Fahamu Nigeria ilivyofanikiwa kukata mbawa za Twitter

Chanzo cha picha, Getty Images
Twitter imekubali msururu wa masharti ya kukomesha marufuku ya miezi saba dhidi yake nchini Nigeria, katika kile kinachoonekana kuwa ushindi mkubwa kwa utawala wa Rais Muhammadu Buhari katika juhudi zake za kudhibiti mtandao huo, baadhi ya wachambuzi wanasema.
Nigeria - nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika - sasa inajiunga na mataifa kama India, Indonesia na Uturuki, ambazo zinadhibiti vikali mitandao ya kijamii. Hili ni jambo ambalo serikali zingine za Kiafrika zinaweza kuzingatia, wakati zinajaribu kuzuia matumizi ya mitandao ya kijamii kuhamasisha vikundi vya upinzani.
Baadhi ya masharti yaliyokubaliwa na Twitter yameibua wasiwasi kuhusu shughuli zake za baadaye nchini Nigeria.
"Kwa hakika kuna wasiwasi kwamba Twitter huenda imekubali mpango ambao ungeruhusu Nigeria kuishinikiza katika maamuzi ambayo haingeweza kufanya vinginevyo," David Greene, mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Marekani la Electronic Frontier Foundation (EFF), aliiambia BBC.
Alisema Twitter ilipaswa kukubali kutii sheria za ndani iwapo tu zitazingatia haki za binadamu. Makubaliano hayo yaliipa serikali faida katika kutekeleza maagizo ya kuiondoa na madai ya data dhidi ya kampuni hiyo, Bw Greene aliongeza.
Kubadli msimamo baada ya kupuuzwa na Nigeria
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema utawala wa Rais Buhari una historia ya kutumia vibaya sheria na uhuru wa kujieleza, huku baadhi ya waandishi wa habari na wanaharakati wakifungiwa kwa kuikosoa serikali.
Sasa kuna wasiwasi kwamba kutakuwa na ongezeko la ukandamizaji kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii na jumbe zaidi zitaripotiwa na kufutwa na Twitter.

Chanzo cha picha, AFP
Twitter imekataa kuzungumzia makubaliano iliyofikia na Nigeria, na kuwaacha wengi wakiwa na maswali.
Kampuni hiyo iliandika tu kwenye Twitter kwamba "imefurahi" "kurejeshwa" na "kujitolea kushirikiana na Nigeria".
Hata hivyo, BBC inaelewa kuwa kampuni hiyo ilikubali masharti yaliyotajwa na serikali kabla ya huduma yake kurejeshwa.
Inajitokeza kama mabadiliko makubwa kwa kampuni iliyotangaza mwaka jana kuwa inafungua makao makuu yake ya Afrika nchini Ghana, ikitaja kama "bingwa wa demokrasia, mfuasi wa uhuru wa kujieleza, uhuru wa mtandaoni, na Mtandao Huria".
Wengi waliuchukulia uamuzi huo kuwa chukizo kwa Nigeria, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Sasa ingawa, Twitter imekuwa moja ya kampuni za kwanza za kidijitali kuangaziwa chini ya sheria mpya ya ushuru ya kidijitali iliyopitishwa mnamo 2020.
Mapema mwezi huu, Waziri wa Fedha Zainab Ahmed alisema kuwa kampuni zinazotoa huduma za kidijitali zitahitajika kulipa ushuru wa 6% kwa mauzo yao kuanzia mwaka huu ili kuongeza mapato ya umma wakati wa "vikwazo vya kifedha vinavyoibuka"..
Twitter imekubali kulipa kodi nchini Nigeria, na kuanzisha taasisi ya kisheria nchini humo, ingawa haijabainika ikiwa hiyo inamaanisha itafungua ofisi au kusajili mpatanishi tu.
"Tofauti inaweza kuwa kubwa kuhusiana na shinikizo kiasi gani Nigeria itaweza kutoa dhidi ya Twitter siku zijazo, na uwezo wa Twitter wa kupinga matakwa ya siku za usoni yasiyo na uwiano kutoka Nigeria," alisema Bw Greene.
Vijana wa Nigeria, hasa wenye ujuzi wa kidijitali, wanaiabudu Twitter. Ni zaidi ya jukwaa, linalotumika kama kduka linalouza kila kitu - kuanzia nafasi za kazi, hadi tovuti ya watu waliopotea, na sehemu ya kiraia kuwajibisha maafisa wa umma.

Chanzo cha picha, Getty Images
Twitter ilipiga hatua zaidi za kisiasa wakati wa maandamano ya #EndSars mnamo 2020 wakati huo ikawa jukwaa pendwa kwa waandamanaji vijana ambao walimlazimisha rais kuvunja Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (Sars), kitengo cha polisi ambacho kilijulikana kwa ukatili wake.
Maandamano ya #EndSars yalibadilika na kuwa wito wa kukomesha utawala mbaya nchini Nigeria na Rais Buhari amesema kuwa waandamanaji walitaka kumuondoa madarakani.
Serikali inalaumu Twitter kwa kushabikia maandamano hayo na inamlaumu wake wa zamani, Jack Dorsey, ambaye alionyesha kuunga mkono waandamanaji, kuwajibika kwa uharibifu uliotokea baada ya maandamano kutekwa nyara na wahalifu.
Wafuasi wa serikali wakishangilia
Kwa njia nyingi, masaibu yaTwitter nchini Nigeria zilionekana kama vita vya kibinafsi kati ya Bw Dorsey na Bw Buhari, na kiele cha vita hivyo ni kufutwa kwa ujumbe wa rais mwezi Juni mwaka jana.
Tweet hiyo ilirejelea vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Biafra vya 1967-70 na kuonya kwamba "wale wanaofanya vibaya leo" watashughulikiwa kwa "lugha watakayoelewa".
Kufuatia kuporomoka kwa Twitter, ni vigumu kuona jinsi maandamano kama vile maandamano ya #EndSars yanaweza kupangwa kwenye jukwaa bila ya kulaumiwa kwa kukiuka sheria za mitaa kama vile "kuchochea vurugu".

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini Gbenga Sesan wa kundi la haki za kidijitali la Nigeria linalofahamika kama Paradigm Initiativ, anaamini kuwa ni serikali iliyoathirika wakati wa marufuku ya miezi saba kwani haikuweza kupata ujumbe wake.
"Washindi halisi ni Twitter na watu wa Nigeria, serikali ndiyo iliyoshindwa zaidi," alisema.
Shirika lake ni sehemu ya muungano unaopinga marufuku hiyo na Bw Sesan anaamini kuwa serikali iliharakisha kutangaza kuondolewa kwa marufuku hiyo ya Twitter ili kuepika fedheha machoni pa watu kwani uamuzi unatarajiwa kutolewa wiki hii katika mahakama ya Ecowas.
"Ni aibu kwake [Rais Buhari] kwa sababu hili ni jambo litakalokumbusha watu jinsi utawala wake ulivyokandamiza uhuru wa kujieleza nchini Nigeria," alisema.












