Urusi yamuachilia mwandishi wa Marekani katika mabadilishano makubwa ya wafungwa na nchi za Magharibi tangu Vita Baridi

Raia watatu wa Marekani waliofungwa nchini Urusi, akiwemo mwandishi wa jarida la Wall Street -Wall Street Journal, Evan Gershkovich, wanatarajiwa kuachiliwa siku ya Alhamisi chini ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa.

Muhtasari

  • Maandamano Nigeria: Kwanini vijana wanaandamana?
  • Kombe la Dunia 2034: Saudia yapanga kujenga uwanja wa mita 350 juu ya ardhi
  • Urusi kuwaachilia Wamarekani wawili katika hatua ya kubadilishana wafungwa
  • Vita vya Ukraine: Ndege za kwanza za kivita za F-16 zawasili Ukraine
  • Kwa picha: Shughuli za mazishi rasmi ya Haniyeh Tehran kabla ya mwili kuhamishiwa Qatar
  • Kenya yaanzisha mpango wa kuwauwa kwa sumu kunguru milioni moja
  • Vybz Kartel aliachiliwa baada ya hukumu ya mauaji kubatilishwa
  • Matumaini ya walionusurika yafifia katika maporomoko ya ardhi India
  • Mazishi ya kiongozi wa Hamas yavutia umati mkubwa wa watu Iran
  • Maduro aahidi kutoa data ya upigaji kura huku waangalizi wakisema uchaguzi wa Venezuela 'si wa kidemokrasia'
  • Chui ashambulia wanaume wawili katika kambi ya jeshi la wanahewa Afrika Kusini
  • Hezbollah yathibitisha kamanda wake alifariki katika shambulizi la Israel
  • Kijana, 17, ashtakiwa kwa mauaji ya wasichana watatu Uingereza
  • Watatu wanaotuhumiwa kupanga njama ya 9/11 wafikia makubaliano ya kukiri mashtaka - Pentagon

Moja kwa moja

Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo, shukran kwa kuwa nasi.

  2. Maandamano Nigeria: Kwanini vijana wanaandamana?

    h

    Shinikizo la kiuchumi

    Jambo kuu ambalo vijana wanalielezea katika wito wao wa kuandamana ni shinikizo la kiuchumi.

    Wananchi nchini humo wanalalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa za msingi kumewafanya washindwe kununua mahitaji ya maisha huku ikiaminiwa kuwa umasikini umekithiri kiasi cha baadhi ya watu kutokuwa na uhakika wa kupata hata mlo mmoja kwa siku. .

    Katika ripoti ya hivi punde iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Nigeria (NBS), ilisema mfumuko wa bei nchini umeongezeka hadi asilimia 34.19 mwezi Juni 2024.

    Na kwa miezi 18 mfululizo, kumekuwa na ongezeko la bei za bidhaa nchini Nigeria, licha ya hatua zinazochukuliwa na mamlaka ya nchi hiyo.

    Ongezeko hilo linaathiri zaidi bidhaa za chakula ambapo takwimu rasmi mpya zilisema lilifikia asilimia 40.87 mwezi Juni 2024 ikilinganishwa na Juni 2023 ambapo kulikuwa na ongezeko la asilimia 15.6.

    Tangu serikali ya Nigeria chini ya Rais Tinubu iondoe ruzuku ya mafuta Mei 29, 2023, bei ya bidhaa za kimsingi imeendelea kupanda.

    Bei ya lita moja ya mafuta imepanda mara nne hali iliyosababisha gharama za usafiri kupanda pamoja na mahitaji ya chakula na mengineyo.

    "Njaa inatuua. Ni mbaya zaidi kuliko hiyo. Tutaangamia.", Alisema mmoja wa wale wanaotaka kuona maandamano, kama alivyosema kwenye ukurasa wake wa tiktok.

    Ukosefu wa usalama

    Sababu ya pili iliyotolewa na wanaoitisha maandamano ni ukosefu wa usalama.

    Ukosefu wa usalama unayakumba karibu maeneo yote ya Nigeria.

