Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mioyo yetu inaumia, asema Rais wa Israeli huku Hamas ikirudisha miili ya mateka

Hamas inasema miili hiyo minne ni ya mama na watoto wake wawili, na pia mwanamume wa miaka 84.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri!

  2. Ukraine inahitaji kujizuia kuikosoa Marekani, mshauri wa usalama wa Ikulu anasema

    Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Ikulu Michael Waltz amesema Ukraine inahitaji kuzuia ukosoaji wake kwa Marekani, wakati Washington inajaribu kupata makubaliano ya amani ili kumaliza vita.

    "Haikubaliki, wao [Ukraine] wanahitaji kujizuia na kuwa na mtazamo chanya na kusaini mkataba huo," anaiambia Fox News. Akizungumzia mkataba unaoshinikizwa na Donald Trump wa kupata madini adimu nchini Ukraine kwa mabadilishano ya misaada, au hata kama fidia kwa msaada ambao Marekani tayari imetoa.

    "Tuliwakilisha Ukraine vizuri, na kwa namna ya kihistoria," mshauri huyo amesema, akiongeza kuwa itakuwa "endelevu" na "hakikisho bora" la usalama ambalo wangeweza kutumaini.

    Hata hivyo, Zelensky amekataa hadharani ombi la Marekani la kupata - na kufaidika na madini ya Ukraine, akisema: "Siwezi kuuza jimbo letu."

    Lakini amesema kuwa nchi hizo mbili zinaweza kusuluhisha tofauti zao.

    Soma zaidi:

  3. Mioyo yetu inaumia, Rais wa Israeli asema wakati Hamas inarudisha mateka wa kwanza waliofariki

    "Mioyo ya taifa zima iko katika hali tete," rais wa Israeli amesema, wakati miili ya mateka wanne waliochukuliwa wakiwa hai na Hamas katika shambulio lake la tarehe 7 Oktoba 2023 iliporejeshwa Tel Aviv.

    Hamas inasema miili hiyo ni ya mama na watoto wawili kutoka kwa familia ya Bibas, ambayo hatima yao imeathiri Israeli, na Oded Lifschitz, 84, mwanaharakati mkongwe wa amani.

    Rais Isaac Herzog aliandika "hakuna la kusema" katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, akiwaomba wanne hao msamaha "kwa kutoletwa nyumbani salama".

    Ni mara ya kwanza kwa kundi la Hamas kuwarudisha mateka waliofariki tangu kuanza kwa usitishaji mapigano mwezi uliopita, huku Israeli ikisema kuwa itathibitisha utambulisho wao baada ya uchunguzi wa kitaalamu.

    Mateka sita walio hai wanastahili kuachiliwa siku ya Jumamosi.

    Katika taarifa kabla ya makabidhiano hayo, familia ya Bibas nchini Israeli ilisema "imekumbwa na msukosuko", na kuongeza kuwa "hadi tutakapopata uthibitisho wa uhakika, safari yetu haijaisha".

    Afisa wa Msalaba Mwekundu alionekana kutia sahihi nyaraka kwenye meza pamoja na wapiganaji wa Hamas waliokuwa na silaha kabla ya jeneza kuwekwa kwenye magari ya Msalaba Mwekundu.

    Soma zaidi:

  4. Azerbaijan yaamuru kusimamishwa kwa matangazo ya BBC News huko Baku

    Serikali ya Azerbaijan imeamuru kusitishwa kwa matangazo ya Kiazabajani ya BBC News katika mji mkuu wa Baku.

    BBC ilisema katika taarifa siku ya Alhamisi kwamba ilifanya "uamuzi ambao haikutaka" kufunga ofisi yake nchini humo baada ya kupokea maagizo yasio rasmi kutoka kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

    Shirika hilo liliongeza kuwa "linasikitika" sana kwa "hatua hii iliyo kinyume na uhuru wa vyombo vya habari".

    Vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali vimeripoti kuwa serikali ilitaka kupunguza idadi ya wafanyikazi wa BBC wanaofanya kazi nchini humo hadi mmoja.

