Ziara ya Samia Uganda: Fahamu mambo yaliyofanyika katika ziara ya rais wa Tanzania nchini Uganda

Chanzo cha picha, Ikulu mawasiliano/twitter
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Uganda Mei 10 na 11 2022 kufuatia mualiko wa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Ilikuwa ni ziara ya pili ya kiserikali ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufanya nchini Uganda tangu aingie madarakani mwezi Machi 2021.
Masuala mbalimbali yamezungumzwa katika ziara hiyo ikiwemo masuala ya nishati, biashara, usafiri, miundo mbinu na sekta ya afya.

Chanzo cha picha, IKULU MAWASILIANO/TWITTER
Haya ndiyo waliyokubaliana katika ziara hiyo.
Kushuhudia utiaji saini wa Hati mbili za ushirikiano (MoU)
Hati hizo ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400KV kutoka Masaka, Mutukula, Nyakanazi hadi Mwanza. Na hati nyingine ilikuwa ni kuhusu ushirikiano wa ulinzi na usalama.
Tanzania kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) kutoka Uganda
Katika utiaji saini huo Rais Museveni alisisitiza juu ya kushirikiana katika utengenezaji wa chanjo na dawa za binadamu na mifugo. Na Tanzania itaanza kununa dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kutoka Uganda.
Kufunguliwa kwa njia ya Mwanza Port Bell Kampala
Njia hii hapo awali ilikuwa haifanyi kazi lakini hivi sasa imeanza kufanya kazi na imepunguza kwa kiwango kikubwa muda wa safari ambapo sasa huchukua siku 4 kutoka siku 9 za awali, kutoka Mwanza Tanzania hadi Uganda.
Kupungiza gharama za usafirishaji
Kwa sasa Uganda italipa dola za Kimarekani 10 kwa roli katika kila kilometa 100 itakayopita katika njia ya Mutukula hadi Dar es Salaam
Tamko la pamoja lililotolewa na kuelezea haja ya nchi hizo mbili kushughulikia vikwazo vilivyosalia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazohusu biashara ili kuongeza kasi ya biashara kati ya Uganda na Tanzania. Viongozi hao wawili waliagiza kwamba maagizo haya yatekelezwe na wizara husika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Sukari
Suala la sukari pia lilijadiliwa ambapo Uganda iliahidi kutuma tani nyingine elfu kumi za sukari kwa Tanzania ili kukabliana na upungufu wa bidhaa hiyo nchini humo.
Kwa miaka kadhaa sasa Uganda imekuwa ikililalamikia Tanzania kwa kuweka vikwazo visivyo na kodi kwenye bidhaa za sukari na maziwa ambavyo vimezuia biashara kati ya nchi hizo mbili.
Elimu
Kuhusu elimu, ilikubaliwa kuwa Uganda itatambua shule dada nchini Uganda ili ishirikiane na Museveni Nursery and Primary School iliyopo katika Kijiji cha Nyabirezi, Wilaya ya Chato, mkoani Geita.

Chanzo cha picha, IKULU MAWASILIANO/TWITTER
Rais Samia na mwenyeji wake pia walipewa taarifa ya ushirikiano wa pamoja kuhusu usalama wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Rais huyo wa Tanzania pia aligusia mpango wa kuendeleza bomba la gesi asilia kuwa na hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya nishati.
Alisema Tanzania inampango wa kutumia kiasi cha dola bilioni 30 kuanzisha mtanbo wa gesi asilia (LNG) ambao utaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa wasfairishaji wakubwa wa nishati hiyo dunaini.
Samia alikutana na Watendaji Wakuu CEOs wa Sekta Binafsi kutoka Tanzania na Uganda.
Samia amerudi jijini Dar es Salaam siku ya Jumatano baada ya kumaliza ziara yake hiyo














