Tunayofahamu kuhusu mkataba wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Raila

Chanzo cha picha, William Ruto/ Facebook
- Author, Dinah Gahamanyi
- Akiripoti kutoka, BBC News Swahili, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kiongozi mkongwe wa upinzani wametia saini mkataba wa kufanya kazi baada ya wiki kadhaa za mashauriano nchini kote kuhusu mkataba huo wa kisiasa.
Hafla hiyo, iliyofanyika KICC jijini Nairobi mnamo Ijumaa, iliashiria kutiwa saini kwa kihistoria wakati viongozi wote wawili waliweka kalamu kwenye karatasi ili kutia muhuri Mkataba wa Makubaliano (MoU) ambao utaelekeza maendeleo ya nchi.
Je, ni masuala gani yaliyokubaliwa na pande mbili?
Suala la kwanza lilikuwa utekelezaji kamili wa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (NADCO) ambayo ilipendekeza mageuzi muhimu ndani ya nchi.Upinzani umekuwa ukitoa wito kwa serikali kutekeleza ripoti hiyo, ukitaja kwamba asilimia 90 ya masuala ya Wakenya yatashughulikiwa.
Ripoti hiyo iliibuka kutokana na maandamano kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 2022 baada ya Raila kudai uchaguzi huo ulivurugwa.
Hii ilichukua hatua ya Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuwaleta Raila na Ruto kwenye meza ya mazungumzo. Hili lilipelekea kuundwa kwa timu ya pande mbili - NADCO - ambayo iliunda ripoti ambayo ilitaka kushughulikiwa kwa gharama ya maisha, ajira kwa vijana na mfumo wa kutekeleza sheria ya kijinsia ya theluthi mbili.
Suala la pili na la tatu linahusisha ushirikishwaji wa makundi yote ya walio wachache na kuimarisha ugatuzi ili kuboresha huduma kwa wananchi katika ngazi ya mtaa.
Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuyalinda maisha ya vijana kwa kuwezesha kujiendeleza katika sekta kama vile teknolojia, uchumi wa bluu, viwanda na madini ili kuunda fursa za ajira.
Wawili hao wameazimia kuwa na uongozi na kudumisha uadilifu ndani ya serikali pana ili kutoa huduma bora.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aidha wamekubaliana kuhusu Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuheshimu haki za Wakenya kuandamana na kuboresha mbinu zao za kushughulikia waandamanaji wanaotekeleza haki zao za Kikatiba.
Wameazimia kwa pamoja kuhakikisha kunakuwa na haki ya watu kukukusanyika na kulipa fidia wale wote wenye madai ya haki za waathiriwa wa utekeji nyara.
Deni la taifa pia ni jambo la msingi katika makubaliano hayo, huku pande zote mbili zikikubaliana kuwa ni lazima ukaguzi wa kitaifa ufanyike ili kujua hali ya nchi.
Wakati huo huo , hatua za uwajibikaji zitaimarishwa ili kutathmini jinsi fedha zinavyotumika, kulingana na makubaliano hayo.
Jambo lingine lilikuwa ni vita dhidi ya rushwa ambapo Ruto na Raila wamekubaliana kuwa wataongeza uwezo wa taasisi zinazotekeleza uwajibikaji kama vile Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na mdhibiti wa bajeti.
Suala la tisa lilihusu kuzuia upotevu wa rasilimali za serikali ili kuimarisha ufanisi.
Jambo la mwisho lilikuwa ni kulinda na kukuza mamlaka ya katiba ili kulinda haki za binadamu, kudumisha utulivu na kuzuia matumizi mabaya ya madaraka.