    BBC inasema kuwa timu yake ya waandishi wa habari mjini Baku imesitisha shughuli zake za uandishi wa habari, huku ikitafuta ufafanuzi kuhusu maelekezo hayo, lakini inasalia na nia ya kuendelea kutoa taarifa kwa lugha ya Kiazabajani.

    "Tunajutia sana hatua hii ambayo ni kikwazo kwa uhuru wa vyombo vya habari, na itazuia uwezo wetu wa kutoa taarifa ndani na kutoka Azerbaijan kwa watazamaji wetu ndani na nje ya nchi," msemaji wa BBC alisema katika taarifa.

    BBC haijapokea chochote kwa maandishi kutoka kwa serikali ya Azerbaijan na imetaka ufafanuzi kupitia njia kadhaa.

    Wizara ya mambo ya nje ya Azerbaijan pia haijajibu ombi la BBC la kutaka maoni yake.

    BBC News imefanya kazi nchini Azerbaijan tangu mwaka 1994, ikitoa taarifa na habari zisizo na upendeleo, mwanzoni kupitia matangazo ya redio na baadaye kupitia majukwaa ya kidijitali.

    Soma zaidi:

  5. Luis Rubiales: Bosi wa zamani wa soka Uhispania apigwa faini kwa kumpiga busu mchezaji

    Bosi wa zamani wa shirikisho la soka nchini Uhispania Luis Rubiales amepatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono kwa kumpiga busu mchezaji Jenni Hermoso bila ridhaa yake na kuamuriwa kulipa faini ya €10,800 (£8,942), Mahakama Kuu ya Uhispania imeamua.

    Aliondolewa kosa la kulazimisha, kwa madai ya kujaribu kumshinikiza Hermoso kusema hadharani kwamba busu hilo lilikuwa la makubaliano.

    Wakati wachezaji wa Uhispania wakipokea medali zao baada ya kuishinda Uingereza mjini Sydney na kushinda Kombe la Dunia la 2023, Rubiales alimshika Hermoso kwa kichwa na kumbusu kwenye midomo.

    Tukio hilo lilisababisha maandamano na wito wa kutaka Rubiales ajiuzulu.

    Uamuzi huo pia ulipiga marufuku Rubiales kwenda ndani ya eneo la mita 200 kutoka Hermoso na kuwasiliana naye kwa mwaka mmoja, mahakama ilisema katika taarifa.

    Waendesha mashtaka walikuwa wamedai kifungo cha jela kwa Rubiales, ambaye wiki iliyopita aliiambia mahakama kwamba "ana uhakika kabisa" Hermoso alikuwa amempa kibali kabla ya kumbusu.

    Alielezea busu hilo kama "tendo la mapenzi".

    Katika ushahidi wake mapema mwezi huu, Hermoso alisisitiza kwamba hakuwa amempa Rubiales ruhusa na kwamba tukio hilo "limechafua moja ya siku za furaha maishani mwangu".

    Rubiales alishtumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia na kujaribu kulazimisha Hermoso kusema busu hilo ilikuwa ya makubaliano.

    Soma zaidi:

  6. Mgawanyiko kati ya Trump na Zelensky unazidi kuongezeka

    Vita vya maneno vilianza na maoni yaliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari huko Mar-A-Lago huko Florida, alipoilaumu Ukraine kwa vita hivyo.

    "Haukupaswa kamwe kuuanzisha. Tungeweza kufikia makubaliano," alisema.

    Trump hakutaja kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin alichukua uamuzi wa kuivamia Ukraine mnamo Februari 2022.

    Siku ya Jumatano, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, alijibu mazungumzo ya Marekani na Urusi nchini Saudi Arabia kwa jinsi Ukraine ilivyotengwa, aliwaambia waandishi wa habari mjini Kyiv: "Tunaona taarifa nyingi potofu na zinatoka Urusi. Kwa heshima zote kwa Rais Donald Trump kama kiongozi ... anaishi katika ulimwengu wa taarifa potofu."

    Aliongeza kuwa anaamini "Marekani ilimsaidia Putin kuondokana na kutengwa kwa miaka mingi".

    Baadaye, Trump alimwita Zelensky "dikteta" na kusema kiongozi huyo amefanya "kazi mbaya".

    Soma zaidi:

  7. Urusi inaanza tena mazungumzo na Marekani 'ya pande zote' - Kremlin

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema kuwa mazungumzo ya Urusi na Marekani ya"pande zote".

    Pia amesema "wanakubaliana kabisa na utawala wa Marekani" kwamba mazungumzo yanahitajika "kuanzisha amani haraka iwezekanavyo".

    Peskov pia imetoa maoni juu ya madai ya mapema ya Urusi kwamba uungwaji mkono wa Zelensky unashuka.

    Anasema hili "liko wazi kabisa" lakini akaepuka kujadili takwimu zozote.

    Ukraine inasema Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 161 katika shambulio la usiku

    Wakati huo huo, Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 161 katika shambulio la usiku mmoja, kwa mujibu wa jeshi la Ukraine.

    Inasema makombora yalilenga miundombinu muhimu katika eneo la kaskazini-mashariki la Kharkiv, na "bomu lililoongozwa" lilipiga lango la jengo la juu huko Kherson, na kusababisha hasara.

    Waziri wa Nishati Ujerumani Galushchenko amesema shambulizi la Urusi liliharibu vifaa vya uzalishaji wa gesi.

    "Madhumuni ya mashambulizi haya ya kihalifu ni kukomesha uzalishaji wa gesi inayohitajika kukidhi mahitaji ya ndani ya wananchi," amesema kwenye mitandao ya kijamii.

    Soma zaidi:

  8. Israel yapokea miili ya mateka wanne walioshikiliwa na Hamas huko Gaza

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imesema miili ya mateka wanne imefikishwa kwa majeshi ya Israel huko Gaza.

    Katika taarifa, inasema kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) sasa litawapeleka kwenye taasisi ya uchunguzi ya Abu Kabir huko Jaffa kwa ajili ya utambuzi rasmi.

    Inasema familia za mateka waliokufa zitajulishwa rasmi baada ya vifo vyao kuthibitishwa kupitia vipimo.

    Pia inaiomba heshima kwa faragha ya familia hizo.

    Kabla ya miili ya mateka wanne kuhamishiwa kwa shirika la Msalaba Mwekundu, Hamas ilitoa taarifa ambapo ilirudia madai yake kwamba mateka wanne ambao miili yao inarejeshwa leo waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel.

    Kwa muktadha: Hamas ilidai mwezi Novemba 2023 kwamba wanafamilia watatu wa familia ya Bibas waliuawa katika shambulizi la anga la Israel, bila kutoa ushahidi. Israel haijathibitisha hili.

    Kundi hilo linasema lilifanya "kila liwezalo kulinda" mateka na "kuhifadhi maisha yao".

    Linasema kwamba "mapigano makali na yanayoendelea ya Israel yalizuia kuwaokoa mateka wote".

    Likiwa linazungumzia moja kwa moja kwa familia za mateka, kundi la Hamas linasema lingeweza lilipenda kuwarejesha mateka wakiwa hai.

    Unaweza kusoma;

  9. Starmer amuunga mkono Zelensky baada ya Trump kumuita 'dikteta'

    Waziri Mkuu Sir Keir Starmer amemuunga mkono Volodymyr Zelensky kama "kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia" baada ya Donald Trump kumuita rais wa Ukraine "dikteta".

    Sir Keir alimpigia simu Zelensky jioni ya Jumatano na kumwambia kuwa ni "vitu halali" kwa Ukraine "kusitisha uchaguzi wakati wa vita kama ilivyokuwa Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia", imesema ofisi ya Waziri Mkuu.

    Rais wa Marekani alimkosoa Zelensky mapema, akisema alifanya "kazi mbaya" na kudai "anakataa kufanya uchaguzi" nchini Ukraine.

    Muda wa miaka mitano wa Zelensky ulikuwa unatarajiwa kumalizika Mei 2024, lakini uchaguzi umesitishwa tangu sheria ya kijeshi ilipoanzishwa baada ya uvamizi wa Urusi.

    Unaweza kusoma;

  10. DRC yaomba msaada wa kijeshi Chad kupambana na waasi

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeomba msaada wa kijeshi kutoka Chad katika jitihada zake za kupambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika mikoa yake ya mashariki.

    Waziri anayeshughulikia masuala ya kikanda wa DRC alikutana na Rais wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, Jumanne akimuwakilisha Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais wa Chad iliyochapishwa kwenye wa Facebook.

    Maelezo ya kina ya mazungumzo yao hajawekwa wazi. Mmoja wa maafisa wa Chad anayeyefahamu mazungumzo hayo alisema Chad inalibeba ombi la kuombwa msaada na Kongo, lakini bado haijafanya maamuzi kuhusu ombi hilo.

    Chanzo kutoka ofisi ya rais DRC kilisema kuwa nchi hiyo imeomba msaada wa kijeshi na kidiplomasia kutoka Chad.

    Hata hivyo chanzo hicho ambacho hakijataka kutambulishwa kwa sababu za ndani, hakijatoa maelezo zaidi.

    Msemaji wa serikali ya Chad, Gassim Cherif, hakujibu ombi la kutoa maoni yake kuhusu hili, kwa mujibu wa Reuters. Kwa upande wake, msemaji wa Rais Tshisekedi, Tina Salama, alisema hana taarifa yoyote kuhusu suala hilo.

    Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad aliiambia Reuters kuwa kupeleka msaada wa kijeshi DRC ni 'taarifa za tetesi'.

  11. Marekani yasusia mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini

    Mkutano wa mawaziri wa masuala ya kigeni wa nchi tajiri duniani (G20) umeanza leo huko Afrika kusini.

    Hata hivyo, Marekani kupitia Waziri wake wa masuala ya kigeni wa Marekani Marco Rubio haitohudhuria mkutano huo.

    Marco Rubio alitangaza kutohudhuria kupitia kwenye mitandao ya kijamii mapema mwezi huu akitaja kuwa ‘’Afrika kusini inafanya mambo ya kutamaushwa’’, akielezea kuwa jukumu lake ni kupigania maslahi ya Wamarekani na sio kufuja kodi wanazozitoa.

    Trump alifuta misaada kwa Afrika Kusini akijibu mswada wa unyakuzi uliotiwa saini hivi majuzi ambao unaweza kuruhusu serikali kutwaa ardhi bila fidia.

    Pretoria imekanusha mara kwa mara kwamba kuna unyakuzi wowote kiholela wa ardhi au mali ya kibinafsi nchini Afrika Kusini.

    Tamko hilo limeendelea kuweka uhusiano wa kidiplomasia baina ya Afrika kusini na Washington njia panda haswa wakati huu wa utawala mpya wa Rais Donald Trump.

    Huenda lengo la mkutano halitaafikiwa ambapo Afrika kusini walitaka kuutumia kukuza masuala muhimu kwa nchi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha za maendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

    Huu ni mkutano wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la G20 yenye uchumi mkubwa tangu Afrika Kusini ilipochukua nafasi ya urais mwezi Disemba mwaka jana.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Israel yajiandaa kukabidhiwa mateka waliokufa kutoka kwa Hamas

    Hamas itakabidhi Israel miili ya mateka wanne waliotekwa Gaza tangu shambulio la kundi hilo dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

    Miili hiyo inajumuisha mama mmoja na watoto wawili kutoka familia ya Bibas, ambao hatima yao imekuwa kivutio cha hisia za Walowezi.

    Mtoto mdogo, Kfir, alikuwa na miezi tisa tu wakati alipotekwa.

