Mwaka mmoja bila Rais Magufuli na maisha yenye rangi mbili Tanzania

    • Author, Yussuf Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Machi 17, 2022, Tanzania inaadhimisha mwaka mmoja wa kifo cha rais wa awamu ya tano wa taifa hilo, John Magufuli.

Magufuli alifariki kutokana na matatizo ya moyo jijini Dar es Salaam.

Makamu wake wa rais wakati huo, Samia Suluhu Hassan, akarithi kiti chake kwa kuapishwa siku mbili tu baadaye yaani Machi 19, 2021 na kuwa Rais wa awamu ya sita na wa kwanza mwanamke katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Swali kubwa sasa, mwaka mmoja tangu kifo cha Magufuli, maisha yakoje nchini Tanzania?

Kiuchumi na Kijamii

Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimi 6.3 kati ya mwaka 2010 mpaka 2019 ikiwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Licha ya kuendelea kuimarika kwa uchumi wake chini ya Rais Samia lakini hilo halitafsiri maisha halisi ya mtanzania, kama mtaalamu huyu wa fedha alivyoiambia BBC: "Ipo tofauti ya ukuaji wa uchumi na maendeleo na uchumi, sasa tunashuhudia angalau ahueni mifukoni ukilinganisha na kipindi cha Rais Magufuli kati ya mwaka 2018 na 2020, ingawa bado mambo magumu, maisha magumu', anasema Raphael Magoha.

Mmoja wa wazazi wa binti ambaye alishindwa kuendelea na shule kwa sababu ya ujauzito, anasema atamkumbuka Rais Magufuli kwa jitihada zake za kukuza uchumi na kuboresha miundo mbinu, lakini sera yake ya mabinti wajawazito kutorudi shuleni lilimtatiza na kukata tamaa ya maisha ya kuchumi ya mwanae huko mbele.

'elimu ndio tegemeo letu sisi masikini, unaamini mtoto wako akisoma atajisaidia na atakuja kusaidia familia, kidogo azime ndoto za maelfu ya mabinti, tunashukuru mama (Rais Samia) kaliona hilo, mabinti wajawazito sasa wameruhusiwa kuendelea na masomo.

Wakati akitoa tamko la kukataza mabinti wajawazito kurejea shuleni Magufuli alisema: "yaani tusomeshe wazazi? nataka niwaambie, ndani ya utawala wangu kama Rais hakuna mwenye mimba atakayerudi shuleni, amechagua maisha hayo ya mtoto akalee vizuri mtoto".

Uhuru wa habari, uhuru wa kujieleza na kukosoa

Moja ya eneo ambalo, lilikuwa linapigiwa makelele na baadhi ya wakosoaji wakati wa utawala wa Rais Magufuli ni hili la uhuru wa habari, kujieleza na kutoa maoni.

"Ilionekana kuikosoa serikali ni dhambi kubwa, ukiikosoa ulionekana si mzalendo, na baadhi ya walioikosoa hawakubaki salama', alisema Adam Michael wa Moshi.

Kiongozi wa upinzani nchini humo aliyegombea urais mwaka 2020 akichuana na Magufuli, Tundu Lissu mara kadhaa alinukuliwa akisema shambulio la risasi dhidi yake mwaka 2017 lilitokana na ukosoaji wake dhidi ya serikali ya Magufuli.

Ingawa BBC haiwezi kuthibitisha hilo, ila Mkuu wa jeahi laPolisi Tanzania Simon Sirro alinukuliwa akieleza Polisi haijakaa kimya kuhusu kushambuliwa kwake na haihusiki na shambulio hilo.

Sirro alisema "kinachofanya uhalifu sio sare, Kinachofanya uhalifu ni mtu anayetekeleza tukio. Kwa hiyo jambo la msingi tunawatafuta waliotekeleza tukio hilo."

Katika eneo la uhuru wa habari, Tanzania ilipitisha sheria ya huduma za habari 2016, na sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015, sheria ya takwimu, 2015 sheria kupata taarifa na kanuni zake 2016.

Sheria hizi zinataja kuwa sababu kuu ya kuporomoka kwa uhuru wa habari na kujieleza katika utawala wake.

Kwa mujibu wa shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka (RSF), katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2016 mpaka 2018 kwenye eneo la uhuru wa habari duniani Tanzania iliporomoka kutoka nafasi 76 hadi ya nafasi ya 93 kati ya nchi 180, ikiporomoka kwa nafasi 17.

'Hakuna aliyeweza kuthubutu kusema kitu wakati huo, pengine kwa uoga au kwa heshima ya Rais, licha ya kuwa na mazuri, lakini sheria hizi zina vipengele vya kubana uhuru wa habari, watu kusema na kukosoa, sishangai leo Nape (Waziri wa habari), anaona umuhimu wa kuzirejea, ukweli nampongeza zina mapungufu, anasema mwandishi wa habari wa kituo cha Clouds FM, Dixon Busagaga.

Waziri wa Habari na Teknolojia ya habari, Nape Nnauye wiki hii ameviambia vyombo vya habari kwamba, serikali ina mpango wa kuzirekebisha baadhi ya sheria hizo kupitia bunge la mwezi wa tisa na kunukuliwa akisema pia kwamba "hatuna mpango (serikali) wa kufungia gazeti, ila tuna mpango wa kushugulika na kosa la mtu kama mtu'.

Hatua hiyo inaungwa mkono na mwandishi mwingine wa habari, ambaye hakutaka kujitambulisha na ambaye alipitia madhira kwenye majukumu ake ya uandishi wakati wa utawala uliopia, anayesema mwaka mmoja uliopita umekuwa na mabadiliko ya kutia moyo kuhusu sekta ya habari na uhuru wa habari kwa ujumla.

'Leo unaweza kukosoa, na tunaona mitandaoni watu wanakosoa ingawa si kwa uhuru mkubwa, ila miaka miwili iliyopita, usingethubutu, hata kwa uhuru mdogo', alisema.

Ikumbukwe siku chache baada ya kuingia madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka 2015 serikali ya Rais Magufuli ilitangaza pia kusitisha matangazo mubashara ya vikao vya bunge, ikisema hatua hiyo ni mkakati wa kupunguza matumizi ya fedha za umma.

Nape kwenye hili amesema hana mamlaka nalo kwa sasa.

Kisiasa na demokrasia

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mikutano ya kisiasa na maandamano ni halali kwa vyama vya siasa na makundi yanayokubalika kisheria.

Lakini alipoingia madarakani Rais Magufuli alinukuliwa akisema shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na maandamano na mikutano ya hadhara isimame hadi uchaguzi ujao (akimaanisha wa mwaka 2020).

Alidai baada ya uchaguzi uliopita, "sasa ni kazi tu".

Ilianza kuzuiwa mikutano ya hadhara baadae mikutano na vikao vya ndani vilikumbwa na kadhia hiyo.

"Amri ya jeshi la Polisi (kuzuia mikutano) ni amri haramu, katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano imeweka haki ya kufanya mikutano, bila mikutano hakuna siasa, kwa hiyo tumepigwa marufuku kufanya siasa', alisema Tundu Lissu alipozungumza na BBC mwaka 2016.

Lakini kuna kilichobadilika leo? Juma Shomvi wa Morogoro anasema "hakuna, bado mikutano haifanyiki, lakini kuna nia njema inayoonekana kupitia mama (Rais Samia), angalau kuna uhuru fulani kiasi wa kukusanyika bila uoga.

Kuhusu hili Lissu alinikuliwa na vyombo vya habari vya ndani wiki hii akisema: "Mimi sio mpiga vigerere, lakini kuna mambo Mama (Rais Samia) ameanza kuyafanya vizuri, kwa sababu ameyafanya vizuri, tutaungana naye ili ayafanye vizuri zaidi. Kuna kazi kubwa iliyopo mbele yake ambayo si rahisi, lazima tumpe moyo.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, bila Magufuli, mbali na viongozi wengine wa kisiasa, Rais Samia ameshakutana na viongozi wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, Tundu Lissu na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, aliyekuwa gerezani kwa miezi 8 kwa tuhuma za ugaidi, kabla ya mwendesha mashtaka kuiambia mahakama hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

'Isingekuwa rahisi wakati wa Magufuli, kushuhudia aina ya vikao na wapinzani, vinavyoendelea sasa, inatia moyo sasa kwenye muelekeo wa siasa na demokrasia, alichobakiza mama (Samia) ni kuruhusu tu mikutano na kuleta katiba mpya', alisema Nassib Kareem (sio jina lake halisi), mtanzania ambaye hakupenda kujitambulisha.

Haki za binadamu, uwajibikaji na utawala bora

Magufuli alisifiwa kwenye kusimamia rasilimali za umma kama madini, mapato ya serikali, ujenzi wa miundo mbinu, mapambano dhidi ya rushwa, na kuongeza uwajibikaji serikalini kupitia kauli mbiu yake maarufu ya "hapa kazi tu".

Pamoja na hayo katika wakati wake, kulikuwa na matukio mengi yaliyopigiwa kelele kukiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

Tumbuatumbua (kuwafukuza) wasaidizi wake, kufukuza wafanyakazi hewa, namna alivyolishughulikia suala la Corona, kuzuia mikutano ya siasa, kuzuia mabinti wanaopata mimba kutorejea shuleni, kupotea watu na an uwepo wa watu 'wasiojulikana', yalikuwa ni baadhi ya masuala yaliyoibua maswali kwa wanajamii.

Lakini kwa sasa, Shomvi anasema "wafanyakazi na wasaidizi wa rais wanapumua, hawana hofu tena, kama wakati wa Magu (Magufuli) na ni rahisi kuwajibika bila woga, ingawa Rais Samia akilegeza kamba, uzembe utarudi serikalini'.

Kwa upande wake Maria Sarungi, mwanaharakati na mtoto wa waziri wa zamani wa serikali ya Tanzania, Prof. Philemon Sarungi, ameandika kwenye mtandao wake wa twitter kwamba watu wana majeraha makubwa, akirejea hali ilivyo sasa Tanzania.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Anna Henga, ambacho kiliwahi kukumbwa na misukosuko wakati wa utendaji wake awamu iliyoipita, ikiwemo kuvamiwa na kushikiliwa kwa afisa wake, Tito Magoti, kinase sasa kuna haueni kubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga, anasema hali ya haki za binadamu imekuwa bora zaidi katika mwaka mmoja wa awamu ya sita, akitaja mambo 6, yaliyoboreshwa:, visa vya kutoweka kwa wanaharakati vimepungua, usawa wa kijinsia unaelekea pazuri kufuatia teuzi mbalimbali, kumekuwa na uhuru wa kujieleza, watetezi tumethaminiwa na hatuonekani kama maadui tena, watoto wa kike kurudi shule, uhuru wa vyombo vya Habari na usalama wa Raia'.

Kauli hii inaungwa mkono na Paulina Adam, mama wa nyumbani anayesema: "Mama (Rais Samia) anaupiga mwingi, leo tu furaha angalau, ila sio mkali kama Magufuli naona watendaji wengine wameanza kuzembea, jeshi la Polisi leo, linatia simanzi".

Kwa maoni na hisia hizi mchanganyiko kuhusu mwaka mmoja uliopita wa kutokuwepo kwa Magufulu 'Bulldoza' na kuingia kwa Rais Samia, inakupa picha kwamba ulikuwa ni mwaka wenye rangi mbili, ya kufurahisha kwa upande mmoja na upande mwingine usiopendeza katika maisha ya watanzania.