Iran yaapa kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Haniyeh

Rais wa Irani Masoud Pezeshkian anasema ataifanya Israel "ijutie" mauaji ya "uoga" ya Haniyeh, akiongeza kuwa Iran "italinda uadilifu wa eneo lake, fahari ya heshima na utu".

Muhtasari

  • Ukraine yazima shambulio 'kubwa' la ndege zisizo na rubani za Urusi
  • Iran yaapa kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Haniyeh
  • Nani anaweza kuchukua nafasi ya Haniyeh?
  • Nyimbo za hasira huku Wapalestina wakiandamana baada ya kifo cha Haniyeh
  • Timu za dharura zafanya msako kwenye vifusi kumtafuta kamanda wa Hezbollah
  • DRC na Rwanda wakubaliana kuhusu amani
  • Vita vya Ukraine: Urusi yadundua droni 19 za Ukraine
  • Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan anusurika katika jaribio la mauaji
  • Ngedere na Bundi wavuruga usafiri wa treni ya SGR
  • Kuuawa kwa kiongozi wa Hamas kunaisongesha Mashariki ya Kati 'karibu na vita'
  • Ismail Haniyeh alikuwa nani?
  • Harris anakaribia kumchagua mgombea mwenza wake na hawa ndio wanaozingatiwa
  • Kifo cha Haniyeh 'kinaifanya dunia kuwa mahali salama' - Waziri wa Israel
  • Israel inafanya 'tathmini ya hali', asema msemaji wa jeshi
  • Mauaji ya Haniyeh 'hayatapita bila kulipizwa kisasi' - afisa wa Hamas
  • Mauaji ya Ismail Haniyeh: Tunachojua kufikia sasa
  • 'Israel ilimuua Ismail Haniyeh kwa shambulizi la anga'-Hamas
  • Viongozi wengine wa Hamas ni akina nani?
  • Iran yasema inachunguza kifo cha Haniyeh
  • Maandamano yaendelea Venezuela huku hasira ikiongezeka kwa matokeo ya uchaguzi yenye utata
  • Israel yadai kumuua kamanda mkuu wa Hezbollah katika shambulizi la Beirut

Moja kwa moja

Na Asha Juma ,Yusuf Jumah & Dinah Gahamanyi

  1. Imekuwa siku ya matukio katika Mashariki ya Kati, lakini kwa sasa tunakomea hapa tukikuacha na taarifa hii kuhusu shambulio 'kubwa' la droni za Urusi:

  2. Ukraine yazima shambulio 'kubwa' la ndege zisizo na rubani za Urusi

    b

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Makumi ya ndege zisizo na rubani zilidunguliwa na makombora ya ulinzi wa anga juu ya mji mkuu

    Ukraine inasema imezuia "mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi" yaliyofanywa na Urusi tangu kuanza kwa vita.

    Mifumo ya ulinzi wa anga ilidungua ndege zisizo na rubani 89 zilizotengenezwa na Iran na kombora lingine usiku kucha, jeshi la wanahewa la Ukraine lilisema Jumatano.

    Mji mkuu wa Kyiv ndio uliokuwa shabaha kuu ya shambulio hilo. Majengo katika jimbo hilo yaliharibiwa na vifusi vilivyoanguka lakini hakukuwa na ripoti za majeruhi.

    Shambulio hilo linakuja zaidi ya miezi 29 baada ya Urusi kuivamia Ukraine kikamilifu.

    Miilipuko ya mabomu ya takriban kila siku imeweka ulinzi wa anga wa nchi hiyo katika hali ya tahadhari wakati wote.

  3. Iran yaapa kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Haniyeh

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Haniyeh, kushoto, alikutana na rais mpya wa Iran wiki hii

    Rais wa Irani Masoud Pezeshkian anasema ataifanya Israel "ijutie" mauaji ya "uoga" ya Haniyeh, akiongeza kuwa Iran "italinda hadhi ya eneo lake, fahari ya heshima na utu".

    Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP, rais wa Iran alimtaja Haniyeh kama "kiongozi shupavu".

    Kiongozi huyo wa kisiasa wa Hamas, ambaye yuko Qatar, alikuwa akizuru Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais wa Pezeshkian.

    Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei pia anasema kulipiza kisasi kifo chake ni "wajibu wa Tehran", akiongeza kuwa Israel - ambayo haijadai kuhusika - ilitoa sababu za "adhabu kali".

    Soma zaidi:

  4. Nani anaweza kuchukua nafasi ya Haniyeh?

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mchakato wa urithi unaweza kuwa wa machafuko na huenda usiwe wa haraka. Unaweza kufungua njia kwa watu wenye itikadi kali zaidi wanaiounga mkono Iran kuiongoza Hamas.

    Mmoja wa watu wanaoweza kuchukua nafasi hiyo ni Yehiya Sinwar - mkuu wa sasa wa kikundi cha Hamas katika Ukanda wa Gaza. Anaaminika kuwa ndiye mpangaji mkuu wa shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel la tarehe 7 Oktoba 2023.

    Na kuna angalau maafisa wawili waandamizi wa Hamas ambao wanaweza kujitokeza kumrithi Haniyeh.

    Khaled Meshaal , anayeonekana kuwa asiyekuwa na itikadi kali sana, anaweza kuwa anajiandaa kuchukua changamoto ya uongozi. Kwa hakika, alikuwa ameiongoza Hamas kwa miaka mingi kabla ya Haniyeh - lakini daima amekuwa na mahusiano magumu na Iran.

    Mgombea mwingine anayetarajiwa ni Zaher Jabareen , ambaye anayehusika na wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel. Anaweza kuwa na fursa muhimu katika mazungumzo yanayoendelea juu ya ubadilishanaji wa wafungwa na Israeli.

    Viongozi hao watatu wa Hamas ni manaibu wa sasa wa Haniyeh.

  5. Nyimbo za hasira huku Wapalestina wakiandamana baada ya kifo cha Haniyeh

    g
    Maelezo ya picha, Watu wakkiandamana katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu baada ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh kuuawa mjini Tehran.

    Huku maduka yakiwa yamefungwa na jua la adhuhuri likiwaka, Wapalestina wawameingia barabarani katikati mwa Ramallah ili kuonyesha hasira zao.

    Ramallah, ambayo ni makao ya Mamlaka ya Palestina inayotawaliwa na Fatah, sio ngome hasa ya Hamas.

    Maandamano hayakuwa makubwa ya mamia ya watu

    Lakini hakuna mtu aanayeweza kuwa na shaka hisia za hasira, hisia ya mshtuko na hasira, iliyotokana na mauaji ya Ismail Haniyh.

    Mabango ya kijani ya Hamas yalipandishwa juu - lakini kwa idadi kubwa - zilionekana rangi nyeusi , nyeupe, kijani na nyekundu, bendera ya Palestina.

    Watoto walipanda mabega ya baba zao, wakiwa wamebeba bunduki za mashine kuchezea.

    Nyimbo za ukaidi zilisikika mitaani. Lakini kuna wasiwasi wa kweli hapa pia. Wapalestina wanahisi kwamba mzozo mpana zaidi unaweza kuzuka, ambao unaweza kuukumba Ukingo wa Magharibi.

    Wanahisi kwamba hivi ndivyo serikali ya mrengo wa kulia ya Benjamin Netanyahu inataka.

    "Nadhani serikali ya Israel ndiyo kwanza imefanya kosa moja kubwa katika maisha yake," mwanasiasa wa Palestina mwenye msimamo wa wastani na mgombea urais wa zamani Mustapha Barghouti aliniambia hapo awali, alipokuwa akijiandaa kujiunga na waandamanaji.

    "Hiki kilikuwa kitendo cha kisiasa, cha jinai na kama wanafikiri kwamba kitendo hiki cha mauaji kitavunja upinzani wa Wapalestina, wamekosea kabisa."

  6. Timu za dharura zafanya msako kwenye vifusi kumtafuta kamanda wa Hezbollah

    g
    Maelezo ya picha, Hezbollah wanasema Shukr alikuwa ndani ya jengo hilo - lakini hawajathibitisha kifo chake

    Vitongoji vya kusini mwa mji wa Dahiya Beirut vimezingirwa na kuna uwepo mkubwa wa wanachama wa kundi la Hezbollah na wanajeshi wa jeshi la Lebanon wakimsaka kwenye vifusi Fuad Shukr, kamanda anayedaiwa kuuawa na Israel

    Maduka yamefungwa na huduma za dharura vinaendelea zinatafuta mwili wake kwenye vifusi vya jengo lililopigwa na makombora Jana.

    Inaaminika kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Hezbollah kulengwa katika ngome yake huko Beirut, lakini eneo kabla ya mzozo wa sasa eneo hilo lilikumbwa na sahmbulio mnamo mwezi Januari, ililomuua afisa wa juu wa Hamas.

    Katika taarifa yake asubuhi ya leo, Hezbollah inasema kamanda mkuu aliyelengwa alikuwa ndani ya jengo hilo wakati shambulio hilo lilipotokea jana, kabla ya jua kutua, lakini haikuthibitisha kuwa aliuawa, kama ilivyotangazwa na jeshi la Israel.

    Bado hatujui jinsi Hezbullah itajibu lakini uhakika ni kwamba italipiza kisasi.

  7. DRC na Rwanda wakubaliana kuhusu amani

    h

    Chanzo cha picha, @Angola_Mirex

    Maelezo ya picha, Mawaziri Thérèse Kayikwamba (kushoto) na Olivier Nduhungirehe (kulia) wakiwa na Tete Antonio kati yao.

    Katika mkutano wa kwanza uliowaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa DR Congo na Rwanda, viongozi hao wamekubaliana kuhusu makubaliano ya amani "kati ya pande zinazozozana mashariki mwa DRC" ambayo yataanza kutekeleza Jumapili tarehe 04 mwezi ujao wa Agosti.

    Ni uamuzi uliotolewa katika kikao kilichofanyika Luanda, Angola Jumanne kati ya Thérèse Kayikwamba Wagner upande wa Kongo na Olivier Nduhungirehe wa Rwanda, akiungana na mwenzao Tete Antonio wa Angola.

    Katika matangazo yaliyochapishwa na wizara za pande zote mbili, Rwanda na DRC, walisema kuwa tukio hilo litadhibitiwa na chombo cha pamoja cha ufuatiliaji wa masuala ya usalama kati ya Rwanda na Congo.

    Rwanda inasema kuwa "bado inaendelea kuwa na nia ya kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo kwa kutatua vyanzo vya mzozo huu".

    Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwasaidia wapiganaji wa M23, na Rais Félix Tshisekedi aliendelea kusema kwamba hatazungumza na M23, akisema kwamba Rwanda iko nyuma yake. Rwanda inakana shutuma hizo.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Vita vya Ukraine: Urusi yadundua droni 19 za Ukraine

    f

    Chanzo cha picha, YASUYOSHI CHIBA

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi inadai kuwa ndege 19 zisizo na rubani za Ukraine na kombora moja zilidunguliwa usiku kucha katika maeneo mbalimbali ya Urusi na Crimea.

    Ujumbe wa wizara ya ulinzi katika mitandao ya kijamii umesema kuwa ndege 11 zisizo na rubani zilidunguliwa katika eneo la Belgorod usiku, nne katika eneo la Bryansk na moja katika maeneo ya Kursk, Kaluga, Rostov na Crimea.

    Wizara hiyo inasema pia kwamba "kombora lililoongozwa na Neptune-MD liliharibiwa katika eneo la Kursk."

    Gavana wa jimbo la Kursk Alexey Smirnov aliandika katika telegramu usiku kuhusu moto uliowaka kutokana na shambulio la Ukraine katika kituo fulani karibu na Kursk.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan anusurika katika jaribio la mauaji

    TH

    Chanzo cha picha, AP Via Getty

    Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Jeshi la Sudan, amenusurika jaribio la mauaji lililosababisha vifo vya watu watano.

    Msemaji wa jeshi Nabil Abdallah aliambia BBC kuwa jenerali na makamanda wote waliokuwepo wako salama.

    Alilaumu Vikosi vya (RSF) kwa shambulio hilo na kulitaja kundi hilo kuwa 'hasimu pekee kwa jeshi’

    Jenerali Burhan alikuwa akihudhuria sherehe ya kufuzu kwa wanajeshi kutoka vyuo vya anga na majini huko Jebit, mashariki mwa Sudan.

    Makombora mawili yalilenga eneo hilo mwishoni mwa tukio.

    Wanajeshi wa RSF hawajatoa tamko lolote kuhusu shambulio hilo.

    Unaweza pia kusoma

  10. Ngedere na Bundi wavuruga usafiri wa treni ya SGR

    TH

    Bundi na Ngedere watajwa kuwa chazo cha kukwamisha usafiri wa treni baada ya kutokea kwa hitilafu ya umeme kati ya stesheni ya Kilosa na Kidete mkoani Morogoro.

    Jana – 30 Julai 2024 – treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma ililazimika kusimama njiani kwa takribani saa mbili kutokana na hitalafu hiyo ya umeme ambayo iliathiri kituo cha kupozea umeme namba 7 cha Godegode majira ya usiku.

    “Taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na Wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system)” imesema taarifa ya Shirika la Reli Tanzania likiomba radhi wasafiri kwa usumbufu.

    TRC imesema hitilafu hiyo ilitatuliwa majira ya saa sita usiku na kuwezesha treni kuendelea na safari ambapo iliwasili Dodoma dakika chache kabla ya saa nane usiku.

    Taarifa hii imeibua maoni mbali mbali mitandao wengi wakionesha kustaajabishwa na sababu za hitilafu zilizotolewa.

    “Daah! Huu mradi nina wasiwasi nao sana. Yakija kutokea ya Mabasi ya Mwendokasi nitaamini kweli shida tuliyonayo kama taifa itachukua miaka 100 kuwa serious na mambo ya msingi” aliandika Joel Ntile, mtumiaji wa Twitter.

    “Si mlisema treni inauwezo wa kuhifadhi umeme wa kutosha kutumia masaa kadhaa??” alihoji @INFLUENCERjr

    Safari za treni kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma ilianza rasmi tarehe 25 Julai 2024 baada ya kutanguliwa na ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro iliyoanza 14 Juni 2024.

    Mwanzoni mwa mwezi Julai, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilisema zaidi ya watu 4000 wanatumia treni hiyo kila siku kwa safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro, idadi iliyotarajiwa kuongezeka baada ya safari za kati ya Dar es Salaam na Dodoma kuanza.

    Kesho Agosti Mosi, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi safari hizi za treni na kusafiri kwa treni hiyo ya reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Kuuawa kwa kiongozi wa Hamas kunaisongesha Mashariki ya Kati 'karibu na vita'

    Mauaji ya kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh yamelileta eneo hilo karibu na vita vya pande zote kuliko wakati mwingine wowote hapo awali, Nader Hashemi, profesa wa Masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Georgetown, anaiambia BBC.

    "Hili ni tukio kubwa," anasema. "Nadhani inaathiri pia matukio ya Lebanon kwa sababu saa chache tu zilizopita Israel ilijaribu kumuua kiongozi mkuu wa Hezbollah kusini mwa Beirut na dhana ilikuwa kwamba Iran na Hezbollah hazikuwa na nia ya kuzidisha hali kuwa mbaya zaidi."

    Lakini mauaji ya Haniyeh yamebadilisha mtazamo huo, anaongeza. "Sasa Iran imepata motisha ya kujaribu na kuzidisha mzozo huu."

    Israel jana ilidai kumuua Fuad Shukr, kiongozi mkuu wa kundi linalojihami la Hezbollah.

    Rais wa Palestina analaani vikali mauaji - vyombo vya habari vya serikali

    Wakati huo huo, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ametaja mauaji ya Haniyeh kuwa "kitendo cha woga na tukio hatari".

    Pia ametoa wito kwa Wapalestina "kuungana, kuwa na subira na imara wakati wa uvamizi wa Israel" katika taarifa iliyotolewa na shirika la habari la serikali Wafa.

    Mamlaka ya Palestina ya Abbas inatawala Ukingo wa Magharibi kwa kiwango fulani huku Israel ikidhibiti wa jumla wa eneo hilo.

    Soma zaidi:

  12. Ismail Haniyeh alikuwa nani?

    Sebastian UsherMchambuzi wa Mashariki ya Kati

    TH

    Chanzo cha picha, EPA

    Alizaliwa katika kambi ya wakimbizi huko Gaza mwaka 1963, Ismail Haniyeh alikuwa mwanachama muhimu wa Hamas tangu kuanzishwa kwake.

    Alifungwa na Israel mara kadhaa na wakati fulani alifukuzwa kwenda kuishi Lebanon kusini kwa miezi sita.

    Mnamo 2003, alinusurika jaribio la mauaji la Israeli, pamoja na mwanzilishi wa Hamas.

    Miaka mitatu baadaye, alikuwa waziri mkuu wa Palestina kwa muda mfupi baada ya Hamas kushinda uchaguzi - lakini mpasuko mkali kati ya Hamas na kundi lingine kuu la Wapalestina, Fatah, ulifuata mwaka mmoja baadaye.

    Akizingatiwa sana kama muelewa wa uhalisia wa mambo, Haniyeh alisemekana kudumisha uhusiano mzuri na vikundi vingine hasimu vya Palestina.

    Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mwaka 2017. Katika miaka ya hivi karibuni, aliishi uhamishoni, akiishi Uturuki na Qatar.

    Alikuwa akitekeleza jukumu muhimu katika mazungumzo juu ya mpango wa kusitisha mapigano huko Gaza.

  13. Harris anakaribia kumchagua mgombea mwenza wake na hawa ndio wanaozingatiwa

    th

    Chanzo cha picha, Shutterstock

    Kamala Harris ataanza ziara ya Marekani na mgombea mwenza wake mpya wiki ijayo, kuashiria kwamba kuna uwezekano amesalia na siku chache tu kabla ya kutangaza chaguo lake.

    Idadi kubwa ya wagombea wa nafasi ya makamu wa rais wa chama cha Democratic imepunguzwa hadi kundi la watu watano, kulingana na CBS, mshirika wa BBC wa Marekani.

    Josh Shapiro, gavana wa Pennsylvania

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Gavana huyu mwenye mvuto na mashuhuri anaweza kumsaidia Bi Harris kushinda Pennsylvania - jimbo ambalo ni lazima Wanademokrasia walishinde.

    Bw Shapiro, 51, ameidhinishwa na watu mashuhuri tangu achaguliwe mwaka wa 2022 na ameingia kwenye chama cha Democrats katika jimbo ambalo lilimunga mkono Trump katika uchaguzi wa 2016.

    Alinasa vichwa vya habari vya kitaifa baada ya kufanya kazi haraka kujenga upya daraja lililoporomoka kwenye barabara kuu ya Philadelphia mwaka jana. Ukarabati huo wa haraka ulisifiwa na wengi kama njia bora ya kudhihirisha uwezo wake.

    Mark Kelly, Seneta wa Arizona

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Seneta huyo wa jimbo muhimu la kuamua mshindi ana wasifu wa kuvutia ambao unaweza kuwavutia wapiga kura wa pande zote mbili .

    Rubani wa zamani wa jeshi la Wanamaji na mwanaanga wa NASA amewahi kuwa kwa misheni kwa siku zaidi ya 50 angani kwenye misheni nyingi.

    Lakini Bw Kelly, 60, ni mpya zaidi kuhudumu Washington. Aliapishwa rasmi mnamo Desemba 2020.

    Mkewe ni Gabby Giffords, ambaye alipigwa risasi kichwani 2011 huko Arizona alipokuwa akihudumu katika Baraza la Wawakilishi.

    Bi Giffords tangu wakati huo amekuwa mmoja wa sauti zinazoongoza juu ya sheria za usalama wa bunduki, na hadithi ya kibinafsi ya wanandoa hao inaweza kuwagusa wapiga kura.

    Andy Beshear, gavana wa Kentucky

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Gavana wa Democratic amekuwa karibu na Bi Harris kwa muda mrefu.

    Bw Beshear, mwenye umri wa miaka 46, ameweza kujitengenezea maisha yenye mafanikio kama Mwanademokrasia katika jimbo ambalo Donald Trump alishinda kwa pointi 20 katika uchaguzi uliopita. Ni sifa ya kuvutia ambayo inaweza kufanya tiketi ya Kidemokrasia kuwa nzuri

    Tim Walz, gavana wa Minnesota

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Bw Walz ni kiongozi aliyejaribiwa katika vita ambaye alihudumu kwa miaka 12 katika Congress kabla ya kuwa gavana mnamo 2018.

    Amepata mnato wa kitaifa kwa kuwataja Donald Trump na JD Vance, kama watu "ajabu".

    Maneno hayo yalishikamana na Wanademokrasia kadhaa - akiwemo Bi Harris. "Yeye ni mtu wa ajabu," Bw Walz alisema kuhusu Trump wakati wa hafla ya kuchangisha pesa siku ya Jumatatu.

    Pete Buttigieg, Waziri wa Uchukuzi

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kampeni kwa Ikulu ya White House haitakuwa jambo geni kwa Bw Buttigieg.

    Kama meya wa South Bend, Indiana, alikuwa kipenzi cha kushangaza cha wapiga kura huria katika kampeni yake ya 2020 iliyoshindwa.

    Tangu wakati huo, amehudumu kama Katibu wa Uchukuzi wa shirikisho na amekuwa mmoja wa watu bora i kwa mawasiliano ya Ikulu ya White House.

    Ustadi wake katika mahojiano na mbele ya umati umekuwa ukionyeshwa kikamilifu katika wiki za hivi karibuni huku Bi Harris aakikaribia kumtaja mgombea mwenza.

    Unaweza pia kusoma

  14. Kifo cha Haniyeh 'kinaifanya dunia kuwa mahali salama' - Waziri wa Israel

    Israel haijatoa tamko rasmi kuhusu kifo cha Haniyeh lakini kumekuwa na hisia kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kama vile waziri wa turathi Amichay Eliyahu, mwanachama wa mrengo wa kulia wa Israel.

    Aliandika kwenye mtandao wa X kwamba kifo cha Haniyeh "kinaifanya dunia kuwa mahali salama".

    Eliyahu alisema kwenye mtandao wa X: “Hii ndiyo njia sahihi ya kuusafisha ulimwengu kutokana na uchafu huu,” kabla ya kuendelea kusema “hakuna tena maafikiano ya amani ya kufikirika au makubaliano ya muda, hakuna tena huruma kwa wanadamu hawa”.

    Pia alisema “kile watakachopitia” “kitaimarisha uwezo wetu wa kuishi kwa amani na wale wanaotaka amani”.

    IDF inasema haitatoa maoni

    Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Israeli limeambia vyombo kadhaa vya habari - ikiwa ni pamoja na CNN na shirika la habari la Agence France-Presse - kwamba halitajibu ripoti za vyombo vya habari vya kigeni kuhusu kifo cha Haniyeh.

    Soma zaidi:

  15. Israel inafanya 'tathmini ya hali', asema msemaji wa jeshi

    Bado hatujapata jibu la moja kwa moja kutoka kwa Israeli kuhusu kifo cha Haniyeh.

    Lakini Daniel Hagari, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), anasema kwamba "hakuna mabadiliko katika sera ya ulinzi wa nyumbani".

    Katika chapisho kwenye X, aliandika: "Kwa wakati huu, IDF inafanya tathmini ya hali ilivyo. Ikiwa mabadiliko yoyote yataamuliwa, tutaarifu umma mara moja."

    Urusi na Uturuki zashutumu muaji ya kiongozi wa Hamas

    Sasa tunasikia maoni kutoka nchi nyingine kuhusu habari za asubuhi hii.

    Wizara ya mambo ya nje ya Urusi inaelezea mauaji ya Haniyeh kama "mauaji yasiyokubalika kabisa ya kisiasa", kulingana na shirika la utangazaji la serikali Ria.

    Naibu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mikhail Bogdanov, anasema kifo cha kiongozi wa Hamas "kitasababisha kuongezeka zaidi kwa mvutano".

    Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Uturuki pia inalaani "mauaji ya aibu huko Tehran", ikisema katika taarifa iliyonukuliwa na Reuters kwamba "shambulio hili pia linalenga kueneza vita vya Gaza katika mwelekeo wa kikanda".

  16. Mauaji ya Haniyeh 'hayatapita bila kulipizwa kisasi' - afisa wa Hamas

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ismail Haniyeh

    Afisa mkuu wa Hamas ameapa kwamba kundi hilo litajibu mauaji ya Haniyeh.

    Moussa Abu Marzouk aliutaja uvamizi huo kuwa "kitendo cha woga ambacho hakitapita bila kulipizwa kisasi," kulingana na televisheni ya Al-Aqsa inayoendeshwa na Hamas.

    Mauaji mengine ambayo Iran inasema Israel imetekeleza katika ardhi yake

    Israel na Iran zimekuwa katika vita nyuma ya pazia kwa muda mrefu - mara nyingi zikishambuliana bila kukiri kuhusika.

    Lakini Iran inaamini kuwa Israel pia imefanya mauaji kadhaa yaliyolengwa katika ardhi yake.

    Baadhi ya kesi zinazojulikana zaidi ni pamoja na kuuawa kwa mwanasayansi mkuu wa nyuklia wa Iran Mohsen Fakhrizadeh kwa kutumia silaha za kuongozwa na vifaa maalum mnamo 2021, na kupigwa risasi kwa Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi ya Iran, Kanali Sayad Khodai, huko Tehran mnamo mwezi Mei 2022.

    Awali, Israel iliapa kumaliza uongozi wa Hamas

    Baada ya mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba yaliyotekelezwa na Hamas - ambayo yaliua watu 1,200 na mamia ya wengine kuchukuliwa mateka - viongozi wa Israel waliapa "kuliangamiza kundi la Hamas".

    Watu kadhaa wakuu wa Hamas wanaaminika kuuawa na Israel tangu wakati huo - ikiwa ni pamoja na naibu kiongozi wa kisiasa Saleh al-Arouri na Marwan Issa, naibu kamanda wa tawi la kijeshi la Hamas.

    Wana watatu wa Ismail Haniyeh na wajukuu zake wanne pia waliuawa katika shambulizi la anga la Israel huko Gaza mnamo mwezi Aprili.

    Soma zaidi:

  17. Mauaji ya Ismail Haniyeh: Tunachojua kufikia sasa

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ikiwa ndio unajiunga nasi, haya ndio tunayojua hadi sasa kuhusu kifo cha kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh:

    • Katika taarifa yake Jumatano asubuhi, Hamas ilisema Haniyeh aliuawa katika uvamizi wa Israel alipokuwa ziarani Tehran kuhudhuria kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian.
    • Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran pia limethibitisha kifo chake
    • Wanajeshi wa Israel na viongozi wakuu ndani ya serikali yake bado hawajajibu madai hayo
    • Kifo cha Haniyeh - ambaye kwa muda mrefu alikuwa akiongoza harakati za kisiasa za Hamas alipokuwa akiishi uhamishoni nchini Qatar - ni pigo kubwa kwa kundi la Palestina.
    • Iinafanyika saa chache baada ya Israel kumshambulia kamanda mkuu wa Hezbollah mjini Beirut, kulipiza kisasi shambulio la roketi katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israel mwishoni mwa juma lililoua watu 12.
    • Mashambulizi yaliyolengwa dhidi ya viongozi wawili wakuu wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika muda wa saa 24 yameibua hofu ya kutokea mzozo zaidi katika eneo hilo.
    • Afisa mkuu wa Hamas ameapa kwamba kundi hilo litajibu mauaji ya Haniyeh, na kuyataja kuwa ni "kitendo cha kioga ambacho hakitapita bila kuadhibiwa"
    • Israel imeapa mara kwa mara "kuwaangamiza" viongozi wakuu ndani ya uongozi wa Hamas, kufuatia uvamizi wa Oktoba 7 karibu na mpaka wa Israel na Gaza, ambao ulisababisha vifo vya watu 1,200 na kusababisha mamia kuchukuliwa mateka.

    Pia unaweza kusoma:

  18. 'Israel ilimuua Ismail Haniyeh kwa shambulizi la anga'-Hamas

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh aliuawa mjini Tehran, Jeshi la walinzi wa Iran limesema mapema Jumatano, na Hamas imeilamu Israel kwa shambulio hilo.

    Israel iliapa kumuua Haniyeh na viongozi wengine wa Hamas kutokana na shambulio la Oktoba 7 la kundi hilo dhidi ya Israel ambalo liliua watu 1,200 na kusababisha wengine 250 kuchukuliwa mateka.

    IDF au Jeshi la Ulinzi la Israeli limeambia vyombo kadhaa vya habari - ikiwa ni pamoja na CNN na shirika la habari la Agence France-Presse - kwamba halitajibu ripoti za vyombo vya habari vya kigeni kuhusu kifo cha Haniyeh.

    Israel mara nyingi haifanyi hivyo linapokuja suala la mauaji yanayotekelezwa na shirika lao la kijasusi la Mossad.

    Hamas imesema Haniyeh aliuawa katika shambulio la anga la 'Wazayuni kwenye makazi yake mjini Tehran' baada ya kushiriki katika hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Iran.

    "Hamas inawatangazia watu wa Palestina na watu wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na watu wote walio huru duniani, ndugu kiongozi Ismail Haniyeh kuwa shahidi," taarifa hiyo fupi ilisema.

    Katika taarifa nyingine, kundi hilo limemnukuu Haniyeh akisema kuwa kadhia ya Palestina ina "gharama" na "tuko tayari kwa gharama hizi: kuuawa kama shahidi kwa ajili ya Palestina, na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya utukufu wa taifa hili.”

    Soma zaidi:

  19. Viongozi wengine wa Hamas ni akina nani?

    Ingawa Ismail Haniyeh alichukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Hamas - kutokana na jukumu lake la kuongoza oparesheni za kisiasa za kundi la Palestina wakati akiishi uhamishoni nchini Qatar na Uturuki - kuna watu wengine wa ngazi za juu wa Hamas.

    Yahya Sinwar - ambaye kwa kiasi fulani Israel inasema alihusika na kusimamia uvamizi wa Oktoba 7 ambao uliua takriban watu 1,200 na kusababisha utekaji nyara wa zaidi ya 200 - wote wametoweka kutoka Ukanda wa Gaza, na Israeli bado inamsaka.

    Sinwar ndiye mwanzilishi wa kikosi cha usalama cha Hamas kinachojulikana kama Majd, ambacho kinasimamia masuala ya usalama wa ndani, huwachunguza watu wanaoshukiwa kuwa majasusi wa Israel na kuwasaka maafisa wa kijasusi na usalama wa Israel.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mnamo Septemba 2015, Marekani ilijumuisha jina la Sinwar kwenye orodha yake ya "magaidi wa kimataifa"

    Mohammed Deif, kiongozi asiyeweza kujulikana aliko wa tawi la kijeshi la Hamas - ambalo linajulikana kama Brigedi za Izzedine al-Qassam - ni kiongozi mwingine mkuu ambaye bado yuko kwenye orodha ya wanaosakwa zaidi na Israeli.

    Israel ilimfunga gerezani mwaka wa 2000, lakini alitoroka mwanzoni mwa uasi wa pili wa Wapalestina, au intifada mwanzoni mwa miaka ya 2000. Tangu wakati huo, hajaacha alama yoyote ya kuweza kujulikana aliko . Mara ya mwisho vikosi vya usalama vya Israel vilijaribu na kushindwa kumuua Deif ilikuwa mwaka 2014, wakati wa shambulio kwenye Ukanda wa Gaza.

    Soma zaidi kuhusu uongozi wa kundi hilo la wanamgambo hapa.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Iran yasema inachunguza kifo cha Haniyeh

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Ulinzi la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limetoa rambirambi zake kufuatia kifo cha Ismail Haniyeh mjini Tehran.

    Taarifa iliyotolewa na chombo chake cha habari cha Sepah news ilisema inachunguza "sababu na ukubwa wa tukio" na itatangaza ilichobaini baadaye.

    Iliongeza kuwa Haniyeh na mmoja wa walinzi wake "waliuawa".

    IRGC ni kikosi kikubwa cha kijeshi, kisiasa na kiuchumi nchini Iran, chenye uhusiano wa karibu na kiongozi mkuu, Ayatollah Ali Khamenei.

    Soma zaidi: