Moja kwa moja, Iran yasema vita na Marekani huenda vikaanza tena

Kwa mujibu wa Mohammad Asadi, Naibu Mkaguzi wa IRGC, majeshi ya Iran yako tayari kujibu shambulio lolote litakaloweza kutokea.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Vita vya Ukraine: Zelensky asema Urusi imezidisha mashambulizi ya droni ndani ya wiki moja

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi imeongeza kasi ya mashambulizi dhidi ya nchi yake, ikitumia takriban droni 1,600 za mashambulizi, mabomu yaliyoongozwa karibu 1,100 na makombora matatu ndani ya wiki moja.

    Zelensky amesema Moscow inalenga kuzidiwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine kupitia mashambulizi makubwa ya mfululizo, akisisitiza kuwa uwasilishaji wa makombora ya ulinzi kila siku bado ni wa muhimu. Ameongeza kuwa shinikizo la kimataifa dhidi ya Urusi haipaswi kulegezwa, akionya kuwa kupunguzwa kwa vikwazo kunaipa Urusi nafasi ya kuongeza fedha za kuendesha vita.

    Wakati huohuo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema imeidungua jumla ya droni 215 za Ukraine katika usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi, katika maeneo mbalimbali ya Urusi pamoja na Bahari ya Azov na Bahari Nyeusi.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, droni hizo zilidunguliwa katika mikoa ya Belgorod, Bryansk, Voronezh, Kaluga, Kursk, Novgorod, Oryol, Pskov, Rostov, Smolensk, Tver na Tula, pamoja na mkoa wa Moscow, Krasnodar Krai, Crimea iliyounganishwa na Urusi, Bahari ya Azov na Bahari Nyeusi.

    Soma zaidi:

  2. Saudi Arabia yatangaza sheria mpya za kwenda kufanya ibada ya Hajj huko Makka

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka za Saudi Arabia zimeweka masharti mapya kwa mahujaji wa Hajj, zikizuia watoto walio chini ya umri wa miaka 15 kushiriki katika ibada hiyo ya kila mwaka, kuanzia msimu wa Hajj 2025 hadi Hajj 2026.

    Mamlaka hizo zimethibitisha kuwa visa zilizotolewa kwa waombaji walio chini ya umri huo zimesitishwa, huku mashirika ya ndege yakielekezwa kuzuia mahujaji wa kundi hilo kupanda ndege.

    Familia zilizoathiriwa na uamuzi huo zitarejeshewa fedha zote zilizolipwa kwa maombi yaliyofutwa.

    Wizara ya Hijja na Umrah ya Saudi Arabia imesema uamuzi huo umechukuliwa ili kuhakikisha usalama na kudhibiti idadi ya watu wakati wa ibada ya Hajj, ambayo huhudhuriwa na mamilioni ya waumini kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

    Wizara hiyo imesema watoto walio chini ya miaka 15 wako katika hatari zaidi na hawawezi kustahimili changamoto za kimwili za ibada hiyo, ikitaja uchovu, upungufu wa maji mwilini na ajali katika maeneo yenye msongamano mkubwa.

    Ingawa hakuna kikomo cha juu cha umri kwa Hajj, mahujaji walio chini ya miaka 18 wanatakiwa kusafiri wakiwa na mlezi au mtu mzima anayewahudumia.

    Masharti haya hayahusiani na Umrah, ambapo watoto bado wanaruhusiwa kushiriki, ingawa baadhi ya vizuizi vya msimu vinaweza kuwekwa nyakati za msongamano mkubwa.

    Hatua hii ni sehemu ya mabadiliko mapana yanayolenga kuboresha usimamizi na usalama wa Hajj, ambayo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kila mwaka duniani.

    Soma zaidi:

  3. Mali yakamata wanajeshi wanaoshukiwa kushirikiana na waasi wakati mvutano ukiongezeka

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kijeshi mjini Bamako, Mali, amesema kundi la wanajeshi wamekamatwa kuhusiana na mashambulizi makubwa ya pamoja yaliyofanywa hivi karibuni na wanamgambo wa jihadi na makundi ya wanaotaka kujitenga nchini humo.

    Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa Ijumaa usiku, ofisi ya mwendesha mashtaka imesema uchunguzi ulibaini kuwa baadhi ya wanajeshi, wakiwemo wanaohudumu kazini, waliofukuzwa au waliostaafu, walihusika kupanga, kuratibu na kutekeleza mashambulizi hayo.

    Kati ya wanajeshi watano waliotambuliwa mara moja ni Sajini, askari wa cheo cha kiufundi, mshauri mkuu wa kamanda wa kikosi kuhusu masuala ya askari na mwanajeshi mstaafu.

    Mwanajeshi aliyefukuzwa kazi Alassane Diallo maarufu kama Abedi aliuawa katika mapigano yaliyotokea Kati, imeeleza taarifa hiyo.

    Wakati huohuo, wachunguzi wamesema baadhi ya wanasiasa pia walihusika katika mashambulizi hayo, wakimtaja Dkt. Oumar Mariko, kiongozi maarufu wa upinzani anayeishi uhamishoni.

    Dkt. Mariko hivi karibuni alitajwa kwenye vyombo vya habari baada ya kuripotiwa kukutana na wanamgambo wa kundi la jihadi la JNIM lenye uhusiano na Al Qaeda, katika mazungumzo ya kutaka kuachiliwa kwa mateka.

    “Tayari kukamatwa kwa awamu ya kwanza kumefanyika kwa mafanikio, na washukiwa wengine wote, washirika na wasaidizi wao wanaendelea kusakwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo, ikiongeza kuwa uchunguzi zaidi utaendelea.

    Kukamatwa huko kunakuja wakati ambapo wanamgambo wa jihadi wakitoa wito wa kuungana kwa nguvu moja kuiondoa serikali ya kijeshi na kuanzisha utawala wa mpito mpya.

    Unaweza pia kusoma :

  4. Shirika la ndege la Spirit Airlines lafuta safari baada ya kukosa msaada wa dola milioni 500

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la ndege la gharama nafuu la Marekani, Spirit Airlines, limetangaza kusitisha shughuli zake.

    Uongozi wa shirika hilo umesema uamuzi huo umetokana na kushindwa kupata msaada wa kifedha wa dola milioni 500 kutoka kwa utawala wa Trump.

    Spirit ilikuwa katika mazungumzo na serikali ya Marekani kuhusu mpango wa kuiokoa kampuni hiyo dhidi ya kufilisika, lakini mazungumzo hayo yalivunjika.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake Jumamosi, Spirit Airlines imesema kwa masikitiko makubwa imeanza mara moja mchakato wa kusitisha shughuli zake kwa utaratibu.

    Shirika hilo lilikuwa likijaribu kujinasua kutoka hatua za kufilisika kwa mara ya pili katika miaka ya karibuni, lakini kupanda kwa bei ya mafuta ya ndege kutokana na vita kati ya Marekani, Israel na Iran kuliongeza shinikizo kubwa la kifedha.

    Kwa mujibu wa kampuni hiyo, safari zote zinazokuwa zimeratibiwa za Spirit zimefutwa.

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa abiria walionunua tiketi moja kwa moja kupitia Spirit kwa kutumia kadi ya benki au kadi ya malipo watarejeshewa fedha moja kwa moja kupitia njia waliyotumia kulipa.

    Walionunua tiketi kupitia mawakala wa safari wametakiwa kuwasiliana moja kwa moja na mawakala wao ili kurejeshewa fedha.

    Hata hivyo, fidia kwa waliolipia tiketi kwa vocha, pointi za safari au njia nyingine itaamuliwa baadaye katika mchakato wa mahakama ya kufilisika.

  5. 'Marekani yadanganya kuhusu gharama za vita vya Iran' - Araqchi

    Maafisa wa Iran watoa majibu yanayofanana kwa Trump

    Chanzo cha picha, TANSIM

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema Idara ya Ulinzi ya Marekani inatoa taarifa za uongo kuhusu gharama halisi za vita dhidi ya Iran.

    Kauli hiyo inajiri baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth kusema kuwa Marekani imetumia takriban dola bilioni 25 katika vita hivyo.

    Akijibu madai hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Araqchi amesema Pentagon inadanganya, akidai kuwa hatua ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imeigharimu Marekani dola bilioni 100 hadi sasa, kiasi ambacho ni mara nne zaidi ya kilichotajwa rasmi.

    Araqchi ameongeza kuwa gharama zisizo za moja kwa moja kwa walipa kodi wa Marekani ni kubwa zaidi, akisema gharama ya kila mwezi kwa kila familia ya Marekani inakaribia dola 500 na inaendelea kuongezeka kwa kasi.

    Amesema sera ya “Israel kwanza” inaifanya Marekani kuwa ya mwisho.

    Kauli hiyo inakuja wakati Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth akitetea matumizi ya vita dhidi ya Iran mbele ya Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Baraza la Wawakilishi.

    Hegseth amesema gharama ya vita hivyo hadi sasa inakadiriwa kuwa dola bilioni 25, akisisitiza kuwa matumizi hayo yalikuwa ya lazima kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia.

    Soma zaidi:

  6. Iran yasema vita na Marekani huenda vikaanza tena

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohammad Jafar Asadi, Naibu Mkaguzi wa Makao Makuu ya Khatam al Anbiya ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, amesema kuna uwezekano wa mzozo mpya kuzuka tena kati ya Iran na Marekani.

    Amesema dalili zinaonyesha kuwa Marekani haizingatii ahadi wala makubaliano yoyote.

    Kwa mujibu wa Asadi, kauli na hatua nyingi za viongozi wa Marekani zinalenga zaidi vyombo vya habari, kwa lengo la kuzuia bei ya mafuta kushuka na kujinasua katika matatizo waliyojitengenezea wenyewe.

    Ameongeza kuwa majeshi ya Iran yako tayari kujibu shambulio lolote litakaloweza kutokea.

    Kauli hiyo inatolewa wakati makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani yakikaribia kumalizika ndani ya takriban wiki tatu.

    Hata hivyo, licha ya usitishaji huo wa mapigano, mvutano bado umeendelea katika Mlango wa Hormuz, ambao bado umefungwa.

    Soma zaidi:

  7. Harusi ya TikTok Kenya yavutia zaidi ya watazamaji 50,000 mitandaoni

    Gladys na Bernard Orieny, maarufu kama Janabi Junior, waliapa kiapo cha ndoa katika hafla iliyoongozwa na 'mchungaji wa TikTok', Askofuu Auka.

    Chanzo cha picha, Socials/ Tiktok

    Maelezo ya picha, Wanandoa walikuwa na kamera wakila kiapo cha kuoana huku watazamaji wakiandika ujumbe za kuwapongeza.

    Wanandoa wa kizazi cha Gen Z nchini Kenya wameandika historia kwa kufunga ndoa kupitia TikTok, katika sherehe iliyofanyika usiku wa Ijumaa tarehe 1 Mei 2026.

    Gladys na Bernard Orieny, maarufu kama Janabi Junior, walikula kiapo cha ndoa katika hafla iliyoongozwa na 'mchungaji wa TikTok', Askofuu Auka.

    Sherehe hiyo ilianza saa nne usiku na kuendelea hadi baada ya usiku wa manane, ikifanyika mtandaoni pekee huku zaidi ya watu 50,000 wakifuatilia mubashara.

    Harusi hiyo, imetajwa kama “isiyo na gharama kubwa,” na kuwavutia wakenya walioko nchini humo na ughaibuni.

    'Askofu' Auka alibainisha katika video hiyo iliyoonekana na BBC Swahili kuwa hii ilikuwa harusi ya pili kuiongoza kupitia mtandao wa TikTok.

    Bi harusi alivalia gauni jeupe lakuvutia na ushungi uliolingana, huku bwana harusi akiwa na koti jeupe la suti aina ya Tuxedo, tai nyeusi na suruali nyeusi.

    BBC haijathibitisha kikamilifu iwapo wanandoa hao wameoana rasmi au ni sherehe.

    Tofauti na harusi za jadi zinazofanyika makanisani, misikitini au ofisi ya Mwanasheria Mkuu, sherehe hii ilifanyika kikamilifu mtandaoni kutoka nyumba moja jijini Nairobi.

    Wanandoa walikuwa na kamera wakila kiapo cha kuoana huku watazamaji wakiandika ujumbe za kuwapongeza.

    Hata hivyo, Wataalamu wa sheria wamebainisha kuwa ili ndoa itambuliwe kisheria nchini Kenya, lazima izingatie masharti ya Sheria ya Ndoa, ikiwemo kusajiliwa na kuhalalishwa na mtu aliyepewa leseni.

    Tukio hili linaonyesha ushawishi unaokua wa majukwaa ya kidijitali kama TikTok katika kubadilisha namna kizazi cha Gen Z kinavyosherehekea na kuadhimisha hatua muhimu za maisha.

    g

    Chanzo cha picha, socials

    Maelezo ya picha, Ni picha ya ndoa ya kwanza kufungwa mubashara katika mtandao wa Tiktok nchini Kenya

    Unaweza pia kusoma:

  8. Rais wa Namibia Netumbo Nandi - Ndaitwah amaliza kulipa deni lote la IMF

    Netumbo Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama sugu wa chama tawala tangu awe na umri wa miaka 14

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Netumbo Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama sugu wa chama tawala tangu awe na umri wa miaka 14

    Rais wa Namibia, Netumbo Nandi‑Ndaitwah, ameiongoza nchi yake kufikia hatua muhimu ya kiuchumi kwa kukamilisha malipo ya deni la Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

    Namibia imelipa jumla ya dola milioni 23.9, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa madeni ya nje na kuimarisha uthabiti wa uchumi wa taifa hilo.

    Kukamilika kwa deni hili kunatajwa kuongeza uhuru wa kifedha wa Namibia na kuipa serikali nafasi pana zaidi ya kuelekeza rasilimali zake katika miradi ya maendeleo ya ndani.

    Hatua hii imepokelewa kama ushindi mkubwa katika usimamizi wa fedha za umma chini ya uongozi uliopo, ikionyesha uthabiti wa kiuchumi wa nchi hiyo katika ukanda wa Kusini mwa Afrika. Kwa mujibu wa takwimu hadi Machi mwaka huu, malipo hayo yamefikia jumla ya dola milioni 23.8875.

    Namibia sasa imejiunga na mataifa mengine ya Afrika, ikiwemo Msumbiji, ambayo yamefanikiwa kufuta madeni yao kwa IMF, ikifuata mwenendo wa kupunguza mikopo ya nje na kuimarisha nidhamu ya kifedha.

    Akiwa na umri wa miaka 72 rais wa kwanza mwanamke Namibia alishinda uchaguzi kwa 57% ya kura huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26% ya kura, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.

    Netumbo Nandi-Ndaitwah ameingia madarakani mwezi Disemba 2024.

  9. Marekani yauza silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.6 kwa washirika wake wa kikanda

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imeidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya jumla ya dola bilioni 8.6 kwa washirika wake katika Mashariki ya Kati, uamuzi uliotolewa zaidi ya wiki tatu baada ya kusitishwa kwa mapigano kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Nchi zitakazonufaika na silaha hizo ni Israel, Qatar, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Kwa mujibu wa mpango huo, Qatar itapatiwa mfumo wa ulinzi wa anga na makombora wa Patriot pamoja na vifaa husika, wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 4.

    Aidha, mauzo ya mifumo ya silaha za mashambulizi ya usahihi wa hali ya juu pia yameidhinishwa, yakiwa na thamani ya dola milioni 992.4.

    Kuwait imeidhinishwa kupokea mfumo jumuishi wa amri ya vita wenye thamani ya dola bilioni 2.5, huku Israel ikiruhusiwa kununua mifumo hiyo hiyo ya silaha za mashambulizi ya usahihi yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 992.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imeidhinisha mauzo ya mfumo huo huo kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 147.

    Soma zaidi;

  10. Uhaba wa vileo washuhudiwa Saudi Arabia kutokana na vita mashariki ya kati

    f

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Duka pekee la serikali la pombe nchini Saudi Arabia linakabiliwa na upungufu wa bidhaa mbalimbali, kuanzia bia na mvinyo hadi tequila, huku wateja wakiiambia Reuters kuwa usambazaji umechelewa kutokana na athari za vita vya Iran.

    Duka hilo lililopo katika eneo la kidiplomasia mjini Riyadh linafanya kazi bila jina wala bango la kunadi biashara.

    Lilifunguliwa mwaka 2024 kuhudumia mabalozi wasio Waislamu, na mwaka uliopita likapanua huduma zake kwa wafanyakazi matajiri wasio Waislamu kutoka nje ya nchi.

    Hata hivyo, marufuku kamili ya matumizi ya pombe iliyoanza kutumika mwaka 1952 bado yanaendelea nchini Saudi Arabia. Licha ya msimamo wake wa kihafidhina, taifa hilo limeruhusu duka moja lenye leseni kwa lengo la kuvutia wafanyakazi wa kigeni.

    Kwa mujibu wa Reuters, watu watano waliolitembelea duka hilo siku za hivi karibuni walisema rafu zake zilikuwa na bidhaa kidogo za pombe, ambazo ni ghali na zingine za kampuni zisizojulikana sana.

    Unaweza kusoma pia:

  11. Marekani kuondoa wanajeshi 5,000 Ujerumani kufuatia mvutano na Merz

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Idara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuondoa takriban wanajeshi wake 5,000 nchini Ujerumani.

    Hatua hiyo inaonekana kama ujumbe wa kisiasa kwa mshirika wake wa NATO, huku mvutano kati ya Rais Donald Trump na mataifa ya Ulaya ukiongezeka kufuatia vita vya Iran.

    Trump alikuwa ametishia mapema wiki hii kupunguza uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Ujerumani.

    Kauli hiyo ilijiri baada ya mzozo wa maneno kati yake na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ambaye alisema "Wamarekani hawana mkakati" na hangeweza kuona "ni njia gani ya kutoka" ambayo wanaweza kuchagua.

    "Wairani ni wazi wana ustadi mkubwa wa kufanya mazungumzo, au tuseme, ni wastadi sana wa kutofanya mazungumzo, kuwaruhusu Wamarekani kusafiri hadi Islamabad na kisha kuondoka tena bila matokeo yoyote," alisema. Akaongezea kuwa "taifa zima" akirejelea Marekani ilikuwa "linafedheheshwa" na uongozi wa Iran.

    Msemaji wa Pentagon Sean Parnell amesema mchakato wa kuondoa wanajeshi hao unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita hadi kumi na mbili.

    Trump pia amependekeza kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Italia na Uhispania.

    "Italia haijatusaidia chochote na Uhispania imekuwa ya kutisha," aliongeza, akiwakosoa kwa majibu yao kuhusu vita nchini Iran. "Katika hali zote walisema, 'Sitaki kujihusisha.'

    Soma Pia:

  12. Trump asema ataongeza ushuru kwa magari yanayoagizwa kutoka Ulaya hadi asilimia 25

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza ushuru unaotozwa magari na malori yanayoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya hadi asilimia 25, hatua inayoongeza kwa kasi mvutano wa kibiashara kati ya Washington na Brussels.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump ameshutumu Umoja wa Ulaya kwa kile alichokiita kutotekeleza makubaliano ya biashara ambayo tayari yalikuwa yameafikiwa, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

    “Nimefurahi kutangaza kwamba… wiki ijayo nitaongeza ushuru unaotozwa Umoja wa Ulaya kwa magari na malori,” alisema Trump Ijumaa.

    Tume ya Ulaya imejibu kwa kusema itaendelea kuweka chaguo zote mezani ili kulinda maslahi ya Umoja wa Ulaya.

    Tume hiyo imesema EU inatekeleza wajibu wake katika makubaliano hayo, lakini pia inatafuta ufafanuzi zaidi kutoka Marekani kuhusu upande wake wa utekelezaji.

    Hatua ya Trump kulenga sekta ya magari imechukuliwa kama pigo kubwa, ikizingatiwa sekta hiyo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Ulaya.

    Hatua hiyo inakuja chini ya mwaka mmoja tangu EU na Marekani zikubaliane makubaliano katika uwanja wa gofu wa Turnberry nchini Scotland, yaliyopunguza ushuru wa bidhaa nyingi za Ulaya hadi asilimia 15.

    Makubaliano hayo yalionekana kuiletea EU nafuu baada ya Trump kutishia ushuru wa hadi asilimia 30 chini ya mpango wake mpana wa kile alichokiita “Siku ya Ukombozi.” Kwa upande wake, Ulaya ilikubali kuwekeza Marekani na kufanya mabadiliko yaliyotarajiwa kuongeza mauzo ya bidhaa za Marekani.

    Alipoulizwa ni kwa namna gani EU imekiuka makubaliano hayo, Trump hakutoa ufafanuzi.

    Alisema: “Tuna makubaliano ya biashara na Umoja wa Ulaya. Hawakuyazingatia ipasavyo, ndiyo maana nimeongeza ushuru kwa magari na malori.”

    Soma zaidi:

  13. Trump: Vita na Iran vimekwisha, lakini hatutaondoka haraka

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mbele ya Bunge la Marekani kuwa vita na Iran “vimekwisha,” huku akisisitiza kuwa hana nia ya kusitisha mzozo huo kwa haraka.

    Rais huyo pia amejaribu kuimarisha hoja yake kwamba hahitaji idhini ya wabunge kuendelea na operesheni hiyo ya kijeshi.

    Katika barua aliyowasilisha kwa viongozi wa Bunge Ijumaa, Mei mosi, wakati ukikaribia mwisho wa muda wa kuwasilisha taarifa kuhusu vita hivyo, Trump alisema hakuna mapigano yoyote yaliyotokea kati ya pande hizo mbili tangu kusitishwa kwa mapigano.

    Ameiambia Congress kuwa “mapigano yaliyoanza Februari 28, 2026 yamekamilika.”

    Kwa mujibu wa Sheria ya Madaraka ya Vita ya mwaka 1973 nchini Marekani, rais anaweza kutumia nguvu za kijeshi bila idhini ya Bunge kwa siku 60 pekee. Baada ya hapo, anatakiwa kusitisha operesheni, kupata idhini ya Bunge, au kuomba nyongeza ya siku 30 endapo kuna dharura ya kijeshi inayohusiana na usalama wa majeshi ya Marekani wakati wa uondoaji.

    Trump pia amesema Marekani haina mpango wa kusitisha mapambano na Iran mapema, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha “tatizo lilelile kujirudia baada ya miaka michache.”

    Wakati huohuo, shirika la habari la IRNA liliripoti kuwa Tehran imewasilisha pendekezo jipya la mazungumzo na Marekani kupitia wapatanishi wa Pakistan, lakini Trump alilikataa haraka pendekezo hilo.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya Jumamosi ya tarehe 2/05/2026.