    Ripoti ya kampuni ya ushauri ya Beacon, ambayo inachambua usalama katika bara la Afrika Magharibi, ilisema kuwa watu wengi waliuawa katika miezi sita ya kwanza ya 2024 kuliko miezi sita ya kwanza ya miaka kadhaa iliyopita.

    Mmoja wa walioomba maandamano hayo yafanyike alisema “hapa Kaskazini jambo kubwa linalotutia wasiwasi ni ukosefu wa usalama.

    h

    Chanzo cha picha, Usman Rafukka

    Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Kabiru Adamu alieleza kuwa “katika nusu ya kwanza ya mwaka, kulikuwa na vifo 5,710...idadi iliyoonekana tangu mwaka 2013 Nigeria ilipokuwa nchi yenye idadi kubwa ya watu waliouawa kuhusiana na ugaidi nchini humo ."

    Serikali ya Nigeria imesema kuwa inajitahidi kadiri iwezavyo kutatua tatizo la usalama linaloathiri mikoa ya nchi hiyo.

    Hata hivyo, tatizo la utekaji nyara linaendelea kaskazini-magharibi mwa nchi, huku kaskazini-mashariki, mwezi Juni, kulitokea shambulio la kigaidi katika eneo la Gwoza katika jimbo la Borno, ambalo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa muda mrefu.

  3. Kombe la Dunia 2034: Saudia yapanga kujenga uwanja wa mita 350 juu ya ardhi

    g

    Chanzo cha picha, Saudi 2034

    Maelezo ya picha, Taswira ya Uwanja wa Neom unaopendekezwa

    Saudi Arabia imewasilisha mipango ya kujenga viwanja 11 - ikiwa ni pamoja na uwanja mmoja wa mita 350 kutoka usawa wa ardhi, kama sehemu ya jitihada za nchi hiyo kuandaa Kombe la Dunia la 2034.

    Uwanja unaopendekezwa kujengwa katika eneo la Neom, jiji ambalo bado halijajengwa kaskazini-magharibi mwa nchi, utaweza kufikiwa tu kupitia lifti za mwendo wa kasi na magari yasiyo na dereva.

    Uwanja huo, ambao ni sehemu ya mradi wa nchi hiyo wa 'The Line' wa kuleta mseto wa uchumi wa ufalme huo mbali na mafuta, unatarajiwa kuandaa mechi ya robo fainali.

    Nia ya Saudi Arabia haijapata pingamizi na nchi hiyo ina muda hadi tarehe ya mwisho ya Oktoba kuwasilisha mipango yake.

    Kati ya viwanja 11 vipya, vinane vitakuwa katika mji mkuu Riyadh - ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Kimataifa wa King Salman wenye uwezo wa kuwapokea watu 92,760, ambapo mechi za ufunguzi na fainali zitachezwa.

    f

    Chanzo cha picha, Saudi 2034

    Maelezo ya picha, Uwanja wa Prince Mohammed bin Salman utajengwa juu ya mwamba, takriban mita 200 kutoka ardhini.

    Miji ya Jeddah, Al Khobar na Abha pia itapokea mechi za Kombe la Dunia 2034.

    Itakuwa mara ya kwanza kwa mashindano hayo yaliyopanuliwa kufanyika katika nchi moja tu ambapo timu 48 zitashiriki katika Kombe la Dunia la FIFA , kwa mara ya kwanza.

    Wenyeji wanatarajiwa kuthibitishwa rasmi na kongamano la Fifa tarehe 11 Disemba.

  4. Urusi yamuachilia mwandishi wa Marekani katika mabadilishano makubwa ya wafungwa na nchi za Magharibi tangu Vita Baridi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Evan Gershkovich alifungwa jela kwa ujasusi nchini Urusi mwezi Julai

    Raia watatu wa Marekani waliofungwa nchini Urusi, akiwemo mwandishi wa jarida la Wall Street -Wall Street Journal, Evan Gershkovich, wanatarajiwa kuachiliwa siku ya Alhamisi chini ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa.

    Gershkovich, mwanajeshi mkongwe wa kikosi cha majini cha Marekani Paul Whelan, na mwandishi wa habari wa redio ya Urusi na Marekani Alsu Kurmasheva wataachiliwa huru chini ya makubaliano yaliyokubaliwa na utawala wa Biden, afisa mkuu wa Marekani alithibitisha.

    Wafungwa wengine wanaaminika kuwa sehemu ya mpango huo. Makabidhiano hayajafanyika bado lakini yanatarajiwa baadaye leo.

    Hii inakuja siku kadhaa baada ya taarifa za uvumi kuhusu mabadilishano makubwa ya wafungwa kati ya nchi mbalimbali, ambayo uliongezeka baada ya wapinzani kadhaa na waandishi wa habari waliofungwa nchini Urusi kuhamishwa kutoka mahabusu zao za magereza na kupelekwa sehemu zisizojulikana.

  5. Vita vya Ukraine: Ndege za kwanza za kivita za F-16 zawasili Ukraine

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vyanzo kadhaa vya habari vinasema kuwa ndege za kwanza za kivita za F-16, ambazo Ukraine imekuwa ikingojea kwa muda mrefu, zimewasi nchini humo.

    Kyiv bado haijathibitisha rasmi kupokea ndege hizi za kivita na haijatoa maoni yoyote juu yake.

    Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Lithuania Gabrielius Landsbergis alitaja kwenye mtandao wa kijamii na kusema kuwa jambo lisilowezekana limewezekana kabisa.

    Awali Bloomberg ilitangaza taarifa hiyo na baadaye AP yamethibitisha kutumwa kwa ndege hizo Ukraine, likimnukuu afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake.

    Gazeti la Uingereza la Daily Telegraph kwamba jeshi la Ukraine tayari limefanya misheni ya kwanza ya mapigano kwa kutumia ndege za kivita za Magharibi aina ya F-16 na, kulingana na taarifa hiyo , zilitumika kwa madhumuni ya ulinzi wa anga.

    Ikiwa habari hii itathibitishwa, kuwasili kwa ndege hizi za kivita kunachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa ulinzi wa anga wa Ukraine.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Kwa picha: Shughuli za mazishi rasmi na maarufu ya Haniyeh Tehran kabla ya mwili kuhamishiwa Qatar

    Shughuli za mazishi rasmi ya Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati za Hamas Ismail Haniyeh zilianza Alhamisi asubuhi katika mji mkuu wa Iran, Tehran, ambako aliuawa pamoja na walinzi wake katika makazi yake katika mji mkuu wa Iran, Tehran, siku ya Jumatano.

    Iran ilitangaza kuwa msafara wa mazishi utafanyika kwa ajili ya Haniyeh mjini Tehran, kabla ya mwili wake kuhamishiwa Qatar mchana wa leo, ambako alikuwa anaishi Doha, na atazikwa huko katika mazishi rasmi siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa Hamas ilitangaza. .

    Kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Iran, Ali Khamenei, alimuombea marehemu Haniyeh , katika ua wa Chuo Kikuu cha Tehran, Alhamisi asubuhi.

    Hizi ni baadhi ya picha za mazishi hayo:

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Maelfu ya Wairani wakimuomboleza Ismail Haniyeh mbele ya Khamenei
    g

    Chanzo cha picha, Farsnews

    Maelezo ya picha, Khamenei aliongoza sala ya mazishi ya Ismail Haniyeh katika ua wa Chuo Kikuu cha Tehran Alhamisi asubuh
    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Soma zaidi:

  7. Kenya yaanzisha mpango wa kuwauwa kwa sumu kunguru milioni moja

    f

    Ukisema ni "Ndege wavamizi wa ajabu " huenda ikasikika kama filamu ya kufikirika na ya kutisha ya Hollywood, lakini kwa wakazi wa pwani ya kenya sio jambo la kufikirika.

    Maafisa wa pwani ya Kenya wana wasiwasi mkubwa juu ya kero inayoletwa na kunguru hao ambao asili yao ni India kiasi kwamba sasa wameanza harakati za kuwaua milioni moja.

    Ndege hawa huwalenga wanadamu, kama katika filamu ya kutisha ya Alfred Hitchock The Birds, lakini hawa kwa miongo kadhaa wamesababisha usumbufu mkubwa, kwa kuwinda wanyamapori, kuvamia maeneo ya kitalii na kushambulia vibanda vya kuku.

    Sumu sasa inatumika katika miji ya Watamu na Malindi kuua kundi la kwanza la spishi hii ndogo katili.

    Kampeni hii kabambe ya kutega sumu inalenga kuwakomesha kunguru kuelekea mji mkuu, Nairobi.

    Ndege hao, wanaojulikana pwani kama "kunguru" au "kurabu", walitoka India na sehemu nyingine za Asia, na mara wamekuwa wakihamia mara kwa mara mahali pengine kwa kutumia usafiri wa meli za biashara.

    Lakini inaaminika kuwa waliletwa kimakusudi katika Afrika Mashariki karibu miaka ya 1890 katika jitihada za kukabiliana na tatizo la taka lililokuwa likiongezeka katika visiwa vya Zanzibar, ambavyo wakati huo vilikuwa chini ya ulinzi wa Uingereza. Kutoka huko, walienea hadi bara na kupanda pwani hadi Kenya.

  8. Vybz Kartel aliachiliwa baada ya hukumu ya mauaji kubatilishwa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Vybz Kartel ameishi gerezani kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya hatia dhidi yake kubainika kuwa si salama

    Msanii wa dancehall kutoka Jamaica, Vybz Kartel ameachiliwa huru kutoka gerezani baada ya majaji kuamua kwamba hapaswi kushtakiwa tena kwa mauaji.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 48, ambaye jina lake halisi ni Adidja Palmer, alifungwa mwaka 2014 lakini hukumu yake imebatilishwa na majaji wa Uingereza mwezi Machi.

    Alikuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya Clive "Lizard" Williams nchini Jamaica lakini amekuwa akisisitiza kuwa hana hatia.

    Ingawa hukumu yake libatilishwa miezi kadhaa iliyopita na jopo la mahakama ya Privy mjini London, mamlaka nchini Jamaica ilikuwa na muda wa kuamua kama angeshtakiw tena au la.

    Siku ya Jumatano, majaji wa mahakama ya rufaa nchini Jamaica waliamua kesi hiyo isirudishwe mahakamani, ikimaanisha kwamba Kartel, ambaye anasemekana kuwa na afya mbaya, anaweza kuachiliwa.

  9. Matumaini ya kupata manusura yafifia katika maporomoko ya ardhi India

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Matumaini ya kupata manusura zaidi yanafifia huku shughuli za uokoaji zikiendelea huko Kerala, ambapo maporomoko makubwa ya ardhi yamesababisha vifo vya watu 182, kulingana na maafisa.

    Takriban watu 200 bado hawajulikani walipo baada ya maeneo ya Mundakkai na Chooralmala katika wilaya ya Wayanad kujaa matope na maji siku ya Jumanne.

    Shughuli za uokoaji zimetatizwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo wiki nzima.

    Jeshi linajenga daraja la muda hadi Mundakkai, upande wa pili wa mto uliojaa maji ili kuwasaidia wakazi waliokwama na kutafuta manusura zaidi.

    Siku ya Alhamisi, Wayanad ilisalia katika hali ya tahadhari kwa mvua zaidi huku shule na vyuo zikifungwa.

    Maafisa walisema karibu watu 1,600 wameokolewa kutoka vijiji vilivyoathiriwa na mashamba ya chai lakini bado idadi kubwa haijulikani ilipo.

    Soma zaidi:

  10. Yoro kuwa nje kwa miezi mitatu naye Hojlund kwa wiki sita

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Beki mpya wa Manchester United aliyenunuliwa kwa pauni milioni 52, Leny Yoro atakuwa nje kwa miezi mitatu na mshambuliaji Rasmus Hojlund atakosa wiki sita kutokana na majeraha aliyoyapata katika mchezo wa kujiandaa kwa amsimu wa Jumamosi dhidi ya Arsenal.

    Vyanzo vya habari vilithibitisha habari hiyo zaidi ya saa moja kabla ya United kupata ushindi wa 3-2 dhidi ya Real Betis ya La Liga mjini San Diego.

    Wote wawili walilazimishwa kutoka katika kipindi cha kwanza cha kichapo cha 2-1 kwenye Uwanja wa SoFi mjini Los Angeles.

    Yoro alirekodiwa katika video akiwa katika kambi ya mazoezi ya United katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA), siku ya Jumanne akiwa amevalia kiatu cha kujikinga na kutumia magongo.

    Unaweza pia kusoma

  11. Mazishi ya kiongozi wa Hamas yavutia umati mkubwa wa watu Iran

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelfu wamejitokeza kuhudhuria mazishi ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, nchini Iran ambaye aliuawa katika shambulizi mjini Tehran siku ya Jumatano.

    Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, anaongoza sala hiyo kabla ya kiongozi huyo kuzikwa nchini Qatar.

    Vyombo vya habari vya Marekani vimewanukuu maafisa wa Iran wakisema kiongozi huyo mkuu ameamuru shambulio la moja kwa moja dhidi ya Israel, na ndio chanzo cha shambulio lililotokea nchini Iran.

    Israel haijatoa maoni yoyote kuhusu mauaji hayo moja kwa moja.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema nchi yake imetekeleza "pigo kali" kwa maadui zake katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kamanda mkuu wa Hezbollah nchini Lebanon saa chache kabla ya shambulio la Tehran.

    Alionya Waisrael kwamba "bado kuna changamoto siku za usoni", huku hofu ya mzozo mkubwa katika Mashariki ya Kati ikiongezeka.

    "Tangu kutokea kwa shambulizi Beirut, tumesikia vitisho kutoka pande zote," alisema kwenye ujumbe uliopeperushwa kwenye Televisheni.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya dhidi ya "kuongezeka kwa hatari" kwa uhasama katika eneo hilo.

    Soma zaidi:

  12. Maduro aahidi kutoa data ya upigaji kura huku waangalizi wakisema uchaguzi wa Venezuela 'si wa kidemokrasia'

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesisitiza kuwa chama chake kiko tayari kuwasilisha majumuisho yote ya kura kutokana na uchaguzi wenye utata nchini humo baada ya waangalizi wa uchaguzi kusema kuwa "hauwezi kuchukuliwa kuwa wa kidemokrasia".

    Tamko la Baraza la Kitaifa la Uchaguzi (CNE) kwamba Bw Maduro alishinda limesababisha maandamano ya siku mbili, huku upinzani nchini humo ukisema kwamba hesabu za kura zinaonyesha mgombea wake, Edmundo González, alishinda kwa kura nyingi.

    Mashirika yasiyo ya kiserikali yanasema kumekuwa na vifo vya takriban watu 11 katika ghasia zinazohusiana na maandamano huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

    Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, Bw Maduro alisema tena kwamba sababu ya serikali yake kutochapisha matokeo ya uchaguzi ni "udukuzi" kwenye tovuti ya baraza la uchaguzi.

    Pia alidai alikuwa na "uthibitisho" kuwa kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado anahusika na "vurugu" zinazoshuhudiwa.

    Alidai kuwa waandamanaji walikuwa wanakiuka katiba na kuomba Mahakama ya Juu Zaidi kuchukua hatua, ambayo inaweza kusababisha kukamatwa kwa watu wengi wa upinzani au waandamanaji.

    Soma zaidi:

  13. CrowdStrike yashtakiwa na wanahisa wake kwa hitilifau ya kiufundi iliyotokea kote duniani

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kampuni ya CrowdStrike imeshitakiwa na wanahisa baada ya sasisho bovu la programu ya kampuni hiyo ya usalama wa mtandao kuharibu zaidi ya kompyuta milioni nane na kusababisha usumbufu wa kiufundi kote duniani .

    Kesi hiyo inashutumu kampuni hiyo kwa kutoa taarifa "za uwongo na za kupotosha" kuhusu majaribio yake ya programu.

    Pia inasema bei ya hisa ya kampuni ilishuka kwa 32% katika siku 12 baada ya tukio, na kusababisha hasara ya thamani ya $25bn (£14.5bn).

    CrowdStrike inakanusha madai hayo na inasema itajitetea dhidi ya kesi iliyopendekezwa dhidi yake.

    Kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya Austin, Texas, inadai kuwa wasimamizi wa CrowdStrike walilaghai wawekezaji kwa kuwafanya waamini kuwa masasisho ya programu ya kampuni yalijaribiwa vya kutosha.

    Kesi hiyo inatafuta kiasi ambacho hakijabainishwa cha fidia kwa wawekezaji waliokuwa na hisa za CrowdStrike kati ya tarehe 29 Novemba na 29 Julai.

    Inamtaja afisa mkuu mtendaji George Kurtz, ambaye alisema katika mkutano mnamo 5 Machi kwamba programu ya kampuni hiyo "imeidhinishwa, imejaribiwa na kuthibitishwa."

    CrowdStrike iliambia BBC News kwamba inapinga madai hayo.

    "Tunaamini kuwa kesi hii haina mashiko na tutatetea kampuni kwa nguvu," msemaji alisema.

  14. Chui ashambulia wanaume wawili katika kambi ya jeshi la wanahewa Afrika Kusini

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chui amewashambulia wanaume wawili katika kambi ya jeshi la wanahewa la Afrika Kusini ambalo linapakana na mbuga maarufu duniani ya Kruger National Park.

    Mmoja wa waliovamiwa ambaye ni mwanajeshi, alikuwa ameenda kukimbia.

    Mwingine, raia anayefanya kazi kwenye kituo hicho, alikutana na chui huyo akiwa anatembea, msemaji wa jeshi la wanahewa alisema.

    Wawili hao walilazwa hospitalini wakiwa na mikwaruzo lakini hawakuwa na majeraha makubwa, Brig Jenerali Donavan Chetty aliambia BBC.

    Mmoja ameruhusiwa kwenda nyumbani na mwingine anatarajiwa kuondoka siku ya Alhamisi.

    Siku ya Jumatano, chui huyo alichukuliwa na kuhamishwa hadi kwenye hifadhi karibu kilomita 100 (maili 62) kutoka kambi ya jeshi la wanahewa la Hoedspruit, kufuatia mashambulizi ya wiki iliyopita.

    Jenerali Chetty alisema kukutana na chui ni jambo la kawaida, lakini huwa sio hatari kwa wale wanaoishi na kufanya kazi karibu na mbuga hiyo.

    Mbuga hiyo, ambayo ni kitovu cha utalii kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori, imezungushiwa uzio.

    Hata hivyo, Jenerali Chetty alisema ni vigumu kuzuia chui, ambao wanajulikana kuwa wepesi wa kuruka uzio.

    Chui ni wanyama ambao huwa na shughuli nyingi nyakati za usiku hasa kutafuta mawindo mbalimbali, wakiwemo nyumbu, swara na samaki, tovuti ya Mbuga ya Kitaifa ya Kruger inasema.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Hezbollah yathibitisha kamanda wake alifariki katika shambulizi la Israel

    .

    Chanzo cha picha, Hezbollah handout

    Hezbollah imethibitisha kuwa mmoja wa makamanda wake wakuu wa kijeshi aliuawa katika shambulio la anga la Israel huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

    Siku ya Jumatano jioni, kundi linaloungwa mkono na Iran lilisema mwili wa Fuad Shukr ulipatikana kwenye vifusi vya jengo ambalo lilishambuliwa siku ya Jumanne.

    Watu wengine wanne waliuawa katika shambulizi hilo, wakiwemo watoto wawili. Awali, jeshi la Israel lilisema Shukr alikuwa akilengwa "kuuawa na ujasusi" .

    Israel iliongeza kuwa shambulizi hilo lilikuwa jibu kwa shambulio la roketi ambalo liliua watu 12 katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israel siku ya Jumamosi, ambayo Israel inasema kamanda huyo alisaidia katika masuala ya kupanga.

    Hezbollah imekanusha kuhusika na shambulizi hilo.

    Fuad Shukr, ambaye alikuwa na umri wa miaka sitini, anaaminika kuwa mshauri mkuu wa kijeshi wa kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.

    Shambulizi hilo lililenga jengo moja huko Haret Hreik, sehemu ya kitongoji cha Dahiyeh cha Beirut.

    Ni eneo lenye watu wengi. Dahiyeh yenyewe imezungukwa na vituo vya ukaguzi vya Hezbollah.

    Watoto waliouawa katika shambulizi hilo la anga ni mvulana wa miaka 10 na dada yake mwenye umri wa miaka sita.

    Shukr atazikwa siku ya Alhamisi, taarifa hiyo ilisema.

    Soma zaidi:

  16. Kijana, 17, ashtakiwa kwa mauaji ya wasichana watatu Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, Picha za Familia

    Kijana wa miaka 17 ameshtakiwa kwa mauaji ya wasichana watatu katika hafla ya kucheza densi huko Southport.

    Bebe King, 6, Elsie Dot Stancombe, 7, na Alice Dasilva Aguiar mwenye umri wa miaka tisa walifariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kisu kwenye hafla iliyopewa jina Taylor Swift katika mji wa Merseyside siku ya Jumatatu.

    Kijana huyo, ambaye anatazamiwa kufikishwa katika mahakama ya jiji la Liverpool baadaye Alhamisi, pia ameshtakiwa kwa makosa 10 ya kujaribu kuua.

    Watoto wengine wanane na watu wazima wawili waliokuwa kwenye hafla hiyo walijeruhiwa, huku baadhi yao wakiaminika kuwa bado katika hali mbaya.

    Mshitakiwa ambaye jina lake haliwezi kutajwa kwa sababu ya umri wake pia amefunguliwa shtaka la kumiliki kifaa chenye makali.

    Polisi wa Merseyside walitangaza mashtaka hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mara tu baada ya saa sita usiku.

    Soma zaidi:

  17. Watatu wanaotuhumiwa kupanga njama ya 9/11 wafikia makubaliano ya kukiri mashtaka - Pentagon

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanaume watatu kati ya wanaotuhumiwa kupanga mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 wameingia katika makubaliano ya kabla ya kesi, Idara ya Ulinzi ya Marekani imesema.

    Khalid Sheikh Mohammad, Walid Muhammad Salih Mubarak Bin Attash, na Mustafa Ahmed Adam al-Hawsawi wamezuiliwa katika kambi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani Guantanamo Bay, Cuba, kwa miaka mingi bila kufikishwa mahakamani.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, watu hao watakiri kuwa na hatia kwa makubaliano kuwa upande wa mashtaka ukubali kutoomba hukumu ya kifo.

    Masharti ya makubaliano hayo bado hayajatolewa.

    Takriban watu 3,000 huko New York, Virginia na Pennsylvania waliuawa katika mashambulizi ya al-Qaeda, ambayo yalisababisha "Vita dhidi ya Ugaidi" na uvamizi wa Afghanistan na Iraq.

    Mpango huo ulitangazwa kwa mara ya kwanza katika barua iliyotumwa na waendesha mashtaka kwa familia ya waathiriwa, kulingana na The New York Times.

    Hili lilikuwa shambulio baya zaidi kwenye ardhi ya Marekani tangu shambulio la mwaka 1941 la Japani kwenye Bandari ya Pearl, Hawaii, ambapo watu 2,400 waliuawa.

    “Kwa makubaliano ya kuondolewa kwa adhabu ya kifo kama adhabu inayowezekana kutolewa, washtakiwa hawa watatu wamekubali kukiri makosa yote yaliyokuwa yakishitakiwa likiwemo la mauaji ya watu 2,976 waliotajwa kwenye hati ya mashtaka,” ilisema barua hiyo kutoka kwa mwendesha mashtaka mkuu, Admiral Aaron Rugh.

    Watu hao wametuhumiwa kwa msururu wa mashtaka, ikiwa ni pamoja na kushambulia raia, mauaji kinyume na sheria za vita, utekaji nyara na ugaidi.

    Wanatarajiwa kuwasilisha maombi yao rasmi mahakamani mapema wiki ijayo, gazeti la Times liliripoti.

    Soma zaidi:

  18. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 01/08/2024