Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hezbollah ni nini huko Lebanon na itaingia vitani na Israeli?
Takriban watu tisa waliuawa na karibu 3,000 walijeruhiwa nchini Lebanon siku ya Jumanne wakati vifaa vya mawasiliano- 'Pager' za mkono zinazotumiwa na wanachama wa kundi lenye silaha la Hezbollah kulipuka, waziri wa afya wa nchi hiyo amesema.
Hezbollah iliilaumu Israel kwa shambulio hilo lililopangwa, lakini jeshi la Israel lilikataa kutoa maoni yake.
Mapigano ya mpakani kati ya Israel na Hezbollah yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, yakichochewa na vita huko Gaza.
Milipuko hiyo imekuja saa chache baada ya baraza la mawaziri la usalama la Israel kusema lengo jipya la vita vya Gaza ni kurejea salama kwa makumi ya maelfu ya wakaazi waliokimbia makazi yao kaskazini mwa nchi hiyo.
Hezbollah ni nini?
Hezbollah ni shirika la Waislamu wa madhehebu ya Shia ambalo lina ushawishi mkubwa kisiasa na linadhibiti jeshi lenye nguvu zaidi nchini Lebanon.
Ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na mamlaka kuu ya Shia katika eneo hilo, Iran, ili kuipinga Israel. Wakati huo, wanajeshi wa Israel walikuwa wameikalia kwa mabavu sehemu ya kusini mwa Lebanon, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Hezbollah imeshiriki katika chaguzi za kitaifa tangu 1992 na imekuwa sehemu kuu ya kisiasa.
Mrengo wake wenye silaha umefanya mashambulizi mabaya dhidi ya wanajeshi wa Israel na Marekani nchini Lebanon. Wakati Israeli ilipojiondoa kutoka Lebanon mwaka 2000, Hezbollah ilichukua sifa kwa kuwasukuma nje.
Tangu wakati huo, Hezbollah imedumisha maelfu ya wapiganaji na safu kubwa ya makombora kusini mwa Lebanon. Inaendelea kupinga uwepo wa Israel katika maeneo ya mpakani yenye mzozo.
Imetangazwa kuwa shirika la kigaidi na mataifa ya Magharibi, Israel, nchi za Ghuba ya Kiarabu na Jumuiya ya Kiarabu.
Mnamo mwaka wa 2006, vita vikali vilizuka kati ya Hezbollah na Israel, vilianza wakati Hezbollah ilipofanya shambulio baya la kuvuka mpaka.
Wanajeshi wa Israel walivamia kusini mwa Lebanon kujaribu kuondoa tishio la Hezbollah. Hata hivyo, ilinusurika na tangu wakati huo imeongeza idadi ya wapiganaji na kupata silaha mpya na bora zaidi.
Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah ni nani?
Sheikh Hassan Nasrallah ni mhubiri wa Shia ambaye ameongoza Hizbullah tangu 1992.
Alichukua jukumu muhimu katika kuigeuza kuwa nguvu ya kisiasa, na vile vile ya kijeshi.
Ana uhusiano wa karibu na Iran na Kiongozi wake Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei.
Kuanzia wakati huo 1981, wakati Kiongozi Mkuu wa kwanza wa Iran, Ayatollah Ruhollah Khomeini, alipomteua kuwa mwakilishi wake wa kibinafsi nchini Lebanon.
Nasrallah hajaonekana hadharani kwa miaka mingi, ikidaiwa kwa kuhofia kuuawa na Israel.
Hata hivyo, anasalia kuheshimiwa na Hezbollah, na hutoa hotuba kwenye televisheni kila wiki.
Je, majeshi ya Hezbollah yana nguvu kiasi gani?
Hezbollah ni mojawapo ya vikosi vya kijeshi vilivyo na silaha nyingi, zisizo za serikali duniani. Inafadhiliwa na ina vifaa vya Iran.
Sheikh Hassan Nasrallah amedai kuwa ina wapiganaji 100,000, ingawa makadirio huru yanatofautiana kati ya 20,000 na 50,000.
Wengi wamefunzwa vizuri na vita vikali, na vita katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria .
Ina wastani wa roketi na makombora 120,000-200,000, kulingana na Kituo cha Utafiti wa Kimkakati na Kimataifa .
Silaha zake nyingi zimeundwa na roketi ndogo zakurushwa kutoka eneo la ardhini hadi sehemu nyingine ya ardhi .
Lakini pia ilifikiriwa kuwa na makombora ya kukinga ndege na meli, pamoja na makombora ya kuongozwa yenye uwezo wa kushambulia ndani kabisa ya Israel.
Silaha hizo ni za kisasa zaidi kuliko zinazomilikuwa na Hamas, katika Ukanda wa Gaza.
Je, Hezbollah inaweza kwenda vitani na Israel?
Hapo awali mapigano ya hapa na pale yaliongezeka tarehe 8 Oktoba - siku moja baada ya shambulio lisilokuwa la kawaida la Hamas dhidi ya Israeli - wakati Hezbollah ilipofyatua silaha kuelekea sehemu za Israeli, kwa mshikamano na Wapalestina.
Tangu wakati huo, imerusha makombora kaskazini mwa Israeli na maeneo ya Israeli kwenye Milima ya Golan, kurusha makombora ya vifaru kwenye magari ya kivita, na kushambulia malengo ya kijeshi kwa droni za vilipuzi.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vimelipiza kisasi, kwa kutumia mashambulizi ya anga, na mizinga n dhidi ya maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon.
Umoja wa Mataifa unasema mashambulizi hayo yamewalazimu zaidi ya watu 90,000 nchini Lebanon kutoka makwao, huku takriban raia 100 na wapiganaji 366 wa Hezbollah wakiuawa katika mashambulizi ya Israel.
Nchini Israel, maafisa wanasema raia 60,000 wamelazimika kuyaacha makazi yao na watu 33 wameuawa, wakiwemo raia 10, kwa sababu ya mashambulizi ya Hezbollah.
Licha ya mapigano hayo, waangalizi wa mambo wanasema kuwa hadi sasa pande zote mbili zimelenga kuzuia uhasama bila kuvuka mipaka na kuingia katika vita kamili. Lakini hofu ni kwamba tukio baya sana linaweza kusababisha hali hiyo kutoweza kudhibitiwa.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah