Raila Odinga kuzikwa Jumapili Bondo magharibi mwa Kenya

Kulingana na familia yake, Bw. Odinga aliomba kuzikwa ndani ya muda mfupi iwezekanavyo, ndani ya saa 72.

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah, Asha Juma, Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Habari za hivi punde, Kenya yatoa ratiba ya mazishi ya Raila Odinga

    .

    Chanzo cha picha, Mitandao ya Kijamii

    Kamati ya Kitaifa inayoandaa Mazishi ya Kitaifa ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga imetangaza kwamba mazishi yake yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, magharibi mwa Kenya.

    Naibu Rais Kithure Kindiki, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo pamoja na kakake mkubwa wa Bw. Odinga Dkt Oburu Oginga, ametoa tangazo hilo katika hotuba ya kitaifa muda mfupi uliopita.

    Kulingana na familia hiyo, Bw. Odinga aliomba kuzikwa ndani ya muda mfupi iwezekanavyo, ndani ya saa 72.

    "Tumeamua kuharakisha mchakato wa maandalizi ya mazishi ya Odinga kwa kusawazisha matakwa ya Odinga, matakwa ya familia, jamii, na masharti mengine ambayo lazima izingatiwe," kamati hiyo ilisema.

    Mwili wa Raila Amolo Odinga unatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi kutoka India.

    Kutoka uwanjani JKIA, mwili utapelekwa moja kwa moja katika makafani ya Lee na baadaye kupelekwa katika Bunge la kitaifa ambapo Wakenya watapata furda ya kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa sita mchana.

    Baadaye, mwili utarudishwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee Funeral Home kwa maandalizi ya mwisho.

    Ijumaa, ibada ya kitaifa ya mazishi itafanyika katika Uwanja wa Nyayo.

    Viongozi kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo, ambayo itasimamiwa kama ibada rasmi ya kitaifa.

    Jioni ya siku hiyo, mwili utafikishwa nyumbani kwake Karen ambapo utalazwa kwa mara ya mwisho.

    Jumamosi, mwili utasafirishwa hadi Uwanja wa Moi, Kisumu, ambapo wananchi wataruhusiwa kuuaga kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.

    Kutoka hapo, msafara wa mazishi utaelekea kwa barabara hadi Siaya. Maziko yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo.

    Maelezo zaidi:

  2. Habari za hivi punde, Mwili wa Raila Odinga kusafirishwa Mumbai

    Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, unatarajiwa kusafirishwa hadi Mumbai kwa ndege iliyopangwa kuondoka saa nne usiku kutoka Kochi.

    Mwili huo utasafirishwa hadi Kenya kutoka Mumbai, kulingana na P Sreekumar, katibu wa kibinafsi wa Gavana wa jimbo la Kerala Rajendra Vishwanath Arlekar.

    Gavana Arlekar alitoa heshima zake kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya katika uwanja wa ndege wa Kochi na kuweka shada la maua kwenye jeneza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

    Bw Modi alimtaja Bw Odinga kama ``rafiki mkubwa wa India.''

    Katika salamu za rambirambi, Gavana Arlekar alisema: ``Nimehuzunishwa sana na kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Bw Raila Odinga. Alikuwa mwanasiasa mkubwa na rafiki wa mpendwa wa India. Natoa rambirambi zangu za dhati kwa familia yake na watu wa Kenya.''

  3. Tunachokijua kufikia sasa kuhusu usafirishaji wa mwili wa Raila Odinga kutoka India hadi Kenya

    Baadhi ya wanachama wa kamati ya mazishi iliyoteuliwa na Rais Ruto wanaelekea Mumbai kisha wafululilize hadi Kerala kuchukua mwili wa Raila Odinga ambao tayari umewekwa kwa jeneza.

    Wakiongozwa na mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi watakabidhiwa mwili huo ulioko hospitali ya Devamatha mji wa Koothattukulam eneo la Kerala na serikali ya India kisha warudi Mumbai na kuuleta jijini Nairobi.

    Wakenya wataruhusiwa kuomboleza kwa kuangalia mwili kama njia ya kumpa heshima ya mwisho hapo kesho mwili ukifika.

    Kwasasa shughuli za kutayarisha mwili zinaendelea Kerala wakisubiri ujumbe wa Kenya kufika.

    Balozi wa Kenya huko India Peter Munyeri na gavana wa Kerala watakuwa wakilaki ujumbe huo kutoka Kenya.

    Mwili wa Raila Odinga utafika Mumbai saa nane usiku huu.

    Haya yanajiri huku Naibu Rais Kithure Kindiki akiongoza kamati ya mazishi kupanga ratiba.

    Rais Ruto ametangaza kuwa Raila Odinga atapatiwa mazishi ya kitaifa.

    Hivi sasa uwanja wa Nyayo unatayarishwa ili hafla nzima ifanyike hapo haya ni kwa mujibu wa Rais Ruto .

    Soma pia:

  4. Mashabiki wa Arsenal Kenya wamuomboleza Odinga

    G

    Chanzo cha picha, Raila/X

    Wakenya wanaendelea kukumbuka maisha ya kinara wa Odm Raila Odinga ambaye hakuwa mwanasiasa tu bali pia shabiki shakiki wa timu ya Uingereza ya Arsenal.

    Kifo chake kimewapa huzuni mashabiki wa spoti hasa wale walioshabikia timu ya Wanabunduki.

    Raila Odinga hakujulikana tu kwa siasa zake zenye msimamo dhabiti bali pia kwa mapenzi yake ya dhati kwa soka.

    Alikuwa kinara na shabiki wa Gor Mahia, mabingwa mara 21 wa Ligi kuu ya kandanda nchini Kenya, klabu ambayo aliifuatilia si kwa sababu ya umaarufu wake, bali kwa sababu ilikuwa sehemu ya maisha ya watu wa kawaida aliowatetea kila siku.

    Lakini zaidi ya hapo, Raila alikuwa mfuasi wa kweli wa Arsenal.

    Wakati mashabiki wengi waligeuka au kukata tamaa, Raila alibaki imara akiitazama kila msimu kwa matumaini makubwa.

    Kwa zaidi ya miongo mitatu, aliitaja Arsenal kwa upendo katika mazungumzo yake binafsi na hata katika mijadala mikubwa.

    Aliamini, kama alivyofanya katika siasa, kwamba ushindi wa kweli unahitaji muda, uvumilivu na imani isiyotikisika.

    Soka kwake haikuwa burudani ya jioni au sehemu ya hadithi nzuri.

    Lilikuwa darasa la kushindwa kwa heshima, la kuamka baada ya kuanguka, na la kushikilia matumaini hata pale ambapo hakuna anayeyaona.

    Baada ya kifo chake, mashabiki waliandika kwa uchungu: “Raila Odinga apumzika baada ya kungoja miaka 80 kuona Arsenal ikitwaa UCL,” aliandika mmoja.

    Mwingine akaandika: “Amefariki kabla hajaiona ndoto yake ikitimia. Arsenal inapaswa kumheshimu. Raila hakuwa shabiki wa kawaida.”

    Raila aliishi maisha ya kusubiri mabadiliko

    Si tu kwenye siasa, bali pia kwenye uwanja wa soka.

    Alijua kuwa si kila ndoto hutimia maishani, lakini aliendelea kuamini. Na kwa hilo, aliwaunganisha watu si kwa maneno, bali kwa msimamo na moyo wake.

    Katika historia ya Raila Odinga, soka halitakuwa kipengele cha kusahaulika. Itakuwa ni ushahidi wa namna alivyoweza kuishi kwa imani, mpaka mwisho.

    Raila aliwahi kuonekana akivalia jezi za Arsenali na hata kusafiri Uingereza kutazama mechi Uwanjani Emirates. Aliwahi kuwa shabiki wa Man Utd kabla ya kutosa timu hiyo na kuwa shabiki wa wanabunduki.

    Soma pia:

    G

    Chanzo cha picha, Raila/FB

  5. 'Tumempoteza kigogo wa Afrika'- Bobi Wine

    g

    Chanzo cha picha, Bobi Wine/X

    Kiongozi wa Chama cha Nationa Unity Platform(NUP) nchini Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu kama Bobi Wine amemsifia Odinga kama kiongozi ambaye kwa miongo kadhaa aliendelea kuwa sauti ya matumaini kwa waliodhulumiwa,

    Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Bobi Wine alisema: “Tumepokea kwa huzuni kuu taarifa za kifo cha Mheshimiwa Raila Odinga. Alikuwa nguzo ya mapambano ya haki na uhuru. Alinyanyaswa, alifungwa, lakini hakuwahi kunyamaza. Raila alibeba ndoto za wengi waliotaka kuona Afrika inayosimamia utu wa watu wake.”

