Aneera Kabeer: Mwanamke wa Kihindi aliyebadili jinsia ambaye ombi lake la kutaka kufa limezua taharuki

Mnamo Novemba mwaka jana, Aneera Kabeer alihudhuria mahojiano yake ya 14 ya kutafuta kazi katika miezi miwili akiwa amevalia kofia, barakoa iliyoficha sehemu kubwa ya uso wake, na nguo za kiume.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 35, anasema kilikuwa kitendo cha kukata tamaa kutokana na matamshi ya kuchukiza aliyokumbana nayo kwenye mahojiano ya awali.

Alipata kazi ya muda - katika shule ya serikali katika jimbo la kusini mwa India la Kerala - lakini anadai alifukuzwa kazi isivyo halali chini ya miezi miwili baadaye.

Mkuu wa shule hiyo alikataa kutoa maoni yake. P Krishnan, afisa wa wilaya, alisema kwamba mkuu wa shule alimweleza kwamba Bi Kabeer hakufukuzwa kazi na badala yake, "hakuelewa hali hiyo".

Kutokana na chaguzi, Bi Kabeer aliwasiliana na huduma za usaidizi wa kisheria za serikali mwezi Januari - alitaka wakili awasilishe maombi ya euthanasia, au "mauaji ya huruma", kwa niaba yake.

"Nilichotaka ni kufanya kazi na kupata riziki. Lakini ikawa vigumu hata kufanya hivyo," Bi Kabeer asema.

Alikuwa amesoma kuhusu nchi ambazo ziliruhusu euthanasia na India iliruhusu tu euthanasia isiyo kamili.

"Nilijua singepata kibali cha kisheria hapa, lakini nilitaka kutuma ujumbe," anasema.

Badala yake, alitaka kupata usikivu wa serikali - na alifanya hivyo. Serikali ilijibu upesi, na sasa ana kazi nyingine.

Maandamano na ahadi

Bi Kabeer anaonyesha wazi kwamba hakuwa na nia ya kujitoa uhai, na alichofanya hakikusudiwa kuwa mfano kwa wengine.

Lakini aina kama hizi za maandamano sio kawaida nchini India.

Kwa miaka mingi Wahindi wanaotafuta haki au mabadiliko ya kimfumo wamegoma kula, wamesimama kwenye maji hadi kiunoni kwa siku nyingi na kushikilia panya hai midomoni mwao.

Wanasosholojia wamependekeza kwamba mfumo wa uasi usio na vurugu wa Mahatma Gandhi, ambao ulijumuisha muda mrefu wa mgomo wa chakula, ulionyesha nguvu ya kile wanachoita maandamano ya "utendaji" - haswa katika nchi kama India, ambapo serikali mara nyingi huchelewa kujibu.

Anagha Ingole, anayefunza sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Hyderabad, anasema kuwa vitendo kama vya Bi Kabeer vinanuiwa kukumbusha serikali kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake.

"Katika kesi hii, serikali ilikosa kutimiza ahadi yake rasmi ya kulinda haki ya raia kufanya kazi," asema Bi Ingole, ambaye amefanya kazi pakubwa katika masuala ya ubaguzi wa kijamii.

India inakadiriwa kuwa na takriban watu milioni mbili waliobadili jinsia, ingawa wanaharakati wanasema idadi hiyo ni kubwa zaidi. Mnamo 2014, Mahakama Kuu ya India iliamua kwamba wana haki sawa na watu wa jinsia nyingine.

Hata hivyo, bado wanatatizika kupata elimu na huduma za afya. Na wengi wanalazimika kujikimu kimaisha kwa kuombaomba au kufanya ukahaba.

Bi Kabeer anasema jamii inahitaji uwakilishi wa kisiasa na nafasi za kazi.

"Sijawahi kutaka kuchukua hatua kali kama hiyo lakini nilikuwa na chaguo gani?" anauliza.

Kupambana kuwa yeye mwenyewe

Akikulia katika wilaya ya Palakkad katikati mwa Kerala, Bi Kabeer anasema alijitahidi kwa miaka kutambua jinsia aliyopewa wakati wa kuzaliwa.

Hakutaka kuzungumza juu ya familia yake ambayo, alisema, ilikuwa bado inakabiliana na kifo cha hivi karibuni cha kaka yake.

Bi Kabeer alikuwa bado kijana alipojaribu kutafuta watu wengine waliobadili jinsia huko Palakkad. Lakini aliacha baada ya jaribio moja kama hilo kumalizika kwa kukamatwa kwake.

Hata alikimbia kutoka nyumbani hadi mji wa Bangalore baada ya kuona picha za watu waliobadili jinsia kwenye gazeti. Alipata jumuiya inayounga mkono watu waliobadili jinsia ambao walimkubali. Lakini maisha yalikuwa magumu - wengi wao waliomba kwa miaka mingi kutafuta pesa kwa ajili ya upasuaji wa kubadili jinsia.

Akiwa amevunjika moyo Bi Kabeer alirudi nyumbani.

"Nilijaribu sana kuishi jinsi familia yangu ilitaka niishi," anakumbuka.

Hii ilijumuisha kuvuta sigara, na kujiunga na gym na kozi za kukuza utu - yote hayo, watu walio karibu naye walisema, yangemfanya "mwanamume".

Lakini kujifanya mtu ambaye hakuwa ilimfanya kuwa mnyonge.

Pia alisoma kwa bidii - alikuwa na shauku ya kufundisha tangu alipokuwa mdogo na alikuwa akifundisha watoto katika kijiji chake.

Hilo lilimfanya aendelee hata baada ya kuondoka nyumbani na kuishi maisha aliyoyataka.

Bi Kabeer sasa ana digrii tatu za uzamili, ikiwa ni pamoja na moja ya elimu, na amefaulu mtihani wa serikali unaomruhusu kufundisha wanafunzi wa shule za upili.

Lakini katika mahojiano ya kazi, alikumbana na maswali yasiyofaa - mtahini mmoja alimuuliza jinsi angeweza kuaminiwa kutoangalia wanafunzi kupitia njia ya ngono.

Alipoanza kufundisha mnamo Novemba 2021, anadai alikumbana na matamshi yasiyofaa kutoka kwa wenzake lakini anasema kwamba wanafunzi walimuunga mkono.

Lakini Bi Kabeer anasema, aliombwa ghafula kuacha kwenda shuleni tarehe 6 Januari - kufukuzwa kwake, anadai, kulikwenda kinyume na sheria.

Akiwa ameachwa bila kazi, aliingiwa na woga na hata akaenda kwenye maduka karibu na shule ili kuuliza ikiwa wangemwajiri kama muuzaji lakini aliktaliwa.

Hapo ndipo alipotfuta msaada wa kisheria.

Habari hizo zilienea, na waziri wa elimu wa Kerala alijibu mara moja - alikutana na Bi Kabeer na sasa ameanza kazi nyingine ya muda katika ofisi ya serikali huko Palakkad.

Lakini wengine kama yeye bado wanangojea msaada.

Njia ndefu ya kupata haki

Mnamo mwaka wa 2018, Shanavi Ponnusamy aliandika barua kwa Rais wa India Ram Nath Kovind, pia akitaka mauaji ya huruma.

Mwaka uliotangulia aliwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu ya nchi hiyo baada ya kudaiwa kunyimwa kazi na Air India, wakati huo shirika la ndege la taifa, kwa kuwa hawakuwa na sera ya kuajiri wafanyakazi waliobadili jinsia.

Shirika la ndege na serikali hazikujibu ombi hilo kwa miezi kadhaa. Baadaye, kampuni hiyo ilitishia kumshtaki kwa kuiharibia jina.

Kesi ilipokuwa ikiendelea, huku akitumia akiba yake, ndipo Bi Ponnusamy aliamua kumwandikia rais barua hiyo.

Ni nini kilibadilika kwake? "Hakuna," anasema.

Hakupata jibu na Air India sasa imenunuliwa na kampuni ya kibinafsi, na hivyo kufifisha matarajio ya kupata kazi kwake. Lakini amewasilisha kesi katika mahakama kuu ya Madras, akiomba fidia kwa gharama za kisheria ambazo ametumia kufikia sasa.

"Ikiwa kuna mfumo wa aina hii, watu kama sisi wataishije?" anauliza.