    Hamas inadai pia kwamba mwili wa nne ni wa Oded Lifshitz, mwenye umri wa miaka 84, ambaye alikuwa mtetezi maarufu wa amani.

    Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Hamas kuachilia miili ya mateka waliokufa tangu kuanza kwa mkataba wa kusitisha mapigano mwezi uliopita.

    Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema,‘‘ taifa lake limegubikwa na huzuni’’, akisubiri kukabidhiwa miili hiyo.

    Mateka sita walio hai wanatarajiwa kuachiliwa Jumamosi ijayo.

    Habari za kifo cha Shiri Bibas, mwenye umri wa miaka 33, na watoto wake (ambao sasa wangekuwa na umri wa miaka mitano na miwili) zimechochea huzuni kote nchini.

    Hata hivyo, serikali imesema itathibitisha majina ya waliofariki baada ya kufanya uchunguzi wa maiti wa kina.

    Hamas ilidai kwamba Shiri, Kfir na ndugu yake Ariel walikufa katika shambulio la angani la Israel, lakini hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha hilo.

    Familia ya Bibas ilikamatwa pamoja na baba yao, Yarden, kutoka kibbutz Nir Oz, wakati wanamgambo wa Hamas walipovamia mipaka ya Israel.

    Mkataba wa kusitisha mapigano ulioanza kutekelezwa tarehe 19 Januari ulikubali kubadilishana miili ya mateka wanne.

    Pande hizo mbili pia zilikuwa zimekubaliana kubadilishana mateka 33 kwa takriban wafungwa 1,900.

    Mazungumzo ya kuendelea na awamu inayofuata ya mkataba, ambapo mateka waliobaki wangeachiliwa na vita kumalizika, yalitarajiwa kuanza mapema mwezi huu, lakini bado hayajaanza.

    Mateka 24 na zaidi ya wafungwa 1,000 wamebadilishana hadi sasa, huku mateka 70 waliotekwa mnamo Oktoba 7 wakiwa bado wanashikiliwa Gaza.

    Inakadiriwa kuwa nusu ya mateka wote waliobaki Gaza bado wapo hai.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Kaburi la Firauni wa kwanza lagunduliwa Misri

    Wanaaikolojia wa Misri wamegundua kaburi la Firauni tangu ufukuaji wa mfalme Tutankhamun mwongo mmoja uliopita.

    Kaburi la Mfalme Thutmose wa pili ilikuwa kaburi la mwisho la kifahari kugunduliwa katika utawala wa Misri wa karne ya 18.

    Kikosi mseto cha Uingereza na Misri kimegundua kaburi hilo katika bonde la magharibi la Theban Necropolis karibu na mji wa Luxor.

    Watafiti walidhani maziarani ya mafirauni wa utawala wa karne ya 18 yalikuwa yametangana kwa zaidi ya kilomita mbil, karibu na bonde la wafalme.

    Kikosi hicho kiligundua kaburi hilo katika Eneo ambalo linaaminika kuzikwa wanawake waliokuwa na mamlaka, lakini walipofungua kaburi hilo walikuta nakshi ambazo huwa ni ishara alikuwa ni firauni.

    ‘’Sehemu ya dari ya kaburi ilikuwapo: dari iliyochorwa kwa buluu na nyota za manjano. Na dari kama hiyo, iliyochorwa kwa buluu na nyota za manjano, hupatikana tu katika makaburi ya mfalme,” alisema Mkurugenzi wa Utafiti wa Msafara Dr. Piers Litherland.

    Akizungumza na kipindi cha BBC cha Newshour, alielezea hisia alizopata wakati wa kugundua.

    “Hisia za kuingia katika maeneo haya ni za mshangao wa kipekee, kwa sababu unapokutana na kitu ambacho hukutarajia kukiona, inakuwa ni hali ya kihisia inayosumbua sana,” alisema.

    “Na nilipotoka, mke wangu alikuwa akinisubiri nje na jambo la pekee niliweza kufanya ni kulia kwa sauti.”

