Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Hatupaswi kulipa Uingereza kwa mkataba uliovunjwa - Rwanda

Uingereza ililipa pauni milioni 240 kwa Rwanda kwa mpango huo, ambao haukuanza na umetupiliwa mbali na serikali mpya.

Muhtasari

  • Hatupaswi kulipa Uingereza kwa mkataba uliovunjwa - Rwanda
  • Jeshi la Israel lawataka wakazi wa Gaza kuhama
  • Seneta wa Kwanza wa Democratic apinga ugombea wa Biden
  • Kwa nini Nato ilianzishwa?
  • Binti ya rais atumai kujitokeza kwake kutabadilisha sheria za kupinga mapenzi ya jinsia moja
  • Msako mkali waanzishwa baada ya wanawake watatu kuuawa Kaskazini mwa London
  • Msichana aliyekuwa hali mahututi aliombewa badala ya kupewa dawa - Mahakama yaarifiwa
  • Mwanamke wa Ireland ashtakiwa kwa kujaribu kujiua katika UAE
  • Urusi yaahidi kuwaachilia Wahindi wanaopigana katika jeshi lake
  • Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua watu 29 katika kambi ya Gaza ya waliotoroka makazi yao
  • Picha za Messi na Lamine Yamal akiwa mtoto zaibuka mitandaoni
  • Maandamano ya Gen Z: Ukarabati wa bunge la Kenya kugharimu zaidi ya $1.1m
  • Mahakama ya Urusi yaamuru kukamatwa kwa mke wa Alexei Navalny
  • Mwanasiasa wa Korea Kusini awalaumu wanawake kwa ongezeko la visa vya kujiua kwa wanaume
  • Kome la Ulaya 2024: Uhispania yaichapa 2-1 Ufaransa huku Yamar aking’ara
  • Biden aitetea Nato kwa ukakamavu alipowapokea viongozi wa muungano huo

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi & Seif Abdalla & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo. Kwaheri.

  2. Hatupaswi kulipa Uingereza kwa mkataba uliovunjwa - Rwanda

    Rwanda imesema haitakiwi kuirudishia Uingereza pesa baada ya makubaliano ya mamilioni ya pauni ya wahamiaji kati ya nchi hizo mbili kufutiliwa mbali.

    Waziri Mkuu mpya wa Uingereza na kiongozi wa Chama cha Leba Keir Starmer alitangaza mwishoni mwa juma kwamba mpango wa kuwafukuza baadhi ya watu wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda "umekufa na kuzikwa".

    Mpango huo ulibuniwa na serikali ya awali ya Conservative, ambayo tangu kuuzindua mwaka 2022 imelipa Rwanda £240m ($310m).

    Uamuzi wa kisheria ulimaanisha kuwa mpango huo haujaanza na Uingereza ilionyesha matumaini Jumatatu kwamba pesa kutoka kwa mpango huo zinaweza kurejeshwa.

    Siku iliyofuata, msemaji wa serikali ya Rwanda aliiambia televisheni ya taifa ya nchi hiyo: "Jambo hili lieleweke wazi, kulipa pesa hakukuwa sehemu ya makubaliano."

    Alain Mukuralinda alisema mkataba huo "haujaweka wazi" pesa zinapaswa kurejeshwa na kwamba Uingereza iliwasiliana na Rwanda na kuomba ushirikiano, ambao "ulijadiliwa kwa kina".

    Mnamo mwezi Januari, baada ya miezi 21 ya mpango huo kukwama, Rais wa Rwanda Paul Kagame alipendekeza pesa zingine zingeweza kurejeshwa ikiwa hakuna waomba hifadhi waliotumwa nchini humo.

    Lakini serikali ya Rwanda baadaye ilisema "sio wajibu" kurejesha pesa kwa Uingereza.

    Waziri Mkuu Starmer aliutaja mpango huo kuwa "ujanja" baada ya Chama cha Labour kushinda uchaguzi kwa kishindo wiki iliyopita.

    Chama chake kimeahidi badala yake kuunda Kamandi mpya ya Usalama Mipakani ili kukabiliana na magenge yanayosafirisha watu.

    Upinzani dhidi ya mswada huo pia ulitoka pande nyingine - Mahakama ya Juu Zaidi ya Uingereza ilipoamua mpango huo kuwa kinyume cha sheria, mashirika ya haki za binadamu yaliutaja kuwa ni wa kikatili na wa kibabe, huku wapinzani ndani ya Chama cha Conservative wakishinikiza kufanyiwa marekebisho ambayo yangeulinda vyema mpango huo dhidi ya pingamizi za kisheria.

    Serikali iliyopita ilisema mpango huo ulilenga kuwazuia watu kuvuka Mlango-Bahari wa Uingereza kwa boti ndogo.

    Uhamiaji haramu ni mojawapo ya changamoto kuu zinazoikabili serikali ya Uingereza.

    Soma Zaidi:

  3. Jeshi la Israel lawataka wakazi wa Gaza kuhama

    Jeshi la Israel limewaambia wakazi wote wa mjini Gaza kuhama eneo la kusini hadi katikati mwa Ukanda wa Gaza, huku mashambulizi makali yakiendelea.

    Vipeperushi vilivyorushwa kutoka kwa ndege vinaelekeza "kila mtu katika mjini Gaza" kuondoka katika eneo linalotajwa kuwa "eneo hatari la mapigano" kupitia njia zilizowekwa salama - zilizowekwa alama kama barabara mbili zinazoelekea kwenye makazi huko Deir al-Balah na al-Zawaida.

    Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu amri za kuwahamisha wakazi zinazotolewa na Israel.

    Katika muda wa wiki mbili zilizopita, wanajeshi wa Israel wametoa amri ya kuwataka wenyeji kuondoka na kuingia tena katika maeneo kadhaa ya mji wa Gaza ambako wanaamini Hamas na Palestina Islamic Jihad wamejipanga upya tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

    Mapigano hayo yanaendelea huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu uwezekano wa kusitisha vita na kuachiliwa huru kwa mateka kati ya Israel na Hamas yakitarajiwa kuanza tena nchini Qatar.

    Mazungumzo hayo yatahudhuriwa na wakuu wa kijasusi wa Misri, Marekani na Israel.

    Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu robo-milioni bado wanaishi mjini Gaza - na wengine walionekana wakihama kuelekea kusini.

    Hata hivyo, wakazi wengine hawakutaka kuondoka."Sitaondoka Gaza. Sitafanya kosa la kijinga ambalo wengine wamefanya. Makombora ya Israel hayatofautishi kati ya kaskazini na kusini," mkazi wa Gaza Ibrahim al-Barbari, 47, aliambia BBC.

    "Ikiwa kifo ni hatima yangu na ya watoto wangu, tutakufa kwa heshima katika nyumba zetu," alisema.

  4. Seneta wa kwanza wa Democratic apinga ugombea wa Biden

    Seneta wa kwanza wa chama cha Democratic amehoji hadharani uwezo wa rais Joe Biden katika uchaguzi, baada ya wabunge saba kuvunja ukimywa na kumtaka mzee huyo wa miaka 81 kujiuzulu.

    Seneta Michael Bennet aliiambia CNN kwamba alitarajia rais angeshindwa na Donald Trump kwa "kura nyingi", lakini alisita kumwambia asitishe ugombea wake.

    Maswali yameibuka kuhusu uwezo wa Bw Biden kushika wadhifa huo baada ya utendaji mbaya wa mdahalo wa urais dhidi ya Trump mwishoni mwa mwezi uliopita.

    Rais anasisitiza kuwa anaweza kumshinda mpinzani wake, na anaendelea kuungwa mkono na washirika wakuu baada ya wabunge wa chama cha Democrat kukutana kujadili uongozi wake siku ya Jumanne.

