Jinsi kuzeeka kwa retina kunavyoweza kueleza iwapo una hatari ya kifo cha mapema au la

Umri halisi wa retina, unaweza kuonyesha kiwango cha kuzeeka kwa umri wa mtu. Ni umri gani alionao au iwapo ana ujana zaidi kuliko umri aliozaliwa nao ikiwa ni pamoja na kubashiri iwapo una hatari ya kufariki mapema au la.

Umri wa kibaiolojia wa retina, ambayo ni nyama iliyo nyuma ya mboni ya jicho, hutambuliwa kwa hali ya mishipa ya damu na neva kwenye retina yenyewe, ambayo inaaminiwa kuharibika kutokana na mchakato wa kuzeeka kwa mwili zaidi ya viungo vingine vya mwili.

Jopo la wanasayansi kutoka Uchina na Australia kwa pamoja lilifanya utafiti wa hali hii na kuchapisha matokeo yake katika jarida la Uingereza la uchunguzi na tiba ya magonjwa ya macho.

Kulingana na utafiti huo ambao "wanazeeka haraka" au wenye utofauti wa umri wa retina , ambao ni tofauti kati ya umri wao wa kuzaliwa na umri wao wa kibaiolojia wa zaidi ya miaka 10 , wana hatari ya asilimia 49 hadi 67 ya kufa katika kipindi cha miaka 11, baada ya uchunguzi.

Ingawa awali kulikuwa na utafiti ambao ulionyesha kwamba vipimo vya skani vinaweza kutoa taarifa juu ya hatari ya magonjwa ya moyo, ikiwa ni pamoja na hatari ya kuwa na ugonjwa wa kudumu wa figo, utafiti huu ni wa kwanza ambao umeonyesha kwamba retina inaweza kuelezea uwepo wa magonjwa ya moyo na ubongo, na pia kubashiri kiwango cha kuzorota kwa mwili mzima.

Mahesabu ya uhakika ya kuaminika yamefanyika hadi yameweza kuelezea kwa usahihi umri wa kibaiolojia wa retina ya binadamu na wanasayansi wanasema fursa za kukosewa kwa mahesabu hayo ni kujumlisha au kutoa miaka 3.5.

Jopo la watafiti lilfanya uchunguzi wa kubashiri pengo la umri wa retina miongoni mwa watu wenye umri wa kati 47,000 na wazee, wakazi wa Uingereza, wakatathimi vipimo vyao vya skani za retina zao.

Watafiti hao walibaini kwamba miaka 11 baadaye watu 1,871 katika uchunguzi uliofanyika hapo juu walikuwa wamekufa, wengi wao wakiwa ni wale waliokuwa na hali ya kuzorota kwa retina zao na mara nyingi walikufa kwa saratani.

Katika utafiti huu ambao umri wa kibaiolojia wa retina zao ulikuwa ni mwaka mmoja tu kuliko umri wao wa kuzaliwa walikuwa na ongezeko la hatari ya 2% wa sababu zote za kifo kwa kipindi cha miaka 11 iliyofuata.

Aidha kulikuwa na ongezeko la 3% la kifo kinachotokana na sababu mbali mbali isipokuwa kifo kitokanacho na magonjwa ya moyo au saratani katika kipindi cha miaka 11 baada ya kupimwa.

Ingawa bado haijafahamika bado ni kwanini retina ni kiashirio kizuri cha kuzeeka kwa binadamu na kuzeeka kibaiolojia, timu hiyo ya wanasayansi inatumai kuendelea na tafiti zaidi.

Unaweza pia kusoma:

Kutengeneza picha ya retina kama njia ya kwanza ya kugundua umri wa kibaiolojia ni jambo rahisi zaidi na la garama nafuu zaidi kuliko mbinu nyingine. Itachukua dakika tano tu kupigwa picha ya skani na kubaini umri wa retina yako, umri wake wa kibaiolojia, na uwezekano wako wa kufariki mapema au la.