Mzozo wa Ukraine: Tutajuaje kuwa vita vimeanza?

Kila mtu anajaribu kubahatisha nia ya Rais Vladimir Putin nchini Ukraine. Marekani inawaondoa wafanyakazi wa ubalozi huku hofu ya mzozo ikiongezeka. Lakini labda tayari umeanza kulingana na mtaalam wa usalama na ulinzi Jonathan Marcus.

Hatari ya vita vya pande zote kati ya Urusi na Ukraine inatawala vichwa vya habari.

Maswali yanaulizwa. Je, Urusi itashambulia? Je, Rais Vladimir Putin ameamua vita liwe liwalo? Au diplomasia inaweza kuleta amani?

Lakini hatuwezi kuona ndani ya akili ya Rais Putin.

Kwa hivyo hapa kuna swali lingine - tutajuaje wakati uhasama utakapoanza?

Vifaru vikisonga, makombora yakirushwa

Jibu linaonekana wazi.

Vifaru vya Urusi vikivuka mipaka ya Ukraine, au msururu mkubwa wa roketi au mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Ukraine, itaashirika kuzuka kwa mgogoro na awamu mpya ya mzozo.

Kengele za kwanza zitatoka kwa jeshi la Ukraine lenyewe, lakini satelaiti za nchi za Magharibi na ndege za kukusanya taarifa za kijasusi zinaweza kuona maandalizi ya mashambulizi yanayokaribia.

Pengine kutakuwa na dalili za wazi za mashambulizi yanayokaribia, anasema Michael Kofman, mtaalamu wa masuala ya jeshi la Urusi katika kituo chenye makao yake nchini Marekani cha Uchambuzi wa jeshi la wanamaji.

Lakini swali pia linaweza kujibiwa kwa njia nyingine na kwa hili tunahitaji kusimama kando na kutazama kampeni ya Urusi dhidi ya Ukraine kwa ukamilifu.

Tunahitaji kuangalia mbinu inayotumiwa na Moscow. Na kwa maana hii unapouliza - tutajuaje ikiwa mgogoro umeanza - basi jibu linaweza kuwa ni tayari umeanza.

Uadui umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa.

Shinikizo la kijeshi

Tuanzie mahali tulipo.

Urusi tayari inakalia Crimea - sehemu ya Ukraine - na inatoa msaada kwa waasi wanaoipinga Kyiv katika mkoa wa Donbas.

Hakika ilikuwa ni uingiliaji wa kijeshi wa Urusi dhidi ya vikosi vya Ukraine mnamo 2014 ambao ulizui kushindwa kwa waasi wanaoungwa mkono Urusi. Mapigano ya hapa na pale yameendelea tangu wakati huo. Pande zote zinaunga mkono juhudi za kimataifa za amani huko, lakini maendeleo kidogo yamepatikana.

Tishio la kutumia nguvu

Zaidi ya shinikizo hili pia kuna tishio la kutumia nguvu kubwa ya kijeshi.

Kuongezeka kwa vikosi vya Urusi karibu na mipaka ya Ukraine ni ya kushangaza. Hii ni pamoja na kupelekwa kwa vikosi huko Belarui - ambayo pia inashiriki mpaka na Ukraine - ambayo inaweza kutoa sehemu ya karibu kwa shambulio kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Kuongezeka huku kunatajwa na wasemaji wa Kirusi kama zoezi na hivyo hakuna tishio. Lakini ukubwa wake, aina ya vikosi vilivyotumwa, na kuwasili kwa taratibu kwa vifaa inaonyesha kuwa hii ni zaidi ya mambo ya kawaida.

Wachambuzi wamefuatilia shughuli hizo za kijeshi kwa kutumia picha za kiraia za satelaiti. Video nyingi za simu zimewekwa mtandaoni zikionyesha treni za vifaa vinavyoelekea Ukraine au Belarus. Na tathmini ya machapisho ya mitandao ya kijamii, yanayohusiana na vitengo vinavyoonekana kuwa kwenye harakati, hutoa picha ya kile kinachoendelea.

Bila kujali kinachosemwa na Urusi, Ukraine na marafiki zake wan chi za Magharibi wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi.

Mbinu inayoweza pia kutumiwa na Moscow ni jaribio la kushawishi hatua.

Kwa upande mmoja Urusi inasema haijitayarishi kwa vita, ingawa inaonekana kana kwamba inafanya hivyo. Lakini ina kitu cha kusema ambapo mbali na Ukraine kuwa mwathirika, kwa kweli ni Urusi yenyewe ambayo inadai kutishwa.

Hiki ndicho kiini cha hati zilizokabidhiwa kwa Marekani ambazo zinataka kusitishwa na kwa namna fulani upanuzi wa Nato na kuunda fursa mpya ya ushawishi kwa Moscow.

Wakati baadhi ya vipengele vya wasiwasi wa Russia, kama mazungumzo juu ya mifumo ya silaha inaonekana sana kama wazo nzuri, juu ya upanuzi wa Nato hakuna uwezekano wa kupata mabadiliko yoyote - na pengine inalijua hili.

Kulemaza

Kuna uwezekano mwingine katika mbinu tofauti za Urusi. Mashambulizi ya mtandao na uharibifu, kwa mfano. Zaidi ya wiki moja iliyopita tovuti kadhaa za serikali zilidukuliwa ingawa haikuwa wazi mahali shambulio hilo lilitoka.

Hivi majuzi zaidi Serikali ya Uingereza imedai ushahidi kwamba Moscow imechagua watu binafsi kuunda serikali mpya huko Kyiv - ingawa hakuna ushahidi kamili unaothibitisha kuhusika kwa Moscow katika shughuli kama hizo.

Michael Kofman anasema kuwa mtandao unaweza kuwa sehemu muhimu ya shambulio lolote la Urusi, kwa sababu yaweza kulemaza miundombinu muhimu na kuvuruga uwezo wa Ukraine wa kuratibu juhudi za kijeshi.

Mistari isiyoonekana vizuri kati ya vita na amani

Wakati Urusi ilipoiteka Crimea tulisikia mazungumzo mengi na madai ya kukanushwa kwa operesheni hiyo, ambayo washiriki wake, ingawa walikuwa na sare, hawakuvaa nembo ya kijeshi.

Lakini hakukuwa na shaka kwamba askari hawa walikuwa nani. Na Crimea ilikamatwa kwa kutumia mbinu kijeshi ya zamani.

Lakini jeshi la Urusi limefafanua fundisho la kisasa ambalo huona vita na amani kama mwendelezo ambapo zana tofauti hutumiwa katika hatua tofauti, wakati mwingine kwa mpangilio, wakati mwingine kwa pamoja, ingawa kwa lengo moja.

Na ndio maana mzozo tayari umeunganishwa. Swali pekee ni Rais Putin yuko tayari kwenda umbali gani?