    Rais wa Marekani anafuatiliwa zaidi wiki hii anapoandaa mkutano wa viongozi wa dunia wa Nato, huku suala la msaada wa Ukraine likiwa kwenye ajenda.

    Soma zaidi:

  5. Kwa nini Nato ilianzishwa?

    Mkutano huu wa Nato unaadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo.

    Ilianzishwa mwaka 1949 miaka minne baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia kwa ajili ya ulinzi wa pamoja wa wanachama wake, iliunganisha usalama wa Marekani na washirika wake wa Ulaya dhidi ya Umoja wa Kisovyeti.

    Kufikia 1949, dikteta wa Kisovieti Stalin alikuwa ameweza kuweka serikali za kikomunisti katika nchi nyingi za Ulaya Mashariki kufanya kama "eneo lisilo na vita" kulinda Umoja wa Soviet dhidi ya mashambulizi. Kulikuwa na hofu kwamba Umoja wa Kisovieti ungeweza kufanya vivyo hivyo kwa nchi za Ulaya Magharibi.

    Kizuizi cha Berlin cha 1948 kilishawishi Magharibi kwamba walihitaji shirika la kujihami, katika tukio la shambulio la Soviet dhidi ya nchi ya kibepari.

    Marekani ilikuwa na wasiwasi kwamba Ukomunisti sasa ungeenea katika nchi nyingine na kuundwa kwa Nato kulimaanisha kwamba Marekani inaweza kuweka silaha katika nchi wanachama.

    Shirika lilishuhudia mwisho wa ukomunisti - kushinda kambi ya Soviet bila kurusha risasi. Iliingia vitani kwa mara ya kwanza katika Balkan katika miaka ya 1990.

    Kisha ilianzisha njia mpya - inayoitwa "nje ya eneo" operesheni nje ya mipaka ya Nato, haswa shughuli zake nchini Afghanistan na vita pana dhidi ya ugaidi.

    Soma zaidi:

  6. Binti ya rais atumai kujitokeza kwake kutabadilisha sheria za kupinga mapenzi ya jinsia moja

    Binti wa rais wa Cameroon amesema anatumai kuwa kujitokeza kwake kama anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja kunaweza kusaidia kubadilisha sheria inayopiga marufuku mahusiano ya jinsia moja nchini mwake.

    Brenda Biya aliliambia gazeti la Le Parisien kwamba kulikuwa na watu wengi katika hali kama yake na anatumai kuwatia moyo.

    Msichana huyo mwenye umri wa miaka 27 alisambaza picha yake akimbusu mwanamke mwingine wiki iliyopita, jambo lililozua hisia tofauti nchini Cameroon.

    "Nina kupenda kupita maelezo na ninataka ulimwengu ujue," alisema kwenye ujumbe wa Instagram na picha yake wakikumbatiana na mwanamitindo wa Brazil Layyons Valença.

    Katika mahojiano na gazeti la Ufaransa Le Parisien, alisema hakuwa amemjulisha mtu yeyote katika familia yake kabla ya kuweka ujumbe huo mtandaoni.

    "Kutoka nje ni fursa ya kutuma ujumbe mzito," alisema.

    Aliongeza kuwa anaona sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja, ambayo ilikuwepo kabla ya babake kuingia madarakani, kwamba "si ya haki na ninatumai kwamba simulizi yangu itaibadilisha hilo".

    Paul Biya, 91, amekuwa rais wa Cameroon tangu 1982 na ni mmoja wa viongozi waliokaa madarakani muda mrefu zaidi barani Afrika.

    Biya alisema amekuwa na mwanamitindo huyo wa Brazil kwa muda wa miezi minane na tayari amempeleka Cameroon mara tatu bila kuwaambia familia yake walikuwa kwenye uhusiano.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Msako mkali waanzishwa baada ya wanawake watatu kuuawa Kaskazini mwa London

    Msako mkali umeanzishwa baada ya wanawake watatu kuuawa ndani ya nyumba moja.

    Wanawake hao walipatikana wakiwa wamejeruhiwa vibaya katika eneo la Ashlyn Close, Bushey, Hertfordshire, kabla ya 19:00 saa za eneo Jumanne.

    Wote walifariki dunia katika eneo la tukio, polisi walisema.

    Msako unaendelea kumtafuta Kyle Clifford, 26, kutoka eneo la Enfield, ambaye anasakwa kuhusiana na vifo hivyo. Anaaminika kuwa huko Hertfordshire au London kaskazini na anatembea na mshale, polisi walisema.

    Det Supt Rob Hall, kutoka Hertfordshire Police, alitoa wito kwa yeyote anayefahamu alipo awasiliane na jeshi mara moja.

    Polisi walisema waathiriwa hao watatu wanaaminika kuwa na uhusiano na wakaomba faragha yao kuheshimiwa.

    Det Supt Hall alisema: "Wakati bado tuko katika hatua za awali za uchunguzi huu, tunamtafuta Kyle Clifford ambaye tunaamini anaweza kuwa katika maeneo ya Hertfordshire au London kaskazini.

    “Kutokana na uzito wa tukio hilo, ningeomba yeyote anayefahamu alipo awasiliane na polisi mara moja.

    Pia alitoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa katika eneo la Ashlyn Close kati ya muda wa chakula cha mchana na 19:00 siku ya Jumanne, na ambaye anaweza kuwa na kitu cha kusaidia katika uchunguzi, kuwasiliana na polisi.

    Soma zaidi:

  8. Msichana aliyekuwa hali mahututi aliombewa badala ya kupewa dawa - Mahakama yaarifiwa

    Msichana aliyekuwa hali mahututi aliombewa badala ya kupewa dawa - Mahakama yaarifiwa

    Washiriki wa kundi la kidini nchini Australia wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kumuua msichana mwenye umri wa miaka minane mwenye kisukari kwa kumnyima matibabu na badala yake kusali.

    Elizabeth Struhs alipatikana amefariki dunia katika nyumba moja huko Toowoomba - karibu kilomita 125 (78 mi) magharibi mwa Brisbane - mnamo Januari 2022, baada ya kudaiwa kuwa bila insulini kwa siku kadhaa.

    Waendesha mashtaka wanasema kikundi hicho kiliepuka matumizi ya dawa na kumwamini Mungu "kumponya" mtoto - "imani kali" ambazo tayari zilikuwa zimemaliza maisha ya Elizabeth katika hali kama hiyo miaka mitatu iliyopita.

    Wazazi wa msichana huyo ni miongoni mwa washtakiwa 14, ambao wote wamekataa mawakili.

    Pia wote wamechagua kutojibu mashtaka yoyote.

    Wanaume wawili - babake Elizabeth Jason Struhs, 52, na kiongozi wa kundi la kidini Brendan Stevens, 62 - wameshtakiwa kwa mauaji, huku waendesha mashtaka wakisema walijua hatua za kundi hilo huenda zikamuua Elizabeth.

    Mama wa msichana huyo, Kerrie Struhs, 49, kaka Zachary Struhs, 21, na wengine kumi - wenye umri wa miaka 22 hadi 67 - wanatuhumiwa kwa mauaji.

    Kesi ilipoanza katika Mahakama Kuu ya Queensland siku ya Jumatano, kundi hilo liliwasilishwa mmoja baada ya mwingine, wakiwa wamevalia nguo za gerezani, wakisimama katika nafasi zao kkwenye chumba cha mahakama kilichorekebishwa mahususi ili wote watoshee.

    Soma zaidi:

  9. Mwanamke wa Ireland ashtakiwa kwa kujaribu kujiua katika UAE

    Mwanamke wa Ireland anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu - ikiwa ni pamoja na kujaribu kujiua na kunywa pombe - katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na ameharibiwa hati yake ya kusafiria.

    Inafahamika kuwa Tori Towey amekuwa akifanya kazi kama mhudumu wa ndege na yuko Dubai - jiji kubwa zaidi katika UAE.

    Wakili na mtetezi wa haki za binadamu anayemsaidia alisema kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amezidiwa na amechoka lakini alikuwa na matumaini ya kuondoka Dubai hivi karibuni.

    Radha Stirling, ambaye anaendesha kundi la Waliozuiliwa huko Dubai, alisema alizungumza na Bi Towey Jumatano asubuhi na kwamba "mambo yanaonekana kusonga mbele".

    Kitengo cha usaidizi cha waathiriwa cha polisi wa Dubai sasa kimewasiliana na Bi Towey.

    "Natarajia kwa msukumo wa kidiplomasia tunaweza kumrudisha nyumbani hata kabla ya tarehe ya mahakama wiki ijayo, lakini bila shaka lazima tujipange kwa sababu kuna uwezekano kwenda vibaya sana na hata kufungwa jela," aliambia BBC News NI.

    Bi Stirling hapo awali alisema Bi Towey alishtakiwa kwa unywaji wa pombe na kujaribu kujiua, mambo ambayo alisema kihistoria yalikuwa kinyume cha sheria huko UAE.

    "Serikali ya Ireland iko nyuma yetu kuhakikisha polisi wa UAE wanafuta kesi dhidi yake," alisema.

    BBC imewasiliana na serikali ya UAE ili kutoa maoni yake kuhusu kisa hicho.

    Soma zaidi:

  10. Urusi yaahidi kuwaachilia Wahindi wanaopigana katika jeshi lake

    Urusi imeahidi kuwachilia huru raia wote wa India wanaopigana katika jeshi lake, wizara ya mambo ya nje ya India imesema.

    Tangazo hilo lilitolewa mwishoni mwa ziara ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi mjini Moscow, ambapo alizungumzia suala hilo na Rais Vladimir Putin.

    Delhi imekuwa ikitaka kuachiliwa kwa Wahindi, ambao wanasema walishawishiwa kwenda Urusi kwa ahadi ya kazi zisizo za kijeshi katika jeshi, lakini baadaye wakalazimishwa kupigana nchini Ukraine.

    Takriban wahindi wanne wameuawa katika mapigano hayo.Siku ya Jumanne, Waziri wa

    Mambo ya Nje Vinay Kwatra alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Bw Modi "amezungumzia vikali suala la kuachiliwa mapema" kwa Wahindi ambao "wamepotoshwa katika huduma ya jeshi la Urusi".

    "Upande wa Urusi uliahidi kuwaachilia mapema raia wote wa India kutoka kwa jeshi la Urusi," aliongeza.

  11. Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua watu 29 katika kambi ya Gaza ya waliotoroka makazi yao

    Takriban Wapalestina 29 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la anga la Israel kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao nje ya shule kusini mwa Gaza, maafisa wa hospitali wanasema.

    Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema shambulio hilolimepiga karibu na lango la shule ya al-Awda katika mji wa Abasan al-Kabira, mashariki mwa mji wa Khan Younis.

    Jeshi la Israel lilisema limetumia "mabomu yenye usahihi kumlenga "gaidi kutoka tawi la kijeshi la Hamas" ambaye, lilisema, alishiriki katika shambulio la Oktoba 7 dhidi ya Israel.

    Ilisema ilikuwa "ikiangalia ripoti kwamba raia walijeruhiwa" karibu na shule ya al-Awda, ambayo inawahifadhi watu waliokimbia makazi yao kutoka vijiji vya mashariki vya Khan Younis.

    Tukio hilo limetokea wiki moja baada ya jeshi la Israel kuamuru raia kuhama Abasan al-Kabira na maeneo mengine ya mashariki mwa Khan Younis, na kusababisha makumi ya maelfu kukimbia.

    BBC imezungumza na mashahidi ambao walisema eneo hilo lilikuwa na watu wengi waliokimbia makazi yao wakati huo, na ambao walisimulia matukio hayo ya umwagaji damu kwa kina.

    Shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa na vifo vya wanawake na watoto, kulingana na mashahidi.

  12. Picha za Messi na Lamine Yamal akiwa mtoto zaibuka mitandaoni

    Mwaka 2007, Lionel Messi akiwa mdogo alipiga picha na mtoto kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Camp Nou huko Barcelona kwa picha ya kalenda ya hisani.

    Messi, ambaye alikuwa na umri wa miaka 20, tayari alikuwa amejitengenezea jina na angeendelea kuwa bora zaidi wa wakati wote.L

    akini mpiga picha hakujua kuwa mtoto huyo pia angesababisha mawimbi katika soka la kimataifa chini ya miaka 17 baadaye.

    Messi alikuwa akimuogesha Lamine Yamal - kijana mwenye umri wa miaka 16 ambaye amewashangaza wengi katika mechi za ubingwa wa Ulaya .Bao lake dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali siku ya Jumanne ni moja ambalo litakuwa gumzo kwa miongo kadhaa.

    Akiwa na miaka 16 na siku 362, shambulizi hilo pia lilimfanya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika historia ya mashindano hayo.

    Picha ya Messi na Yamal iliyosahaulika kwa muda mrefu iliibuka tena baada ya babake Yamal kuiweka kwenye Instagram wiki iliyopita ikiwa na maandishi: "Mwanzo wa hadithi mbili."

    Picha hizo zilichukuliwa na Joan Monfort, ambaye anafanya kazi kama mpiga picha wa kujitegemea wa chombo cha habari cha Associated Press.

    Picha hiyo ilitokea baada ya Unicef ​​kucheza mchezo wa bahati nasibu katika mji wa Mataró ambako familia ya Lamine iliishi, alisema.

    "Walijiandikisha kwa bahati nasibu ili picha yao ipigwe huko Camp Nou wakiwa na mchezaji wa Barca. Na walishinda bahati nasibu," Bw Monfort aliambia Associated Press.

    Picha hiyo haikuwa ya moja kwa moja, mpiga picha alisema."Messi ni mvulana anayevutia, ana haya," alisema.

    “Alikuwa akitoka kwenye chumba cha kubadilishia nguo na ghafla akajikuta kwenye chumba kingine cha kubadilishia nguo akiwa na beseni la plastiki lililojaa maji na mtoto ndani yake. Ilikuwa ngumu.

    Hakujua hata jinsi ya kumshika mwanzoni

    Kama Messi, Yamal alienda kuichezea Barcelona, ​​ambapo alikua mwanzilishi na mfungaji mabao mdogo zaidi katika klabu hiyo, na pia mfungaji mdogo zaidi wa mabao katika ligi ya Uhispania.

    Bw Monfort alisema ni wakati tu picha hiyo ilipoanza kusambazwa mitandaoni wiki jana ndipo alipogundua kuwa mtoto huyo alikuwa Yamal.

    "Inafurahisha sana kuhusishwa na kitu ambacho kimesababisha mhemko kama huo," alisema.“Kusema ukweli ni hisia nzuri sana."

  13. Maandamano ya Gen Z: Ukarabati wa bunge la Kenya kugharimu zaidi ya $1.1m

    Tume ya Huduma za Bunge (PSC) imesema takriban Sh150 milioni zitahitajika kukarabati Bunge ambalo liliharibiwa na waandamanaji wanaopinga ushuru wiki mbili zilizopita.

    Kamati hiyo inayoongozwa na spika wa bunge Moses Wetangula imekuwa ikikutana kuchunguza uharibifu uliofanyika kabla ya kukutana na mtaalamu kufanya ukaguzi.

    Baadaye , tume hiyo itawasiliana na mwanakandarasi kufanya marekebisho kabla ya wabunge kurudi na kuendelea na vikao vyao tarehe 23 Julai baada ya kupumzika kwenda likizo ya muda mfupi kuanzia Juni 26 siku moja baada ya kupitisha Muswada tata wa fedha 2024 ambao rais William Ruto aliutupilia mbali.

    Kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya Vyanzo katika bunge ambavyo havikutaka kutajwa vimesema kwamba huku uchunguzi kuhusu uharibifu uliofanywa ukiendelea , gharama ya marekebisho inaweza kuwa juu ya inavyokadiriwa.

  14. Mahakama ya Urusi yaamuru kukamatwa kwa mke wa Alexei Navalny

    Mahakama mjini Moscow imetoa kibali cha kukamatwa kwa mjane wa kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny kwa tuhuma za itikadi kali, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Yulia Navalnaya, ambaye anaishi nje ya Urusi, yanahusiana na madai ya "kushiriki katika jamii yenye msimamo mkali", shirika la habari la Tass lilisema.

    Navalny alikuwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Urusi katika muongo mmoja uliopita.

    Alifariki mwezi Februari katika jela ya Arctic Circle. Mamlaka ya Urusi inasema alikufa kwa sababu za asili - lakini mjane wake anasema Navalny "aliteswa, aliishi bila kula, alikatwa na kuuawa" na rais wa Urusi Vladimir Putin.

    Navalny alikuwa akitumikia miaka 19 jela kwa mashtaka ya itikadi kali ambayo yalionekana kuwa ya kisiasa.

    Akijibu hati ya kukamatwa kwake, Yulia Navalnaya alichapisha kwenye X: "Unapoandika juu ya hili, tafadhali usisahau kuandika jambo kuu: Vladimir Putin ni muuaji na muhalifu wa vita."Mahali pake ni gerezani, na sio pengine The Hague, kwenye seli lilio na TV, lakini nchini Urusi - katika seli ile ile ya mita mbili kwa tatu ambayo alimuua Alexei.

    "Mahakama ya Moscow iliamua kwamba Bi Navalnaya, ambaye ameapa kuendelea na kazi ya mumewe, asakwe na azuiliwe rumande.

    Uamuzi huo unamaanisha kwamba atakakamatwa ikiwa atakanyaga nchini Urusi.

  15. Mwanasiasa wa Korea Kusini awalaumu wanawake kwa ongezeko la visa vya kujiua kwa wanaume

    Mwanasiasa mmoja nchini Korea Kusini amekosolewa kwa kutoa maoni hatari na yasiyothibitishwa baada ya kuhusisha ongezeko la kujiua kwa wanaume na jukumu la "kutawala" kwa wanawake katika jamii.

    Katika ripoti, diwani wa Jiji la Seoul Kim Ki-duck alisema kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika wafanyikazi kwa miaka mingi kunafanya iwe vigumu kwa wanaume kupata kazi na kupata wanawake wanaotaka kuwaoa.

    Amesema nchi hiyo hivi majuzi "imeanza kubadilika na kuwa jamii inayotawaliwa na wanawake" na kwamba hii inaweza "kwa kiasi fulani kuwajibika kwa ongezeko la majaribio ya kujitoa uhai kwa wanaume".

    Korea Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya kujiua kati ya nchi tajiri duniani lakini pia ina rekodi mbaya zaidi juu ya usawa wa kijinsia.

    Maoni ya Diwani Kim yamekosolewa kuwa ya hivi punde zaidi katika msururu wa matamshi ya nje yaliyotolewa na wanasiasa wanaume.

    Diwani Kim, kutoka Chama cha Kidemokrasia, alitoa maoni hayo wakati wa kuchambua data kuhusu idadi ya majaribio ya kujiua yaliyofanywa kwenye madaraja kando ya mto Han wa Seoul.

    Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya baraza la jiji, ilionyesha kuwa idadi ya watu waliojaribu kujiua kando ya mto huo imeongezeka kutoka 430 mwaka 2018 hadi 1,035 mwaka 2023, na kati ya wale wanaojaribu kujitoa uhai, idadi ya wanaume ilikuwa imepanda kutoka 67%. hadi 77%.

  16. Kombe la Ulaya 2024: Uhispania yaichapa 2-1 Ufaransa huku Yamal aking’ara

    Lamine Yamal amekuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya michuano ya Uropa wakati Uhispania ilipoilaza Ufaransa katika shindano la kutinga fainali ya Euro 2024.

    Baada ya Randal Kolo Muani kufunga bao kwa kichwa kutoka kwa pasi ya Kylian Mbappe na kuwapa Ufaransa bao la mapema, Yamal alifunga bao lake la kwanza kutoka nje ya eneo la hatari na kuandika jina lake kwenye vitabu vya rekodi kwa kufunga akiwa na umri wa miaka 16 na siku 362.

    Bao la Yamal lilipatikana dakika ya 21, na Uhispania walikuwa mbele dakika nne baadaye huku shambulio la Dani Olmo likimgusa beki wa Ufaransa, Jules Kounde na kuingia wavuni.

    Ufaransa ilibidi wajitokeze kupambamba zaidi baada ya kipindi cha kwanza cha kusisimua - na walifanya hivyo, huku Aurelien Tchouameni akiokoa mpira wa kichwa na Mbappe akinyimwa nafasi licha ya juhudi zake kubwa za kutafuta bao la kusawazisha.

    Nahodha huyo wa Ufaransa, akicheza bila barakoa jeusi kwa mara ya kwanza tangu avunjike pua mwanzoni mwa michuano hiyo, alipata nafasi kubwa ya kusawazisha dakika za mwisho - lakini alifanya shambulizi lililopaa juu ya lango.

    Uhispania ilifanya mashambulizi mengi zaidi kwenye mechi hiyo huku Ufaransa, kwa upande wao, walifanya mashambulizi machache dhidi ya timu ambayo itamenyana na England au Uholanzi katika fainali ya Jumapili.

  17. Biden aitetea Nato kwa ukakamavu alipowapokea viongozi wa muungano huo

    Rais wa Marekani Joe Biden amewakaribisha viongozi wa Nato mjini Washington DC kwa hotuba aliyotoa kwa ukakamavu ambayo ilionekana kutolewa kuwahakikishia washirika walio ng'ambo na wa nyumbani kwamba anaweza kupambana na changamoto inayokuja ya uchaguzi kutoka kwa Donald Trump.

    Akitoa hotuma fupi lakini yenye matamshi yaliyotolewa kwa nguvu wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, rais Biden alitangaza muungano wa kijeshi "wenye nguvu zaidi kuliko hapo awali" wakatiukikabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika kizazi cha vita nchini Ukraine.

    Aliuita "wakati muhimu" kwa Ulaya na ulimwengu huku akitahadharisha kwamba "watawala wa kiimla wamepindua utaratibu wa kimataifa".

    Bw Biden alitangaza msaada zaidi wa kijeshi kwa ulinzi wa anga wa Ukraine ambao ulikuwa unakabiliwa.

    "Vita vitaisha na Ukraine kusalia kuwa nchi huru na huru," Bw Biden. "Urusi haitashinda. Ukraine itashinda." Alisema.

    Bw Biden na viongozi wa Ujerumani, Italia, Uholanzi na Romania wanachangia betri za makombora za Patriot na mifumo mingine ya ulinzi wa anga kwa Ukraine.

    Rais wa Marekani alizungumza kwa takriban dakika 13 kwa sauti inayosisika yenye tofauti kubwa na sauti ya kuteteleka na ya upole aliyoitoa wakati wa mjadala wa urais wa mwezi uliopita.

  18. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Jumatano tarehe 10.07.2024