    Bobi Wine alimwelezea Raila si tu kama mwanasiasa, bali kama mshumaa uliowaka katikati ya giza la ukandamizaji, akiwaka kwa ajili ya wengine hata alipochomeka mwenyewe.

    “Tumempoteza mtu ambaye hakuwahi kuchoka kusimama upande wa wanyonge. Alipigana hadi pumzi yake ya mwisho, si kwa faida yake binafsi, bali kwa vizazi vya Afrika ambavyo bado vinapigania nafasi ya kupumua kwa uhuru,” aliandika.

    Katika salamu zake za pole, Bobi Wine alielekeza rambirambi zake kwa familia ya Raila, kwa Mama Ida Odinga, na kwa watu wa Kenya waliompenda na kumwamini kwa miaka mingi.

    Pia aliwaenzi wale wote wanaoendelea kupigania haki katika mazingira magumu, akisema kuwa maisha ya Raila ni ushuhuda kwamba mapambano haya yana maana.

    “Pumzika kwa amani Baba wa Mapambano. Afrika haiwezi kukusahau.” Bobi alihitimisha.

    Soma pia:

  6. Tunachojua kuhusu tiba ya asili ya Aryuveda

    Serikali ya jimbo ilianza kuweka Kerala kama kituo cha afya miongo kadhaa iliyopita

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Serikali ya India ilianza kuweka Kerala kama kituo cha afya miongo kadhaa iliyopita

    Galacha wa siasa Raila Odinga amefariki dunia akipokea matibabu ya kiasili ya India yanayofahamaika kama Aryuveda mjini Kerala.

    Awali familia yake ilikuwa imewahakikishia Wakenya kwamba alikuwa akipata nafuu, licha ya uvumi kuenea kuhusu afya yake kuzorota.

    Mapema ya siku ya Jumatano tarehe 15 Oktoba 2025 Odinga alipatwa na mshtuko wa moyo na kuanguka alipokuwa akitembea katika bustani ya hospitali hiyo na baadaye kutangazwa ameaga dunia.

    Lakini tiba ya asili ya India ya Aryuveda ina husu nini?

    Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, anafahamika kwa mapenzi yake ya dhati kwa yoga, lakini serikali yake pia imejitolea kukuza mila nyingine za kiafya zenye mizizi ya kihistoria na kiutamaduni.

    Mojawapo ya mila hizo ni Ayurveda – mfumo wa tiba wa kihistoria unaotegemea mimea, lishe, na tiba ya kukandwa (massage).

    Ayurveda imetumika nchini India kwa karne nyingi na ina mizizi imara katika maandiko ya kale ya Kitahindi yanayozingatia usawa kati ya mwili, akili na mazingira.

    Katika jimbo la Kerala, Ayurveda si tu sehemu ya urithi wa kitamaduni, bali pia ni sekta inayochangia kwa kiasi kikubwa kiuchumi kupitia huduma za afya na utalii wa tiba.

    Mfumo huu unasisitiza tiba ya kinga zaidi ya matibabu ya baadae, na unaendelea kutumika na watu wengi kama mbadala au nyongeza ya matibabu ya kisasa.

    Ayurveda inasalia kuwa miongoni mwa mifumo ya afya ya jadi inayoenziwa sana nchini India hadi leo.

    Kulingana na waziri mkuu wa India Nahendra Modi akimuomboleza Odinga ametaja kuwa familia ya Odinga imekuwa ikienzi tiba asiili ya Aryuveda kutokana na ufanisi wake katika matibabu ya binti yao aliyepata nafuu kwa kufuata miko yake.

    Soma pia:

  7. Rais Tinubu afariji wakenya baada ya kifo cha Odinga

    Rais Tinubu

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Rais Tinubu

    Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Kenya kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Raila Amolo Odinga.

    Katika ujumbe wake, Rais Tinubu amesema anaungana na Wakenya wote katika huzuni kubwa kufuatia kuondokewa na kiongozi ambaye alikuwa na nafasi ya kipekee si tu katika historia ya Kenya, bali pia barani Afrika.

    “Raila Odinga alikuwa zaidi ya mwanasiasa, alikuwa sauti ya matumaini, aliyeamini kwa moyo wake wote katika demokrasia, haki na mshikamano wa watu. Mchango wake katika kupigania mageuzi ya kweli na katika kujenga taasisi imara za taifa lake hautasahaulika kamwe,” asema Rais Tinubu.

