Wabunge vinara wanawake 19 wa Chadema 'kuvuliwa ubunge'

w
Maelezo ya picha, Halima Mdee

Baraza Kuu la Chadema limeunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa viti maalum, miongoni mwao ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake BAWACHA Halima Mdee.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema baada ya uamuzi wa baraza kuu, hatua inayofuata ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuandika barua ya kumtaarifu Spika wa Bunge la Tanzania kuhusu uamuzi uliofanywa na baraza kuu kwa hatua zaidi ikiwemo ya kutangazwa kuvuliwa ubunge wao baada ya taarifa hiyo kumfikia spika wa Bunge.

Awali spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson alisema kuwa hatma ya wabunge hao, itategemea matokeo michakato halali ya ndani ya chama. Kama mchakato wa usiku wa jana utaonekana halali, wabunge hao wanaweza kuvuliwa ubunge , kwa kuwa sheria ya Tanzania inaeleza iwapo mbunge atafukuzwa uanachama na chama kilichompeleka bungeni, ubunge wake utakoma.

Kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu uwepo wa wabunge hao 19 bungeni licha ya kufukuzwa uanachama, lakini Spika alisistiza pia uwepo wa wabunge hao si jambo ambalo bunge lina majibu bali Tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania ndio ina majibu.

Uamuzi umefikiwa vipi?

Umuazi huo unakuja baada ya wabunge hao 19 kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge wa viti maalumu bila kupata baraka ya chama hicho.

Walituhumiwa pia kupeleka majina yao wenyewe bila idhini ya chama jambo ambalo linatafsiriwa kama usaliti.

Kura zilizopigwa ni 423 Kura za HAPANA ni 5 (1.2%) Kura za wasiofungamana na upande wowote ni 5 (1.2%) Kura za NDIYO ni 413 (97.6%).

Wabunge hao ambao awali walifukuzwa, lakini baadaye walikata rufaa katika baraza hilo wakipinga kamati kuu kuwavua uanachama Novemba mwaka 2020.

Baada ya maamuzi hayo ya kufukuzwa uanachama, aliyekuwa mbunge wa kawe na mwenyekiti wa baraza la wanawake Halima Mdee, amesema kuwa uamuzi huo ni jambo la uhuni.

'' Kilichoendelea pale sio upigaji kura, kilichotokea pale ni uhuni, mimi ni Chadema na nitaendelea kuwa Chadema'' anasema Halima Mdee.

w
Maelezo ya picha, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020 kuisha, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vilijikuta katika njia panda ya kisiasa, si upande wa Tanzania Bara pekee, hadi Zanzibar.

Ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulikuwa na kitendawili cha ikiwa wapeleke majina ya wabunge wa viti maalum ama la.

Kitendawili hiki kilikuwa na jawabu tofauti kutoka kwa wafuasi wa chama hicho na wachambuzi wa siasa.

Mambo yaligeuka baada ya kundi la wabunge 19 wanawake kutoka Chadema kufanya uamuzi wenye utata wa kwenda bungeni na kuapishwa na kuwa wabunge wa Bunge la 12.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri wakiwemo wenyeviti wa vyama vingine vya siasa akiwemo James Mbatia NCCR Mageuzi, Hashim Rungwe - Chauma, na wawakilishi toka ACT wazalendo na CUF.

w
Maelezo ya picha, Wanachama wa Chadema idadi kubwa walipinga hatua ya wabunge hao kukalia viti maaulum bungeni.

Mgeni wa heshima kwenye mkutano alikua Robert Kyagulanyi maarufu Bob wine mwanasiasa wa upinzani kutoka nchini Uganda.

Je ni kina nani wamefukuzwa?

Halima Mdee

Esther Matiko

Grace Tendega

Cecilia Pareso

Ester Bulaya

Agnes Lambart

Nusrat Hanje

Jesca Kishoa

Hawa Mwaifunga

Tunza Malapo

Asia Mohammed

Felister Njau

Naghenjwa Kaboyoka

Sophia Mwakagenda

Kunti Majala

Stella Flao

Anatropia Theonest

Salome Makamba

Conchesta Rwamlaza