Tanzania yaanza mashauriano kukwepa marufuku ya raia wake kuingia Marekani

Muda wa kusoma: Dakika 3

Serikali ya Tanzania imethibitisha kuwa imeanza mashauriano rasmi na Serikali ya Marekani kuhusu masuala ya uhamiaji ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa raia wa Tanzania kuingia nchini humo.

Hilo linafuatia taarifa za hivi karibuni kuwa Marekani inapanga kuongeza orodha ya mataifa yaliyopigwa marufuku ya raia wake kuingia nchini humo, ikiwemo Tanzania.

Akizungumza kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema Tanzania imepata taarifa hiyo na tayari imeanza mazungumzo ya kidiplomasia ili kufahamu kikamilifu maeneo ambayo yanapaswa kurekebishwa.

"Serikali imeona Tangazo la Serikali ya Marekani la kutaka kufanyiwa kazi kwa mambo kadhaa ya kiuhamiaji ambayo yanaweza kusababisha raia wa Tanzania kuzuiwa kuingia Marekani', inasema taarifa ya Msigwa na kuongeza kuwa

"Tayari Serikali ya tanzania kupitia Wizara ya mambo ya nje imeanza kufanya mashauriano nna wenzetu wa upande wa Marekani kujua maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa maboresho hususani yanayohusiana na masuala ya kikonselu ili kuharakisha Tanzania isiwe moja ya nchi ambazo raia wake watazuiwa kuingia Marekani:.

Mashauriano hayo ya masuala ya kikonseli pamoja na mambo mengine yanagusa utoaji wa nyaraka halali za utambulisho na kushirikiana katika masuala ya uhamiaji.

Marekani inataka Tanzania na nchi nyingine kurekebisha masuala haya vinginevyo raia wake watapigwa marufuku kuingia Marekani. Hilo likitokea litawaathiri kuazia wafanyabiashara, wanafunzi na wengine wanaokwenda kwa shughuli mbalimbali.

Mapema wiki hii, vyombo vya habari mbalimbali vya Marekani viliripoti kuwa serikali ya Rais Donald Trump kupitia Wizara ya Mambo ya Nje chini ya Waziri Marco Rubio, inaweza kuongeza mataifa 36 kwenye orodha ya nchi zinazoweza kuingia kwenye marufuku ya raia wake kusafiri kuingia Marekani.

Orodha hiyo ina jumla ya mataifa 25 kutoka Afrika, na mengine kutoka Karibiani, Asia ya Kati na Visiwa vya Pasifiki. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizotajwa. Baadhi ya nchi nyingine kutoka Kusini mwa jangwa la Sahara ni pamoja na Uganda, DRC, Ethiopia, Sudan Kusini, Djibout, Zambia, Zimbabwe, Malawi na Angola.

Kwa mujibu wa taarifa, nchi hizo zimetakiwa ndani ya siku 60 kuwasilisha mipango ya kukidhi vigezo vipya vilivyowekwa na Marekani, ikiwemo uthibitisho wa serikali madhubuti, utoaji wa nyaraka za kuaminika, na kushughulikia visa vya watu wanaoingia Marekani kisha kusalia huko bila vibali halali.

Sababu nyingine zilizotajwa na Marekani ni pamoja na nchi zinazotoa uraia kwa wawekezaji bila masharti ya kuishi nchini humo, pamoja na madai ya matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi na Marekani yanayofanywa na raia wa mataifa hayo wakiwa Marekani.

Hata hivyo Serikali ya Marekani haijaweka wazi lini marufuku hizo mpya zitaanza kutekelezwa, lakini nchi zilizotajwa zimepewa muda kuwasilisha mpango wa awali wa utekelezaji wa masharti hayo.

Kwa sasa, Serikali ya Tanzania inasisitiza kuwa iko tayari kushirikiana na Marekani ili kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha haki za Watanzania zinalindwa katika safari za kimataifa, ikiwemo kuingia Marekani

Katika kipindi cha awamu yake ya kwanza ya urais, Rais Trump aliweka marufuku ya safari kwa mataifa yenye waislamu wengi, hatua ambayo ilizua mjadala mkali na kupingwa mahakamani kabla ya Mahakama ya Juu kuiruhusu katika toleo lake la tatu mwaka 2018.

Marufuku hiyo ilifutwa na Rais Joe Biden, lakini Trump ambaye amekuwa akishughulikia kwa ukubwa wake masuala ya uhamiaji, ameahidi kuirejesha tena akiwa madarakani kwa awamu ya pili, akisema, "itakuwa kubwa zaidi ya mwanzo".