Mzozo wa Ukraine: 'Putin amenihakikishia hakutakuwa na mzozo' - Macron

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameambia wanahabari kwamba rais Urusi Vladmir Putin amewahakikishia kwamba vikosi vya Urusi havitachochea mzozo karibu na mpaka wa Ukraine.
''Nimehakikishiwa kwamba hakutakuwa na mzozo wowote'' , alisema kabla ya kukutana na rais wa Ukraine.
Hatahivyo Urusi imesema kwamba hakikisho lolote 'sio sawa'.
Urusi imekana mipango yoyote ya kutaka kuivamia Ukraine , lakini imewapeleka karibu na mpaka wa Ukraine wanajeshi zaidi ya 100,000.
Hapo awali rais wa Marekani Joe Biden aliapa kufunga bomba muhimu la gesi la Urusi kuelekea Ujerumani iwapo Moscow itaivamia Ukraine.
Akizungumza baada ya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Washington, Bw Biden alisema Marekani "itamaliza" bomba la Nord Stream 2.
Mazungumzo yao yalikuja wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Moscow na kuelezea matumaini kwamba vita vinaweza kuepukwa.
Kuna kuongezeka kwa hofu katika nchi za Magharibi ya uvamizi wa Urusi , ambayo Moscow inakanusha.
Kwa sasa Urusi ina zaidi ya wanajeshi 100,000 waliokusanyika kwenye mipaka ya Ukraine.
Maafisa wa Marekani walisema Jumapili kwamba Urusi imekusanya asilimia 70 ya vikosi vya kijeshi vinavyohitajika kwa ajili ya uvamizi kamili.
Katika wiki za hivi karibuni, Moscow imetaka muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi Nato kupiga marufuku Ukraine kuwa mwanachama, na kwamba kundi hilo lipunguze idadi ya wanajeshi wake mashariki mwa Ulaya.
Nato imekataa matakwa yote mawili. Badala yake imependekeza mazungumzo kuhusu maeneo mengine, kama vile kupunguza silaha za nyuklia.
Mvutano kati ya Urusi, Ukraine na nchi za Magharibi unakuja karibu miaka minane baada ya Urusi kuiteka rasi ya Crimea kusini mwa Ukraine na kuunga mkono uasi katika eneo la mashariki la Donbas.
Moscow inaishutumu serikali ya Ukraine kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya Minsk - mkataba wa kimataifa unaofadhiliwa na Ujerumani na Ufaransa kurejesha amani mashariki mwa nchi, ambapo waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo mengi na takriban watu 14,000 wameuawa tangu 2014.
Biden aaapa 'kukomesha' Nord Stream 2
Bw Biden na Bw Scholz walifanya mkutano na waandishi wa habari baada ya majadiliano yao katika mji mkuu wa Marekani siku ya Jumatatu.
Alipoulizwa kuhusu Nord Stream 2, rais wa Marekani alisema "ikiwa Urusi itavamia... tena, basi hakutakuwa na Nord Stream 2 tena. Tutaimaliza."
Hata hivyo hakutoa maelezo maalum, akijibu swali kuhusu jinsi atakavyofanya hivi kwa kusema: "Nakuahidi tutaweza kufanya hivyo."
Bw Scholz - katika safari yake ya kwanza Washington tangu awe Kansela na chini ya ukosolewaji kwa majibu yake kwa mgogoro wa Ukraine - alikuwa na utata zaidi kuhusu bomba hilo.
Lakini alisema Marekani na Ujerumani "zimeungana kabisa" katika vikwazo dhidi ya Urusi iwapo itaivamia Ukraine, akisema "tutafanya hatua sawa na zitakuwa ngumu sana kwa Urusi".
Bomba hilo la 1,225km (maili 760) la Nord Stream 2 lilichukua miaka mitano kujengwa na kugharimu $11bn (£8bn). Mradi huo wa nishati, ambao ungeendeshwa chini ya Bahari ya Baltic, umeundwa kuongeza maradufu mauzo ya gesi ya Urusi kwenda Ujerumani.
Lakini bado haijaanza kufanya kazi, kama wasimamizi walisema mnamo Novemba haizingatii sheria za Ujerumani na kusitisha idhini yake.

Biashara kuu za Ulaya zimewekeza fedha nyingi katika Nord Stream 2. Lakini makundi mengi yanapinga mpango huo.
Wanamazingira wanahoji jinsi itakavyoendana na juhudi za Ujerumani za kupunguza hewa chafu na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu, huku wanasiasa wa nyumbani na nje ya nchi wakihofia kuwa huenda ikaongeza utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hapo awali ameelezea bomba hilo kama "silaha hatari ya kisiasa ya kijiografia".
Nord Stream 2 yaangaziwa
Kansela mpya wa Ujerumani Olaf Scholz anafanya ziara yake ya kwanza mjini Washington huku kukiwa na ukosoaji wa jibu dhaifu kwa mgogoro wa Ukraine.
Wabunge wa chama cha Republican wameionyesha Berlin kama breki ya vikwazo kwa sababu ya nia yake ya kudumisha uagizaji wa gesi kutoka Urusi.
Baada ya kukutana na kansela Rais Biden alisisitiza kuwa Nord Stream2 haitafanya kazi ikiwa Moscow itaivamia Ukraine.
Bw Scholz hakwenda mbali hivyo, akitaja hitaji la utata wa kimkakati. Lakini alisisitiza kuwa Marekani na Ujerumani zitakuwa na umoja kabisa katika kuchukua hatua sawa katika kukabiliana na uvamizi wowote, na kwamba hatua hizi zitakuwa ngumu sana.
Bw Biden alijitolea kufutilia mbali pendekezo kwamba Ujerumani haikuwa mshirika wa kutegemewa, akisisitiza mara kadhaa kwamba nchi hiyo inaweza kutegemewa .














