Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Babushka Z: Ajuza wa Ukraine aliyegeuzwa nyota wa propaganda ya Urusi
Mwanamke mzee wa Ukraine anayepeperusha bendera nyekundu ya Sovieti amekuwa sura ya propaganda za Kremlin baada ya video ya kukutana kwake na wanajeshi wa Ukraine kusambaa. BBC ilimtafuta "Babushka Z" ili kujaribu kubaini ukweli wa tukio hilo.
"Sidhani wanapaswa kunitukuza. Mimi ni mwanamke wa kawaida tu. Sielewi kwa nini nimekuwa mtu mashuhuri."
Mwanamke huyo ametambuliwa kama Babushka Z - "bibi" kwa Kirusi, herufi ya Z ikiashiria alama iliyochapishwa kwenye magari ya kivita- alishangaa sana BBC ilipomuonesha picha y umaarufu wake mpya. "Sijawahi kuiona popote," anasema.
Video inamuonyesha akitembea kuelekea kwa askari wawili wa Ukraine akiwa ameshikilia bendera ya Usovieti.
Askari hao wanasema wamefika kumsaidia na kumpa mfuko wa chakula. Kisha wanachukua bendera kutoka kwake, na kuitupa chini na kuikanyaga. Kitendo hicho kinamkera mwanamke huyo, anawarudishia chakula. "Wazazi wangu walikufa kwa ajili ya bendera hiyo katika Vita vya Pili vya Dunia," anasema kwa hasira.
Kwa Kremlin, hii ni dhahabu. Ni nadra sana kwa propaganda ya Urusi kuangazia watu moja kwa moja, kwa hivyo walimtumia mwanamke huyo kama mfano usio wa kawaida kwa raia wa Ukraine ambaye anajutia kuanguka kwa Muungano wa Sovieti na kuwachukulia Warusi kuwa wakombozi.
Waukraine wengi - Hata katika maeneo yanayokaliwa na watu wanaozungumza Kirusi- hawajaunga mkono uvamizi wa Urusi, kwa hivyo kupeperusha kwake bendera ya Usovieti kulitumiwa kama uthibitisho kwamba kitendo chake kinaungwa mkono na wenyeji.
Kutoka na hilo waendesha propaganda wa Kremlin walianza shughuli zao. Ndani ya siku chache, picha ya ya mwanamke huyo - ilitumiwa kuendeleza ajenda ya Urusi na kusambazwa kila mahali mtandaoni, kutoka Moscow na Siberia hadi kisiwa cha Sakhalin mashariki ya mbali t.
Sasa anaenziwana picha yake imekuwa ikitumiwa kwenye michoro ya ukutani, mabango, kadi za posta, sanamu na vibandiko vikubwa. Nyimbo na mashairi yametungwa. Maafisa wa Urusi hata waliamua kuzindua sanamu yake huko Mariupol, mji wa Ukraine ambao umeshambuliwa kwa bomu.
Hadi hivi karibuni, hakuna aliyejua utambulisho wa kweli wa Babushka Z. Kwa kweli, hakuna mtu aliyekuwa na uhakika kama alikuwa hai.
Lakini ni mtu halisi. Jina lake ni Anna Ivanovna na tulifanikiwa kumpata Velyka Danylivka, kijiji kilichopo karibu na Kharkiv kaskazini - mashariki mwa Ukraine ambako anaishi na mume wake na mifugo yao.
Mama huyo mwenye umri wa miaka 69-anaonekana kushutuka tulipomuonyesha picha ya sanamu iliyotengnezwa kutokana na picha yake. " Yaani naonekana mzee hivi?", aliuliza. "Ni kama mgeni ananitazama!"
Lakini hadithi yake ni tofauti sana na taswira ambayo vyombo vya habari vya Urusi vimekuwa vikijenga. Yeye haungi mkono vita.
"Nawezaje kuunga mkono kuuawa kwa watu wangu? Wajukuu na vitukuu vyangu wamelazimika kukimbilia Poland. Tunaishi kwa hofu."
Lakini kwanini Anna aliwasalimia askari hao akiwa na bendera ya Uspvieti?
Anasema ameeleweka vibaya. Anadai kuwa aliwachanganya wanajeshi wawili wa Ukraine wakimpa chakula na wanajeshi wa Urusi.
"Nilifurahi kwamba Warusi wangekuja na wasipigane nasi. Nilifurahi kwamba tutaungana tena."
Anna hakuhusisha kitendo chake na mada yoyote ya kisasi ya kisiasa. Bendera nyekundu, anasema, sio bendera ya Umoja wa Kisovyeti, si ya Urusi, lakini "bendera ya upendo na furaha katika kila familia, katika kila jiji, katika kila jamhuri. Si ya umwagaji wa damu. Na yeyote anayesema vinginevyo, anakosea."
Wakati Anna akiongea, kishindo cha mara kwa mara cha mizinga na mapigano kilisikika karibu. Hakukurupuka hata mara moja - ameshaizoea.
"Ningepata nafasi ya kuzungumza na Vladimir Putin ningemwambia, umefanya makosa. Sisi ni wafanyakazi wa Ukraine, tumefanya kosa gani kupitia madhila kama haya? Sisi ndio tumeathirika zaidi."
Lakini Anna ni kizazi cha zama za Usovieti, hayuko tayari kumkosoa hadharani kiongozi wa Urusi..
"Putin ni rais. Tsar, mfalme."
Ijapokuwa amekuwa maarufu mjini Moscow, kijiji cha Anna hakijasazwa na vikosi vya Putin -kimeshambuliwa kwa mabomu mara kadhaa.
Nyumbani kwake piakumeshambuliwa - madirisha yameharibiwa, paa la nyumba limeng'olewa na vipande vya mbao vimetapakaa kila mahali.
"Hebu angalia," Anna alisema. "Hawajali watu nchini Ukraine, wanachotaka ni kunyakua ardhi yetu."
Dmytro Galko kutoka Wizara ya Utamaduni ya Ukraine anakubaliana na hilo. Anasema propaganda za Kirusi hufanya kila kitu kuwa cha mwelekeo mmoja.
"Hawajali kuhusu ukweli, hawajali watu halisi. Hawajali na Anna ni nani, au hatima yake. Ingewezekana, wangemuua, kumzika na kwenye kaburi la kumbukubu. "anasema.
Anna sasa anahofia usalama wake nchini Ukraine, anashambuliwa mtandaoni kwa sababu anaonekana kuwa anaunga mkono Urusi.
Majirani zake wote wanamtenga. Ni kijiji kidogo na kila mtu anamjua mwenzake.
"Sifurahii kuwa wamenifanya maarufu. Kwa sababu huko Ukraine, sasa wananichukulia kuwa msaliti."
Lakini ni wazi kuwa kiwango cha kweli cha umaarufu wake kinaonekana tu kwa Anna mwishoni mwa mahojiano yetu.
Tunapomuaga, anajaribu kutupa bendera yake nyekundu aipendayo.
"Sitaki shida yoyote. Sitaki watu waitumie dhidi yangu."