Shirika la kimatatifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch
limeitaka serikali ya Tanzania kulinda haki za binadamu kuelekea uchaguzi wa
serikali za mitaa.
Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mtaa tarehe 27
Novemba huku wapiga kura wakitarajiwa kuchagua Mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi
mchanganyiko la wanaume na wanawake), wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi
la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.
Nafasi zingine zinazotarajiwa
kugombaniwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo,
Mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume
na Wanawake) na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za
Miji.
Hata hivyo, Human Rights
Watch wanasema ndani ya miezi michache iliyopita kumekuwepo na matukio mengi ya
uvunjifu wa haki za binaadamu nchini Tanzania hali inayotia hofu kuelekea
uchaguzi huo.
“Tangu mwezi Juni, mamlaka
zimewakamata kiholela mamia ya wafuasi wa upinzani, zimedhibiti upatikanaji wa
mitandao ya kijamii, zimefungia vyombo huru vya habari, na zimehusishwa na
kutekwa na mauaji ya wapinzani wa serikali wasiopungua wanane” imesema sehemu
ya ripoti ya Human Rights Watch.
Hatahivyo akizungumza, waziri wa
sheria na katiba nchini humo Palamagamba Kabudi amesema madai hayo yamejazwa chumvi na kwamba hayaendani na hali halisi
nchini Tanzania.
Bwana Kabudi ameitetea serikali ya Tanzania akisema kwamba imekuwa kifua
mbele kulinda haki za kibinadamu na
kwamba uchaguzi wa mitaa utakaofanyika mwezi ujao utakuwa huru na wa haki.
Katika ripoti hiyo, Human
Rights Watch imetaja tukio la kutekwa kwa Edgar Mwakabela, anayejulikana kwa
jina la Sativa. Imezungumzia pia tukio la Kombo Mbwana, mwanachama wa chama cha
upinzani cha Chadema aliyepotea kwa takribani siku 30 na baadae polisi mkoani
Tanga kujitokeza na kuthibitisha kumshikilia.
Human Rights Watch wametaja pia kupotea kwa Dioniz Kipanya, mwanachama wa Chadema wilayani Sumbawanga, mkoa wa Rukwa pamoja na tukio la kupotezwa kwa Deusdedith Soka anayedaiwa kutekwa mnamo tarehe 18 Agosti pamoja na msaidizi wake Jacob Godwin Mlay na dereva bodaboda Frank Mbise.
Kupotea kwa Shadrack Chaula, ambaye hajaonekana tangu tarehe 2 Agosti, mwezi mmoja baada ya kushitakiwa kwa kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan, kumetajwa pia katika ripoti hiyo. Tukio la kuuwawa kwa Ali Mohamed Kibao tarehe 7 Septemba limetajwa pia katika ripoti hiyo.
Matukio mengine yalliyoorodheshwa katika ripoti hiyo ni yale ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA kufungia kampuni ya habari ya Mwananchi kuchapisha maudhui katika mitandao baada ya kuchapisha kibonzo kilichomuonyesha muhusika aliyefanana na Rais Samia akitazama habari mbalimbali zilizohusu matukio ya utekaji.
Akijibu kuhusu kukamatwa kiholela kwa wafuasi wa upinzani na mauaji
ya wakosoaji wa serikali, Kabudi amesema, taarifa hizo hazina msingi na kwamba
zinalenga kuchafua jina zuri la Tanzania kimataifa.
BBC inaendelea na jitihada za kupata maoni ya serikali kutoka kwa msemaji wa serikali