Makadinali wafungiwa ndani ya Kanisa la Sistine kuanza kupiga kura ya siri kumchagua Papa mpya

Hawatakuwa na mawasiliano na ulimwengu wa nje hadi kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki atakapochaguliwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Makadinali wafungiwa ndani ya Kanisa la Sistine kuanza kupiga kura ya siri kumchagua Papa mpya

    .

    Chanzo cha picha, Pool

    Makadinali wamefungiwa ndani ya Kanisa la Sistine ili kuanza kupiga kura ya siri kumchagua papa mpya.

    Hawatakuwa na mawasiliano na ulimwengu wa nje hadi kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki atakapochaguliwa.

    Wale ambao hawatashiriki katika mkutano huo walitoka nje.

    Msimamizi wa sherehe za Papa ndiye aliyefunga milango na mkutano kuanza.

    Neno conclave linatokana na Kilatini kwa "cum clave", au "kufungwa na ufunguo".

    Sasa, Kamera haziruhusiwi tena kwenye kanisa hilo.

  2. Houthi inasema Marekani 'ilikubali kufanya makosa'

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Afisa wa ngazi ya juu wa Houthi amepinga madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kundi linalojihami la Yemen "liliunga mkono mazungumzo" wakati wa kukubaliana kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, na kusema Marekani badala yake "ilikubali kufanya makosa".

    "Kilichobadilika ni msimamo wa Marekani, lakini msimamo wetu unasalia thabiti," mpatanishi mkuu Mohammed Abdul Salam aliambia televisheni ya Al-Masirah inayoongozwa na Houthi.

    Mpatanishi wa Oman alisema Marekani na Wahouthi wamekubaliana "kutolengana tena" baada ya wiki saba za mashambulizi makali ya Marekani dhidi ya Yemen kujibu mashambulizi ya makombora ya Houthi na ndege zisizo na rubani dhidi ya meli za kimataifa katika Bahari ya Shamu.

    Abdul Salam pia alisema makubaliano hayo hayajumuishi kukomesha mashambulizi dhidi ya Israel, ambayo imefanya duru mbili za mashambulizi ya kulipiza kisasi Yemen wiki hii.

    Soma zaidi

  3. Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Cleopa Msuya afariki dunia

    a

    Chanzo cha picha, X

    Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani wa Tanzania, Cleopa David Msuya, amefariki dunia leo katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo. Msuya alikuwa na umri wa miaka 94.

    Akithibitisha taarifa hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo, Mei 7 hadi Mei 13, 2025, ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

    Akitoa taarifa za kifo chake, Rais Samia amesema, “Taarifa zaidi kuhusu msiba zitaendelea kutolewa na Serikali, nawapa pole sana watanzania".

    Msuya alizaliwa tarehe 4 Novemba, 1931 mkoani Kilimanjaro. Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya kwanza na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mnamo Novemba 7, 1980, akichukua nafasi ya Edward Moringe Sokoine aliyekuwa masomoni Ulaya wakati huo.

    Alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 1983, alipoachia nafasi hiyo kwa Sokoine baada ya kurejea. Kwa mara ya pili, Msuya aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu na Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Desemba 1994, akimrithi John Samuel Malecela. Alidumu katika wadhifa huo hadi Novemba 1995, alipokabidhi kijiti kwa Frederick Sumaye.

    Mbali na uwaziri mkuu, Msuya aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini zikiwemo za Waziri wa Fedha, na Waziri wa Viwanda na Biashara, nyadhifa alizotumikia kwa umahiri mkubwa katika vipindi tofauti vya uongozi wa Mwalimu Nyerere na Rais Mwinyi.

    Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 baada ya mfumo huo kurejeshwa, Cleopa Msuya alijitosa katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, hakufanikiwa kushinda uteuzi ndani ya chama hicho, baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Jakaya Mrisho Kikwete na Benjamin William Mkapa, ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.

  4. Waliojaribu kusafirisha maelfu ya mchwa wahukumiwa Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mahakama moja nchini Kenya imewahukumu wanaume wanne kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya $7,700 (£5,800) kwa kujaribu kusafirisha maelfu ya mchwa nje ya nchi.

    Washukiwa hao wanne - Wabelgiji wawili, Mvietnam na Mkenya - walikamatwa mwezi uliopita na mchwa hai wanaoshukiwa kutaka kuwapeleka kwa wanunuaji huko Ulaya na Asia.

    Walikuwa wamekubali mashtaka hayo, huku Wabelgiji wakiambia mahakama kwamba walikuwa wakikusanya mchwa waliokuwa wakitafutwa sana kama burudani na hawakufikiri kuwa ni kinyume cha sheria.

    Lakini akitoa hukumu hiyo siku ya Jumatano, hakimu alisema aina fulani ya mchwa waliokusanywa ni wa thamani na walikuwa na maelfu yao - sio wachache tu.

  5. G-55 watangaza rasmi kujiondoa Chadema

    s

    Chanzo cha picha, the guardian

    Viongozi wa zamani waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania, wakiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, wametangaza rasmi kujiondoa ndani ya chama hicho, wakisema wamechoshwa na kile walichokiita kubaguliwa na ukandamizaji wa haki za wanachama.

    Wakiwa na wanachama wengine wa kundi la G-55, wakiwemo John Mrema, aliyekuwa Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, na Catherine Ruge, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, viongozi hao walizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kwa kina sababu za kuondoka kwao.

    "Sisi tumeamua wote pamoja tunajiondoa Chadema, ili tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka, chadema imeachana na malengo", alisema Kigaila.

    Kwa upande wake Mwalimu ambaye alikuwa mgombea mwenza (Makamu wa rais) wakati wa uchaguzi Mkuu uliopita, alikazia kwa kusema

    "Hatukuingia chadema kufuata vyeo, hatukuingia chadema kufuata fedha, tuliingia chadema kwa sababu tuliamini kuchangia na klupigania mageuzi ya kweli katika nchi hii".

    Kuhusu hatma yao kwenye siasa za Tanzania, kundi hilo la G-55 ambalo linahusishwa na Mwenyekiti aliyepita Freeman Mbowe, ambao baadhi walikuwa sehemu ya sehemu ya Sekretarieti ya chama hicho chini ya yake wanasema hawatakwenda kujiunga na chama tagala, CCM.

    Tunaondoka chadema, tutashauriana na vyama mbalimbali, tutawaambia baadaye tunakwenda wapi", alisema Kigaila na kuungwa mkono na Mwalimu ambaye alisema uelekeo sio CCM...."CCM haiwezi kuwa daraja letu".

    Mpaka sasa, CHADEMA haijatoa tamko rasmi kuhusu uamuzi huo wa viongozi wake wa zamani.

    Soma zaidi:

  6. Waridi wa BBC: 'Mambo ni mawili, umrushe mtoto mtoni au niwauwe nyote wawili'

    Maelezo ya video, Waridi wa BBC: 'Mambo ni mawili, umrushe mtoto mtoni au niwauwe nyote wawili'

    Marion, mwanamke aliyeingia kwenye ndoa akiwa na matumaini ya kuifurahia, lakini badala yake iligeuka na kuwa tamu uchungu.

    Mtoto alipokuwa mgonjwa kila wakati, alitarajia mume wake aliyempenda ndiye atakaye kuwa kimbilio lao. Ila hali ilibadilika kiasi cha kutaka wamrushe mtoto huyo kwenye mto.

    Kipindi anapitia magumu, Mungu hakumuacha peke yake. Alimpa rafiki kwa jina Meresa Achieng aliyesimama naye kwa jua na mvua.

    Kwa mengi zaidi, fuatilia simulizi hii hapa 👇

  7. 'Hakuna anayejua atakayechagulia'

    .

    Watu bado wanaendelea kukusanyika kabla ya mkutano wa Vatican - unaotarajiwa kuanza baadaye leo.

    BBC imezungumza na Padre Thomas Reese, kasisi Mjesuti na mchambuzi mkuu wa Huduma ya Habari za Dini.

    Anasema anasubiri kwa hamu mkutano huo.

    "Nina furaha sana kuhusu nani ataongoza kanisa na kuwa msemaji wa masuala yanayokabili ulimwengu. Tulishuhudia wakati wa Papa Francis jinsi gani alivyoweza kuchangia katika jamii, na ni matumaini yetu kwamba yule atakayechaguliwa atakuwa na mchango wa aina hiyo," alisema.

    Nilimuuliza mawazo yake juu ya nani anaweza kuchaguliwa.

    "Nafkiri hakuna anayejua hadi kufikia sasa! 'Hakuna anayejua atakayechagulia."

  8. Kardinali awasihi wenzake kumchagua Papa anayeweza kuongoza kanisa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kardinali anayeongoza Ibada ya Misa Takatifu kabla ya mkutano wa kumchagua Papa, Giovanni Battista Re, amewataka vijana wenzake kuchagua kiongozi anayeweza kuliongoza Kanisa Katoliki katika kipindi anachokiita “kigumu na chenye changamoto” kwa wakati.

    “Huu ni wito wa kudumisha umoja wa Kanisa... umoja ambao haumaanishi usawa, bali ushirika thabiti na wa kina katika utofauti,” alisema wakati wa Misa.

    Re, ambaye ana umri wa miaka 91, ni mzee sana kupiga kura. Wapiga kura wanatakiwa wawe na umri wa chini ya miaka 80.

    Alisisitiza kuwa kura hiyo ilikuwa ya "umuhimu wa kipekee" na kwamba makadinali walihitaji kuweka kando "kila jambo la kibinafsi".

    Soma zaidi:

  9. Putin anadhihaki juhudi za kutafuta amani za Marekani yasema Ukraine

    Jengo lililoharibiwa

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine ametoa wito wa shinikizo zaidi dhidi ya Moscow kufuatia mashambulizi ya usiku mmoja dhidi ya Kyiv na Zaporizhzhia.

    "Kwa mara nyingine tena, Urusi inashambulia Kyiv. Usiku wenye kelele katika mji mkuu wa Ukraine," Andrii Sybiha anasema katika chapisho kwenye X. "Putin anajibu kwa mashambulizi hayo ya kikatili kwa pendekezo lisilo na masharti la Ukraine la kusitisha mapigano kwa siku 30 au zaidi. Anafanya mzaha wa makusudi kwa juhudi za amani za Marekani."

    Waziri wa mambo ya nje anasema kuadhimisha miaka 80 ya kumalizika kwa Vita vya pili vya dunia pamoja na Vladimir Putin "haikubaliki".

    Kama tumekuwa tukiripoti, gwaride huko Moscow siku ya Ijumaa litaashiria ushindi wa Umoja wa Kisovieti na washirika wake dhidi ya wanazi wa Ujerumani.

  10. Makadinali kutoka kote ulimwenguni wakusanyika kumpigia kura papa ajaye

    Moshi mweupe

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makadinali kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanakusanyika mjini Roma kumchagua papa ajaye baada ya kifo cha Papa Francis siku ya Jumatatu ya Pasaka.

    Hatujui ni muda gani mchakato huu utachukua, mikutano ya awali imechukua siku chache tu, ingawa katika karne za awali kutokubaliana wakati mwingine kulifanya mikutano iendelee kwa miezi.

    Makadinali watashiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter wa Basilica leo asubuhi na baadaye watatembea hadi kwenye Kanisa la Sistine Chapel kupiga kura chini ya picha za Michelangelo.

    Mara tu wanapoingia kwenye kanisa, hawatakuwa na mawasiliano na ulimwengu wa nje hadi papa mpya atakapochaguliwa.

    Kisha tunasubiri moshi utoke dohani. Ukiwa mweusi, kutakuwa na duru nyingi za upigaji kura kesho.

    Moshi mweupe unaashiria kuwa papa mpya amechaguliwa.

    Unaweza kusoma;

  11. Joe Biden: Trump anamridhisha Putin kwa ‘kuinyonga’ Ukraine

    Biden

    Joe Biden ameiambia BBC kwamba shinikizo kutoka kwa utawala wa Trump kwa Ukraine kutoa eneo kwa Urusi ni kuridhisha adui kwa kulegeza msimamo katika mahojiano ya kipekee, yake ya kwanza tangu kuondoka Ikulu ya White House.

    Akizungumza huko Delaware siku ya Jumatatu, alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin anaamini kuwa Ukraine ni sehemu ya Urusi na "mtu yeyote anayefikiri kuwa ataacha" ikiwa eneo fulani litakubaliwa kama sehemu ya makubaliano ya amani "ni upumbavu".

    Biden alisema ana wasiwasi kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Ulaya kuvunjika chini ya Rais Donald Trump, ambao alisema "utabadilisha historia ya kisasa ya dunia".

    Katika mahojiano na kipindi cha Leo cha Radio 4 cha BBC, Biden alipingwa kwa rekodi yake binafsi kuhusu Ukraine na pia uamuzi wake wa kusitisha azma yake ya kuchaguliwa tena 2024 baada ya mjadala uliozua wasiwasi kuhusu kufaa kwake na kukiingiza Chama cha Demokrasia katika mgogoro.

    Alipoulizwa kuhusu namna utawala wa sasa unavyowatendea washirika wa Marekani, rais huyo wa zamani alilaani wito wa Trump wa kutaka Marekani kurudisha Mfereji wa Panama, kuinunua Greenland na kuifanya Canada kuwa jimbo la 51.

    "Kuna nini hapa? Ni rais gani anayewahi kuzungumza hivyo? Sio sisi tulivyo," alisema. "inahusu uhuru, demokrasia, fursa, na sio kunyang'anywa."

  12. Sauti yaonesha jinsi waongoza ndege walivyopoteza mawasiliano na marubani

    Ucheleweshaji wa safari uliendelea kwa siku ya tisa mfululizo kwenye uwanja wa ndege wa Newark Jumanne

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Sauti iliyotolewa hivi karibuni inaonesha wakati waongoza ndege katika mojawapo ya viwanja vya ndege vyenye shughuli nyingi zaidi mjini New York walipopoteza mawasiliano na ndege zilizokuwa chini yao na kumwacha rubani mmoja akiuliza, "Tunakaribia, unatupata?". Rubani aliita mara tano kwa muda wa sekunde 30 kabla ya muongoza ndege kujibu, sauti iliyorekodiwa na LiveATC.net inaonesha.

    Nyakati za wasiwasi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Newark Liberty zilisababisha wafanyikazi wengi kwenda likizo kutokana na kiwewe, na kuchangia mamia ya safari za ndege kuchelewa.

    Waziri wa Uchukuzi wa Marekani Sean Duffy alisema kuwa mawasiliano yalipotea kwa sekunde 30, na kwamba hakuna ndege iliyokuwa hatarini.

    Wengine wachache wamekadiria kuwa mawasiliano yalipotea kwa hadi sekunde 90. "Hizo ni sekunde 90 za anga iliyojaa kabisa ya ndege zinazoruka bila kuwa na muongozo kwenye mojawapo ya viwanja vya ndege vilivyo na shughuli nyingi zaidi Marekani," Seneta wa New York Chuck Schumer alisema Jumanne.

    Sauti iliyotolewa Jumanne na LiveATC.net iko kati ya mnara wa kudhibiti trafiki ya anga huko Philadelphia, na marubani wanaoruka katika eneo karibu na moja ya vitovu vya usafiri vya New York.

    "Nakaribia, unanipata?" rubani mmoja anayewasili kutoka New Orleans anasema, bila jibu. Baada ya majaribio matano zaidi, zaidi ya sekunde thelathini, mnara unajibu: "Nakupata vyema."

    Katika hatua nyingine, mnara wa udhibiti unamwambia rubani wa United Airlines: "Nitakusogeza hapa kwa sababu nimeambiwa tu kwamba mbinu hiyo ilipoteza rada zote." "Skrini tatu kati ya nne za rada zilikuwa nyeusi na hazioneshi masafa."

    Rubani anasikika akijibu kwa utulivu: "Sawa, tuko tayari kusonga mbele." Tukio hilo la tarehe 28 Aprili lilichangia mamia ya safari za ndege kuchelewa kuendelea hadi Jumanne.

    Waziri Duffy alisema kukatika kwa mawasiliano ni "ishara kwamba tuna mfumo dhaifu, na lazima urekebishwe". Utawala wa Shirikisho la Usafiri wa Anga pia ulikiri katika taarifa kwamba "mfumo wetu wa zamani wa udhibiti wa trafiki wa anga unaathiri nguvu kazi yetu".

    Shughuli za udhibiti wa usafiri wa anga katika uwanja wa ndege huko New Jersey zimekuwa na ukosoaji wa mara kwa mara hivi karibuni.

    Wiki iliyopita, United Airlines ilitangaza kuwa inaghairi safari 35 za ndege kwa siku kutoka kwenye ratiba yake ya Newark kwa sababu uwanja wa ndege "hauwezi kushughulikia idadi ya ndege ambazo zimepangwa kufanya kazi hapo".

  13. EU yapanga kuacha uagizaji wa gesi ya Urusi ifikapo mwisho wa 2027

    Kujibu mipango hiyo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumanne kwamba Ulaya ilikuwa ikijiwekea mazingira magumu yenyewe.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tume ya Ulaya imechapisha "ramani" inayoelezea mipango yake ya kukomesha utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya Urusi katika miaka ijayo.

    Chini ya mipango hiyo, uagizaji wa gesi yote ya Urusi na gesi asilia ya kimiminika kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya utapigwa marufuku kufikia mwisho wa 2027.

    "Hatutaruhusu tena Urusi kutumia nishati dhidi yetu... Hatutasaidia tena kwa njia isiyo ya moja kwa moja kujaza masanduku ya fedha [ya Kremlin]," Kamishna wa Nishati wa Ulaya Dan Jorgensen alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Strasbourg Jumanne.

    Kujibu mipango hiyo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumanne kwamba Ulaya ilikuwa ikijiwekea mazingira magumu yenyewe.

    EU iliapa kusitisha uhusiano wake wa nishati na Urusi baada ya Moscow kuanzisha uvamizi wake nchini Ukraine mnamo 2022.

    Vifungu vya mapendekezo ya kisheria vitawasilishwa mwezi Juni vikitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya kufanya "mipango ya kitaifa" ya kukomesha uagizaji wa gesi ya Urusi na mafuta ya nyuklia kulingana na Tume ya Ulaya.

    Nchi wanachama wa EU lazima ziwasilishe mikakati chini ya mipango ya kuchukua nafasi ya uagizaji wa mafuta ya Urusi ifikapo mwisho wa 2027.

    Nchi pia zimetakiwa kueleza mikakati ya kukomesha utegemezi wao kwa Urusi kwa madini ya urani, urani iliyorutubishwa na vifaa vingine vya nyuklia.

    Unaweza kusoma;

  14. Marekani, China kuanza mazungumzo kuhusu vita vya kibiashara wiki hii

    Marekani, China kuanza mazungumzo kuhusu vita vya kibiashara wiki hii

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa Marekani na China wanatazamiwa kuanza mazungumzo wiki hii ili kujaribu kupunguza vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

    Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng atahudhuria mazungumzo hayo nchini Uswizi kuanzia tarehe 9 hadi 12 Mei, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema.

    Waziri wa Hazina ya Marekani Scott Bessent na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) Jamieson Greer watawakilisha Washington katika mkutano huo, ofisi zao zilitangaza.

    Tangu arejee katika Ikulu ya White House, Rais Donald Trump ametoza ushuru mpya wa kuagiza bidhaa za China hadi 145%.

    Beijing imelipiza kwa ushuru 125% kwa baadhi ya bidhaa kutoka Marekani.

    Lakini wataalamu wa biashara duniani wameiambia BBC kwamba wanatarajia mazungumzo kuchukua miezi kadhaa.

    Vyombo vya habari vya serikali ya China viliripoti kuwa Beijing imeamua kushirikiana na Marekani baada ya kuzingatia kikamilifu matarajio ya kimataifa, maslahi ya nchi na maombi kutoka kwa biashara za Marekani.

    Ripoti hiyo iliongeza kuwa China iko tayari kwa mazungumzo lakini ikasisitiza kuwa ikiwa nchi hiyo itaamua kuendelea kupigana vita hivi vya kibiashara, itapigana hadi mwisho.

    Vita vya kibiashara vimezua msukosuko katika masoko ya fedha na kusababisha mitikisiko katika biashara ya kimataifa.

    Unaweza kusoma;

  15. India yaanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Pakistan na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan

    Msemaji wa jeshi la Pakistani anasema Islamabad "itajibu [shambulizi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Serikali ya India inasema vikosi vyake vimeanzisha "Operesheni Sindoor", "kupiga miundombinu ya kigaidi" nchini Pakistani na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan "kutoka ambapo mashambulizi ya kigaidi dhidi ya India yamepangwa na kuelekezwa".

    Katika taarifa, serikali ya India inasema "maeneo tisa yamelengwa".

    "Vitendo vyetu vimekuwa vikizingatia, kupimwa na visivyo vya kuongezeka kwa asili. Hakuna vituo vya kijeshi vya Pakistani ambavyo vimelengwa. India imeonesha kujizuia kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa shabaha na mbinu ya utekelezaji."

    Taarifa hiyo inaongeza kuwa shambulio hilo liliamriwa baada ya shambulio baya la mwezi uliopita la wanamgambo dhidi ya watalii huko Kashmir inayodhibitiwa na India.

    Msemaji wa jeshi la Pakistani anasema Islamabad "itajibu [shambulizi] hili kwa wakati na mahali itakapochagua".

    "Ndege zetu zote za jeshi la anga ni za angani. Hili ni shambulio la aibu na la woga ambalo lilifanywa kutoka ndani ya anga ya India," msemaji huyo anaongeza.

  16. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo