Je wajua athari za kuchelewa kukamilika kwa reli ya SGR Tanzania kiuchumi?

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) nchini Tanzania ni jambo linalongojewa kwa hamu na watanzania pamoja na nchi jirani zitakazonufaika na ujenzi wake. Ni reli yenye upana wa mita 1.435, inayotarajiwa kubeba mamilioni ya abiria na mizigo zaidi ya tani milioni 17 kwa mwaka.
Baada ya kusogezwa mbele majaribio na uzinduzi wa matumizi yake kwa zaidi ya mara tatu kwa sababu kadha wa kadha, serikali ya nchi hiyo imeweka wazi kwamba kabla ya kumalizika kwa mwezi Aprili, 2022 majaribio ya matumizi ya reli hiyo yataanza rasmi kuashiria kuanza kutumika kwa reli hii inayosubiriwa kwa muda sasa.
Wapo wanaosubiri waone tu inafananaje? Inajiendeshaje? Kasi yake ikoje? na wapo wanaosubiri ili waitumie kwa usafiri wao na wengine usafirishaji wa mizigo yao. Wote hawa wanajiuliza nini kinasogeza mbele kuanza kufanya kazi kwa reli hii?
Miaka miwili na nusu ya danadana za kukamilika kwa ujenzi wa SGR
Ujenzi wa reli hii ya kisasa kwa awamu ya kwanza kati ya Dar es salaam - Morogoro (Km 300), ulizinduliwa na Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli Aprili 12, 2017. Ilielezwa ujenzi wa mradi huu ungekamilika ndani ya miezi 30 mpaka kufikia Novemba 2019, haikuwezekana.
Uliongezwa muda wa miezi 18 mpaka Aprili, 2021, ikashindikana pia. Aliyekuwa waziri wa Ujenzi wakati huo, Leonard Chamuriho akaeleza reli hiyo ingeanza kufanya kazi ndani ya miezi minne, yaani Agosti, 2021, ikashindikana tena.
Maelezo zaidi yakaonesha ingeanza kufanya kazi Disemba, 2021, na waziri wa ujenzi na uchukuzi, Makame Mbarawa wakati akieleza mafanikio ya miaka 60 ya sekta ujenzi na uchukuzi.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Januari 17, 2022 Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa akaeleza awamu ya kwanza ya kipande cha Dar es Salaam-Morogoro utakamilika na majaribio yataanza April, 2022.
Uhaba wa fedha kulipa wakandarasi kutekeleza mradi huo na kuchelewa kwa baadhi ya malighafi ndio sababu inayotajwa na wengi kusababisha mradi huo kusogezwa mbele utekelezaji wake mara kwa mara. Lakini Msigwa anaeleza 'wale wanaotuletea maneno kwamba miradi imekwama wameula wa chuya, miradi inaendelea wakandarasi wanalipwa na itakamilika'.
Msigwa anaongeza ''kunaweza kutokea ucheleweshaji wa hapa na pale, kwenye kazi za ujenzi ni vitu vya kawaida, lakini serikali inawasimamia kwa karibu wakandarasi, kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa muda unaotakiwa,'.
Kwa sasa kipande cha Dar es Salaam kimebakiza chini ya asilimia 10 ili kukamilika. Huku nguvu ikielekezwa kuunganisha kipande cha kutoka Pugu hadi Posta, Dar es Salaam kilipo kituo kikuu, shughuli inayotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho mwa mwezi Februari, 2022.
'Tumeagiza mabehewa ya abiria 59 na vichwa vya treni 17 vya umeme kutoka Korea Kusini kwa ajili ya kuanza kutumia katika njia hii', ametamka msemaji wa Serikali.
Wakati michakato ikiendelea juu ya vipande vingine vya awamu ya tatu; Makutupora -Tabora (Km 294), awamu ya nne; Tabora - Isaka (Km 130) na awamu ya tano; Isaka - Mwanza (Km 249), tayari Serikali ya Tanzania imeagiza mabehewa 80 ambayo ni sawa na treni 10 za kisasa ziitwazo Electric Multiple Unit (EMU) kutoka Korea Kusini, hivi sasa utengenezaji wake unaendelea.
Kuchelewa zaidi kuanza kwa reli hii ni mzigo unaoepukika?
Kama alivyotanabaisha msemaji wa Serikali ya Tanzania, Msigwa kwamba kwenye ujenzi ucheleweshaji ni jambo la kawaida. Je mzigo wa ucheleweshaji huu una ukubwa gani? Ni wa nani? Na udhibiti wake ukoje?
Kwa kauli ya Msigwa, kwamba reli hii ya kisasa kwa kipande cha Dar es Salaam mpaka Kilosa, Morogoro kitaanza majaribio mwezi Aprili mwaka huu, maana yeke mradi huu utakuwa umechelewa kuanza majaribio ama kufanya kazi kwa miaka miwili na miezi miezi mitano, takribani miaka miwili na nusu kutoka ratiba iliyotangazwa April 2017.
'Kuchelewa kwa mradi huu kwa sababu yoyote ile kunaathari kiuchumi na kijamii hasa ukizingatia unajengwa kwa pesa za mkopo kwani serekali italazimika kuanza kulipa mkopo kabla hata mradi haujaanza kufanya kazi. Pili kuchelewa kwa mradi kunachelewesha Jamii kuanza kunufaika na mradi husika alisema mtaalamu wa mambo ya kijami, Profesa, Baltazari Namwata wa chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoishia Juni 30, 2020, Ucheleweshaji wa awali wa miezi 18, uliongeza gharama za ziada ya kiasi cha Dola za Marekani 11,222,653.00 sawa na zaidi ya Sh26 bilioni za kitanzania.
Julai 6, 2021 jijini Dodoma, Ummy Mwalimu, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akielezea kuhusu mafanikio ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan na Mwelekeo wa utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 alisema zimetengwa shilingi bilioni 26.07 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,043 ya vyumba vya maabara za sayansi, kwa hivyo fedha hizi zingweza kujenga maboma haya zaidi ya 1,000.
Huu ni mzigo unaoweza kuepukika kwa kuwekeza nguvu kwenye kukamilisha awamu ya kwanza kwa asilimia 100%, kabla ya kuweka miguu yote kwenye awamu zingine ukiacha kipande cha pili cha kutoka Morogoro- Makutupora (Km 422).
Kwa nini ni muhimu reli hii kuanza kazi haraka?
Kuchelewa kuanza kufanya kazi kwa reli hii, kunaikosesha Tanzania na watanzania, faida nyingi, hasa za kiuchumi na kijamii.
Reli hii katika awamu ya kwanza itapita katika mikoa ya Morogoro (Moja ya mikoa mitano mikubwa ya uzalishaji wa chakula nchini wanakozalisha sukari na mazao kama mahindi, viazi, nyanya na mpunga na baadaye kuunganishwa kwenye awamu zinazofuata na mikoa ya Dodoma wanakolima zabibu, na Singida kunakolimwa alizeti, vitunguu, pamba na ufuta.
Miundo mbinu hiyo ya reli pia itapita mkoani Tabora unaostawisha kwa wingi mazao ya mahindi, maharage, karanga, muhogo na mpunga, huku zao kubwa la biashara likiwa ni Tumbaku, hivyo utanufaika kama ilivyo kwa mikoa ya Mwanza na Shinyanga, kunakolimwa zaidi Pamba na mpunga, huku mifugo na samaki aina ya sato na sangara wakichagiza zaidi uchumi wa mikoa ya kanda ya ziwa.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Wakulima na wafanyabiashara wa mazao katika mikoa hii, wataneemeka na usafiri huu. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya mamlaka ya reli Tanzania (TRC), usafirishaji wa mizigo utaongezeka zaidi kwa sababu reli hii itaweza kubeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo mmoja. Haya ni mabilioni ya fedha.
''Tani 10,000 ni sawa na malori 500 ya mizigo, yanayopita na kuharibu barabara. Kwa mantiki hiyo, matumizi ya reli tena ya kisasa yanaokoa gharama zitokanazo na uharibifu wa barabara na wakati huo huo unaongezea kasi ya usambazaji wa mazao na mizigo mingine,'' alisema Profesa Baltazar Namwata.
Faida nyingine za reli hii ya SGR
Ukiacha usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za jirani na pia mizigo kutoka mikoa inakopita reli hii, usafiri wa SGR utachochea maendeleo ya sekta zingine za kiuchumi kama kilimo, viwanda na biashara katika mikoa husika na nchi jirani kama Kenya, DRC, Uganda, Burundi na Rwanda.
'Kuongezeka kwa shughuli za maendeleo za kisekta, kiuchumi kunaendana na ongezeko la huduma za kijamii kama ujenzi wa vituo vya afya, shule na barabara, na kuongezeka pia kwa ajira, kunakosaidia kuongeza kipato cha watu na mzunguko wa fedha, hiki ndicho hasa wananchi wanakililia na kutaka kukiona kikitokea kupitia reli hii ya SGR', anasema Dkt. Isack Kazungu, mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka chuo kikuu cha Ushirika.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Treni ya umeme kwenye reli hii itakayokwenda kwa kasi ya kilomita160 kwa saa kwa treni ya abiria, na kilomita 120 kwa saa kwa treni ya mizigo, itaokoa muda wa abiria na mizigo, kwa kuwa muda ni mali. Kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma utatumika muda wa kati ya saa 2:45 hadi saa 3 kwa treni ya kisasa ya umeme, badala ya saa 8 mpaka 9 zinazotumika hivi sasa ukisafiri kwa kutumia mabasi, au saa 10 kwa treni ya sasa.
Kwa ujumla ni reli muhimu kwa uchumi wa wa taifa la Tanzania, kutokana na uwepo wa bandari ya Dar es Salaam inayotumika sana na nchi za DRC, Uganda, Burundi na Rwanda. Kwa faida hizi, serikali ya Tanzania inao wajibu wa kuhakikisha inakamilika haraka kwa ubora uliopangwa ili kukidhi mahitaji na malengo yaliyokusudiwa.
Kuahirishwa mara kwa mara kwa kuanza majaribio hasa kwa kipande cha ujenzi cha awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaa mpaka Morogoro, kunazua maswali juu uthabiti wa kauli na umakini wa utendaji wa serikali katika kukamilisha miradi hii muhimu kama huu wa reli ya kisasa, utakaogharimu dola bilioni 1.92.
Je kauli ya sasa ya serikali, kupitia msemaji wake, Gerson Msigwa, itakuwa ya mwisho na watanzania na watumiaji wengine wa reli wa nchi jirani wanaoisubiri kwa hamu waanze kucheka? Hilo ni jambo la kungoja na kuona.













