Mahakama ya ICJ kusikiliza kesi ya Sudan dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu

Mahakama Kuu ya Kimataifa ilisema siku ya Ijumaa itasikiliza kesi iliyoletwa na Sudan kutaka hatua za dharura zichukuliwe dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Mahakama ya ICJ kusikiliza kesi ya Sudan dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu

    Wapiganaji wa RSF

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama Kuu ya Kimataifa ilisema siku ya Ijumaa itasikiliza kesi iliyoletwa na Sudan kutaka hatua za dharura zichukuliwe dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na kuishutumu nchi hiyo ya Ghuba kwa kukiuka majukumu chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kwa kuvipa silaha vikosi vya kijeshi.

    Sudan imeishutumu UAE kwa kuwapa silaha wanajeshi wa Kikosi cha wanamgambo wa RSF ambacho kimekuwa kikipigana na jeshi la Sudan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda wa miaka miwili, madai ambayo UAE inakanusha.

    ''Hatua ya Jeshi la Sudan katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ni ''mchezo wa kisiasa, na jitihada la kumburuza katika mzozo rafiki wa Afrika kwenye mzozo ambao wenyewe wameuanzisha na kuuchochea," afisa wa UAE alisema.

    "Pamoja na hayo, UAE inasalia imara katika ahadi yake ya kibinadamu kwa watu wa Sudan, inayolenga kupunguza maafa ya kibinadamu yaliyosababishwa na pande zote mbili zinazopigana."

    Malalamiko ya Sudan kwa ICJ yenye makao yake The Hague, yanahusiana na mashambulizi makali ya kikabila yaliyofanywa na RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu dhidi ya kabila lisilo la Kiarabu la Masalit mwaka 2023 huko Darfur Magharibi.

    Sudan imeomba mahakama ichukue hatua za dharura kuamuru Emirates kuzuia vitendo vya mauaji ya halaiki huko Darfur.

    Mahakama ilisema itasikiliza ombi la Sudan tarehe 10 Aprili.

    Unaweza kusoma;

  2. Watu wanne wauawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani za Urusi, Ukraine yasema

    Zima moto

    Chanzo cha picha, Dnipropetrovsk Regional State Administration

    Watu wanne wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye mji wa kati wa Ukraine wa Dnipro, mkuu wa eneo hilo amesema.

    Serhiy Lysak alisema jengo la mgahawa na majengo kadhaa ya makazi yameteketea baada ya shambulio hilo Ijumaa jioni.

    Aliongeza kuwa "adui alituma zaidi ya ndege 20 zisizo na rubani" katika jiji hilo, na kwamba "wengi wao walipigwa risasi".

    Picha na video ziliibuka baadaye zikiwaonesha maafisa wa zima moto wakikabiliana na moto mkubwa ambao ulikuwa umeteketeza majengo ambayo yalipigwa, na kuvunja vioo na uchafu mwingine uliotawanyika katika mitaa ya jiji.

    Mara moja, ving'ora vilisikika katika mikoa mingine kadhaa ya Ukraine, pamoja na mji mkuu, Kyiv.

    Haikuweza kufahamika mara moja iwapo kulikuwa na majeruhi.

    Oleksandr Vilkul, mkuu wa utawala wa kijeshi katika mji wa nyumbani wa Zelensky Kryvyi Rih, pia alithibitisha kwenye Telegram kwamba kulikuwa na shambulio la kombora la balestiki kwenye mji wa kati siku ya Jumamosi asubuhi, na kwamba hadi sasa watu watano wamejeruhiwa.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliishutumu tena Urusi kwa kulenga miundombinu ya nishati ya Ukraine, kinyume na usitishaji wa muda uliokubaliwa mapema mwezi huu katika mazungumzo yaliyohusisha Marekani.

    Unaweza kusoma;

  3. Tazama: Mtoto azaliwa katika mtaa wa Bangkok baada ya tetemeko

    Maelezo ya video, Mtoto baada ya kuzaliwa Bangkok

    Mwanamke mmoja alijifungua mtoto kwenye barabara moja huko Bangkok muda mfupi baada ya kuhamishwa hospitalini baada ya tetemeko la ardhi nchini Myanmar.

    Mgonjwa huyo alikuwa amelazwa kwenye machela huku wahudumu wa hospitali hiyo wakimzunguka na kujifungua mtoto.

    Wagonjwa kutoka Hospitali ya Kumbukumbu ya King Chulalongkorn na Hospitali ya BNH walikusanyika katika bustani, baadhi yao walikuwa kwenye machela na viti vya magurudumu.

    Wafanyakazi wa hospitali pia walionekana wakihudumia wagonjwa nje ya hospitali.

    Unaweza kusoma;

  4. Kampuni ya AI ya Musk yaununua mtandao wa X

    Musk

    Chanzo cha picha, EPA

    Elon Musk anasema kampuni aliyoianzisha ya matumizi ya akili mnemba, xAI imeununua mtandao wa kijamii X uliokuwa ukijulikana kama Twitter.

    Musk aliununua mtandao wa Twitter mnamo 2022 kwa thamani ya $ bilioni 44. "Mustakabali wa xAI na X umeunganika pamoja," Musk ameandika kwenye X. "Leo tunachukua rasmi hatua ya kuunganisha data, mfumo, usambazaji na talanta." Huenda hatua hiyo imelenga kuwalinda wawekezaji, waliomsaidia kuununua mtandao wa X, dhidi ya kupoteza fedha.

    X na xAI zinamilikiwa kibinafsi na zina wawekezaji wakuu wakuwiana.

    Kadhalika zinatumia baadhi ya rasilimali muhimu kwa pamoja. "Hatua hiyo inaonekana ya busara, ukizingatia mtindo wa sasa wa kuongezeka uwekezaji katika AI, taasisi za data na ukokotoaji," anasema Paolo Pescatore, muasisi wa PP Foresight.

    Musk amekuwa katika kesi na OpenAI, kampuni aliyoiasisi mnamo 2015 na afisa mkuu mtendaji Sam Altman.

    Musk aliishtaki OpenAI na Bwana Altman mwaka jana kwa kutofuata malengo msingi ya kampuni hiyo kwa kujaribu kuishinikiza kampuni hiyo kugeuka kuwa kampuni ya faida.

    Wakosoaji wanasema Musk anawashtaki waundaji wa ChatGPT kwasababu alitaka kuidhibiti kampuni hiyo.

    Mapema mwaka huu mkusanyiko wa makampuni ukiongozwa na Musk uliwasilisha ombi la kuinunua kampuni ya OpenAI kwa takribani $ bilioni 97.4 pendekezo ambalo Altman alilipinga akieleza kuwa kampuni hiyo haiuzwi.

    Mageuzi haya ya kiabiashara yanafanyika wakati Musk akiwa anashughulika zaidi katika siasa, akiwa anahudumu hivi sasa kama msaidizi wa karibu wa rais Donald Trump.

    Unaweza kusoma;

  5. Ebrahim Rasool: Balozi wa Afrika kusini aliyetimuliwa kutoka Marekani asema utawala wa Trump una ubaguzi

    v

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Aliyekuwa balozi wa Afrika kusini nchini Marekani ameiambia BBC kuwa ni “dhahiri” kuwa kuna ubaguzi ndani ya utawala wa Trump.

    Ebrahim Rasool mwenye umri wa miaka 62, aliamrishwa kuondoka Marekani wiki iliopita baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio kumuita "mwanasiasa anayetumia ubaguzi na anayeichukia Marekani".

    Haya yanajiri baada ya Rasool kumtuhumu rais Donald Trump kwa kujaribu "kudhihirisha maonevu ya wazungu kama njia ya kutafuta uungwaji mkono kisiasa".

    Alipoulizwa katika mahojiano na BBC Newshour iwapo anaamini kuwa utawala wa Trump una ubaguzi, Rasool alisema: "Ninadhani hilo ni dhahiri hata bila ya mtu kulaumiwa.”

    BBC imeiomba ikulu ya Marekani tamko kuhusu hili. Katika majohiano ya kwanza anayofanya tangu atimuliwe kutoka Marekani, Rasool ameongeza: "Ninasema kipande cha mbao kikiwa na bawaba, unaanza kushuku ni huo ni mlango."

    Mwanadiplomasia huyo ametaja msisitizo wa utawala wa Trump kuwatimua wahamiaji pamoja na kulengwa kwa wanafunzi wa nchi za kigeni waliounga mkono maandamano ya kusimama na Palestina.

    Anewashutumu pia maafisa wa Trump kwa kuzihamasisha "cbaadhi ya jamii za mrengo wa kulia". Utawala wa Trump umepinga tuhuma za ubaguzi. Rais anasema ana jukumu la kuwarudisha makwao maelfu ya wahamiaji waliongia Marekani kinyume na sheria, hatua anayosema inambatana na sehemu kuu ya kampeni yake yakuchaguliwa katika urais mwaka jana.

  6. Somalia yaipa Marekani vituo vyake vya anga na bandari

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Somalia iko tayari kutoa udhibiti wa kipekee kwa Marekani juu ya vituo vya anga na bandari za kimkakati, rais wake alisema katika barua kwenda kwa Rais Donald Trump, kwa mujibu wa Reuters.

    Katika barua hiyo ya Machi 16, ambayo ilithibitishwa na mwanadiplomasia wa kikanda mwenye ufahamu wa suala hilo, Rais Hassan Sheikh Mohamud alisema udhibiti huo unajumuisha vituo vya anga vya Balidogle na Berbera, pamoja na bandari za Berbera na Bosaso.

    Mawaziri wa mambo ya nje na yule wa habari wa Somalia hawakujibu mara moja maombi ya kuzungumzia hilo.

    Hatua hiyo inaweza kuipa Marekani nafasi ya kuongeza uwepo wake mkubwa zaidi wa kijeshi katika eneo la Pembe ya Afrika wakati inapojaribu kukabiliana na tishio kutoka kwa wanamgambo wa Kiislamu nchini Somalia na katika eneo zima.

    "Rasilimali hizi zilizo katika maeneo ya kimkakati zinatoa fursa ya kuimarisha ushiriki wa Marekani katika eneo hili, kuhakikisha upatikanaji wa masaada ya kijeshi na vifaa bila vikwazo, huku zikidhibiti washindani wa nje kuingia katika maeneo hayo muhimu," barua hiyo ilisema.

    Berbera iko katika eneo la Somaliland lililojitenga, jambo linalomaanisha kuwa ombi la kuihusisha bandari na kituo cha anga kilichopo huko litaiweka serikali ya eneo hilo na Somalia katika mgongano mwingine.

    "Kushirikiana gani? Marekani ilikata tamaa na serikali hii fisadi inayoitwa Somalia. Marekani sasa iko tayari kushirikiana na Somaliland, ambayo imeonyesha dunia kuwa taifa lenye amani, utulivu, na demokrasia," alisema Abdirahman Dahir Aden, waziri wa mambo ya nje wa Somaliland, alipoongea na Reuters.

    "Marekani si wajinga. Wanajua ni nani wanapaswa kushughulika naye linapokuja suala la bandari ya Berbera," aliongeza. Somalia inapinga hatua yoyote ya kuitambua Somaliland kama taifa huru. Balidogle iko takriban kilomita 90 (maili 55) kaskazini-magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu, huku Bosaso ikiwa katika jimbo la Puntland lenye utawala wa ndani.

  7. Idadi ya waliokufa kwenye tetemeko la ardhi Myanmar yafikia zaidi ya 1,000

    BBC

    Chanzo cha picha, c

    Zaidi ya watu 1,000 wameuawa nchini Myanmar na wengine zaidi ya 2,000 kujeruhiwa kufuatia tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 ambalo lilisikika pia katika nchi jirani ya Thailand.

    Wako wafanyakazi zaidi ya 100 Thailand waliokuwa wanaendelea na shughuli za ujenzi wa ghorofa moja hawajapatikana baada ya tengo hilo kubomoka.

    Wengi wa walioaga dunia wako Mandalay, mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar, na mji ulio karibu zaidi na kitovu cha tetemeko la ardhi.

    Wafanyakazi wa uokoaji bado wanahangaika kutafuta manusura nchini Myanmar na Thailand "Tunafukua watu kwa kutumia mikono," timu moja ya uokoaji iliambia BBC huko Mandalay, sio mbali na kitovu cha tetemeko hilo.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea katika eneo la juu ambalo halijakamilika huko Bangkok baada ya kuporomoka - na takriban wafanyakazi 100 wa ujenzi hawajulikani waliko na sita wamekufa, kulingana na maafisa wa serikali ya eneo hilo.

    Serikali ya kijeshi ya Myanmar imetoa ombi la msaada wa kimataifa, ombi adimu kutoka kwa serikali iliyojitenga na ambayo. imewekewa vikwazo vikali na mataifa ya Magharibi katika miaka ya hivi karibuni.

    Udhibiti mkali wa jeshi la Myanmar na kuendelea kukosekana kwa utulivu wa ndani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kunafanya kuwa vigumu kupata taarifa sahihi kuhusu maafa hayo.