    Rais Tinubu pia alimtambua Raila kama mtetezi wa kweli wa Pan-Afrikanism aliyesimamia kwa udhati umoja wa bara, utawala jumuishi na ushirikiano wa kanda mbalimbali.

    ' Na iwe kumbukumbu ya Raila Odinga iendelee kuwa mwanga unaoiongoza Kenya kuelekea amani, umoja, na maendeleo ya kudumu,'' alihitimisha Rais Tinubu.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Kikao cha bunge la taifa la Kenya chaahirishwa

    Picha ya bunge la taifa

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kufuatia tangazo la Rais Ruto kuhusu ratiba ya baada ya kifo cha Raila Odinga, Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula ameaihirisha kikao cha leo.

    Wabunge walionekana kugubikwa na simanzi na wengine kuagua vilio baada ya kupokea taarifa za kufariki kwa mwanasiasa huyo wa upinzani huku wakitakiwa kurejea bungeni kesho saa nane.

    Kwa mujibu wa spika Wetangula muda wa kikao cha kesho utaongezwa ili kuwapa nafasi wabunge kutoa risala zao za rambirambi.

    ''Kikao cha kesho kitaendelea hadi usiku ili kipatie kila mbunge kumuenzi Raila''

    Haya yanajiri baada ya Rais Ruto kutangaza siku saba za maombolezo Kenya nzima na kuzitaka balozi zote na afisi za umma zipeperushe bendera nusu mlingoti.

    Soma pia:

  9. Rais Ramaphosa amuomboleza Raila Odinga

    Cyril Ramaphosa

    Chanzo cha picha, Reuters

    Baada ya kutangazwa rasmi kufariki kwa galacha wa siasa Raila Odinga, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa risala za rambirambi kwa Kenya.

    Akiwa ni kiongozi wa hivi punde kumuomboleza Odinga Rais Ramaphosa alisema: “Taifa la Kenya na bara letu limempoteza kiongozi mzalendo na asiye na ubinafsi ambaye nilimfahamu na kufanya naye kazi kama rafiki na ndugu.''

    Kupitia taarifa aliyetuma kwa vyombo vya habari kiongozi huyo wa Afrika Kusini amemsifia Raila kuwa alihakikisha bara la Afrika lina usalama kutokan na nyadhifa alizokuwa nazo.

    “Raila Odinga alijitolea kuendeleza taifa lake na pia ustawi na kunyamazisha bunduki katika bara letu, kama inavyothibitishwa na uteuzi wake na Muungano wa Afrika kuendeleza amani nchini Côte d’Ivoire mwaka wa 2010.''

    Aidha Ramaphosa amemtaja Raila kama kiongozi aliyejitolea na kuweka masilahi ya nchi na bara lake kwanza.

    Soma pia:

  10. Habari za hivi punde, Rais William Ruto atangaza maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya Raila Odinga

    Rais Ruto akihutubia taifa la Kenya

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Kenya

    Maelezo ya picha, Rais Ruto akihutubia taifa la Kenya

    Rais William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga.

    Katika kipindi hiki, bendera zote za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya heshima na maombolezo.

    Aidha, Rais Ruto ametangaza kusitisha shughuli zake zote za umma na kuwasihi maafisa wengine wa serikali kuchukua hatua kama hiyo ili kutoa nafasi ya kutafakari na kuomboleza maisha ya kiongozi huyo mashuhuri.

    Kwa ajili ya maandalizi ya mazishi ya kitaifa, Rais ametangaza kuundwa kwa kamati maalum ya kushughulikia shughuli hizo, itakayokuwa chini ya uongozi wa Naibu Rais Kithure Kindiki.

    Serikali ya India, kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Kenya, imeahidi kugharamia na kuratibu shughuli za kusafirisha mwili wa marehemu kutoka India hadi Kenya kwa ajili ya mazishi.

    Wakati huo huo, ujumbe wa viongozi wakuu wa serikali, ukiongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Mheshimiwa Musalia Mudavadi, unaondoka nchini Kenya kuelekea India haraka iwezekanavyo ili kushughulikia mipango ya mwisho ya usafirishaji wa mwili wa marehemu.

    Rais Ruto amemsifu marehemu Raila Odinga kama mtu asiye na tamaa ya makuu, mpenda amani, na mzalendo wa kweli.

    “Raila alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyejitolea kwa dhati kwa ajili ya taifa hili. Alisimamia haki, usawa na amani. Ni shujaa ambaye historia haitamsahau,” alisema Rais Ruto.

