Kombe la Dunia 2022: Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia kuiwakilisha Afrika Qatar

Timu za Cameroon, Ghana, Morocco, Senegal na Tunisia zimefuzu kutoka ukanda wa Afrika kucheza fainali za kombe la dunia ziakazopigwa baadae mwaka huu huko Qatar, kufuatia matokeo yao ya michezo ya jana.

Cameroon ikishinda ugenini 2-1 dhidi ya Algeria kwa bao la jioni na kufuzu kwa bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza Algeria kushinda ugenini bao 1-0. Ghana ikaiondosha Nigeria kufuatia sare ya 1-1 ugenini, mchezo wa kwanza uliopigwa Ghana, timu hizo zilienda sare ya 0-0.

Morocco ikachafua sherehe ya kumkaribisha mwanachama mpya wa Jumuia ya Afrika Mashariki, DRC baada ya kuitandika 4-1 huko Casablanca na kuiondosha kwa jumla ya mabao 5-2 kufuatia mchezo wa kwanza mjini Kinshasa kwenda sare a 1-1.

Sadio Mane akafunga penati ya ushindi Senegal ikiondosha kwa matuta Misri baada ya kulingana kwa mabao, kila mmoja akishinda kwake kwa bao 1-0.

Baada ya sare ya nyumbani ya bila kufungana, Tunisia imesongwa mbele kwa bao la ugenini ililolipata kwenye mchezo wa awali.

Bala la Ulaya

Barani Ulaya, Poland na Ureno zimefanikiwa kufuzu baada ya kushinda michezo yao ya jana usiku. Shujaa wa Ureno alikuwa Bruno Fernandes, kiungo wa Ma aliyefunga mabao mawili, Ureno ikizaba Macedonia Kaskazini mabao 2-0.

Poland ikafuzu kwenda Qatar kwa magoli ya Robert Lewandowski na Piotr Zielinski kuwapa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sweden.

Nchi zingine zilizofuzu kutoka bara la Ulaya mpaka sasa ni pamoja na Ubelgiji, Ufaransa, England, Serbia, Uholanzi, Hispania, Croatia, Switzerland

Amerika Kusini, kati na Kaskazini

Canada ilikuwa nchi ya kwanza kufuzu kucheza kombe la dunia kutoka ukanda huu. Brazil, Argentina, Ecuador, Uruguay zimefuzu kutoka ukanda huu. Brazil ikikamilisha ratiba alfajiri ya leo kwa kuzaba 4-0 Bolivia, Argentina ikaenda sare ya 1-1 na Ecuador, Chile ikalala 2-0 dhidi ya Uruguay.

Asia

Qatar yenyewe imefuzu moja kwa moja kutokana na kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ikiungana na Korea Kusini na Iran, Japan Saudi Arabia. Iran jana imeichapa Lebanon 2-0, Syria na Iraq zikaenda sare ya 1-1 huku UAE ikiilaza Korea Kusini kwa bao 1-0.

Mambo muhimu kufahamu kuhusu Kombe la dunia mwaka huu

Droo ya ratiba ya mashindano hayo makubwa kabisa ya soka duniani itafanyika April 1 2022, ikiwa ni miezi saba kabla ya kuanza kwa mashindano hayo Novemba 21, 2022. Mpaka kufikia April 1, ni timu 29 kati ya 32 zitakuwa zimejulikana nafasi tatu kati ya hizo 32 zitapatikana mwezi Juni. Mechi zingne zitaendelea ikiwemo ya baadae usiku leo Visiwa vya Solomon vitakuwa mwenyeji wa New Zeeland.

Fainali ya mashindano hayo yatakayo shirikisha mataifa 32 inatarajiwa kupigwa Disemba 18, 2022. Hata atakuwa mashindano ya kwanza kufanyika msahriki ya kati na yakiwa ya mwisho yakayotumia mfumo wa sasa wa kushirikisha timu 32, kabla ya kuanza kwa mfumo mpya utakaoshirikisha timu 48 kuanzia fainali za mwaka 2026.

Orodha kamili ya timu zilizofuzu mpaka sasa

1: Argentina

2: Ubelgiji

3: Denmark

4: Cameroon

5: Brazil

6: England

7: Croatia

8: Ujerumani

9: Canada

10: Ecuador

11: Ufaransa

12: Japan

13: Iran

14: Morocco

15: Ghana

16: Uruguay

17: Serbia

18: Korea Kusini

19: Saudi Arabia

20: Poland

21: Ureno

22: Qatar

23: Uholanzi

24: Tunisia

25: Hispania

26: Switzerland

27: Senegal