuli za uokozi," msemaji wa shirika la Indonesia la kukabiliana na majanga Raditya Jati amewaambia wanahabari.
"Tunahisi watu wengi zaidi wamefunikwa ndani ya kifusi na tope lakini hatuna hakika juu ya idadi yao kamili," ameeleza mkuu wa shirika hilo kwa upande wa kisiwa cha Flores, Bw Alfons Hada Bethan.
"Waathirika wametapakaa katika maeneo yote. Wapo kwa mamia katika kila wilaya, lakini wengi zaidi wamesalia nyumbani. Wananhitaji dawa, chakula na mablanketi."
Takriaban watu 21 pia wamefariki katika nchi ya Timor Mashariki ambayo pia inafahamika kama Timor Leste, maafisa wa nchi hiyo wamenukuliwa wakithibitisha.
Wengi kati ya waliofariki wanatokea katika katika mji mkuu wa kisiwa hicho unaofahamika kama Dili.
"Bado tunatafuta maeneo yaliyoathiriwa zaidi na majanga haya," Joaquim Jose Gusmao dos Reis Martins, Waziri wa mambo ya ndani na usalama wa jamii nchini Timor, aliwaambia wanahabari.
Waliojeruhiwa katika maeneo ya visiwani wameondolewa na kupelekwa vijiji jirani, pamoja na hospitali na vituo vya afya.
Mafuriko na maporomoko ya udongo hutokea mara kwa nchini Indonesia wakati wa msimu wa masika, ambao kawaida huanzia Novemba hadi Machi.