Neno 'takataka' alilotumia Biden lazua ghadhabu

Joe Biden amekanusha kuwaita wafuasi wa Trump "takataka" katika video zilizoibuka muda mfupi baada ya hotuba ya Harris.

Muhtasari

  • Mgonjwa wa kwanza wa mpox aritopiwa Uingereza
  • Marekani yaionya Israel kuhusu msaada wa Gaza huku muda wa makataa ukiyoyoma
  • Afrika Kusini kumnyang'anya Malkia wa urembo utambulisho wake
  • Trump amjibu Biden bila kupoteza muda kwa neno alilotumia 'takataka'
  • Biden afafanua matumizi ya neno 'takataka' huku wafuasi wa Republican wakimkosoa
  • Biden: Ikiwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wataingia Ukraine, Ukraine inapaswa kuwashambulia
  • RSF, washirika wake, walifanya unyanyasaji wa kingono Sudan, ujumbe wa Umoja wa Mataifa unasema
  • Mshindi wa taji la Urembo nchini Rwanda akamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa
  • Ufaransa yaiunga mkono Morocco katika mzozo kuhusu Sahara Magharibi
  • Wanaharakati kufika mahakama za juu kupinga Tamisemi kusimamia uchaguzi
  • Marekani yasema shambulizi la anga la Israel 'ni la kutisha'

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Habari za hivi punde, Mgonjwa wa kwanza wa mpox aritopiwa Uingereza

    Kisa cha kwanza cha mpox – ugonjwa ambao zamani ulijulikana kama monkeypox – wenye kuhusishwa na mlipuko katika baadhi ya sehemu barani Afrika umegunduliwa nchini Uingereza.

    Ni sehemu ya mlipuko wa Clade 1b, ambao unaonekana kuenea kwa urahisi kati ya watu.

    Mpox ulitangazwa kuwa dharura ya afya duniani na Shirika la Afya Duniani barani Afrika.

    Mgonjwa huyo wa Uingereza alikuwa likizoni barani Afrika hivi majuzi na alianza kuhisi kuumwa saa 24 baada ya kufika nyumbani.

  3. Marekani yaionya Israel kuhusu msaada wa Gaza huku muda wa makataa ukiyoyoma

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Israel inapaswa kushughulikia mara moja "hali mbaya ya kibinadamu" huko Gaza, mjumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameonya, wakati tarehe ya mwisho inakaribia ya kuongeza upatikanaji wa misaada au ikabiliane na kupunguzwa kwa usaidizi wa kijeshi wa Marekani.

    "Maneno ya Israel lazima yalinganishwe na hatua zinazochukuliwa," Linda Thomas-Greenfield alisema. "Kwa sasa, hilo halifanyiki."

    Marekani imempa mshirika wake hadi Novemba 12 "kuongeza" msaada wote, na angalau malori 350 yawe yanaingia Gaza kila siku.

    Lakini Umoja wa Mataifa unasema ni 10% tu kwa wastani ya idadi hiyo imevuka mpaka kila siku tangu wakati huo.

    Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alisema inafanya "kila iwezalo na zaidi ya majukumu yake ya kibinadamu" na akailaumu Hamas.

    Bw Danon pia alikataa ukosoaji wa kimataifa wa uamuzi wa bunge la Israel kupiga marufuku shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa) kufanya kazi nchini Israel.

    Washirika wa Israel wameonya kwamba Unrwa ina jukumu muhimu katika kupeleka misaada ya kibinadamu huko Gaza, ambako ni shirika kubwa zaidi la kibinadamu duniani.

    Soma zaidi:

  4. Afrika Kusini kumnyang'anya Malkia wa urembo utambulisho wake

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Malkia wa urembo Chidimma Adetshina, ambaye amekuwa katikati ya mzozo tatanishi wa utaifa, atanyang'anywa utambulisho wake wa Afrika Kusini na hati za kusafiria.

    Idara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilianza kuchunguza kesi yake baada ya kufika fainali katika shindano la ‘Miss South Africa’, lakini alikosolewa huku watu wakihoji ikiwa anastahili kushiriki kwa sababu mama yake ana asili ya Msumbiji na baba yake ni Mnigeria.

    Alijiondoa katika shindano hilo mwezi Agosti baada ya idara hiyo kutangaza kuwa mamake huenda alifanya "wizi wa utambulisho" ili kuwa raia wa Afrika Kusini.

    Bi Adetshina, mwanafunzi wa sheria, alishinda Miss Universe Nigeria baada ya kualikwa kushiriki na waandaaji.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Trump amjibu Biden bila kupoteza muda kwa neno alilotumia 'takataka'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Trump amejua kuhusu neno alilotumia Joe Biden 'takataka' alipokuwa jukwaani huko Allentown, Pennsylvania, na Seneta Marco Rubio mara moja akarejelea matamshi ya Hillary Clinton ya 2016 akiwaita baadhi ya wafuasi wa Trump "wenye kusikitisha".

    "Takataka nadhani ni baya zaidi?" Trump alisema, kabla ya kuongeza, "Lakini tafadhali msameheni, kwani hajui alichosema".

    Biden amekanusha kwamba aliwataja wafuasi wa Trump kwa pamoja, na kusema alikuwa anazungumza kuhusu mcheshi Tony Hinchcliffe, ambaye alitumia mkutano wa Trump kutaja Puerto Rico kama "kisiwa kinachoelea cha taka".

    Trump baadaye aliandika tena kwenye tovuti yake ya Truth Social, akimshutumu Harris kwa "kuendesha kampeni ya chuki".

  6. Biden afafanua matumizi ya neno 'takataka' huku wafuasi wa Republican wakimkosoa

    .

    Chanzo cha picha, Votolatino.org

    Nianze kwa kukujuza taarifa zinazoendelea Marekani. Rais Joe Biden amezua ghadhabu kwa wafuasi wa Republican katika saa za hivi karibuni.

    Ilianza muda mfupi baada ya Kamala Harris kumaliza kutoa hotuba yake kubwa ya kampeni huko Washington DC.

    Akiongea kwenye hafla kupitia Zoom na wapiga kura hapo awali, Biden alizungumza juu ya watu wa Puerto Rico: "Ni watu wazuri na wenye heshima."

    Kisha alionekana kusema: "Takataka pekee ninayoiona ikielea huko nje ni wafuasi wake ... Walatino anaowatumia vibaya, haikubaliki."

    Warepublican wanasema Biden aliwataja wafuasi wote wa Trump kama "takataka" - huku Biden na Ikulu ya White House wakisema alikuwa akimrejelea haswa mcheshi aliyeshambulia Puerto Rico kwenye mkutano wa hadhara wa Donald Trump, na "maneno ya chuki" dhidi ya kisiwa hicho.

    Wakati Ikulu ya White House ilipotoa nakala ya maoni ya Biden, walijumuisha neno "msaidizi" likiwa kwenye apostrofi - ambayo ingeashiria rais alikuwa anazungumza juu ya mtu maalum badala ya kundi kwa jumla.

    Soma zaidi:

  7. Karibu msomaji wetu katika kipindi hiki cha mchana kwenye matangazo yetu ya moja ya moja. Nitakae kuwa nahodha wako ni mimi Asha Juma.

  8. Ukraine kusajili wanajeshi wengine 160,000, Urusi yasonga mbele eneo la mashariki

    Kifaru

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine inapanga kusajili wanajeshi wengine 160,000 katika jeshi lake huku Urusi ikipata mafanikio katika eneo la mashariki.

    Urusi imekuwa ikisonga mbele katika eneo la mashariki la Donetsk na Jumanne ilisema kuwa imeuteka kikamilifu mji wa wenye shughuli za uchimbaji madini wa Selydove.

    Pia hatua hii inakuja huku kukiwa na ripoti kwamba idadi kadhaa ya wanajeshi wa Korea Kaskazini wametumwa Urusi.

    Jeshi la Ukraine limekuwa chini ya shinikizo kubwa siku za hivi karibuni, kwa sehemu kutokana na nguvu kazi kubwa ya Urusi na rasilimali nyingi zaidi.

    "Kuna mipango ya kuwaita zaidi ya watu 160,000," katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Ukraine, Oleksandr Lytvynenko, aliliambia bunge siku ya Jumanne.

    Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa usajili huo utafanyika kwa muda wa miezi mitatu.

    Pentagon inakadiria kuwa takribani wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini wametumwa kutoa mafunzo mashariki mwa Urusi.

    Marekani ilisema Jumanne "idadi ndogo" ya wanajeshi wa Korea Kaskazini wametumwa Kursk.

    Maelfu kadhaa zaidi wanaelekea huko, ilisema. Korea Kusini imedai kuwa wanajeshi hao wanapewa mafunzo katika maeneo mbalimbali, huku wengi wao wakiwa wamevalia sare za Kirusi ili kujificha.

    Afisa wa ngazi ya juu wa serikali alisema wanaamini hadi wanajeshi 11,000 tayari wametumwa Urusi, na takribani 3,000 magharibi mwa nchi hiyo.

    Wiki iliyopita Rais Vladmir Putin alikana taarifa kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wamewasili nchini Urusi kufuatia ripoti kwamba Pyongyang inajiandaa kutuma maelfu ya wanajeshi wake kusaidia mshirika wake.

  9. China yatangaza mafanikio wakati wanaanga wake wakifikia anga za juu

    Chombo

    Chombo cha anga za juu cha China kikiwa na wafanyakazi watatu akiwemo mhandisi wa anga wa kwanza mwanamke nchini humo kimetia nanga baada ya safari ya zaidi ya saa sita.

    Wafanyakazi watatumia kituo cha anga za juu kwa muda wa miezi sita kufanya majaribio na kufanya matembezi ya anga wakati Beijing inakusanya uzoefu kwa ajili ya dhamira yake ya kumweka mtu kwenye Mwezi ifikapo 2030.

    Beijing ilitangaza urushaji wa Shenzhou 19 kuwa "mafanikio", ni moja ya matukio 100 ambayo China imepanga katika mwaka wa rekodi wa uchunguzi wa anga inapojaribu kumshinda mpinzani wake, Marekani.

    BBC ilipewa nafasi ya kufika kwenye kituo cha kurushia Satellite cha Jiuquan huko Gansu na tulikuwa umbali wa zaidi ya kilomita moja wakati chombo hicho kilipolipuka.

    Miale ya moto ilitoka kwenye kirusha roketi ilipopaa angani, ikimulika Jangwa la Gobi kwa kishindo.

    Mamia ya watu walijipanga barabarani, wakipunga mkono na kuwashangilia wanaanga hao.

    Katika kituo cha anga za juu cha Tiangong, wafanyakazi wa Shenzhou 19 walikutana na wanaanga wengine watatu ambao wanasimamia Shenzhou 18 na watarejea duniani tarehe 4 Novemba.

    Miaka miwili tu iliyopita, Rais Xi Jinping alitangaza kwamba "kuchunguza anga kubwa, kuendeleza sekta ya anga na kujenga China katika nguvu ya anga ni ndoto yetu ya milele".

    Lakini wengine huko Washington wanaona matarajio ya nchi na maendeleo ya haraka kama tishio.

    Mapema mwaka huu, mkuu wa Nasa, Bill Nelson alisema Marekani na China "ziko katika mbio" za kurejea Mwezini.

    Aliwaambia wabunge kwamba anaamini mpango wa China wa anga za juu wa kiraia pia ulikuwa mpango wa kijeshi.

  10. Biden: Ikiwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wataingia Ukraine, Ukraine inapaswa kuwashambulia

    Jeshi la Korea Kaskazini

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Joe Biden ametoa maoni yake kuhusu ripoti za wanajeshi wa Korea Kaskazini kuwasili katika eneo la Kursk nchini Urusi.

    Alisema ana wasiwasi na ripoti hizo. Alipoulizwa ikiwa Ukraine inapaswa kujibu, Biden alijibu: "Ikiwa watavuka mpaka na kuingia Ukraine, basi ndio washambuliwe."

    Unaweza kusoma;

  11. Vikosi vya RSF, washirika wake, walifanya unyanyasaji wa kingono Sudan, ujumbe wa Umoja wa Mataifa unasema

    Mzozo unaoongezeka katika jimbo la Gezira nchini Sudan umewalazimu raia kukimbia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vikosi vya wanamgambo wa Sudan (RSF) na washirika wake wamefanya viwango vya "kushangaza" vya unyanyasaji wa kingono, kuwabaka raia huku wanajeshi wakisonga mbele na kuwateka nyara baadhi ya wanawake kama watumwa wa ngono wakati wa vita vilivyodumu zaidi ya miezi 18, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne, Reuters imeripoti.

    Waathirika wameanzia kati ya miaka minane hadi 75, ilisema ripoti ya ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, huku unyanyasaji mwingi wa kingono ukifanywa na RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu katika jaribio la kuwatisha na kuwaadhibu watu kwa kudhaniwa kuwa na uhusiano na maadui.

    "Kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kijinsia ambao tumeandika nchini Sudan ni cha kushangaza," mwenyekiti wa misheni Mohamed Chande Othman alisema katika taarifa iliyoambatana na ripoti ya kurasa 80 iliyojikita katika mahojiano na waathiriwa, familia na mashahidi.

    Ripoti hiyo ilirejea uchunguzi wa Reuters na makundi ya haki za binadamu kuhusu unyanyasaji mkubwa wa kingono katika mzozo huo. RSF, ambayo inapambana na jeshi la Sudan, haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni. Hapo awali imesema itachunguza tuhuma na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

    Unaweza kusoma;

  12. Mshindi wa taji la Urembo nchini Rwanda akamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa

    Divine Muheto

    Chanzo cha picha, Divine Muheto/Instagram

    Polisi nchini Rwanda wamemkamata mshindi wa taji la taifa la urembo kwa "kurudia" "kuendesha gari akiwa amekunywa pombe kupita kiasi" na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

    Divine Muheto hana leseni ya kuendesha gari na alitoroka eneo la ajali baada ya kugonga miundombinu, polisi walisema katika taarifa.

    Bi Muheto hajajibu hadharani madai hayo. Bi Muheto, 21, alipata umaarufu aliposhinda shindano la urembo la Miss Rwanda mnamo 2022, kabla ya serikali kusitisha shindano hilo baada ya tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya waandaaji.

    Polisi wametangaza kukamatwa kwake leo, siku chache baada ya tetesi kuwa mrembo huyo alihusika katika ajali ya barabarani na baadaye kukamatwa.

    Adhabu ya kuendesha ukiwa umekunywa ni faini ya faranga 150,000 za Rwanda (dola 110), na siku tano rumande.

    Katika miaka ya hivi karibuni maelfu ya watu walikamatwa kwa kosa hili huku polisi wakitekeleza sheria hii. Mnamo 2022 mbunge alijiuzulu na kuomba msamaha kwa kuendesha gari akiwa amelewa.

    Utekelezaji mkali wa sheria za trafiki umepunguza kwa kiasi kikubwa ajali mbaya za barabarani nchini Rwanda, serikali imesema.

    Katika taarifa yake, polisi walisema kuwa kesi ya Bi Muheto ilifikishwa katika ofisi ya mashtaka.

  13. Ufaransa yaiunga mkono Morocco katika mzozo kuhusu Sahara Magharibi

    Maelfu ya watu wa Sahrawi wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini Algeria

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameliambia bunge la Morocco kwamba anaamini Sahara Magharibi inapaswa kuwa chini ya mamlaka ya Morocco, na ameahidi kuwekeza fedha za Ufaransa huko.

    Sahara Magharibi ni eneo la pwani ya kaskazini-magharibi mwa Afrika ambalo limekuwa na mzozo wa miongo kadhaa.

    Wakati fulani lilikuwa koloni la Uhispania, na sasa linadhibitiwa zaidi na Morocco na kwa kiasi fulani na Polisario Front inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inasema inawakilisha watu asilia wa Sahrawi na inataka taifa huru.

    Ufaransa ilikuwa nchi yenye nguvu ya kikoloni katika Morocco na Algeria. Inaungana na mataifa mengine ikiwemo Uhispania, Marekani na Israel kuunga mkono mpango wa Morocco.

    Wabunge walisimama na kumpongeza Macron Jumanne aliposema, "kwa Ufaransa, eneo hili la sasa na la siku zijazo liko chini ya mamlaka ya Morocco".

    Maoni yake siku ya Jumanne huko Rabat yanalingana na matamshi ya mshangao aliyotoa kwa mara ya kwanza mnamo Julai. Akiashiria mabadiliko katika msimamo wa muda mrefu wa Ufaransa kuhusu mpango wa Morocco wa kuipa Sahara Magharibi uhuru wa kujitawala chini ya mamlaka ya Morocco, rais wa Ufaransa alisema huo ndio "msingi pekee" wa suluhu la haki na la kudumu la kisiasa.

    Uungaji mkono wa Ufaransa kwa madai ya eneo la Morocco uliikasirisha Algeria, ambayo ilijibu habari hiyo kwa kumuondoa balozi wake huko Paris. Algiers inachukulia uwepo wa Morocco huko kama uvamizi haramu.

    Wachambuzi wanasema uamuzi wa Ufaransa kuunga mkono madai ya Morocco ni jaribio la kurekebisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, ambao ulikuwa umedorora baada ya Rabat kushutumiwa kwa kujaribu kufanya ujasusi dhidi ya Rais Macron na Ufaransa ikaimarisha vikwazo vya visa kwa raia wa Morocco wanaozuru nchni humo.

    Uhusiano kati ya Morocco na Algeria umekuwa wa wasiwasi hasa katika miaka ya hivi karibuni, na Algiers ilitangaza mwaka 2021 kwamba ilikuwa imekata uhusiano wa kidiplomasia na jirani yake wa magharibi.

  14. Wanaharakati kufika mahakama za juu kupinga Tamisemi kusimamia uchaguzi

    Wapiga kura

    Wakili na wanaharakati nchini Tanzania waliokuwa wakipinga Waziri kutunga kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa na kuusimamia uchaguzi huo wamesema watakata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama uliotolewa jana na kuhalalisha kanuni za uchaguzi zilizotungwa na Waziri na kuruhusu Tamisemi kuendelea kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa.

    Wakili Jebra Kambole akiwa na wanaharakati Bob Wangwe, Dr Ananilea Nkya na Bubelwa Kaiza walifungua shauri mahakamani wakihoji mamlaka ya Waziri wa Tamisemi kutunga kanuni za uchaguzi huo na pia kusimamia, kuendesha na kuratibu uchaguzi wa serikali za mitaa. Walitaka majukumu hayo yapewe Tume Huru ya Uchaguzi.

    “Tutakwenda mahakama ya riufaa ambayo ndiyo ya mwisho. Na yenyewe ikiwa itafanya maamuzi ya ndivyo sivyo, tutaifikia mahakama ya Afrika ya watu na binnadamu au tume ya haki za binadamu ya Afrika tunaamini huko tutapata haki kama tulivyoppata haki ya kesi ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi, mgombea binafsi ya mtikila, au kesi ya kupingwa kwa matokeo ya urais” amesema Kambole

    Kamboleanasema msingi wa moja ya hoja zao ulikuwa ni haki ya asili juu ya nafasi ya Waziri wa Tamisemi na wajibu wake katika kusimamia uchaguzi

    “Mtu anapokuwa anafanya maamuzi au anasimamia jambo hapaswi kuwa na maslahi na jambo hilo, lakini pia, huyo mtu huyo anayesimamia uchaguzi pamoja na kutokuwa na maslahi hawezikuwa na maamuzi kwenye kesi ambayo inamuhusu” amesema Kambole

    Mwanaharakati wa haki za binadamu Dr Ananilea Nkya ameyataja maamuzi ya mahakama kubariki nnafasi ya Tamisemi katika uchaguzi huo kama kupuuzwa kwa sauti za wananchi

    “Kile kilio cha wananchi, kile kilio cha raia, kwamba sisi raia tunataka chaguzi ziwe huru ina maana hakikusikilizwa, ina maana kimepokwa” amesema Nkya

    Chama cha upinzani ACT wazalendo wamesema hawakupendezwa na uamuzi huo wa mahakama ambao unapunguza imani juu ya mchakazo mzima wa uchaguzi.

    “Hatuuamini kwasababu upo chini ya Tamisemi, ambayo ipo chini ya CCM. Na hatuwezi kusema hatushiriki kwasababu itakuwa tunawaachia CCM ushindi bila kupingwa. Kwahivyo, manyago yatakuwepo kwasababu ndio siasa za CCM lakini na sisi tutaenda nazo hivyo hivyo,” amesema Ruqayya Nassir ni Naibu Katibu Mkuu Ngome ya Vijana ACT Wazalendo

    Pamoja na uamuzi wa mahakama kuthibitishwa mamlaka ya Tamisemi katika kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa Dr Nkya anasema bado atakwenda kupiga kura

    “Mimi ni mpiga kura, na mimi huwa siamini katika kuacha kupiga kura, nitakwenda kwenye sanduku la kupiga kura, nitapiga kura yangu. Kwasbabu unapokuwa hauna uongozi bora kwanzia ngazi ya mtaa, unapoteza si tu mabilioni ya fedha unaweza wananchi katika hali ya hofu, kwasababu hawana viongozi waliowachagua wao kupitia sanduku huru la kura” amesema Nkya

    Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mtaa tarehe 27 Novemba huku wapiga kura wakitarajiwa kuchagua Mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.

    Nafasi zingine zinazotarajiwa kugombaniwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.

    Imeandikwa na Sammy Awami.

  15. Marekani yasema shambulizi la anga la Israel 'ni la kutisha'

    Athari za mashambulizi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani watu 93 wameuawa au hawajulikani walipo baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Beit Lahia kaskazini mwa Gaza, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas imesema, katika shambulio ambalo Marekani imelitaja kuwa la "kuogofya".

    Waokoaji walisema jengo la makazi la ghorofa tano lilipigwa, na video kwenye mitandao ya kijamii zilionesha miili iliyofunikwa kwa blanketi sakafuni.

    Jeshi la Israel lilisema "linafahamu ripoti kwamba raia walijeruhiwa leo [Jumanne] katika eneo la Beit Lahia". Imeongeza kuwa taarifa za tukio hilo zinaangaliwa.

    Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vimekuwa vikifanya kazi kaskazini mwa Gaza katika muda wa wiki mbili zilizopita, hasa katika maeneo ya Jabalia, Beit Lahia na Beit Hanoun.

    Mkurugenzi wa hospitali ya karibu ya Kamal Adwan huko Jabalia, Hussam Abu Safia, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watoto walikuwa wakitibiwa katika hospitali hiyo ambayo inatatizika kuwatibu wagonjwa kutokana na ukosefu wa wafanyakazi na dawa.

    "Hakuna kilichosalia katika Hospitali ya Kamal Adwan isipokuwa vifaa vya huduma ya kwanza baada ya jeshi kukamata timu yetu ya matibabu na wafanyikazi," Abu Safia alisema.

    IDF ilivamia hospitali hiyo wiki jana, ikisema ilikuwa ikitumiwa na wapiganaji wa Hamas.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller alisema Marekani "imesikitishwa sana na kupoteza maisha ya raia katika tukio hili.

    Hili lilikuwa tukio la kuogofya na matokeo ya kuogofya".

    Israel inasema operesheni zake kaskazini mwa Gaza zimefanyika ili kuzuia Hamas kujipanga upya na inawatuhumu kwa kujiingiza miongoni mwa raia, jambo ambalo Hamas inakanusha.

    Unaweza kusoma;

  16. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu