Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

"Hatuko hapa kuelekezwa nini cha kufanya kwenye nchi yetu" - Rais Samia

Kauli ya Rais Samia imekuja wiki moja tu tangu Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa wito wa uchunguzi huru kuhusu matukio ya utekaji na mauaji nchini Tanzania.

Muhtasari

  • Jeshi la Mali lasema 'magaidi" wamekabiliwa, washukiwa wamekamatwa
  • Mamia ya wanachama wa Hezbollah wameripotiwa kujeruhiwa baada ya vifaa vyao vya mawasiliano kulipuka
  • Sean 'Diddy' Combs ashtakiwa kwa usafirishaji haramu wa watu na kujipatia faida kupitia ulaghai
  • "Hatuko hapa kuelekezwa nini cha kufanya kwenye nchi yetu" - Rais Samia
  • Watu 10 wafariki baada ya jengo kuporomoka Sierra Leone
  • Watoto wanne walionaswa kwenye friji nchini Namibia wafariki
  • Vita vya Gaza: Israel yaanza kuwarejesha makwao wakazi wa kaskazini
  • Amazon yawaambia wafanyakazi warudi ofisini siku tano kwa wiki
  • Njaa nchini Sudan iliyokumbwa na vita ipo 'karibu kila mahali' - WHO
  • Milio ya risasi yasikika katika mji mkuu wa Mali
  • Tazama video fupi jinsi mshukiwa wa jaribio la mauaji la Trump alivyokamatwa
  • Vita vya Ukraine: Denmark kupeleka kundi jingine la ndege za kivita za F-16 Ukraine mwishoni mwa mwaka 2004
  • Vita vya Ukraine: Iran haikuuza silaha kwa Urusi, rais wa Iran asema
  • Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vyapigwa marufuku na mmiliki wa Facebook
  • Huduma ya ujasusi 'inajua' chapisho la Elon Musk kuhusu Harris, Biden
  • Polisi wa maadili wa Iran 'hawatasumbua' wanawake, rais asema
  • Sean 'Diddy' Combs akamatwa New York City
  • Mtu mwenye silaha alijificha kwa saa kadhaa kabla ya dakika za mwisho za mchezo wa gofu wa Trump

Moja kwa moja

Na Yusuf Jumah, Ambia Hirsi &Dinah Gahamanyi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Jeshi la Mali lasema 'magaidi' wamekabiliwa, washukiwa wamekamatwa

    Mkuu wa Jeshi la Mali Meja Jenerali Oumar Diarra anasema "magaidi" waliojaribu kuvamia chuo cha mafunzo ya kijeshi katika mji mkuu wa Mali, Bamako wamekabiliwa, bila kutoa taarifa kuhusu idadi kamili ya watu waliouawa.

    Alisema hayo wakati wa ziara ya kutathmini eneo la shambulio hilo, ambapo alifichua juhudi zinaendelea kuwapata washirika wa wavamizi hao.

    "Tumewakamata magaidi na tathmini inafanywa,” alisema.

    “Nawapongeza wananchi kwa kutoa taarifa. Msaada wao ulichangia pakubwa kukamatwa kwa washukiwa,” Jenerali Diarra aliongeza.

    Kanda ya video kwenye runinga ya serikali inaonyesha miili ya watu ikiwa imelala chini huku silaha na vifaa vya kinga vikionyeshwa karibu.

    Wanaume kadhaa waliotambulishwa kama washukiwa walionekana wakiwa wamekaa kando wakiwa wamefunga macho huku mikono yao ikiwa imefungwa. Baadhi yao walionekana kujeruhiwa.

    Pia kulikuwa na ripoti za milio ya risasi karibu na uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Bamako wakati wa mchana.

    Kundi la JNIM lenye mafungamano na al -Qaeda lilidai kuhusika na shambulio hilo lilisema lilifanya operesheni ambayo pia ililenga uwanja wa ndege wa kijeshi.

    Uwanja wa ndege mjini Bamako ulifungwa kwa muda kufuatia tukio hilo.

    Jeshi lilisema hali sasa imedhibitiwa, na kutilia mkazo juhudi zinazofanywa kuwasaka washukiwa kupitia taarifa za kijasusi walizokusanya kufikia sasa.

  3. Mamia ya wanachama wa Hezbollah wameripotiwa kujeruhiwa baada ya vifaa vyao vya mawasiliano kulipuka

    Mamia ya wanachama wa kundi lililojihami la Lebanon la Hezbollah wameripotiwa kujeruhiwa baada vifaa vyao vya mawasiliano wanavyotumia kulipuka.

    Shirika la habari la serikali ya Lebanon lilisema kulikuwa na milipuko katika viunga vya kusini mwa Beirut na maeneo mengine kadhaa. Televisheni ya al-Manar ya Hezbollah pia ilisema vifaa hivyo vya kubeba mkononi vililipuka , bila kubaini waliojeruhiwa.

    Video na picha kwenye mitandao ya kijamii zilionekana kuwaonyesha wanaume waliojeruhiwa wakiwa wamekaa au wamelala chini na wengine wakikimbizwa hospitalini. Picha za CCTV ambazo hazijathibitishwa zilionyesha milipuko kwenye maduka.

    Afisa wa Hezbollah aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa ni "ukiukaji mkubwa zaidi wa usalama" tangu uhasama na Israel ulipoongezeka miezi 11 iliyopita sambamba na vita vya Gaza.

    Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa jeshi la Israeli.

    Hata hivyo, matukio hayo yanakuja saa chache baada ya baraza la mawaziri la usalama la Israel kufanya kurejea salama kwa wakaazi kaskazini mwa nchi kuwa lengo rasmi la vita huko Gaza.

    Israel imeonya mara kwa mara kuwa inaweza kuanzisha operesheni ya kijeshi kuwafukuza Hezbollah kutoka mpakani.

    Soma pia:

  4. Sean 'Diddy' Combs ashtakiwa kwa utumwa wa kingono na kujipatia faida kupitia ulaghai

    Msanii wa hip-hop Sean "Diddy" Combs, amefikishwa kortini baada ya kukamatwa huko New York City Jumatatu usiku.

    Hebu tukuletee baadhi ya maelezo ya hati ya mashtaka sasa, ambapo Sean "Diddy" Combs anatuhumiwa kwa ulaghai, utumwa wa kingono na usafirishaji ili kujihusisha na ukahaba.

    Waendesha mashtaka wanasema kuwa ili kuwadhulumu waathiriwa wake, alitegemea "wafanyakazi, rasilimali, na ushawishi" wa himaya yake ya biashara na kuunda "biashara ya uhalifu ambayo wanachama na washirika wake walihusika, na kujaribu kushiriki, kati ya uhalifu mwingine, biashara ya ngono,utumwa, utekaji nyara, uchomaji moto, hongo, na kuwazuilia watu kwa lazima",mashtaka yanasema

    Hapa kuna mashtaka matatu ambayo yamefanywa dhidi ya Sean Combs:

    1. Njama za ulaghai

    2. Ulanguzi wa ngono kutumia nguvu,Utumwa wa kingono na ulaghai

    3. Usafirishaji wa watu kufanya ukahaba

  5. "Hatuko hapa kuelekezwa nini cha kufanya kwenye nchi yetu" - Rais Samia

    Na Rashid Abdallah

    BBC Swahili, Dar Es salaam

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema matukio ya mauaji yanatokea katika kila nchi na Tanzania haijawahi kuagiza Balozi wake aseme jambo kwa nchi nyingine.

    "Utasikia mtoto kabeba bunduki kaenda kushambulia shule, kadhaa wamekufa, kufa kupo tu. Kwa njia yoyote matukio haya yanatokea katika kila nchi."

    Ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya kufunga Mkutano wa Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo, yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

    Rais Samia amesema matukio haya yanapotokea katika nchi nyingine, “sisi hatujawahi kuziambia nchi kupitia balozi wetu, ‘hebu waambie hao.’ Sasa wengine wasiwe mafundi wa kutuelekeza nini cha kufanya."

    Kauli ya Rais Samia imekuja wiki moja tu tangu Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa wito wa uchunguzi huru kuhusu matukio ya utekaji na mauaji nchini Tanzania.

    Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali yake haikubaliani na yanayotokea, na kifo chochote kile kinaumiza na wale wanaotaka kuonesha huruma zao wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa.

    Unaweza pia kusoma

  6. Watu 10 wafariki baada ya jengo kuporomoka Sierra Leone

    Maafisa wa uokoaji nchini Sierra Leone wanaendelea na shughuli ya kuwatafuta manusura zaidi baada ya jengo la ghorofa saba kuporomoka katika mji mkuu Freetown na kusababisha vifo vya takriban watu 10.

    Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la nchi hiyo ya Afrika Magharibi (NDMA) lilisema watu saba wameokolewa kufikia sasa, lakini "watu zaidi wamenaswa".

    Iliongeza kuwa baadhi ya wale waliokuwa kwenye vifusi "wameweza kuwasiliana na jamaa zao" kwa mujibu wa waokoaji.

    Jengo hilo lililo mashariki mwa Freetown liliporomoka kati ya saa tano na saa sita majira ya ndani (12:00 na 13:00 BST) siku ya Jumatatu, NDMA ilisema.

    Mkazi wa eneo hilo Mohamed Camara aliangua kilio alipoambia shirika la habari la AFP kwamba mke wake na watoto watatu walikuwa wamenasa kwenye vifusi

    Jengo hilo lilitumika kwa madhumuni ya makazi na biashara, kulingana na tathmini za awali zilizofanywa na NDMA.

    Mkuu wa shirika hilo Brima Sesay alisisitiza umuhimu wa "kuhamasisha umma kuhusu hatari zinazohusiana na kuwatumia wakandarasi wasio na ujenzi".

    Sierra Leone ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, na mara nyingi majengo hujengwa kwa vifaa vya hali duni.

  7. Watoto wanne walionaswa kwenye friji nchini Namibia wafariki

    Polisi nchini Namibia wanachunguza kifo cha watoto wanne waliokuwa wakicheza kwenye jokofu tupu katika Mkoa wa Zambezi kaskazini-mashariki.

    Watoto hao wenye umri wa kati ya miaka mitatu na sita, walipatikana ndani ya friji isiyotumika katika eneo lenye watu wengi katika mji wa Katima Mulilo siku ya Jumatatu alasiri.

    Polisi wanaamini kuwa watoto hao walinaswa kwa bahati mbaya walipokuwa wakicheza na kuzidiwa ndani lakini uchunguzi unaendelea.

    Kati ya watoto hao wanne, wawili walikosa hewa hadi kufa kwenye friji huku wengine wawili wakifia hospitalini wakipokea matibabu, shirika la utangazaji la umma liliripoti.

    "Nilipoingia, niliwaona wahudumu wa afya wakihudumia binti yangu na msichana mwingine. Waliwakimbiza hospitalini, huku wengine wawili wakiwa wamepakiwa kwenye magari ya polisi ya kuhifadhia maiti,” Aranges Shoro, baba wa watoto hao, aliambia gazeti la kibinafsi la The Namibian.

    Wawili hao ambao walikimbizwa katika hospitali ya karibu ya Jimbo la Katima Mulilo walitangazwa kufariki walipofika, tovuti ya habari ya shirika la utangazaji la umma NBC iliripoti .

    Haijabainika kwa nini friji hiyo isiyofanya kazi iliachwa nje ya nyumba ya mojawapo ya familia zilizoathirika.

  8. Vita vya Gaza: Israel yaanza kuwarejesha makwao wakazi wa kaskazini

    Israel imewahamisha baadhi ya raia wake kaskazini mwa nchi kuwa lengo rasmi la vita, ofisi ya waziri mkuu imesema.

    Uamuzi huo ulifikiwa na baraza la mawaziri la usalama la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu siku ya Jumatatu.

    Takriban watu 60,000 wamehamishwa kutoka kaskazini mwa Israel kutokana na mashambulizi ya karibu kila siku ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran katika nchi jirani ya Lebanon.

    Mapigano ya mpakani yaliongezeka tarehe 8 Oktoba 2023 - siku moja baada ya shambulio baya dhidi ya Israel na wapiganaji wa Hamas kutoka Ukanda wa Gaza - wakati Hezbollah iliposhambulia Israel, kamhatua ya kuunga mkono Wapalestina.

    "Baraza la Mawaziri la Usalama limeimarisha malengo ya vita hivyo kujumuisha yafuatayo: Kuwarejesha wakazi wa kaskazini kwa usalama nyumbani kwao," taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu ilisema.

    "Israel itaendelea kuchukua hatua kutekeleza lengo hili," iliongeza.

    Mapema Jumatatu, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema njia pekee ya kuwarejesha wakazi wa kaskazini mwa Israel kwenye makazi yao ni kupitia "hatua za kijeshi", wakati wa mkutano na mjumbe wa Marekani Amos Hochstein.

  9. Amazon yawaambia wafanyakazi warudi ofisini siku tano kwa wiki

    Amazon iimewaarifu wafanyakazi wake kurudi ofisini siku tano kwa wiki inapomaliza sera yake ya kazi ya mseto.

    Mabadiliko hayo yataanza kutumika kuanzia Januari, afisa mkuu mtendaji Andy Jassy alisema katika memo kwa wafanyakazi .

    "Tumeamua kuwa tutarejea kuwa ofisini kama tulivyokuwa kabla ya Covid-19 kuanza," alisema, na kuongeza kuwa itasaidia wafanyakazi "kutayarishwa vyema ili kubuni, kushirikiana na kuunganishwa vya kutosha kwa kila mmoja".

    Bwana Jassy kwa muda mrefu amejulikana kama mtu anayeshuku kazi ya mbali, lakini wafanyakazi wa Amazon hapo awali waliruhusiwa kufanya kazi nyumbani siku mbili kwa wiki.

    Msukumo wa Amazon wa kuwarejesha ofisini wafanyakazi wa shirika umekuwa chanzo cha mvutano ndani ya kampuni hiyo ambayo inaajiri zaidi ya watu milioni 1.5 duniani kote katika majukumu ya muda .

    Wafanyakazi katika makao makuu yake ya Seattle walifanya maandamano mwaka jana huku kampuni hiyo ikiimarisha posho kamili ya kazi ya mbali ambayo iliwekwa wakati wa janga hilo.

  10. Njaa nchini Sudan iliyokumbwa na vita ipo 'karibu kila mahali' - WHO

    Njaa katika Sudan iliyokumbwa na vita "ipo kila mahali", Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeambia kipindi cha BBC Today baada ya kuzuru nchi hiyo.

    "Hali nchini Sudan inatisha sana... idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao - sasa ni kubwa zaidi duniani, na, bila shaka,kuna njaa," mkurugenzi mkuu Tedros Adhanom Ghebreyesus alimwambia Mishal Husain.

    Alisema watu milioni 12 tayari wamekimbia makazi yao, akiongeza kuwa umakini katika jumuiya ya kimataifa kwa Sudan ulikuwa "wa chini sana" na ubaguzi wa rangi ni sababu.

    Maelfu ya watu wameuawa tangu kuzuke vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha (RSF).

    "Fikiria: uharibifu, watu kuhama, magonjwa kila mahali, na sasa njaa," Dk Tedros aliambia BBC.

    Alisema hivi majuzi alitembelea kambi ya wakimbizi wa ndani na hospitali moja nchini Sudan.

    "Unaona kuna watoto wengi na unaona tu ngozi na mifupa, wamedhoofika."

    Takriban watu milioni 25 - nusu ya wakazi wa Sudan - "wanahitaji msaada", Dk Tedros alisema.

    Alisisitiza kuwa Sudan "haipati uangalizi unaostahili", na ndivyo ilivyokuwa kwa migogoro mingine ya hivi majuzi barani Afrika.

    "Nadhani mashindano yanachezwa hapa. Hivyo ndivyo ninavyohisi sasa. Tunaona muundo wa aina hiyo sasa."

    Dk Tedros - ambaye alikulia wakati wa vita nchini Ethiopia - alisema: "Hasa katika Afrika, nadhani umakini ni mdogo sana."

    "Hiyo ni sehemu ya kusikitisha, kwa sababu unaona mara kwa mara, sio tu nchini Sudan," aliongeza.

  11. Milio ya risasi yasikika katika mji mkuu wa Mali

    Milio ya risasi imesikika katika mji mkuu wa Mali, Bamako, na kusababisha ripoti kwamba kambi moja ya usalama imeshambuliwa.

    Video kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi ukipaa kutoka sehemu ya jiji, huku baadhi wakipendekeza kuwa moshi huo huenda unatoka katika kituo cha polisi au cha kijeshi.

    Vyanzo vya usalama viliambia vyombo vya habari vya Ufaransa RFI na AFP kwamba watu wenye silaha walishambulia kambi moja au zaidi katika mji mkuu.

    Mali ni mojawapo ya nchi kadhaa za Afrika Magharibi ambazo zimekuwa zikipambana na waasi wa Kiislamu kwa zaidi ya muongo mmoja. Lakini haijulikani ni nani aliyehusika na ufyatuliaji huo wa risasi .

    Jeshi lilichukua mamlaka katika mapinduzi mwaka wa 2021, na kuishutumu serikali kwa kushindwa kufanya vya kutosha kuzima uasi huo.

    Hata hivyo, miaka mitatu baadaye, hakuna dalili ya mashambulizi kumalizika.

    Walioshuhudia waliambia shirika la habari la Reuters kwamba milio ya risasi ilianza mwendo wa saa 05:30 saa za huko (05:30 GMT).

    Watu waliokuwa wakielekea msikitini kwa ajili ya sala ya asubuhi walirejea majumbani huku milio ya risasi ikivuma, Reuters ilisema.

  12. Tazama video fupi jinsi mshukiwa wa jaribio la mauaji la Trump alivyokamatwa

    Mtu mwenye bunduki alijificha kwa takriban saa 12 vichakani kabla ya Donald Trump kucheza mchezo ambao haukuwa umepangwa wa gofu katika klabu yake iliyopo kando ya bahari huko Florida - akiwaacha wenyeji wakiwa na mshangao kwa kile maafisa wanasema linaonekana kuwa jaribio la pili la kumuua rais huyo wa zamani katika muda wa miezi mingi.

  13. Vita vya Ukraine: Denmark kupeleka kundi jingine la ndege za kivita za F-16 Ukraine mwishoni mwa mwaka huu

    Ukraine itapokea kundi jingine la ndege za kivita aina ya F-16 kutoka Denmark mwishoni mwa mwaka 2024, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Troels Lund Poulsen amesema.

    "Denmark itatoa kundi la ziada la ndege katika nusu ya pili ya 2024," mkuu wa idara ya ulinzi amesema, bila kutaja ni ndege hizo ngapi zitapelekwa Kiev au ni wakati gani hasa zitakapopelekwa

    Ndege za kwanza aina ya F-16 kutoka Denmark ziliwasili nchini Ukraine mapema mwezi Agosti.

    Mwishoni mwa Agosti, moja ya ndege za kivita aina ya F-16 zilizonunuliwa na mataifa ya Magharibi ilianguka nchini Ukraine.

    Tukio hilo lilitokea wiki tatu tu baada ya ndege za kwanza za Marekani kuwasili nchini Ukraine.

    Rubani, maarufu wa Ukraine, Alexey Mes, ambaye alikuwa ni mmoja wa marubani wa kwanza kufanyiwa mafunzo ya kutumia F-16, alifariki katika tukio hilo.

    Awali F-16 iliundwa ili kupiga jeki F-15 katika miinuko ya chini, lakini hivi karibuni iligundulika kuwa - kama vile Vita vya Pili vya Dunia Supermarine Spitfire - fremu ya anga ya F-16 iliiruhusu kubeba mizigo mizito zaidi, mafuta zaidi na rada kubwa zaidi. "F-16 ni karibu kisu bora kabisa cha Jeshi la Uswizi," Bolton anasema.

    F-16, katika Karne ya 21, imekuwa muhimu vile vile kama ndege ya mashambulizi ya ardhini - si kitu ambacho wabunifu wake walikuwa nacho kwenye mawazo mapema miaka ya 1970. Kubadilika huko kuliiruhusu kutekeleza majukumu zaidi na zaidi, ambayo ilifanya izidi kuvutia kwa vikosi vya anga. "Pale ambapo kuna mzozo, pengine kuna F-16 inayohusika mahali fulani," anasema Robinson.

    Kufahamu umuhimu wa ndege ya kivita ya F-16 katika vita vya Ukraine soma: Kwa nini ndege hii ya kivita bado inahitajika sana nchini Ukraine?

    Unaweza pia kusoma:

  14. Vita vya Ukraine: Iran haikuuza silaha kwa Urusi, rais wa Iran asema

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema serikali yake haijapeleka silaha zake zozote nchini Urusi tangu ilipoingia madarakani mwezi Agosti.

    "Hatukutoa silaha kwa Urusi," Pezeshkian alisema katika mkutano na waandishi wa habari, shirika la habari la Mehr liliripoti.

    Aliongeza kuwa Iran na Urusi zina haki ya kudumisha uhusiano na kusema vita nchini Ukraine vilichochewa na nchi za NATO kuvunja ahadi yao ya kutopanua upande wa mashariki.

    Mapema mwezi Septemba, vyombo vya habari vya Magharibi viliripoti kuwa Urusi imepokea makombora ya masafa mafupi kutoka Iran kwa ajili ya matumizi katika vita dhidi ya Ukraine.

    Nchi za Magharibi baadaye zilithibitisha hilo rasmi.

    Vita vya Ukraine: mengi zaidi:

  15. Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vyapigwa marufuku na mmiliki wa Facebook

    Mmiliki wa Facebook Meta anasema kuwa kampuni hiyo inapiga marufuku mitandao kadhaa ya vyombo vya habari vya serikali ya Urusi, kwa madai kuwa vinatumia mbinu za udanganyifu kutekeleza shughuli za ushawishi na kukwepa kugunduliwa kwenye majukwaa yake.

    "Baada ya kutafakari kwa kina, tulipanua utekelezaji wetu unaoendelea dhidi ya vyombo vya habari vya serikali ya Urusi, Rossiya Segodnya, RT na mashirika mengine yanayohusiana nayo sasa yamepigwa marufuku kwenye programu zetu duniani kote kwa kuingiliwa masuala ya nchi za kigeni," Meta alisema.

    Marufuku hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa siku chache zijazo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimekuwa vikichunguzwa zaidi juu ya madai kwamba wamejaribu kushawishi siasa katika nchi za Magharibi.

    Pamoja na Facebook, ambayo ni kampuni kubwa ya mitandao ya kijamii ya Meta inamiliki Instagram, WhatsApp na Threads.

    Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa msimamo wa kampuni kubwa zaidi ya mitandao ya kijamii kuhusu kampuni za vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

    Vita vya Ukraine: mengi zaidi:

  16. Huduma ya ujasusi 'inajua' chapisho la Elon Musk kuhusu Harris na Biden

    Elon Musk aliandika kwamba "hakuna anayejaribu" kumuua Joe Biden au Kamala Harris katika tweet iliyofutwa tangu wakati huo.

    Huduma ya Siri ya Marekani inasema "inajua" chapisho la mtandao wa kijamii la Elon Musk ambapo alisema kwamba "hakuna mtu anayejaribu" kumuua Rais Joe Biden au Makamu wa rais Kamala Harris.

    Bw Musk amefuta chapisho hilo na kusema lilikusudiwa kuwa mzaha.

    Chapisho lake kwenye X, zamani ikitwa Twitter, lilikuja saa chache baada ya mshukiwa wa jaribio la kumuua Donald Trump katika uwanja wake wa gofu huko Florida siku ya Jumapili.

    Bilionea huyo wa teknolojia ni mshirika wa karibu wa Trump, ambaye ameapa kumsajili Bw Musk kusimamia "tume ya ufanisi wa serikali" ikiwa atashinda muhula wa pili kama rais wa Marekani.

    Watumiaji wengi wa X walikosoa maoni ya Bw Musk - ambayo yaliambatana na emoji iliyoibua maswali - huku wengine wakidai kuwa ujumbe huo ulikuwa aina ya fulani ya uchochezi dhidi ya Rais wa Marekani na Makamu wa Rais.

    Katika taarifa, Ikulu ya White House ililaani ujumbe huo, ikisema kuwa "maneno haya ni ya kutowajibika".

    Unaweza pia kusoma:

  17. Polisi wa maadili wa Iran 'hawatasumbua' wanawake, rais asema

    Rais mpya wa Iran amesema kuwa polisi wa maadili hawatawasumbua tena wanawake kuhusu uvaaji wa hijabu ya lazima, siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa wanawake bado wanaadhibiwa vikali kwa kuvunja kanuni kali ya mavazi.

    Kauli hiyo ya Rais Masoud Pezeshkian ilitolewa katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 akiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukamatwa kwa madai ya kutovaa hijabu ipasavyo na hivyo kuzua maandamano nchi nzima.

    Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulisema serikali ya Iran "imeongeza juhudi" tangu kipindi hicho kukandamiza haki za wanawake na masuala yoyote ya uanaharakati.

    Lakini siku ya Jumatatu, Pezeshkian alisema kwamba polisi wa maadili ya serikali hawapaswi tena kuwakabili wanawake mitaani.

    Pezeshkian, ambaye alikua rais baada ya mtangulizi wake kufariki katika ajali ya helikopta, anaonekana kama kiongozi anayeweza kuleta mageuzi.

    Alikuwa akijibu maswali ya mwanahabari wa kike ambaye alisema alichukua muda mrefu kufika kwenye mkutano na waandishi wa habari ili kukwepa gari za polisi. Alikuwa amevaa kilemba kichwani mwake huku nywele zikionekana.

    Ulikuwa mkutano wa kwanza wa Pezeshkian na wanahabari tangu aingie ofisini mwezi Julai, akichukua nafasi ya Ebrahim Raisi ambaye alikuwa na muelekeo wa kihafidhina.

    Alipoulizwa na Pezeshkian iwapo polisi bado walikuwa mitaani alithibitisha kuwa ndivyo ilivyokuwa.

    Katika kujibu Rais alisema : "Polisi wa maadili hawapaswi kukabiliana na wanawake. Nitafuatilia ili wasiwasumbue ".

  18. Puff Daddy kwa jina maarufu Sean 'Diddy' Combs akamatwa New York City

    Mwanamuziki maarufu wa hip-hop Puff Daddy amekamatwa katika jiji la New York kwa mashtaka ambayo hayajabainishwa, mamlaka ya shirikisho ililiambia shirika la utangazji mshirika wa BBC wa Marekani CBS.

    Kukamatwa kwa Diddy Manhattan kunafuatia uvamizi wa mali zake mbili huko Los Angeles na Miami mnamo Machi kama sehemu ya "uchunguzi unaoendelea" wa mamlaka kuhusiana na biashara ya ngono.

    Wakili wa Bw Combs, Marc Agnifilo, alisema "wamekatishwa tamaa" na kukamatwa kwa mteja wake ambaye alimtaja kuwa "mtu asiye na hatia".

    Mwanamuziki huyo amekabiliwa na msururu wa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na tuhuma za kumnyanyasa mpenzi wake wa zamani Casandra "Cassie" Ventura. Sheon amekana madai yote dhidi yake.

    Alikamatwa kuhusiana na uchunguzi unaoendelea na maafisa wa usalama wa ndani wa Marekani, vyanzo vingi vya sheria viliiambia CBS.

    Mwanasheria wa Marekani katika Wilaya ya Kusini ya New York Damian Williams alithibitisha kukamatwa kwake katika taarifa yake Jumatatu usiku.

  19. Mtu mwenye silaha alijificha kwa saa kadhaa kabla ya dakika za mwisho za mchezo wa Trump wa gofu

    Mtu mwenye bunduki alijificha kwa takriban saa 12 vichakani kabla ya Donald Trump kucheza mchezo ambao haukuwa umepangwa wa gofu katika klabu yake iliyopo kando ya bahari huko Florida - akiwaacha wenyeji wakiwa na mshangao kwa kile maafisa wanasema linaonekana kuwa jaribio la pili la kumuua rais huyo wa zamani katika muda wa miezi mingi.

    Kulikuwa na joto na mawingu Jumapili alasiri wakati Trump na rafiki yake wa karibu, mmiliki wa makazi Steve Witkoff, walipowasili kwenye uwanja wa kimataifa wa Gofu wa Trump huko West Palm Beach.

    Rais huyo wa zamani alikuwa katika awamu ya tano ya mchezo huo saa saba na dakika 7:31(17:31 GMT), eneo lililo karibu na barabara zenye shughuli nyingi lililopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Palm Beach, wakati mmoja wa walinzi wake alipoona bunduki ikijitokeza kwenye majani karibu na shimo la sita la uwanja wa gofu.

    Trump - ambaye alihamishwa bila kujeruhiwa - alisimulia Jumatatu usiku kwamba alisikia risasi "labda nne au tano" zikilia karibu.

    Afisa wa ujasusi alikuwa amefyatua risasi kuelekea kwa mshukiwa, ambaye alikuwa umbali wa yadi 300-500 na hakuwa na njia ya wazi ya kumtazama Trump, wachunguzi wa shirikisho walisema.

    "Huduma za ujasusi zilijua mara moja kuwa ni risasi, na walinikamata," Trump alisema wakati wa hafla iliyorushwa moja kwa moja kwenye X, zamani ikiitwa Twitter, akizungumza kutoka kwenye makao yake ya kifahari ya Mar-a-Lago.

    Alikuwa amejificha pale kwenye upande wa uzio wa umma tangu 07:59 saa za huko Jumapili asubuhi, kulingana na rekodi za simu za rununu, zilizotajwa na maafisa wa shirikisho.

    Soma zaidi:

  20. Uhali gani?...Tunakualika kwa matangazo haya ya moja kwa moja ya leo Jumanne kwa habari za kikanda na kimataifa tukisema shukran kwa kujiunga nasi.