    Dr. Litherland alisema kugunduliwa kwa kaburi hili kumemaliza siri ya mahali walipo makaburi ya mfalme wa kwanza wa nasaba ya 18.

    Watafiti waligundua mabaki ya mfalme Thutmose wa pili karne mbili zilizopita lakini alikozikwa hakujawahi kupatikana kufikia sasa.

    Kugunduliwa kwa kaburi hili la firauni linakamilisha zaidi ya miaka 12 ya kazi ya pamoja ya timu ya Dr. Litherland kutoka Taasisi ya Utafiti ya New Kingdom na Wizara ya Utalii na Antikithi za Misri.

    Thutmose II alikuwa mzalendo wa Tutankhamun, ambaye utawala wake unakadiriwa kuwa ni kati ya 1493 hadi 1479 KK.

    Kaburi la Tutankhamun liligunduliwa na wanaaikolojia wa Uingereza mnamo mwaka 1922.

    Mfalme Thutmose II anafahamika zaidi kama mume wa Malkia Hatshepsut, ambaye anahesabiwa kuwa ni miongoni mwa firauni maarufu zaidi wa Misri na miongoni mwa firauni wachache wa kike waliotawala kwa haki zao wenyewe.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Liverpool yavutwa shati EPL, City yang'olewa mabingwa Ulaya

    Liverpool imetoka sare ya 2-2 dhidi ya Aston Villa pale Villa Park na kuifanya kuongoza msimamo wa ligi kwa alama 8.

    Ikisalia michezo 12 kabla ya ligi kumaliza, ni Arsenal inayoweza hasa kuipelekesha Liverpool katika kusaka ubingwa huo.

    Liverpool inakutana na Manchester City katika mchezo ujao, mchezo mgumu licha ya City kuonekana kuwa katika kiwango kibovu msimu huu, ikiondolewa katika ligi ya mabingwa Ulaya na Real Madrid, na ikiwa haina matumaini hata ya kushika nafasi ya pili katika ligi kuu msimu huu, achilia mbali ubingwa.

    Kocha wa Liverpool, Arne Slot, hajafurahia matokeo ya jana, kwa sababu baada ya Villa itakipiga na Newcastle, mchezo mwingine mgumu.

    Arsenal yenyewe itacheza na Westham mwishoni mwa wiki kabla ya kuwafuata Nottigham Forest.

    Kuna uwezekano Arsenal akapunguza tofauti ya alama mpaka tano, kama itashinda mchezo wake mmoja wa mkononi. Liverpool imecheza michezo 26, Arsenal 25.

    Kwingineko, Manchester City imeondolewa katika ligi ya mabingwa Ulaya, kwa jumla ya mabat 6-3, kufuatia kichapo cha jana cha mabat 3-1. katika mchezo wa awali wiki iliyopita, city ilichapwa 3-2.

    Huu unaweza kawa mwisho wa zaman kwa City na kocha wake, Pep Guardiola kwa kuwa hawana chao pia fatica ligi kuu England, wakiwa nafasi ya 4 kwa kutofauti ya alama 17 dcidi ya vinara Lverpool.

    Ikisalia michezo 12 kabla ya msimu kumaliza, kuna uwezetano mkubwa city kuambulia patupu msimu huu.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Kenya yaijibu Sudan kuhusu uwepo wa waasi wa RSF jijini Nairobi

    Saa chache baada ya serikali ya Sudan kutangaza itachukua hatua kali dhidi ya serikali ya Kenya kwa kukaribisha wanamgambo wa RSF jijini Nairobi kufanya mkutano wao, Kenya imebainisha mchango wake katika kutatua mgogoro wa Sudan.

    Kupitia taarifa rasmi kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri na wizara ya mambo ya kigeni imeeleza kuwa haijakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa, misingi ya Umoja wa Afrika wala Mkataba wa kuzuia uhalifu wa Kimbari kama inavyodaiwa na Sudan.

    Kenya ikionekana kutetea uwepo wa waasi wa RSF jijini Nairobi imesisitiza kuwa kama ilivyokuwa desturi kwa mataifa yanayokumbwa na migogoro, ni kawaida kwa pande zinazohasimiana kufanya mikutano ya amani katika nchi jirani ili kufikia suluhu ya kudumu.

    "Msimamo wa Kenya uko wazi: tunatoa nafasi ya mazungumzo, bila kuchukua upande wowote, kwa sababu tunaamini katika uwezo wa mazungumzo ya amani kutatua mizozo ya kisiasa," ilisema taarifa hiyo.

    Serikali ya Kenya ambayo imekosolewa kwa kuruhusu RSF imeeleza lengo lake ni kutoa fursa vikosi vya RSF pamoja na mashirika ya kiraia ya Sudan kujadili na kutafuta njia ya kurudisha utawala wa kiraia nchini Sudan.

    ‘’Tuna imani kwamba watu wa Sudan wataweza kupata suluhu ya haraka na endelevu kwa mgogoro huu,’’ tamko la serikali ya Kenya limeeleza.

    Aidha ,Kenya imetambua kuwa mgogoro wa kisiasa unaendelea kuathiri raia wengi wa Sudan na hivyo imeahidi dola milioni 2 kusaidia kupunguza janga la kibinadamu linaloikumba nchi hiyo.

    Wakati huo huo Wanamgambo wa RSF wamepanga kutoa tamko kwa wanahabari leo baada ya kuthibitsha kuwa watatia saini makubaliano ya kuunda serikali mbadala ndani ya Sudan.

    Makubaliano hayo yanatarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Ijumaa hii.

    Mwaka 2002, mazungumzo ya amani yaliyofadhiliwa na Kenya yalimaliza vita vya kiraia vya Sudan kupitia Mkataba maarufu wa Machakos na kuzaa serikali mpya.

    Hali hiyo, Kenya imependekeza kuwa mgogoro wa kisiasa hausuluhishwi na harakati za kijeshi.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Rais Trump amemuita Rais Zelensky 'dikteta' huku mgawanyiko kati ya viongozi hao wawili ukizidi kuongezeka

    Rais Donald Trump alitumia siku nzima kumshambulia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, akimwita "dikteta" na kuzidi kuongeza mvutano kati ya viongozi hao wawili.

    Mashambulizi yake yanafuatia kauli ya Zelensky, alivyojibu mazungumzo kati ya Marekani na Urusi huko Saudi Arabia ambapo Kyiv haikushirikishwa, akisema kuwa rais wa Marekani alikuwa "anadanganywa" na Moscow.

    Akizungumza katika mkutano wa uwekezaji unaoungwa mkono na Saudi Arabia huko Florida, Trump alisema jambo moja tu ambalo Zelensky "alikuwa mzuri ni kumchezia Joe Biden."

    Lugha ya "dikteta" ilichochea ukosoaji wa haraka kutoka kwa viongozi wa Ulaya, wakiwemo Kanzlera wa Ujerumani, Olaf Scholz, ambaye alisema, "ni jambo lisilo sahihi na hatari kukanusha uhalali wa kidemokrasia wa Rais Zelensky."

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, aliweka wazi kuwa alimuunga mkono Zelensky alivyozungumza nae kwa. Msemaji wa Downing Street alisema Sir Keir "aliweka wazi msaada wake kwa Rais Zelensky kama kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini Ukraine."

    Miaka mitano ya uongozi wa Zelensky ulipaswa kumalizika Mei 2024, lakini Ukraine imekuwa vitani tangu Urusi ivamie rasmi Februari 2022 hali iliyofanya kusitishwa kwa shughuli zotezote kuhusiana na uchaguzi.

    Waziri Mkuu wa Sweden, Ulf Kristersson, pia alikosoa matumizi ya neno "dikteta" kulikofanywa na Trump, huku Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, akisema kauli hizo "hazina maana."

    Soma pia:

  17. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya habari zetu