Jeshi la
wanamaji na anga la Sri Lanka limetumwa kuwaokoa mabaharia wa Iran,
ambao walituma ishara ya dharura baada ya meli yao kuanza kuzama karibu na
kisiwa hicho, mamlaka ya Sri Lanka yanasema.
Waziri wa
mambo ya nje, Vijitha Herath, aliambia bunge kwamba ishara ya kutokea kwa hatari iliyojituma kutoka kwa meli "IRIS Dena" iliwafikia alfajiri.
Inasemekana kulikuwa na watu 180 ndani ya meli hiyo.
Herath amesema
mabaharia 30 waliojeruhiwa waliokuwa ndani ya meli hiyo wamesafirishwa hadi
hospitalini katika bandari ya Galle nchini Sri Lanka.
Chanzo cha
kuzama kwa meli hiyo hakijulikani. Mbunge wa upinzani aliuliza kama meli hiyo
ilishambuliwa kwa bomu kama sehemu ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi
ya Iran - hakuna jibu rasmi lililotolewa.
Watu 140 hawajulikani
walipo baada ya meli ya Iran kuzama pwani ya Sri Lanka
Wakati huo huo, jeshi la
wanamaji la Sri Lanka limethibitisha kuwaokoa watu 32 baada ya kupokea simu ya
dharura kutoka kwa meli ya wanamaji ya Iran 'IRIS Dena' mapema asubuhi ya leo.
Budhika
Sampath, msemaji wa jeshi la wanamaji la Sri Lanka anasema: "Ingawa
ilikuwa nje ya maji yetu, ilikuwa ndani ya eneo letu la utafutaji na uokoaji.
Kwa hivyo tulilazimika kuchukua hatua kulingana na wajibu wa kimataifa."
Anaongeza
kuwa: "Tuliwakuta watu wakielea juu ya maji, tukawaokoa, na baadaye
tulipouliza tuligundua kuwa watu hao walikuwa wa meli ya Iran."
Pia anasema
kwamba kulingana na nyaraka za meli hiyo watu 180 wanaaminika kuwa ndani yake,
ingawa idadi kamili ya waliopotea haijulikani.
Msemaji huyo
anasema wakati wa kuanza kwa shughuli za uokoaji hawakuona chombo hicho lakini
waliona viraka vya mafuta juu ya maji na maboya ya kuokoa maisha yakielea.
Pia
anaiambia BBC kwamba anakataa ripoti za shambulio la manowari lililosababisha
kuzama, na kwamba chanzo cha ajali hiyo hakijulikani.