Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump athibitisha rasmi kuishtaki BBC

Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Rais ya Air Force One Ijumaa jioni, Trump alisema: “Tutawashtaki kwa chochote kati ya dola bilioni 1 hadi 5, pengine wiki ijayo.”

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Iran yaikamata meli ya mafuta katika mlango bahari wa Hormuz

    Jeshi la Iran (IRGC) limethibitisha kuikamata meli ya mafuta jana Ijumaa katika mlango bahari wa Hormuz.

    Meli ya mafuta ya Talara, iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Visiwa vya Marshall ilikuwa ikisafiri kutoka Falme za Kiarabu (UAE) kwenda Singapore.

    IRGC lilisema iligundulika kuwa meli hiyo "inakiuka sheria kwa kubeba mizigo isiyoruhusiwa", lakini haikutoa maelezo zaidi kuhusu ukiukaji huo.

    Ripoti zinaonyesha kuwa ilikuwa ikibeba kwa wingi gesi ya salfa.

    Iran mara kwa mara imekuwa ikikamata meli za mafuta na meli za mizigo zinazosafiri ndani na karibu na Ghuba yake, ambayo ni njia muhimu ya dunia kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa.

    Mara nyingi imetaja ukiukwaji wa safari za baharini kama vile biashara za magendo au haramu.

  2. Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha ujumbe wa kuchunguza ukweli kuhusu mauaji ya Sudan

    Wajumbe wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa wamepitisha azimio la ujumbe huru wa kuchunguza ukweli kuhusu mauaji ya halaiki yaliyoripotiwa huko Al-Fashir, Sudan.

    Katika kikao maalum cha baraza huko Geneva kuhusu hali ya jiji la Darfur ambalo lilidhibitiwa kijeshi mnamo Oktoba, hatua hiyo ilipitishwa bila kura ikiwa ni ishara ya kuungwa mkono kimataifa.

    Jopo hilo pia litachunguza na kutambua wahusika wa ukiukwaji unaodaiwa kutekelezwa na vikosi vya Rapid Support Forces na washirika wao huko Al-Fashir.

    Balozi wa ujumbe wa kudumu wa Uingereza huko Geneva alisema ujumbe wa kutafuta ukweli utaandika na kuhifadhi ushahidi wa ukiukwaji huo, ambao utaweka msingi wa haki na uwajibikaji wa siku zijazo.

    Katika hotuba ya ufunguzi kwa wajumbe, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa alihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

    RSF imekanusha kuwalenga raia au kuzuia misaada, ikisema vitendo hivyo vinatekelezwa na makundi ya wahalifu.

    Soma Zaidi:

  3. Maaskofu wakatoliki Marekani walaani utekelezaji wa sera ya uhamiaji ya Trump

    Mkutano wa maaskofu wakatoliki wa Marekani umelaani msako mkali uliotekelezwa na idara ya uhamiaji nchini ambao rais wa Marekani Donald Trump anatetea kwa kile alichokiita "mageuzi ya msingi ya uhamiaji."

    "Tunasumbuliwa na vitisho dhidi ya utakatifu wa nyumba za ibada na hali maalum ya hospitali na shule," maaskofu walisema katika ujumbe maalum, wa kwanza wa aina yake katika kipindi cha miaka 12.

    Idara ya usalama wa ndani, ambayo inasimamia shughuli za uhamiaji, haikutoa maoni yoyote kuhusu hili.

    Ujumbe huo unarejelea ukosoaji kama huo uliotolewa na Papa Leo, ambaye ametoa wito wa "tafakari ya kina" kuhusu namna wahamiaji wanavyotendewa nchini Marekani chini ya utawala wa Trump.

    Utawala wa Trump umeendeleza ajenda kali ya uhamiaji tangu alipoingia madarakani mapema mwaka huu.

    Trump amefuta sera ambayo inaweka kikomo cha kukamatwa kwa wahamiaji karibu na maeneo nyeti, ikiwa ni pamoja na makanisa, hospitali na shule, na kupeleka maafisa wa shirikisho kote Marekani ili kuimarisha zoezi la ukamataji huko.

    Katika ujumbe wao, maaskofu walionyesha wasiwasi kuhusu kile walichokielezea kama "hali ya hofu na wasiwasi kuhusu maswali ya utambulisho" na utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

    Walisema wamesikitishwa na mjadala na kashfa za wahamiaji, na wanapinga "kuhamishwa kwa watu wengi bila ubaguzi."

  4. Maandamano Tanzania: Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wawajibike, yasema TEC

    Baraza la maaskofu wa Kanisa katoliki nchini Tanzania limetaka mamlaka zinazohusika ziendelee kulaani mauaji yaliyofanyika na kukiri waliouawa ni watanzania.

    Rais wa baraza la maaskofu, Wolfgang Pisa akisoma tamko hilo kuhusu maandamano yaliyoshuhudiwa hivi karibuni, amesema Kuuawa kwa watu hovyo, ukosefu wa demokrasia ni miongoni mwa sababu za watu kuandamana.

    “Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wawajibike, au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi. Hasira ya Wananchi ipo katika kuona hakuna anayewajibika kwa matendo maovu waliyofanyiwa raia”. Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa TEC.

    Amesema kwakuwa jambo hilo limesababisha maafa, baraza linashauri ufanyike uchunguzi utakaowashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi likipendeza wadau kutoka tume huru isiyofungamana na upande wowote kama jumuiya na taasisi za kimataifa,dini na asasi za kiraia na wataalamu wa haki na mambo ya kidemokrasia na serikali iwe tayari kupokea na kufanyia kazi ripoti watakayotoa.

    Hapo jana akizungumza na BBC John Heche makamo mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA alisema “Tunahitaji tume huru,kutoka Umoja wa mataifa au Umoja wa Afrika au SADC lakini kwanza tunataka kujua idadi ya watu waliouawa, majeruhi na baadhi ambao hawajulikani walipo’’.

    Akihutubia bunge, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitangaza kuwa serikali imeunda tume maalumu kuchunguza matukio yaliyotokea wakati wa maandamano hayo.

    "Serikali imechukua hatua ya kuunda tume itakayochunguza kwa undani kilichotokea ili tujue kiini cha tatizo. Taarifa ya tume hiyo itatuongoza katika mazungumzo ya kuleta maridhiano na kudumisha amani," alisema.

    Aidha alitangaza msamaha kwa vijana waliokamatwa kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyofanyika kuanzia siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025.

    Soma Zaidi:

  5. Homa ya kutokwa damu yaua sita Ethiopia

    Wizara ya Afya nchini Ethiopia imethibitisha kwamba mlipuko wa hivi karibuni wa homa ya kutokwa na damu ambayo uliosababisha vifo vya watu sita katika eneo la kusini mwa nchi, unasababishwa na virusi vya Marburg.

    Taarifa hiyo imefafanua kwamba aina ya virusi waliyoigundua inafanana na ile iliyoripotiwa hapo awali katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

    Mgonjwa wa kwanza kuripotiwa katika mlipuko huu alianza kwa kupata homa kali, akafuatiwa na kutokwa damu na kushindwa kwa viungo mwilini ndani ya muda mfupi.

    Baadhi ya wahudumu wa afya na wanajamii waliokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mgonjwa huyo pia waliambukizwa.

    Kufikia sasa, watu takribani tisa wanakadiriwa kuwa wameambukizwa virusi hivyo.

    Huu ni mlipuko wa kwanza wa Marburg kuwahi kuripotiwa nchini Ethiopia.

    Ethiopia imesema kuwa timu maalumu za kukabiliana na hali ya dharura zimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini humo ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

  6. Trump apunguza ushuru wa bidhaa 200 za vyakula huku wasiwasi wa mfumuko wa bei ukiongezeka

    Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa ushuru wa bidhaa zaidi ya 200 za chakula, ikiwa ni pamoja na vyakula vikuu kama vile kahawa, nyama ya ng'ombe, ndizi na sharubati ya machungwa, huku wasiwasi ukiongezeka miongoni mwa watumiaji nchini Marekani kuhusu gharama kubwa ya mahitaji hayo muhimu.

    Msamaha huo mpya ambao ulianza kutekelezwa usiku wa Alhamisi unaashiria mabadiliko makubwa kwa Trump, ambaye kwa muda mrefu amesisitiza kwamba ushuru mkubwa wa uagizaji bidhaa alioweka mapema mwaka huu hautachochea mfumuko wa bei.

    Aidha Trump alisisitiza kwamba kwa ujumla, Marekani "haina mfumuko wowote wa bei."

    Katika hatua nyingine wabunge wa democrats wameshinda katika uchaguzi wa majimbo na mitaa huko Virginia, New Jersey na New York City, ambapo wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa wapiga kura kuhusu gharama za maisha, ikiwa ni pamoja na bei kubwa za chakula, ikiwa miongoni mwa agenda muhimu.