    Mazishi ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika katika siku zijazo, huku taifa likiendelea kuomboleza mmoja wa viongozi wake wakuu waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya demokrasia na haki za Wakenya.

    Viongozi wa serikali ya Kenya wakisikiliza hotuba ya Rais

    Chanzo cha picha, Statehouse

    Maelezo ya picha, Viongozi wa serikali ya Kenya wakisikiliza hotuba ya Rais
    Kifo cha Kinara Raila Odinga chashtua wabunge wa Kenya

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Kenya

    Maelezo ya picha, Kifo cha Kinara Raila Odinga chashtua wabunge wa Kenya
  11. Rigathi Gachagua amtaja Raila kama nguzo ya demokrasia nchini Kenya

    g

    Chanzo cha picha, Rigathi/X

    Kinara wa chama cha DCP nchini Kenya Rigathi Gachagua amemuomboleza Odinga kama mtu aliye na heshima kubwa nchini Kenya na Kimataifa.

    Akiungana na wakeya wote kuombolezamkifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Raila Odinga kupitia ujumbe wake katika mtandao wa kijamii wa X alimtaja kama ''baba wa demokrasia'' na shujaa shupavu wa ukombozi wa pili wa taifa.

    Amemkumbuka Raila alivyojitoa kupigania utawala wa kidemokrasia licha ya kupitia mateso ya kifungo,utesaji nakuwekwa kizuizini mara kadhaa.

    ''Pumzika kwa amani Baba, na nuru ya milele ikuangazie daima'' Gachagua asema.

    Soma pia:

  12. Katika picha: Rais Ruto amfariji Mama Ida Odinga

    Picha ya Rais Ruto akiwa na mkewe Raila odinga

    Chanzo cha picha, Statehouse

    Maelezo ya picha, Picha ya Rais Ruto akiwa na mkewe Raila odinga

    Rais William Ruto amemfariji Mama Ida Odinga nyumbani kwake Karen kufuatia kifo cha mume wake, Raila Odinga.

    Akiwa ameandamana na viongozi mbalimbali wa serikali, Rais Ruto alimpa pole Mama Ida, familia ya Odinga, na kuwatia moyo katika kipindi hiki kigumu.

    Rais Ruto anatarajiwa kuhutubia taifa wakati wowote kutoka sasa.

    Akiwa ameandamana na viongozi wengine kumfariji Mama Ida Odinga

    Chanzo cha picha, Statehouse

    Maelezo ya picha, Akiwa ameandamana na viongozi wengine kumfariji Mama Ida Odinga
    Rais Ruto akimkumbatia kakake Raila Odinga nyumbani kwao Karen

    Chanzo cha picha, Statehouse

    Maelezo ya picha, Rais Ruto akimkumbatia kakake Raila Odinga nyumbani kwao Karen
    g

    Chanzo cha picha, Statehouse

    Galacha wa siasa Raila Odinga alifariki dunia mapema hii leo akiwa na umri wa miaka 80 akipokea Matibabu India.

  13. Waombolezaji wamiminika nyumbani kwa Odinga Bondo

    Waombolezaji wa eneo la Kisumu wamemiminika katika eneo la makazi la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga kuuungana na familia wakati huu wa kuomboleza.

    Kupitia vyombo habari vya eneo, waombolezaji wanabubujikwa na machozi huku wakiwa wameshika matawi kama ishara ya kuomboleza na familia ya Odinga.

    Waombolezaji wengine wameshuhudiwa katika barabara za eneo la Kisumu wakipiga mayowe, kama namna ya kutoa risala zao.

    Hili ni eneo ambalo Raila Odinga amekuwa na wafuasi wengi.

  14. Umoja wa Afrika wamkumbuka Odinga

    Hj

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa wa upinzani Kenya, na Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri hiyo, Raila Amolo Odinga

    Kwa niaba ya Umoja wa Afrika, vyombo na taasisi zake, mwenyekiti huyo ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Odinga, Serikali na wananchi wa Kenya, na na Afrika nzima inayoomboleza msiba huu mkubwa.

    Amemtaja Odinga kama mtu mashuhuri katika maisha ya kisiasa na mpiganaji thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia watu na ameacha alama isiyofutika sio tu kwa Kenya bali katika bara zima la Afrika.

    Mwenyekiti Youssouf anasema, "Afrika imepoteza mmoja wa wanawe wenye maono; kiongozi aliyejitolea maisha yake kutafuta haki, demokrasia na umoja. Urithi wake utaendelea kujenga Afrika yenye amani, ustawi na demokrasia."

  15. Uhuru Kenyatta: Nimempoteza rafiki na kaka

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Uhuru kenyatta

    Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma rambi rambi zake kwa familia ya Raila Odinga.

    Katika ujumbe wake katika mtandao wa Instagram, Uhuru amemtaja marehamu kama mwenzake wa kisiasa katika safari yake yote ya kisiasa.

    ‘Nimepoteza rafiki na kaka. Kwangu mimi, Raila alikuwa zaidi ya mwenzangu wa kisiasa, alikuwa sehemu ya pekee ya safari yangu, katika utumishi wa umma na maishani’- Uhuru Kenyatta.

  16. Rais wa Zambia amtaja Odinga kama mtetezi wa demokrasia

    Hj

    Chanzo cha picha, Ikulu Zambia

    Rais wa Zambia Hakainde Hichilema atuma salamu za pole kufuatia kifo cha mwanasiasa wa Kenya, Raila Odinga.

    Katika taarifa yake kupitia X amesema, "nasikitisha kusikia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya RailaOdinga. Tunatuma rambirambi zetu kwa watu wa Kenya, familia ya Odinga, Rais wa Kenya William Ruto na wote walioguswa na mtetezi huyu mkuu wa demokrasia.

    Hichilema amesema urithi wa Odinga utadumu na amemtakia apumzike kwa amani ya milele.

  17. Waziri mkuu wa India Narendra Modi amtaja Odinga kama rafiki

    Picha ya pamoja ya Raila Odinga na Narendra Modi

    Chanzo cha picha, Narendra/Twitter

    Maelezo ya picha, Picha ya pamoja ya Raila Odinga na Narendra Modi

    Waziri mkuu Narendra modi ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.

    Kupitia ukurasa wake wa X au Twitter Narendra amemtaja Raila Odinga kama kiongozi mashuhuri na rafiki wa dhati wa India.

    Modi alisema kuwa mchango wa Raila Odinga katika kukuza uhusiano kati ya India na Kenya ulikuwa wa kipekee, na kwamba kumbukumbu zake zitaendelea kuenziwa na wengi.

    Aliongeza kuwa Raila alikuwa sauti ya hekima, demokrasia, na mshikamano barani Afrika, na kwamba dunia imepoteza kiongozi wa kweli.

    Waziri Mkuu Modi alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Raila Odinga, wananchi wa Kenya, na wote walioguswa na msiba huu, akiwatakia faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.

    Modi ameweka bayana kuwa Raila alipendelea tiba ya Ayurveda na tiba asili za India kutokana na ufanisi wake katika afya ya binti yake.

    'Alikuwa na mapenzi kwa India kuanzia tiba zetu na utamaduni wetu''

    Raila Odinga amefariki dunia akipokea matibabu nchini India.

  18. Kifo cha Raila Odinga: Wabunge washindwa kujizuia bungeni

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kimesababisha uchungu na simanzi kwa wafuasi wake na Wakenya kwa ujumla.

    Raila alifariki siku ya Jumatano, Oktoba 15, alipokuwa akipatiwa matibabu nchini India.

    Bungeni, wabunge wa ODM waliangua vilio baada ya kupokea habari hizo za kuhuzunisha.

    Baadhi ya wabunge walitiririkwa na machozi na kushindwa kujizuia huku wakimsifu waziri mkuu huyo wa zamani.

    Mwakilishi wa Kike wa Busia Cathrtine Omayo na Mbunge wake wa Likoni Mishi Mboko walishindwa kujizuia wakati taarifa za kifo cha Raila kilipotangazwa.

    Wakenya wanaendelea kutoa heshima zao kwenye mitandao ya kijamii wakimkumbuka kwa namna mbalimbali.

  19. Habari za hivi punde, Rais Ruto na mamia ya Wakenya wamuomboleza Raila Odinga

    Rais wa Kenya William Ruto pamoja na mamia ya Wakenya wamewasili nyumbani kwa Raila Odinga Karen jijini Nairobi kuomboleza na familia yake.

  20. Rais Samia atuma salamu za rambirambi

    Hj

    Chanzo cha picha, IKULU

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametuma salamu za rambi rambi baada ya kifo cha mwanasiasa wa upinzani nchini Kenya, bwana Raila Odinga.

    Kupitia ukurasa wake wa Instgram Samia amesema, "imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote."

    Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki, na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi.