Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Donald Trump aapishwa rasmi kuwa rais wa Marekani
Rais mteule wa Marekani pamoja na makamu wake JD Vance hatimaye wameapishwa rasmi kuwa rais na makamu wake wa Marekani. Kiongozi huyo sasa atakuwa rais wa 47 kulitawala taifa la Marekani.
Muhtasari
- Rais Trump apinga sera za enzi ya Biden
- Trump aapishwa rasmi kuwa rais wa Marekani
- Jeshi la DRC na M23 watuhumiwa kutumia mabomu katika maeneo ya makazi
- Mke wa kwanza wa mfalme wa Wazulu ashindwa kuzuia ndoa ya tatu ya mumewe
- Polisi wa Afrika Kusini wanamsaka mshukiwa mkuu katika sakata la mgodi wa Stilfontein
- Papa asema mpango wa Trump wa kuwafukuza wahamiaji ni wa kuchukiza
- Trump aahidi hatua za haraka kutengua sera za Biden
- Watu wanane wafariki kwa moto katika nyumba ya kutunzia wazee
- Mke wa Trump azindua sarafu yake ya mtandaoni
- Utajiri wa mabilionea duniani uliongezeka mara tatu zaidi mwaka 2024- Ripoti
- China yamnyonga dereva aliyewaua makumi ya watu katika shambulio la gari
- Mwanaume akamatwa kwa kumchoma kisu mwigizaji wa Bollywood
- Wachimba madini haramu saba wauawa nchini Ghana
- Blinken amshukuru Waziri Mkuu wa Qatar kwa 'jukumu muhimu' katika juhudi za upatanishi
- TikTok yarejesha huduma zake Marekani baada ya ahadi ya Trump
- Wafungwa 90 wa Kipalestina wachiwa huru baada ya Hamas kuwaachia mateka watatu wa Israel
Moja kwa moja
Ambia Hirsi & Rashid Abdallah
Mabadiliko yanakuja haraka - Trump
Trump anazungumza juu ya kimbunga huko North Carolina na moto wa LA.
Anasema moto huo uliathiri baadhi ya matajiri na wenye nguvu zaidi, ambao baadhi yao wameketi hapa hivi sasa.
"Hawana nyumba tena.," anaambia hadhira ya Capitol Rotunda. Anasema Marekani ina mfumo wa afya ambao hautoi wakati wa maafa, lakini anasema pesa nyingi zinatumika kwa hilo "kuliko popote duniani".
Anaongeza kuwa nchi ina mfumo wa elimu ambao "unafundisha watoto wetu kujionea aibu".
"Yote haya yatabadilika, kuanzia leo, na yatabadilika haraka sana," Trump anasema.
Habari za hivi punde, Trump: Maisha yangu yaliokolewa 'kwa sababu'
Trump sasa anashughulikia jaribio la mauaji dhidi yake. Anaanza kwa kusema kwamba “hatima tukufu” ya taifa letu haitakataliwa tena.
Akitafakari kuhusu jaribio la maisha yake, anasema katika kipindi cha miaka minane "amejaribiwa zaidi ya rais yeyote".
Anaongeza kuwa wengine "wamejaribu kusimamisha kazi yetu" na kujaribu kuchukua uhuru wake "na kwa kweli maisha yangu".
Anasema maisha yake yaliokolewa "kwa sababu" - "kuifanya Marekani kuwa bora tena" - kauli mbiu yake ya mizunguko miwili ya kampeni.
Rais Trump apinga sera za enzi ya Biden
Trump anaendelea kutumia hotuba yake ya kwanza kushambulia utawala wa Biden na kushughulikia mzozo wa wahamiaji.
Anasema changamoto za nchi hiyo "zitaangamizwa", akiongeza kuwa Marekani inakabiliwa na mzozo wa "imani juu ya uanzishwaji wa itikadi kali na ufisadi".
Utawala uliopita, anasema, umetoa hifadhi na ulinzi kwa "wahalifu hatari" ambao wameingia nchini kwetu kinyume cha sheria. Serikali imetoa "ufadhili usio na kikomo kwa ulinzi wa mipaka ya kigeni" lakini inakataa kutetea mipaka ya Marekani, anadai.
"Sasa tuna serikali ambayo haiwezi kudhibiti hata shida rahisi nyumbani," Trump anasema.
Habari za hivi punde, Trump: 'Enzi bora za Marekani zinaanza hivi sasa'
Donald Trump anaanza hotuba yake kama rais kwa kuhutubia marais wenzake na wengine wanaohudhuria hafla hiyo, akiwemo Makamu wa Rais wa zamani Kamala Harris na Rais wa zamani Joe Biden. "Enzi ya dhahabu ya Marekani inaanza hivi sasa," anasema. "Kuanzia leo, nchi yetu itastawi na kuheshimiwa. "Nitaiweka Marekani mbele."
Trump aapishwa rasmi kuwa rais wa Marekani
Rais mteule wa Marekani pamoja na makamu wake JD Vance hatimaye wameapishwa rasmi kuwa rais na makamu wake wa Marekani.
Kiongozi huyo sasa atakuwa rais wa 47 kulitawala taifa la Marekani.
Makamu wa Rais Mteule JD Vance aapishwa rasmi
Rais Joe Biden na Makamu wake pia wamewasili
Rais mteule Trump na Makamu wake JD Vance wawasili tayari kwa sherehe ya kuapishwa
Mabilionea waliowasili kushuhudia kuapishwa kwa Trump
Pia kumekuwa na baadhi ya mabilionea wa teknolojia tuliowaona hapo awali katika Kanisa la St John, wakiwemo Mark Zuckerberg, Lauren Sanchez, Jeff Bezos, Sundar Pichai na Elon Musk.
Mfalme Charles atuma risala za pongezi kwa Trump
Mfalme Charles ametuma ujumbe wa pongezi kwa Rais Trump katika kuapishwa kwake, akitafakari juu ya uhusiano maalum wa kudumu kati ya Uingereza na Marekani, imesema Buckingham Palace.
Marais wa zamani wawasili kwa sherehe ya kuapishwa kwa Trump
Jeshi la DRC na M23 watuhumiwa kutumia mabomu katika maeneo ya makazi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa ripoti inayolishutumu jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kundi la wanamgambo wa M23 kwa kutumia mabomu katika maeneo yenye wakazi wengi mashariki mwa DRC.
Katika ripoti iliyotolewa leo (Jumatatu), shirika hilo limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuchunguza tuhuma hizo na kuwapeleka wahalifu mahakamani.
Kati ya Januari na Julai 2024, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na jeshi la Congo (FARDC) walirusha mabomu katika maeneo yenye watu wengi zaidi ya mara 150.
Mashambulizi haya, ambayo yaliua zaidi ya raia 100 na kujeruhi mamia, yalikiuka sheria za kimataifa na huenda yanajumuisha uhalifu wa kivita, imesema Amnesty International.
Amnesty International iliwahoji watu 60, ilitembelea maeneo kadhaa yaliyoshambuliwa na kuchambua makumi ya picha, video na taarifa zilizothibitishwa kutoka pande zinazopigana.
Pia unaweza kusoma:
Mke wa kwanza wa mfalme wa Wazulu ashindwa kuzuia ndoa ya tatu ya mumewe
Mke wa kwanza wa Mfalme wa Zulu wa Afrika Kusini Misuzulu kaZwelithini ameshindwa jaribio lake la kisheria la kuzuia mpango wa mumewe wa kuoa mke wa tatu.
Malkia Ntokozo kaMayisela alifika mahakamani kupinga harusi inayotarajiwa kufanyika baadaye wiki hii.
Licha ya uamuzi huo, haijulikani ikiwa harusi hiyo itaendelea kama ilivyopangwa au la.
Siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya Afrika Kusini vilinukuu barua inayoelezwa ni kutoka kwa mfalme ikisema sherehe hiyo imesitishwa "kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa nyumba ya kifalme."
Ndoa za wake wengi zinatambuliwa nchini Afrika Kusini ikiwa tu zitasajiliwa kama harusi za kitamaduni.
Mfalme wa Wazulu hana mamlaka rasmi ya kisiasa na jukumu lake kama mfalme Afrika Kusini kwa kiasi kikubwa ni la kitamaduni tu, lakini bado ana ushawishi mkubwa na hupata bajeti ya kila mwaka inayofadhiliwa na serikali ya dola milioni kadhaa.
Kabla ya kutawazwa, mfalme ali muoa Mayisela mwaka 2021 kwa ndoa ya kiraia/kiserikali.
Katika mabishano yake ya kisheria yaliyosikilizwa katika mahakama kuu siku ya Jumatatu, malkia kupitia wakili wake alisema mfalme hawezi kuoa mtu mwingine yeyote kwani ndoa yao bado iko hai.
Chini ya sheria ya Afrika Kusini, ndoa ya serikali lazima ivunjwe au igeuzwe kuwa ya kitamaduni kabla ya mwanaume kuoa wake wengine.
Katika kukataa ombi la kusitisha ndoa ya mfalme na Nomzamo Myeni, Jaji Bongani Mngadi amesema kwa vile malkia amesharidhia wazo la mumewe kuoa wanawake wengine, hawezi kuzuia ndoa hiyo kutofanyika.
Kulingana na kile kilichosemwa mahakamani siku ya Jumatatu, wanandoa hao walikubali mwaka jana kubadilisha ndoa yao ya kiraia kuwa ya kitamaduni. Lakini mfalme alituma maombi ya talaka, akisema uhusiano wao umevunjika.
Tangu kutawazwa kwake Oktoba 2022, kumekuwa na utata kuhusu baadhi ya maamuzi ambayo Mfalme Misuzulu ameyafanya.
Mwezi Desemba, aliisimamisha kazi bodi ya Ingonyama Trust, ambayo inamiliki na kudhibiti ardhi kubwa ya kijamii huko KwaZulu-Natal, ambayo inaelezwa ipo kwa manufaa na ustawi wa jamii chini ya uongozi wa mfalme.
Mfalme Misuzulu ndiye mdhamini pekee na mwenyekiti wa hazina lakini hana mamlaka ya kuajiri au kuwafuta kazi wajumbe wa bodi.
Hivi karibuni pia amewafuta kazi wasaidizi wake wawili wa karibu, akiwemo waziri mkuu wake wa utamaduni, na kuwaweka wengine haraka - hatua ambayo iliibua taharuki miongoni mwa watu wake wa karibu.
Ufalme wake pia unahojiwa na baadhi ya watu na kesi ya kisheria inaendelea kupinga kutambuliwa kwake kama mfalme na serikali.
Alirithi kiti cha hicho mapema kuliko ilivyotarajiwa baada ya babake, Mfalme Goodwill Zwelithini, kufariki wakati wa janga la Covid mwezi Machi 2021 kutokana na matatizo yanayohusiana na kisukari.
Zwelithini alikuwa mfalme aliyetawala muda mrefu zaidi katika taifa la Wazulu, akiwa amehudumu kwa takriban miaka 50.
Polisi wa Afrika Kusini wanamsaka mshukiwa mkuu katika sakata la mgodi wa Stilfontein
Polisi nchini Afrika Kusini wameanzisha msako wa kumsaka mwanaume anayedaiwa kuwa ni mhusika mkuu, ambaye anatuhumiwa kuendesha shughuli katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa ambapo maiti 78 zilitolewa wiki iliyopita.
Jeshi la polisi linasema maafisa walimsaidia James Neo Tshoaeli, raia wa Lesotho, anayejulikana kama Tiger, kutoroka baada ya kuvutwa kutoka kwenye mgodi wa Stilfontein.
Zaidi ya wachimbaji haramu 240 walitolewa wakiwa hai katika mgodi huo baada ya polisi kuzuia chakula na maji kwa miezi kadhaa katika jaribio la kuwalazimisha kutoka nje ya mgodi.
Taarifa ya polisi siku ya Jumatatu inasema, baadhi ya wachimba migodi wanamshutumu Tshoaeli kwa kuhusika na "vifo, kuwashambulia na kuwatesa" katika mgodi huo.
Tshoaeli pia anadaiwa kujilimbikizia na kuficha chakula mbali na wachimba migodi wengine, ambao wengi wao walionekana wamedhoofika walipotoka shimoni.
Kamishna wa polisi Patrick Asaneng amesema watu watafukuzwa kazi punde tu watakapowapata maafisa waliomsaidia Tshoaeli kutoroka.
Baada ya miezi kadhaa polisi kufunga shimo hilo huko Stilfontein, mahakama iliiamuru serikali wiki iliyopita kuwezesha shughuli ya uokoaji.
Wachimbaji hao ambao wengi wao ni wahamiaji wasio na hati walikuwa chini ya ardhi tangu Novemba mwaka jana, wakati polisi walipoanzisha operesheni nchi nzima kulenga uchimbaji haramu wa madini.
Chama cha wafanyakazi na wanaharakati wa haki za binadamu wameishutumu serikali kwa kusimamia "mauaji."
Lakini polisi wamejitetea, wakisema walikuwa wakishughulikia uhalifu na wale wanaosimamia uchimbaji haramu wa madini na kudhibiti mtiririko wa vifaa, walijaribu kuwazuia watu wasitoke nje.
Pia unaweza kusoma:
Papa asema mpango wa Trump wa kuwafukuza wahamiaji ni wa kuchukiza
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema mipango ya Donald Trump ya kuwatimua wahamiaji wasio na vibali katika ardhi ya Marekani utakuwa wa kuchukiza ikiwa utatimizwa.
Akizungumza na kipindi cha Televisheni huko Italia kutoka katika makazi yake ya Vatikani, Francis amesema, “hilo siyo sahihi. Sivyo unavyotatua matatizo.”
Trump ameahidi kuanza zoezi kubwa la kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali nchini Marekani punde tu atakapoingia madarakani.
Katika ujumbe kwa Trump uliosambazwa siku ya Jumatatu, Papa Francis alimpa "salamu" na kumtaka aongoze jamii bila ya "chuki, ubaguzi au kutengwa" na kukuza "amani na upatanisho kati ya watu."
Papa anajulikana kwa kuwa na mtazamo chanya kuhusu wahamiaji. Wakati wa hadhara ya umma Agosti iliyopita, alisema "kuunda mipango kwa njia zote ili kuwafukuza wahamiaji" ni "dhambi kubwa."
Mwaka 2016, kabla ya uchaguzi wa kwanza wa urais uliompa ushindi Trump, Papa Francis alisema "mtu anayefikiria tu kujenga kuta ... na sio kujenga madaraja, sio Mkristo."
Akizungumzia ahadi ya Trump ya kujenga ukuta kwenye mpaka wa Mexico ili kuwazuia wahamiaji kusafiri kwenda Marekani, Francis alisema: "Nasema kwamba mtu huyu si Mkristo ikiwa amesema hivyo."
Francis na Trump baadaye walikutana wakati Trump na familia yake walipotembelea Roma mwaka 2017.
Kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2024, Papa alikataa kusema ni nani anataka watu wampigie kura kati ya Trump au mpinzani wake wa chama cha Democratic, Kamala Harris, na kusema watu wachague "uovu hafifu" kulingana na uwelewa wao.
Wakati wa mahojiano ya jana jioni, Francis pia aligusia suala la uhamiaji huko Ulaya, akisema kuna "ukatili mwingi" na kila mtu "ana haki ya kubaki nyumbani na haki ya kuhama."
Papa pia aliongeza kuwa baadhi ya nchi za kusini mwa Ulaya zinazopokea wahamiaji "hazina watoto na zinahitaji wafanyakazi."
"Katika baadhi ya nchi hizi, kuna vijiji vizima ambavyo havina watu. Sera nzuri ya wahamiaji inaweza kuzisaidia nchi kama Italia na Uhispania pia," alisema.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Francis aliulizwa kuhusu vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati na kusema hajui ni kwa nini kuleta amani limekuwa jambo gumu sana.
Francis, 88, amekuwa kwenye wadhifa huo tangu 2013, alipochaguliwa kumrithi Papa Benedict XVI.
Pia unaweza kusoma:
Trump aahidi hatua za haraka kutengua sera za Biden
Katika mkesha wa kurejea White House, Donald Trump ameahidi kutia saini amri nyingi za kiutendaji zitakazo tengua sera za Biden.
Mrepublikan huyo ameahidi kuchukua hatua juu ya masuala mengi, kwa kutumia mamlaka yake ya urais, ikiwemo kuzindua mpango wa kuwahamisha wahamiaji wasio na vibali na kupunguza kanuni za kulinda mazingira.
Trump anatarajiwa kusaini zaidi ya maagizo 200 leo. Haya yatajumuisha maagizo ya kiutendaji, ambayo yatapaswa kuwa sheria, na matangazo mengine ambayo sio ya kisheria.
Trump aliahidi sera ambazo zitaongeza programu za kijasusi kwa kutumia akili bandia, kuunda Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge), kuweka hadharani taarifa kuhusiana na mauaji ya John F Kennedy mwaka 1963, kuliamuru jeshi kuunda ngao ya ulinzi wa anga ya Iron Dome na kuondoa sera za kuajiri watu tofauti, usawa na ushirikishwaji katika jeshi.
Pia aliwaambia wafuasi wake atawazuia wanaume waliobadili jinsia kushindana katika vipengele vya michezo ya wanawake na kurudisha udhibiti wa elimu kwa serikali za majimbo ya Marekani.
Trump pia anatarajiwa kuzungumzia uhamiaji, lakini wataalamu wanasema ahadi yake ya kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji wasio na vibali itakabiliwa na vikwazo vikubwa, na uwezekano wa kugharimu mabilioni ya dola.
Pia unaweza kusoma:
Watu wanane wafariki kwa moto katika nyumba ya kutunzia wazee
Watu wanane wamefariki na saba wamejeruhiwa katika moto uliotokea katika nyumba ya wazee nje ya mji wa Belgrade huko Serbian siku ya Jumatatu.
Serikali kupitia runinga ya taifa ya Serbia RTS, inasema moto huo umesababishwa na uchomaji moto wa makusudi.
Moto ulianza asubuhi huku watu 30 wakiwa katika nyumba hiyo, imeripoti RTS, ikimnukuu mkuu wa idara ya hali ya dharura, Luka Causevic.
Moto ulizimwa na majeruhi wote walipelekwa katika hospitali za Belgrade. Mwanamke mmoja yuko katika hali mbaya katika mashine ya kupumua, imeripoti RTS.
Ofisi ya waendesha mashtaka imesema moto huo ulisababishwa na mmoja wa wazee hao ambaye alikuwa miongoni mwa waliofariki.
Mke wa Trump azindua sarafu yake ya mtandaoni
Mke wa rais anayekuja, Melania Trump amezindua sarafu yake ya mtandaoni usiku wa kuamkia kuapishwa kwa mumewe kama rais wa Marekani.
Tangazo hilo linakuja saa chache baada ya Rais mteule Donald Trump naye kuzindua sarafu yake ya mtandaoni ya $Trump.
Alichapisha taarifa ya sarafu yake ya $MELANIA kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.
Kulingana na tovuti ya CoinMarketCap, $Trump ina thamani ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 12, huku ya $Melania ikiwa na thamani ya dola 1.7.
Katika siku za nyuma Trump aliwahi kuiita sarafu ya mtandaoni kuwa ni utapeli, lakini wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2024 alikuwa mgombea wa kwanza wa urais kukubali michango kupitia sarafu hizo za kidijitali.
Katika kampeni, Trump pia alisema ataunda hifadhi ya kimkakati ya sarafu ya bitcoin na kuteua wadhibiti wa fedha ambao wana mtazamo chanya kuhusu sarafu za mtandaoni.
Kufuatia ushindi wa Trump, sarafu ya bitcoin ilipanda thamani. Na kwa sasa bitcoin moja ni sawa na dola ya Marekani 107,000, kulingana na Coinbase.
Sarafu nyingine, ikiwa ni pamoja na dogecoin - ambayo imepigiwa upatu na mfuasi wa Trump, bwana Elon Musk - pia imeongezeka thamani mwaka huu.
Chini ya Rais Joe Biden, wasimamizi wa fedha walieleza wasiwasi wao kuhusu sarafu za mtandaoni wakija utapeli na utakatishaji wa pesa na wakakabiliana na kampuni za sarafu hizo za kidigitali.
Pia unaweza kusoma:
Kuapishwa kwa Trump 2017 katika picha
Miaka minane iliyopita, Donald Trump aliingia madarakani kama rais wa 45 wa Marekani.
Hivi ndivyo ilivyokuwa: