Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania:Mkutano wa Rais Samia na Lissu umepokelewa vipi?
Rais wa Tanzania Samia Suluhu amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzani nchini humo (CHADEMA), Tundu Lissu,mkutano uliopokelewa kwa hisia tofauti na kada mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mkutano wa aina hii ilibidi usubiri kwa zaidi ya mwaka mmoja, tangu Rais Samia aingie madarakani, kufuatia kifo cha Rais John Magufuli, mwezi machi mwaka 2021. Rais Samia yuko Ubelgiji kwa ziara ya kikazi.
Lissu,mgombea urais mwaka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020,yuko uhamishoni kwa miaka zaidi ya minne tangu jaribio la kuuawa kwa risasi mjini Dodoma mwa Septemba 2017.
Kwa sasa anaishi uhamishoni Ubelgiji alikokuwa anapatiwa matibabu huku akiendelea na wadhifa wake kama makamu mwenyekiti, kufuatia mwenyekiti wa chama hicho,Freeman Mbowe kushikiliwa kutokana na tuhuma za ugaidi.
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alionesha kwa umma dhamira yake na kukutana na vyama vya siasa, na kurejea kauli hiyo mara kadhaa kabla ya kukutana nao vyama kadhaa katika mkutano uliofanyika Dodoma, mkutano ambao CHADEMA hawakuhudhuria.
Fatma Karume, mwanaharakati na mwanasheria, pamoja na kupongeza amesema hatua ya Rais Samia kukutana na Lissu imeleta furaha na faraja kwa wengi. Akitaka pia wanasiasa wa upinzani waliokuwa uhamishoni kwa sababu za kisiasa kurejea nchini na kuwa huru kuendelea na shughuli zao.
Kwa mujibu wa Tundu Lissu, miongoni mwa mambo 6 aliyozungumza na Rais Samia, ni pamoja na hilo la kuhakikishiwa usalama wakrejea nyumbani yeye na wenzake aliowataja, Wabunge wa zamani wa CHADEMA, Ezekiel Wenje na Godbless Lema walioko uhamishoni Canada
Masuala mengine yaliyogusiwa katika mazungumzo hayo ni pamoja na suala la Freeman Mbowe, anayeendelea na kesi ya ugaidi kwenye mahakama kuu divisheni ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi,haki ya vyama va siasa vya upinzani kufanya siasa, katiba mpya, maslahi ya Lissu mwenyewe yatokanayo na nafasi ya ubunge na wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa CHADEMA.
Viongozi mbalimbali wa siasa za Tanzania kutoka chama tawala, wakiwemo mawaziri wa sasa na wa zamani nao wameonesha kufurahia hilo,mmoja wapo ni waziri wa zamani wa viwanda na biashara,Profesa Kitila Mkumbo na waziri wa fedha na mipango wa nchi hiyo, Mwigulu Nchemba aliyeandika 'taifa letu umoja wetu'.
Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, pamoja na kusema hekima imetawala na kufungua mlango wa mazungumzo, hatua hiyo aliipongeza kwa kuchapisha moja za video za wanamuziki wa DRC Congo, inayogusia kupiga makofi, na ambayo imetafsiriwa kama ni namna alivyoamua kupongeza ahatua hiyo. Video hiyo kwa muda mfupi ikatazamwa na watu zaidi ya 2,700.
Jamii na watu wengine nchi ya Afrika Mashariki, wameguswa na uamuzi huo, licha ya wachache kuona kama ni uamuzi uliochelewa sana kufanyika.
Baadhi ya wananchi wa nchi jirani ya Kenya, walionekana kuunga mkono hatua hiyo ya Rais Samia kukutana na kiongozi wa upinzani, wakifananisha tukio hilo na lililofanyika kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa muda mrefu, Raila Odinga na kushikana mikono.
Lissu ameiambia BBC kwamba nafasi aliyoipata ya kuzungumza na Rais Samia ni muhimu sana na amemshukuru Rais huyo kwa kumpatia nafasi hiyo, akitaka wananchi wakiwemo kutoka upinzani kuungana naye na kushirikiana na serikali ili kujenga nchi mpya yenye maendeleo.
Mkutano huu sa Rais Samia na Lissu, umedaiwa na wengi kufungua upya sura ya siasa na demokrasia nchini Tanzania, huku njia ya maridhiano ikitajwa kama hatua muhimu na pili itakayopaswa kufuatwa.