Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Shirika la Afya Duniani WHO laitaka Marekani kutathmini uamuzi wake

Hatua hiyo inajiri baada ya Rais Donald Trump kutia saini agizo la kutaka kujiondoa katika WHO.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Ambia Hirsi & Rashid Abdalla

  1. Shirika la Afya Duniani WHO laitaka Marekani kufikiria uamuzi wake

    Shirika la Afya duniani limejutia hatua ya Marekani kutaka kujiondoa katika shirika hilo.

    Hatua hiyo inajiri baada ya Rais Donald Trump kutia saini agizo la kutaka kujiondoa katika WHO .

    Agizo hilo lilisema Marekani inajiondoa "kwa sababu ya WHO kutoshughulikia janga la Covid-19 ambalo liliibuka Wuhan, China, na majanga mengine ya afya ya ulimwengu, kushindwa kwake kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka, na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa yasiyofaa.

    Hatahivyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari WHO imetoa wito kwa Marekani kufikiria tena uamuzi huo.

    Shirika hilo limesema kuwa ushirikiano wa Marekani umeliwezesha kuokoa idadi kubwa ya maisha mbali na kuwaokoa Wamarekani na watu wote duniani kutokana na athari za Kiafya.

    Shirika hilo limeongezea kwamba Marekani ni miongoni mwa waanzilishi wa shirika hilo na imeshiriki katika usimamizi wa shirika hilo pamoja na wanachama wengine 193.

    WHO limeongzea kwamba kupitia mchango wa Marekani na wanachama wengine katika kipindi cha miaka saba iliopita shirika hilo limefanikiwa kuidhinisha idadi kubwa ya mabadiliko katika historia yake ikiwa ni pamoja na kupitia ushiriki wake kikamilifu katika Bunge la Afya Duniani na Bodi ya Utendaji.

    Trump alikosoa jinsi shirika hilo la kimataifa lilivyoshughulikia janga la Covid-19 na kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka kwa taasisi hiyo ya Geneva wakati wa janga hilo.

    Rais Joe Biden baadaye alibatilisha uamuzi huo.

    Agizo hilo lilisema Merekani inajiondoa "kwa sababu ya WHO kutoshughulikia janga la Covid-19 ambalo liliibuka Wuhan, China, na majanga mengine ya afya ya ulimwengu, kushindwa kwake kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka, na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa yasiyofaa. ushawishi wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO".

    Amri hiyo ya utendaji pia ilisema hatua hiyo ilitokana na "malipo yasiyofaa" ambayo Marekani ilitoa kwa WHO, ambayo ni sehemu ya Umoja wa Mataifa.

    Trump alipokuwa bado ofisini kwa mara ya kwanza alikosoa shirika hilo kwa "kuipendelea China" katika kukabiliana na janga la Covid-19.

  2. Lissu: Sijawahi kugombana na Mbowe,

    Makamu mwenyekiti wa chama hicho Lissu ambaye anawania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho kwenye uchaguzi amesema kuwa yeye binafsi hajawahi kugombana na Mbowe.

    Akihutubia mkutano huo, Lissu alisema, " Binafsi sijawahi kugombana na Mbowe kwa miaka 20 tuliyokuwa pamoja kwenye chama, tumetofautiana kimtazamo tu. Na naamini hili litaendelea baada ya leo.

    Kauli hiyo inakuja huku Lissu na Mbowe wakitarajiwa kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa kuchagua viongozi wa juu wa chama hicho hapo baadaye.

    "Baada ya uchaguzi, kamati kuu itakayoanza kazi Febrauri 23 inapaswa kuanza kurejesha nidhamu, maadili kwa kutambua kuwa hakuna matusi kwenye utamaduni wa Chadema," ameeleza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati alipokuwa akifungua mkutano wa chama hicho ulioanza leo jijini Dar es Salaam.

    Akihutubia mamia ya wanachama, na wageni mbalimbali kwenye mkutano huo, Mbowe alisema kuwa chama hicho kinapaswa kusafishwa na kuhakikisha maadili na nidhamu inakuwepo ndani ya chama hicho.

    Alisema, "Lazima tusafishe chama… yale yanayobomoa na kuchafua chama lazima tusafishe. Tukitoka uchaguzi tukasafishe hayo ili chama kiwe salama kama waasisi walivyo hakikisha chama hicho kiko salama."

    Ajenda mbalimbali zitakuwepo kwenye mkutano huo, mojawapo ni ile ya uchaguzi ya mwenyekiti ambapo Mbowe atawania nafasi hiyo dhidi ya makamu wake, Tundu Lissu na kada wa chama hicho, Odero Odero.

    Kiburi baada ya ushindi

    Mwenyekiti wa chama hicho ametoa rai kuwa baada ya uchaguzi kumalizika watakaoshinda mbali na kuendeleza mema ndani ya chama hicho, basi wahakikishe wanaunganisha wanachama wa chama hicho.

    "Tusijenge kiburi cha kushinda uchaguzi," alisema Mbowe wakati akihitimisha hotuba ya kufungua mkutano huo huku akiwataka wanachama kusimama na kushikana mikono na kusema kauli mbiu ya mkutano huo 'Stronger Together'

    Ulinzi waimarishwa

    Katika eneo la Mlimani City panapofanyika Mkutano huo, Jeshi la polisi limeimarisha ulinzi.

    Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema, " Kuna shughuli mbalimbali katika eneo hili la Mlimani lakini pia mkutano unaondelea una watu wengi wakiwemo wanadiplomasia hivyo tunaimarisha ulinzi ili pia zisiathiri shughuli nyingine katika eneo hilo zikiwemo za kibiashara."

    Chadema yaivaa CCM

    Kiongozi wa upinzani alikosoa Chama tawala CCM kwa kile alichodai kuwa hakijaweza kuzika umaskini nchini Tanzania.

    Mbowe alisema, " CCM kugawia wazee visenti wanavyoviita Mfuko wa TASAF ili kumaliza matatizo ya umaskini… Kweli hiyo ndio njia? Kama chama (Chadema) tunaendaje kurudisha furaha ya waliokosa furaha na matumaini? .Chadema tunaweza vipi… ? tuna wajibu mkubwa, mbele yetu."

    Baada ya kufunguliwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika ametoa taarifa ya miaka mitano ya chama hicho huku akieleza mafanikio na changamoto zinazoikumba chama hicho,

    Hata hivyo uchaguzi wa chama hicho utafanyika baadaye huku mkutano huo mkuu ukitarajiwa kuhitimishwa kesho Jumatano.

  3. Wahouthi 'kupunguza' mashambulizi katika Bahari ya Shamu

    Waasi wa Houthi wa Yemen wametangaza kwamba watapunguza mashambulizi yao katika Bahari ya Shamu kwa meli zinazoshirikiana na Israel baada ya kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza, lakini wakaonya kwamba mashambulizi makubwa zaidi yanaweza kurejea ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

    Tangazo la Houthis linaweza lisitoshe kuhamasisha makampuni ya kimataifa kuingia tena kwenye njia ya baharini, ambayo ni muhimu katika kubeba shehena za nishati kati ya Asia na Ulaya.

    Mwaka jana, mashambulizi ya makombora ya Houthi ya Yemen yalipunguza msongamano katika eneo hilo kwa nusu na, hasa ikiathiri zaidi mapato ya Misri kutoka kwenye Mfereji wa Suez, unaounganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Mediterania.

    Jacob P. Larsen, mkuu wa Baraza la Kimataifa la Usafiri wa Baharini la Baltic (BIMCO), shirika kubwa zaidi la meli duniani, aliuita uamuzi wa Wahouthi "Usitishaji wa mapigano ulio tete".

    Inasemekana kuwa hata mabadiliko kidogo tu kutoka kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza yanaweza kusababisha kuongezeka kwa uhasama, ambapo Wahouthis wanaweza tena kutekeleza vitisho vyao dhidi ya meli za kimataifa.

    Soma zaidi:

  4. Rais wa Korea Kusini akanusha kuamuru kukamatwa kwa wabunge

    Rais wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol amejitokeza kwa mara ya kwanza katika kesi yake ya kuondolewa madarakani, ambapo alikanusha kuamuru kukamatwa kwa wabunge wakati wa jaribio lake la kuweka sheria ya kijeshi.

    Bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imani na Yoon mwezi uliopita, na wiki jana mahakama ya kikatiba ilianza kesi ya kuamua iwapo itamwondoa madarakani kabisa.

    Yoon pia anakabiliwa na uchunguzi tofauti wa jinai ikiwa aliongoza uasi. Amekuwa kizuizini tangu wiki iliyopita.

    Usalama ulikuwa mkali siku ya Jumanne huku Yoon akisafirishwa kwa gari kutoka kituo cha kizuizini, ambako anazuiliwa, hadi mahakama ya kikatiba.

    Polisi waliunda kuta za watu na kuweka vizuizi vya kuzuia ghasia ili kuwazuia mamia ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika karibu wasikaribie sana.

    Wikiendi iliyopita ilishuhudiwa vurugu wakati makumi ya wafuasi wa Yoon walipambana na wasimamizi wa sheria.

    Siku ya Jumanne, Yoon aliulizwa ikiwa alikuwa amewaamuru makamanda wa kijeshi "kuwatoa nje" wabunge kutoka bungeni usiku aliotangaza sheria ya kijeshi, ili kuwazuia wasibatilishe amri yake.

    Akajibu: "Hapana."

    Awali makamanda wa kijeshi walikuwa wamedai kwamba Yoon alitoa amri kama hiyo tarehe 3 Disemba, baada ya wabunge kupanda uzio na kuvunja vizuizi vya kuingia ndani ya jengo la bunge na kupiga kura ya kukataa tamko la sheria ya kijeshi la Yoon.

    "Mimi ni mtu ambaye nimeishi kwa imani thabiti katika demokrasia huria," Yoon alisema katika hotuba yake ya ufunguzi siku ya Jumanne.

    "Kwa vile mahakama ya kikatiba ipo ili kulinda katiba, ninaomba mchunguze kwa kina vipengele vyote vya kesi hii," aliwaambia majaji.

    Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, ambayo ilidumu kwa takriban saa mbili, Yoon na mawakili wake walidai kuwa amri hiyo ya sheria ya kijeshi ilikuwa "utaratibu ambao haukusudiwa kutekelezwa".

    Soma zaidi:

  5. Trump amshauri Putin 'kutoiharibu' Urusi na kufanya makubaliano na Ukraine

    Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa anapanga kukutana na rais wa Urusi katika siku za usoni.

    Aliongeza kuwa Vladimir Putin "anaiangamiza Urusi" kwa kutotaka kufikia makubaliano ya kumaliza vita nchini Ukraine.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, kwa upande wake, alionya kwamba Washington haiwezi kuweka muda wa kumaliza mzozo huo.

    “Lazima akubali kufikia makubaliano. "Nafkiri anaiangamiza Urusi kwa kutofanya makubaliano," Rais wa Marekani alisema, akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya White House (iliyonukuliwa na AFP).

    "Nafkiri Urusi itakuwa katika matatizo makubwa."

    "Hawezi kuwa na furaha kwamba haendelei vizuri," Trump aliendelea. "Watu wengi walidhani vita vingeisha ndani ya wiki moja, lakini sasa vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka mitatu."

    Kulingana na yeye, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky yuko tayari kufikia mpango wa kumaliza vita. Hata hivyo, Zelensky bado hajatoa maoni yake juu ya taarifa hii; kauli zake za awali ziliondoa makubaliano yoyote isipokuwa mazungumzo ya amani ya haki na kurejea kwa maeneo yaliyokaliwa.

    Trump pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba anapanga kukutana na Putin hivi karibuni.

    Kulingana naye, tayari mchakato wa maandalizi ya mkutano huo unaendelea.

    "Tutajaribu kufanya hivi haraka iwezekanavyo. Unajua, vita kati ya Urusi na Ukraine haikupaswa kuanza hata kidogo,” alisema Rais wa Marekani.

    Wakati waandishi wa habari walipomkumbusha Trump kwamba aliahidi kumaliza vita katika siku yake ya kwanza kama rais, alitania: "Bado kuna nusu ya siku."

    Saa chache kabla ya kuapishwa kwa Rais wa Marekani, Putin mwenyewe bila kutarajiwa alizungumza kuhusu mawasiliano na Trump katika mkutano wa Baraza la Usalama la Urusi.

    Alimpongeza Trump hadharani kwa kuchukua madaraka na kwa mara nyingine tena akatangaza kuwa tayari kwa mazungumzo, lakini wakati huo huo alitaka yafanyike "kwa misingi ya usawa na ya kuheshimiana," akitaja "utulivu wa kimkakati na usalama."

    "Jambo muhimu zaidi hapa ni kumaliza sababu kuu za mzozo," Putin alirudia tena ombi lake, baada ya karibu miaka mitatu ya kuhalalisha uvamizi kwa Ukraine, ukweli ni kwamba nchi za Magharibi zilikataa kujadili madai ya mwisho ya kijiografia ya Moscow.

    Soma zaidi:

  6. Trump anatafuta kuondoa haki ya uraia wa kuzaliwa huku akitangaza hali ya dharura mpakani

    Akiwa kwenye meza yake katika Ofisi ya Ikulu, Rais Donald Trump alitia saini msururu wa maagizo na amri zinazolenga kukandamiza uhamiaji.

    Kuanzia agizo la kushughulikia ufafanuzi wa uraia wa kuzaliwa, hadi agizo la kutangaza uhamiaji haramu kwenye mpaka kuwa dharura ya kitaifa, Trump alichukua hatua za haraka za kuimarisha ulinzi katika mpaka wa Marekani na Mexico.

    Lakini baadhi ya mipango yake - hasa kuhusu kubadilisha ufafanuzi wa uraia wa kuzaliwa - kuna uwezekano wa kukabiliana na vikwazo vikubwa.

    Tayari anakabiliwa na upinzani kisheria kutoka kwa mashirika ya kutetea uhamiaji, ambayo yamejibu kwa hasira kutokana na matangazo yake.

    Soma zaidi:

  7. Watu 10 wafariki katika ajali ya moto kwenye hoteli ya Uturuki

    Hoteli moja imeshika moto katika eneo la mapumziko la Uturuki la Bolu na kusababisha vifo vya watu 10 huku wengine 32 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya.

    Wawili kati ya waliofariki waliruka kupitia madirisha ya hoteli hiyo, ripoti za Uturuki zilisema.

    Moto ulizuka katika Hoteli ya Ghorofa 12 ya Grand Kartal saa 03:27 kwa saa za eneo (00:27 GMT) wakati ambapo ni kipindi cha likizo yenye shughuli nyingi iliyokuwa na watu 234, aliongeza.

    Picha zinazosambaa nchini Uturuki zilionyesha kitani kikining'inia kwenye madirisha ambayo ilitumiwa na wale wanaojaribu kutoroka jengo lililokuwa likiungua.

    Hoteli hiyo ilikuwa ikichunguza iwapo wageni walikuwa wamenaswa kwenye vyumba vyao moto huo ulipokuwa ukienea.

    Juhudi za uokoaji ziliendelea hadi asubuhi, na waziri wa mambo ya ndani alisema huduma za dharura zimetuma watu 267 katika eneo la tukio.

    Milima ya Bolu ni maarufu kwa watelezi kutoka Istanbul na mji mkuu Ankara.

    Mkufunzi wa mchezo wa kuteleza kwenye theluji Necmi Kepcetutan aliiambia TV ya Uturuki kuwa alifanikiwa kutoroka kwa sababu anaifahamu hoteli hiyo, huku wageni ambao hawakuifahamu vizuri kama yeye hawakubahatika.

    "Watu walikuwa wakipiga kelele madirishani, 'Tuokoe,' kwa sababu kulikuwa na moshi mwingi ndani. Tulitoa watu 20-25 nje," aliiambia NTV.

    Mazingira yaliyosababisha moto huo bado hayajafahamika.

  8. Waasi wa Mali wamwachilia huru mateka raia wa Uhispania

    Muungano wa waasi wa Tuareg kaskazini mwa Mali umemwachilia huru Mhispania aliyetekwa nyara Afrika Kaskazini Januari 17, wasemaji wawili wa kundi hilo wamesema siku ya Jumatatu.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania ilisema siku ya Ijumaa, mwanaume mmoja raia wa Uhispania alitekwa nyara Afrika Kaskazini.

    Gazeti la El Pais liliripoti mtu huyo alitekwa nyara kusini mwa Algeria na kundi la Kiislamu na kupelekwa Mali, ingawa Wizara ya Mambo ya Nje haikuthibitisha habari hiyo.

    Katika chapisho kwenye X, mmoja wa viongozi wa Azawad Liberation Front (FLA), amesema raia wa Uhispania aitwaye Gilbert Navarro "aliyetekwa nyara nchini Algeria siku chache zilizopita" na kusafirishwa na watekaji wake hadi kaskazini mwa Mali ameachiliwa na vikosi vya FLA siku ya Jumatatu.

    “Mateka huyo atakabidhiwa kwa nchi ya Algeria,” amesema Attaye Ag Mohamed, msemaji wa kundi hilo.

    Msemaji mwingine wa FLA, Mohamed Elmaouloud Ramadane, amesema kwenye X, FLA imemwachilia Navarro, akiwa na afya njema.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Trump atangaza mpango wa kuwafuta kazi zaidi ya watu 1,000 waliohudumu wakati wa Biden

    Rais Donald Trump amesema siku ya Jumanne kuwa anapanga kuwaondoa kazini zaidi ya watu 1,000 walioteuliwa na utawala wa Rais wa zamani Joe Biden, akitangaza kuwafuta kazi wanne kwenye mtandao wa kijamii, akiwemo mpishi mashuhuri Jose Andres na jenerali mkuu wa zamani Mark Milley.

    "Ofisi yangu ya utumishi wa Rais iko katika mchakato wa kuwatambua na kuwaondoa zaidi ya wateule elfu moja wa Rais kutoka kwa utawala uliopita, ambao hawaambatani na maono yetu," Trump alisema katika chapisho kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth.

    Hatua hiyo imezua wasiwasi kwamba rais anapanga kuwaondoa wote walioteuliwa wakati wa utawala wa Biden na kuwaweka watu wanaoamini ajenda yake.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Maporomoko ya ardhi yaua watu 16 Indonesia

    Maporomoko ya ardhi katika mji wa Pekalongan katika jiji la Java nchini Indonesia yamesababisha vifo vya watu 16 na kujeruhi 10, amesema afisa wa kukabiliana na majanga nchini humo.

    Bergas Caturasi amesema katika kituo cha runinga cha Kompas kuwa, maporomoko hayo ya ardhi yalisababishwa na mvua kubwa katika eneo hilo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shughuli ya kuwatafuta waliotoweka imetatizwa na mvua, ikinukuu taarifa ya idara ya kukabiliana na majanga nchini humo.

    "Msako unaendelea, kwa sababu hatuna muda wa kutosha. Tunakimbizana na hali ya hewa," amesema Caturasi.

  11. Trump amekula kiapo bila ya kuweka mkono wake juu ya Bibilia

    Rais wa Marekani, Donald Trump alikula kiapo chake Jumatatu akiwa ameinua mkono wake wa kulia juu, bila kuuweka mkono wake wa kushoto juu ya Biblia mbili ambazo mkewe Melania alizishikilia alipokuwa amesimama kando yake.

    Shirika la habari la Reuters, limeripoti kuwa wataalamu wanasema, tukio hilo halina athari yoyote kwa kiapo chake, lakini limeibua mjadala katika mitandao ya kijamii, kwa kutoweka mkono kwenye Biblia, ambayo ni maandiko matakatifu ya Wakristo na Wayahudi.

    “Kile anachotumia rais ajaye kuapa, iwe ni Biblia, hati ya kihistoria au bila ya chochote, si muhimu ili kutwaa mamlaka,” anasema Jeremi Suri, profesa wa historia na masuala ya urais wa Chuo Kikuu cha Austin, Texas.

    "Hakuna kitu katika Katiba kinachosema rais anapaswa kuunganisha kiapo chake na Mungu kwa njia yoyote ile," anasema. "Kiapo ni kwa Katiba."

    Ameongeza kuwa Katiba inaruhusu rais mteule kuapa au kuthibitisha. Waanzilishi wa Marekani waliliweka hilo hivyo wakijua kuna wengine wanaweza kutokea wasio amini Mungu.

    Wasemaji wa Trump hawakujibu ombi la kuzungumzia suala hilo.

    Timu yake inasema, Trump alichagua Biblia ambayo Rais wa 16 Abraham Lincoln aliapishwa nayo na Bibilia nyingine ni ile ambayo Trump alipewa na mama yake.

  12. Kiongozi wa upinzani Msumbiji yuko tayari kuhudumu katika serikali ya mpinzani wake

    Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Msumbiji Venâncio Mondlane ameiambia BBC kuwa yuko tayari kuhudumu katika serikali ikiwa Rais Daniel Chapo atatimiza matakwa yake ya kumaliza mzozo wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata.

    Chapo alisema ameunda timu ambayo "inazingatia" iwapo mpinzani wake anafaa kualikwa kujiunga na serikali mpya " jumuishi".

    Wawili hao walielezea misimamo yao katika mahojiano tofauti na BBC, na kutoa hisia kwamba walikuwa tayari kuungana baada ya vifo vya takriban watu 300 katika machafuko ya baada ya uchaguzi.

    Mondlane alikataa kushindwa kwake katika uchaguzi wa Oktoba, akisema matokeo yalichakachuliwa - jambo ambalo Chapo alilikanusha.

    Mahakama ya juu zaidi ya Msumbiji ilimtangaza Chapo kuwa mshindi kwa kupata asilimia 65 ya kura dhidi ya 24 za Mondlane.

    Chapo alikuwa mgombea wa chama tawala cha Frelimo, kwani mtangulizi wake, Filipe Nyusi, alilazimika kuachia ngazi baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Kuna maiti kwenye kila mtaa wa Gaza – Waokoaji

    Idara ya Ulinzi wa Raia ya Gaza – chombo kikuu cha kukabiliana na matukio ya dharura katika ukanda huo - inahofia kuwa kuna miili zaidi ya 10,000 ambayo bado imezikwa chini ya kifusi.

    "Katika kila mtaa kuna maiti. Katika kila kitongoji kuna maiti chini ya majengo," anasema Abdullah Al-Majdalawi, mfanyakazi kutoka Idara ya Ulinzi wa Raia mwenye umri wa miaka 24.

    "Baada ya kusitishwa kwa mapigano tulipokea simu nyingi kutoka kwa watu wakisema, tafadhali njoo, familia yangu imezikwa chini ya vifusi."

    Msemaji wa shirika hilo Mahmoud Basal aliambia BBC, wanataraji kuondoa miili hiyo ndani ya siku 100, lakini kuna uwezekano wa juhudi hizo kutatizika kutokana na upungufu wa tingatinga na vifaa vingine muhimu.

    Picha mpya kutoka Ukanda wa Gaza kufuatia usitishaji vita wa Jumapili zinaonyesha uharibifu mkubwa uliotokea wakati wa miezi 15 ya mashambulizi ya Israel, hasa kaskazini mwa eneo hilo.

    Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa 60% ya miundo mbinu kote Gaza imeharibiwa.

    Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), vita hivyo vimewaacha zaidi ya wakazi milioni mbili wa Gaza bila makazi, bila kazi, na kutegemea chakula cha msaada ili kuishi.

    Siku ya Jumatatu, malori zaidi 915 yaliingia katika eneo hilo, unasema Umoja wa Mataifa, idadi kubwa zaidi tangu kuanza kwa vita miezi 15 iliyopita.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Trump awasamehe washtakiwa 1,600 wa ghasia katika Bunge la Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump ametoa msamaha au mabadiliko kwa zaidi ya watu 1,500 waliopatikana na hatia au kushtakiwa kwa kuhusika na ghasia katika Bunge la Marekani miaka minne iliyopita.

    Wanachama kumi na wanne wa Proud Boys na Oath Keepers, vikundi viwili vya siasa kali za mrengo wa kulia, ni miongoni mwa wale ambao hukumu zao zimebadilishwa na rais mpya wa Republican alipoingia madarakani Jumatatu.

    Trump pia alitia saini agizo la kuiagiza Idara ya Sheria kufuta kesi zote zinazosubiriwa dhidi ya washukiwa wanaotuhumiwa katika ghasia hizo.

    Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Trump kuapishwa kama rais wa 47 wa Marekani.

    Januari 6, 2021 wafuasi wa Trump walivamia majengo ya Bunge wakati wabunge wakikutana kudhibitisha ushindi wa Joe Biden.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Trump atia saini agizo la kuchelewesha kuipiga marufuku TikTok

    Rais Donald Trump ametia saini agizo la kuipa TikTok nyongeza ya siku 75 ili kutii sheria inayotaka iuzwe au kupigwa marufuku nchini Marekani.

    Agizo hilo lilikuwa miongoni mwa maagizo mengi ambayo Trump alitia saini Jumatatu jioni.

    Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, amesema: "Nikwambie kitu. Kila tajiri amenipigia simu kuhusu TikTok."

    Alipoulizwa na mwandishi wa habari kwa nini amebadili msimamo wakati alitaka ipigwe marufuku 2020, Trump alijibu: "Kwa sababu nilipaswa kuitumia."

    Ameelezea uwezekano wa kuwepo kwa ubia, wa umiliki wa 50-50 kati ya "Marekani" na mmiliki wake wa China, ByteDance. Lakini hakutoa maelezo zaidi juu ya namna gani mpango huo utafanya kazi.

    Trump pia alisema ushuru mpya wa biashara kwa China unaweza kutegemea makubaliano juu ya umiliki wa mtandao huo. Ikiwa Beijing itakataa makubaliano "kitakuwa kitendo cha uhasama," alisema.

    Siku ya Jumamosi jioni, programu hiyo inayomilikiwa na Wachina iliacha kufanya kazi kwa watumiaji wa Marekani, baada ya sheria ya kuipiga marufuku kwa misingi ya usalama wa taifa kuanza kutumika.

    Ilirejea kwa watumiaji wake milioni 170 nchini Marekani baada ya Trump kusema atatoa agizo ili kuipa programu hiyo ahueni atakapoingia madarakani.

    Kampuni mama ya TikTok, Bytedance, hapo awali ilipuuza sheria inayotaka TikTok kuuzwa ili kuepuka kupigwa marufuku. Sheria hiyo iliidhinishwa na Mahakama ya Juu siku ya Ijumaa na kuanza kutumika Jumapili.

    Trump aliunga mkono marufuku ya TikTok wakati wa muhula wake wa kwanza katika Ikulu ya White House.

    Mtendaji mkuu wa TikTok, Shou Zi Chew alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Trump siku ya Jumatatu.

    Mabilionea na watu mashuhuri wameonyesha nia ya kutaka kuinunua TikTok, akiwemo mmiliki wa X. Musk, Shark Tank na Kevin O'Leary.

  16. DR Congo: Maelfu ya raia wakimbia mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23

    Ripoti kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinaarifu kuwa maelfu ya raia wanayakimbia mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi wa kundi la M23.

    Jeshi na washirika wake wamekuwa wakijaribu kuukomboa mji wa Masisi ambao hivi karibuni uliangukia mikononi mwa waasi hao.

    Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaonya kuwa raia wako katika hatari kubwa huku silaha nzito zikitumiwa katika maeneo ya makazi ya raia vitongojini.

    Shirika la kimataifa la madaktari wasio na mipaka MSF limesema risasi zilipiga hospitali ya Masisi.

    Maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu wanasema hospitali kuu ya mji wa Goma imelemewa na idadi kubwa ya majeruhi.

    Waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanaonekana kudhamiria kupanua sehemu wanayodhibiti katika eneo mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini.

    Takriban watu robo milioni wameyakimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

    Wakati mapigano yanapoendelea kwa kasi, raia wako katika hatari ya mara kwa mara.

    Maelezo zaidi:

  17. Trump atia saini agizo la kuiondoa Marekani WHO

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

    "Hili ni jambo kubwa," rais mpya wa Marekani aliyeapishwa alisema alipokuwa akiidhinisha hati hiyo baada ya kurejea tena katika Ikulu ya Marekani.

    Ilikuwa ni moja ya amri kadhaa za utendaji alizotia saini siku ya kwanza madarakani.

    Hii ni mara ya pili kwa Trump kuamuru Marekani kujiondoa kuwa mwanachama wa WHO.

    Trump alikosoa jinsi shirika hilo la kimataifa lilivyoshughulikia janga la Covid-19 na kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka kwa taasisi hiyo ya Geneva wakati wa janga hilo.

    Rais Joe Biden baadaye alibatilisha uamuzi huo.

    Agizo hilo lilisema Merekani inajiondoa "kwa sababu ya WHO kutoshughulikia janga la Covid-19 ambalo liliibuka Wuhan, China, na majanga mengine ya afya ya ulimwengu, kushindwa kwake kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka, na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa yasiyofaa. ushawishi wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO".

    Amri hiyo ya utendaji pia ilisema hatua hiyo ilitokana na "malipo yasiyofaa" ambayo Marekani ilitoa kwa WHO, ambayo ni sehemu ya Umoja wa Mataifa.

    Trump alipokuwa bado ofisini kwa mara ya kwanza alikosoa shirika hilo kwa kuwa "kuipendelea China" katika kukabiliana na janga la Covid-19.

    rump alishutumu WHO kwa kuegemea China kwa jinsi ilivyotoa mwongozo wakati wa mlipuko huo.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Natumai hujambo

    Ikiwa ndio mwanzo unaungana nasi Rais mpya wa Marekani Donald Trump ametia saini sheria kadha wa kadha siku yake ya kwanza madarakani,ikiwa ni saa chache tangu kuapishwa kuwa Rais.

    Miongoni mwa amri ya rais aliyotekeleza ni pamoja na:

    • Kutangaza hali ya hatari katika mpaka wa kusini na Mexico kama sehemu ya kuzuia wahamiaji kuingia Marekani na kuyaorodhesha magenge ya wauza dawa za kulevya kama makundi ya kigaidi.
    • Aidha amewapa msamaha takriban watu elfu moja mia tano waliohusishwa na shambulizi la Januari 6 mwaka 2021 ambapo wafuasi wake walivamia bunge wakijaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020.
    • Trump pia ametia saini agizo la kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani WHO na katika makubaliano ya tabia nchi yaliyofikiwa Paris na pia kuruhusu mtandao wa kijamii wa Tiktok.
    • Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Rais Trump amesema aliokolewa na Mungu ili kuifanya Marekani yenye nguvu tena na kuahidi kuwa mpatanishi wa amani.