Tetemeko la ardhi Uturuki: Jinsi walionusurika wanavyokabiliana na kiwewe

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyoikumba Uturuki na Syria hivi majuzi imepanda zaidi ya 50,000 - na kuwaacha watu wengi zaidi bila makazi.
Imeathiri vibaya afya ya akili kwa wale waliopatwa na mkasa huo, moja kwa moja na pia kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
BBC imezungumza na walionusurika, makundi ya uokoaji, na wataalamu.
Ilikuwa ni baada ya usiku wa manane tulipowasili Antakya, tukitembea gizani katika jiji lililoachwa magofu kabisa.
Gari letu lilikuwa limeharibika na dereva alikataa kutupeleka katikati ya jiji.
Ilikuwa siku ya tatu baada ya mitemeko ya ardhi kupiga kusini-mashariki mwa Uturuki. Timu yetu ilikuwa imetoka Maras, kitovu cha mitetemeko hiyo.
Tayari maelfu ya watu walithibitishwa kufariki na idadi hiyo imeendelea kuongezeka tangu wakati huo.
Tulipokuwa tukishuka kwenye barabara kuu kuelekea Antakya, king'ora cha mara kwa mara cha ambulensi kilisikika kupitia vifusi.
Malori ya misaada, tingatinga na watu waliojitolea wote walikuwa wamekwama kwenye foleni za magari ambayo yameenea kwa maili. Ilikuwa ni hali ya mtafaruku kabisa kwenye baridi kali.
Burak Galip Akkurt na timu yake kutoka chama cha waokoaji wa kujitolea cha Uturuki, Akut, walikuwa wakifanya kazi katika jengo la orofa nne. Walishuku kulikuwa na watu 10 waliozikwa wakiwa hai chini ya vifusi, watano kati yao wakiwa watoto.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mijengo yao ilipenya giza la mabaki hayo huku wakipiga kelele kwa kuuliza swali ambalo limezoeleka sana: "Je, kuna mtu yeyote anayenisikia?"
Walingoja kwa ukimya, wakitarajia sauti hafifu ijibu au hata kusikia sauti.
"Unaposikia sauti kutoka chini ya vifusi, unajisikiaje?" Nilimuuliza Burak kwa utulivu.
Alihitaji kutengwa na hisia zake ili aendelee na juhudi za uokoaji, alielezea, lakini itampata mara tu misheni itakapomalizika na atatafuta msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na kila kitu alichokishuhudia.
"Si rahisi sana kupona kutokana na mambo uliyoyaona. Inasikitisha, na ya kushangaza pia."
Hakuna mtu aliyenusurika kutoka chini ya vifusi vya ghorofa waliyokuwa wakifanya kazi usiku huo.
Siku iliyofuata nilikutana na Dilek Eger. Aliokolewa kutoka kwa jengo katika mji jirani wa Iskenderun, baada ya kunaswa kwa saa nane.
“Tetemeko lile lilikuwa la ajabu sana, mara nilinyanyuka kitandani na kukimbilia chumba cha wazazi wangu, nikawa napiga kelele, lakini mama, baba, kaka wote walikuwa kimya, nilifikiri nitarukwa na akili. ," aliniambia.

Chanzo cha picha, Reuters
Wazazi na kaka wa Dilek walipoteza maisha chini ya vifusi. Alikuwa amekwama, amezungukwa na glasi iliyovunjika, na sehemu ya juu tu ya kichwa chake ikionekana. Rafiki wa familia aliweza kumtambua na kumwokoa kwa mikono yake mitupu na kisu.
Siku mbili za mwanzo hakuweza kulia hata kidogo, lakini akiwa amejilaza kwenye sofa la sebuleni kwa bibi yake huku akiniongelea kwa upole kupitia msukosuko wake huo, alianza kupitiwa na hisia zote.
Alipoibusu picha ya mama yake na yeye mwenyewe akiwa amekumbatiana, alianza kulia.
"Mama yangu alitoa pumzi yake ya mwisho mikononi mwangu," alisema. "Hata wakati wa kufa aliniokoa, kwani alikuwa juu yangu, sikuweza kufanya chochote kwa ajili yake.
"Ndugu yangu alikuwa amekwama kwenye chumba kingine, na baba yangu alikuwa akiugua kwa maumivu. Wakati huu ulimwengu wote unaanguka. Unashuhudia kifo cha kila mtu unayempenda. Sijisikii kuwa na hasira au kulipiza kisasi. Najiona mtupu tu. ."
Dilek ni mmoja wa maelfu ya watu walionusurika tetemeko la ardhi, lakini sasa anakabiliwa na maisha ambayo yanaweza kuwa na kovu milele.
Wiki hii nilipokea ujumbe mfupi kutoka kwa mtu mwingine aliyenusurika. Aliandika hivi: “Sisi tulio hai sasa tutakaa chini ya vifusi hadi siku tutakapokufa.
Wanasaikolojia wanasema waathirika wa tukio hilo la kutisha watakuwa wakipitia awamu: mshtuko wa awali, wasiwasi na hofu hivi karibuni vitabadilishwa na hali ya kukataa.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Cagay Duru kutoka Chama cha Wanasaikolojia wa Kituruki alisema haikuwa rahisi kukabiliana na kiwewe kwa kiwango hiki, lakini kuzungumza juu yake, kuelezea hisia na mawazo juu ya kile kilichotokea inapaswa kuwa hatua ya kwanza kuelekea uponyaji.
Alionya kwamba ikiwa usaidizi wa kisaikolojia na kijamii haukuwepo kwa wale wanaohitaji wakati wa mchakato huu wa huzuni, basi watu wengi wanaweza kuishia na matatizo makubwa kama vile ugonjwa wa mkazo wa baada ya kiwewe (PTSD), huzuni au matumizi mabaya ya madawa ya kulevya.
"Inabidi sote tuulizane: Habari yako? Je, kuna chochote ninachoweza kukufanyia?
"Lazima tuseme: niko hapa kwa ajili yako. Lazima tutoe ujumbe kwamba tuko katika mshikamano na wale wanaohitaji na tunajaribu kuelewa uzoefu wao, tupo kuwasikiliza, kuwasaidia na kushiriki hisia hizi zote. ."
Kawaida haimaanishi kurudi jinsi maisha yalivyokuwa kabla ya tetemeko la ardhi, itakuwa kawaida mpya. Kawaida hiyo mpya ingehitaji kujengwa na ingechukua muda.
Lakini ugumu wa kazi hiyo ulisisitizwa wakati seti mpya ya mitetemeko ya ardhi ilipopiga mji ambao tayari ulikuwa umeharibiwa wa Hatay.
Hii haikuwa na nguvu kama ile miwili ya mwanzo, lakini bado watu waliojawa na hofu walikuwa mitaani, wakilia kwa kukata tamaa, wakijiuliza ikiwa walikuwa wakikabiliwa na jinamizi lisilo na mwisho. Wengine walikasirika, wakiuliza ni nini zaidi kingefanywa kuokoa maisha.
Sasa huko Istanbul, nimeondoka kwenye eneo la maafa, lakini bado nimezingirwa na kiwewe; nikitizama runinga na simu yangu ya mkononi kama mamilioni ya wengine.
Kwa vile jiji kubwa la Uturuki liko kwenye eneo linaloweza kukumbwa na tetemeko, watu hapa hawawezi kujizuia kuuliza: Je, watakuwa wakipitia mkasa huo katika siku zijazo? Je, wanaweza kufanya nini ili kulizuia?
Huzuni inapoanza, kiwewe kikubwa na jinsi ya kukabiliana nayo imekuwa changamoto nyingine kubwa kwa Uturuki.















