Makamu wa Rais Zanzibar Othman Masoud, Lissu wazuiwa kuingia Angola
Viongozi zaidi 40 kutoka nchi mbalimbali afrika akiwemo Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, na mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha ACT nchini Tanzania, Othman Masoud Othman wamezuiwa kuingia nchini Angola na mamlaka za Sereikali nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na chama cha ACT inasema, makamu huyo alizuiwa katika uwanja wa ndege pamoja na kiongozi mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu.
‘Viongozi hao wanashikiliwa kwenye uwanja wa ndege wa Luanda na hati zao za kusafiria zinashikiliwa'. Ilisema sehemu ya taarifa ya chama hicho kilichotaka pia Ofisi ya Ubalozi wa Angola nchini Tanzania, kutoa maelezo ya kilichotokea.
Viongozi wengine waliozuiwa ni Pamoja na rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama, Waziri mkuu wa zamani wa Lesotho, mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzani Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, Kiongozi wa upinzani Uganda, Robert Kyagulanyi (Bbobi Wine), na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna.
Sifuna alithibitisha kupiti mtandao wake wa X, ‘ Tulialikwa na Rais wa UNITA, Adalberto Costa nchini Angola. Serikali imetuzuia kuingia’.
Kwa upande wake Lissu aliandika ‘ kilichofanywa na mamlaka za uhamiaji za Angola hakikubaliki na kinapaswa kulaaniwa’.
Viongozi hao walikuwa sehemu ya viongozi zaidi ya 40 walizuiliwa ambao waliwasili Angola kushiriki katika mazungumzo ya siku nne ya jukwaa la Demokrasia Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation, ambayo yalikuwa yaanze leo Machi 13 mpaka 16.
Mamlaka za Angola, hazijajitokeza kueleza kwa upande wao, licha ya jitihada za upande wa pili kutaka maelezo yao.