Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
DR Congo yajiunga na EAC:Anayefaidika ni nani wakati DRC inapojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki?
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwa ni mwanachama wake wa saba na kupanua eneo la jumuiya hiyo ya kibiasharahuku ikiwezesha ufikiaji wa Bahari ya Atlantiki na kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wazungumzaji wa Kifaransa katika kile kilichoanza kama klabu ya koloni za zamani za Uingereza.
Ni mabadiliko gani yanayofanyika mara moja?
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wameidhinisha kuingizwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika umoja huo katika mkutano wa kilele siku ya Jumanne, lakini ingawa imekuwa mwanachama rasmi, hakuna mengi yanayoweza kubadilika mara moja.
Wabunge wa Kongo bado wanapaswa kuidhinisha sheria na kanuni za EAC kabla ya kuanza kutumika.
Raia wa Kongo wanaotaka kutembelea nchi nyingine wanachama - Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda - bila visa wanaweza kuhitaji kusubiri kwa muda mrefu zaidi kwa sababu ushirikiano kamili katika EAC unaweza kuchukua miezi au hata mwaka.
Kwa mfano, Sudan Kusini ilichukua muda wa miezi minne kutoka kwa mkataba wa jumuiya mwezi Aprili 2016 hadi kuwa mwanachama kamili wa EAC mwezi Agosti mwaka huo.
Kwanini DR Congo wanataka kujiunga na EAC?
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilituma maombi ya uanachama mwaka wa 2019, ikitumai kuboresha uhusiano wa kibiashara na kisiasa na majirani zake wa Afrika Mashariki.
Itawaruhusu raia wa Kongo kusafiri kwa uhuru hadi nchi nyingine na biashara itakuwa ya haraka zaidi, rahisi na ya bei nafuu, ambayo inapaswa kunufaisha wafanyabiashara na watumiaji katika nchi zote.
Nchi hiyo inapakana na wanachama wote wa EAC isipokuwa Kenya, na inatumai kuvutia wawekezaji zaidi kutoka kanda hiyo.
Kujiunga na kambi hiyo kunaipa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ufikiaji bora wa vifaa kama vile bandari za Bahari ya Hindi za Dar es Salaam na Mombasa.
Ushuru wa kuagiza bidhaa zinazokubaliwa kuwa zinatengenezwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zitaondolewa au kupunguzwa sana wakati wa kuingia katika nchi nyingine, huku kusafirisha bidhaa kutakuwa nafuu zaidi.
"Tumekuwa tukingojea tangazo hili kwa muda mrefu. Tumefurahi sana," Ley Molo Ley, mfanyabiashara wa Kongo anayeishi karibu na mpaka wa Uganda, aliiambia BBC.
Kwa sasa si rahisi kwa wafanyabiashara wa Kongo kusafiri hadi Uganda, alisema: "Ili Mkongo apate hati za kusafiria kutembelea Uganda, anahitaji kulipa $45 (£35) katika mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. kufikia upande wa Uganda, wanahitaji kulipa $50 kwa visa. Kisha kuna malipo ya kipimo cha Covid-19, hivyo kwa jumla unalipa takriban $120."
Vipi kuhusu wanachama wengine?
Roman Waema, mkuu wa Muungano wa Madereva wa Malori ya Masafa Marefu na Wafanyikazi Washirika wa Kenya, anatazamia mwisho wa kungoja ambao analazimika kuvumilia kwa sasa ili kuingia DR Congo.
"Kwa sasa tunakabiliwa na mambo mengi, kama vile kupanga foleni ili kupata visa ya kuingia DRC, kusubiri siku kadhaa ili bidhaa zetu ziweze kupitishwa mpakani na hivyo kuingia kwenye gharama kubwa za maegesho, ada za kuhifadhi, pamoja na gharama nyinginezo kabla ya kufika tunakoenda. " alisema.
Mchakato wa kusafirisha bidhaa kuvuka mipaka unapaswa kuwa rahisi zaidi - kwa sasa mamlaka katika maeneo ya mipaka yote yanaendesha mifumo tofauti.
"Kutakuwa na uondoaji wa haraka wa bidhaa. Mara tu kituo cha mpakani cha pamoja kitakapofunguliwa, maafisa wa forodha kutoka Uganda na DRC watakaa katika jengo moja kupitisha bidhaa na watu," anasema Guma Morris, ambaye anasimamia ofisi ya Mamlaka ya Mapato ya Uganda Katika mpaka wa Mpondwe.
Kujumuishwa kwa soko la walaji la DR Congo la karibu watu milioni 90 kutapanua soko la EAC hadi karibu milioni 300, na kufungua jumuiya hiyo kwa uchumi wa Kongo ambao una utajiri wa kila aina ya maliasili.
Dk Abel Kinyondo, mwanauchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anaamini kuwa kujumuishwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutakuza nguvu ya mazungumzo ya umoja huo duniani kote.
"Idadi ni muhimu katika biashara ya kimataifa - kuongezwa kwa uchumi wa DRC kwa jumuiya kunamaanisha kuongezeka kwa uwezo wa kununua," alisema.
Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki amefurahi sana. "Sisi ni majirani na DRC, lakini hatufanyi biashara nayo sana kwa sababu tu hakuna mfumo. Bidhaa nyingi zinazokuja DRC zinatoka nje ya Afrika Mashariki kama vile Zambia na Asia," aliiambia BBC.
"Kwa hiyo, tunatazamia kuweka utaratibu ambao utahakikisha biashara kati yetu na DRC inaimarika."
Kinadharia, nchi za Afrika Mashariki zinaweza kupata ufikiaji wa Afrika Magharibi na Bahari ya Atlantiki kupitia DR Congo, lakini mitandao ya barabara na reli ya nchi hiyo itahitaji kuboreshwa kwa kiwango kikubwa kwanza. Njia pekee ya kuvuka nchi hii kubwa, ambayo ni theluthi mbili ya ukubwa wa Ulaya Magharibi, kwa sasa ni kwa ndege.
Upanuzi huu unaowezekana wa uhusiano wa kibiashara kutoka Bahari ya Hindi hadi Atlantiki utasaidia kupanua uwezo wa kiuchumi wa kanda wakati ambapo bara hili linafanya kazi ya kutekeleza Mkataba wa Biashara Huria wa Bara la Afrika (AfCFTA).
Changamoto ni zipi?
Haitakuwa rahisi kujumuisha nchi kubwa kama hiyo yenye changamoto nyingi katika EAC.
Miundombinu duni na ukosefu wa usalama nchini imekuwa suala la wasiwasi kwa nchi washirika wa EAC.
"Ukiangalia vituo vya mpaka vinavyoingia au vinavyopakana na DRC, mara tu unapofika kwenye mipaka hii, kiuhalisia miundombinu inakomea hapo," alisema Damali Ssali, mtaalam wa biashara.
"Hata miundombinu inayotakiwa kuchochea biashara mpakani sio nzuri ukilinganisha na nchi nyingine, halafu ukiingia DRC lazima njia za kuelekea miji mikubwa zifanyiwe kazi maana barabara ni nyingi ni mbovu sana'
Kisha kuna ukosefu wa usalama.
Mnamo Disemba 2021, wanajeshi wa Uganda walivuka hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mwaliko wa serikali ya Kongo kusaidia kuondoa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), moja ya vikundi vingi vyenye silaha vinavyofanya uharibifu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali mashariki mwa nchi.
"Ukosefu wa usalama unazuia biashara - hata hivyo, biashara rasmi zaidi kati ya EAC na DRC inaweza kweli kupunguza migogoro katika eneo la mashariki mwa DRC kwani itapunguza magendo kutokana na ushirikiano mkubwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na forodha, biashara na usalama," anasema Penina Simba, mshauri wa biashara.
Je, EAC itatumia lugha gani?
Kwa sasa Kiingereza na Kiswahili ndizo lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ingawa kumekuwa na mazungumzo kuhusu kuanzisha Kifaransa, ambacho kinazungumzwa nchini Rwanda na Burundi.
Lugha rasmi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni Kiswahili, Kifaransa, Kilingala, Kituba (Kikongo) na Tshiluba. Wataalamu wanasema asili ya lugha nyingi katika eneo hili inapaswa kuangaliwa kama fursa na sio kizuizi.
Kumekuwa na msukumo wa kukuza matumizi makubwa ya Kiswahili, hasa baada ya Umoja wa Afrika kukipitisha kama lugha rasmi ya kazi mwezi Februari 2022. Hata hivyo, baadhi ya mikoa kama vile Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na sehemu za mataifa mengine ya EAC haizungumzi kiswahili
"Kusonga mbele, tunatarajia EAC ambayo ni ya lugha nyingi, ambayo inaweza kusababisha mwingiliano zaidi kati ya raia wa EAC na nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa katika Afrika ya Kati," Bw Simba alisema.
Unaweza pia kusoma