    Trump pia aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya rais Air Force One kwamba angeendelea na malipo ya $2,000 kwa Wamarekani wenye kipato cha chini na cha kati ambayo yangefadhiliwa na mapato ya ushuru mwaka ujao.

    "Ushuru huo unaturuhusu kutoa gawio ikiwa tunataka kufanya hivyo. Sasa tutafanya gawio na pia tunapunguza deni," alisema.

  7. Dar-es Salaam na Dodoma kuwa na treni za kisasa

    Serikali ya Tanzania inapanga kuanzisha treni za kisasa za mijini katika Dar es Salaam na Dodoma, hatua inayolenga kupunguza msongamano na kuboresha usafiri wa umma katika miji hiyo mikubwa.

    Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo unazingatia ongezeko la kasi la wakazi, hasa jijini Dar es Salaam ambalo linatarajiwa kufikia takriban milioni 10 ifikapo mwaka 2030.

    Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bunge jijini Dodoma Novemba 14, 2025, Rais Samia alisema mipango ya usafiri wa mijini inaenda sambamba na ujenzi na ukamilishaji wa njia kuu za reli katika nchi nzima.

    Alisema Serikali inaendelea kukamilisha vipande vilivyosalia vya reli ya kisasa ya SGR katika ushoroba wa kati, ikiwemo Makutupora–Tabora, Tabora–Isaka, Isaka–Mwanza na Tabora–Kigoma. Ujenzi wa reli ya Uvinza–Musongati kuelekea Burundi pia utaendelezwa.

    Serikali imepanga kuanzisha miradi mipya ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma, na reli nyingine kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay inayogusa maeneo ya Mchuchuma na Liganga.

    Kwa upande wa reli zilizopo, Serikali inatekeleza maboresho ya TAZARA ambayo yanatarajiwa kuanza kupitia uwekaji wa jiwe la msingi nchini Zambia. Reli ya zamani ya Meter Gauge (MGR) itafanyiwa ukarabati katika vipande vya Tabora–Kigoma, Kaliua–Mpanda, Tanga–Arusha na Ruvu–Mruazi.

    Rais Samia alisema sekta binafsi itashirikishwa katika uendeshaji wa baadhi ya reli, hatua itakayoanza na kuingizwa kwa mwendeshaji binafsi kwenye reli ya TAZARA ili kupunguza gharama za usafirishaji.

    Katika sekta ya anga, Serikali imepanga kuongeza ndege nane kufikia mwaka 2030 ili kukuza uwezo wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kupanua safari za ndani na nje ya nchi. Aidha, Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kinapangwa kuwa kitovu cha safari za kimataifa.

    Ujenzi wa viwanja vya ndege vya Msalato, Mwanza, Iringa na Mpanda unaendelea kama sehemu ya mpango wa kufungua nchi na kuimarisha miundombinu ya uchumi.

  8. Trump athibitisha rasmi kuishtaki BBC

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema atachukua hatua za kisheria dhidi ya BBC kufuatia jinsi hotuba yake ilivyohaririwa na kipindi cha Panorama, baada ya shirika hilo kuomba msamaha lakini kukataa kumlipa fidia.

    Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya Air Force One Ijumaa jioni, Trump alisema: “Tutawashtaki kwa chochote kati ya dola bilioni 1 hadi 5, pengine wiki ijayo.”

    BBC imesema uhariri wa hotuba ya tarehe 6 Januari 2021 ulipelekea “taswira isiyo sahihi kwamba Rais Trump alitoa wito wa moja kwa moja wa kuchochea vurugu.” Ingawa shirika hilo liliomba msamaha, limesisitiza halitalipa fidia ya kifedha.

    Sakata hilo limesababisha kujiuzulu kwa Mkurugenzi Mkuu wa BBC Tim Davie na Mkuu wa Habari Deborah Turness.

    Trump aliwaambia waandishi kuwa anaamini hana budi kuwashtaki: “Walidanganya. Walibadilisha maneno yaliyotoka mdomoni mwangu.”

    Alisema hakuzungumzia suala hilo na Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, lakini Starmer ameomba kuzungumza naye, na atampigia simu mwishoni mwa wiki.

    Mapema wiki hii, mawakili wa Trump walitishia kuishtaki BBC kwa fidia ya dola bilioni 1 iwapo haitatoa ufafanuzi wa wazi, kuomba msamaha rasmi na kumlipa fidia.