Wakristo wa India wanaogopa kushambuliwa au kufungwa jela kwa kubadili dini

Jumapili moja ya mwezi Oktoba,Mchungaji Somu Avaradhi alipigwa na butwaa alipoingia kanisani mwake mjini Hubballi katika jimbo la Karnataka kusini mwa India.

"Kuna watu walikuwa wameketi ndani, wakiimba nyimbo za kidini za Kihindu na kupiga kelele," aliambia BBC.

Anasema aliwaita polisi, lakini walipofika, waandamanaji walimtuhumu kwa kumtukana na kumlazimisja mwanamume wa dhehebu la Kihidu kubadili dini na kujiunga na Ukristo. Mchungaji huyo alikamatwa - kushtakiwa kwa "kuzua hisia za kidini za tabaka lolote" - na kuzuiliwa gerezani kwa siku 12 kabla ya kuachiliwa kwa dhamana.

Kisa hiki sio cha kwanza -ripoti ya Evangelical Fellowship of India (EFI) iliorodhesha visa 39 za vitisho au unyanyasaji dhidi ya Wakristo kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu katika jimbo la Karnataka.

Hii ni pamoja na mashambulio dhidi ya wachungaji kutoka kwa washiriki wa makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia, na hata matukio ambapo waliripotiwa kuwazuia kufanya ibada. Wakristo ni jamii ya wachache nchini India ambako idadi kubwa ya watu ni waumini wa Wahind

Wawakilishi wa Wakristo wanasema mashambulio hayo yameongezeka tangu mwezi Oktoba, baada ya Chama cha Bharatiya Janata (BJP), ambacho kiko mamlakani huko Karnataka na pia kitaifa, kusema kinafanyia kazi sheria "kali" dhidi ya ubadilishaji wa kidini katika jimbo hilo.

Wakosoaji wameelezea rasimu ya sasa ya muswada huo kama ya "kibabe" -inajumuisha vifungo vya jela vya hadi miaka 10 kwa wale ambao watapatikana na hatia ya kuwashawishi wengine kwa "nguvu" kubadili dini, kutumia mbinu za "ulaghai" au ndoa, na ikiwezekana kunyimwa faida za serikali kwa wale wanaobadili dini- kutoka moja hadi nyingine.

Kila uamuzi kama huo utachunguzwa kwa kuwa wale watakaochagua kubadili dini watahitajika kuwaarifu maafisa wa eneo hilo miezi miwili kabla - na maafisa watachunguza sababu kabla ya kuruhusu jambo hilo lifanyike.

Viongozi wa Kikristo wana wasiwasi kuwa mswada huo mpya utawapa ujasiri wafuasi wa itikadi kali za Kihindu kulenga zaidi jamii yao.

"Pindi mswada huo utakapopitishwa, tutakabiliwa na mateso na matatizo zaidi," Peter Machado, Askofu Mkuu wa Bangalore, aliiambia BBC Hindi.

Muswada huo ni mfano wa sheria iliyoanzishwa mwaka jana katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh, ambalo pia linatawaliwa na BJP.

Katika Jimbo hilo, sheria hiyo ilibuniwa ili kukabiliana na kile kilichoitwa "jihad ya mapenzi", njama maarufu ya mrengo wa kulia ya Kihindu kwamba wanaume wa Kiislamu huwarubuni wanawake wa Kihindu kubadili dini kwa kupendekeza ndoa.

Polisi katika eneo hilo wamesajili zaidi ya visa 100 vya madai ya uongofu wa lazima, tovuti ya habari ya Print iliripoti mwezi Novemba.

Mchungaji Vijayesh Lal, katibu mkuu wa EFI, ambayo inaendesha makanisa 65,000 nchini India, alidai kuwa mtindo wa Karnataka ulikuwa sawa na kile kilichotokea Uttar Pradesh kabla ya sheria kuanzishwa.

Suala la kubadili dini ni mada yenye utata nchini India. Makundi ya mrengo wa kulia kwa muda mrefu yameshutumu wamishonari wa Kikristo kwa kuwabadilisha kwa nguvu Wahindu maskini kwa kuwapa pesa au usaidizi mwingine kama hongo - madai wanayokanusha.

Lakini Dalits (ambao awali hawakuguswa) wamejulikana kihistoria kugeukia Ukristo ili kuepuka uongozi wa tabaka la Wahindu wenye msimamo mkali. Licha ya sheria za kuwalinda, jamii hiyo mara kwa mara wamekuwa wahanga wa sio tu ubaguzi bali pia unyanyasaji.

Wachungaji wa Kikristo na makasisi huko Karnataka wanahofia hali itakavyokuwa siku zijazo. Hapo awali, mashambulizi hayo yalifanywa katika maeneo michache ya jimbo hilo, lakini sasa wilaya 21 kati ya 31 zimeripoti angalau tukio moja la vurugu.

"Nimekuwa hapa kwa miaka 40 lakini kusema kweli sijui kwa nini madai haya yanaibuka sasa.Tuna marafiki wengi miongoni mwa waumini wa Kihindu tunaoishi pamoja ," alisema Kasisi Thomas T, rais wa jumuiya wachungaji katika wilaya ya Belagavi.

Bw Thomas anasema mnamo mwezi wa Novemba, polisi wa eneo hilo waliambia jumuiya hiyo isifanye mikutano ya maombi ili kuepuka mashambulizi ya makundi ya mrengo wa kulia.

Afisa wa polisi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia BBC Hindi kwamba ingawa vituo vya polisi vimewashauri makasisi kuwa waangalifu, hakuna "sera ya serikali nzima" iliyotolewa kuhusu suala hilo.

Padre Francis D'Souza, kasisi katika kanisa la mtaani huko Belagavi, wiki iliyopita alidai kwamba mwanamume mwenye upanga alijaribu kumshambulia. Kisa hicho kinachunguzwa na maafisa wakuu wa polisi wamemhakikishia ulinzi Padri D'Souza.

"Lakini bado nina hofu ," anasema.

Wawakilishi kutoka jumuiya hiyo wamehoji haja ya kuwepo kwa sheria ya kupinga uongofu, wakisema kwamba katiba ya India inatoa haki kwa kila mtu "kueneza dini".

Hakuna sheria ya kitaifa inayozuia kubadili dini, na majaribio ya hapo awali ya kuwasilisha miswada kama hiyo bungeni yameshindwa. Lakini mataifa mbalimbali yametunga sheria kwa miaka mingi kudhibiti uongofu wa kidini.

wa BJP Arvind Bellad,ambaye aliongoza maandamano makubwa dhidi ta Mchungaji Somu, aliuliza kwa nini ni Wakristo pekee wanahofu kuhusu mswada huo mpya wa sheria.

"Kipengele cha kuvutia ni kwamba jumuiya nyingine za wachache kama Waislamu au Masingasinga au Majaini hawana wasiwasi kuhusu sheria hii mpya," aliongeza.

Waziri mkuu kiongozi wa serikali ya jimbo la Basvaraj Bommai amesema ni wale tu wanaojaribu kuwarubuni watu wabadili dini tofauti ndio wanaohitaji kuogopa sheria.

Lakini Askofu Mkuu Machado anasema kwamba mashambulizi na mazungumzo kuhusu mswada huo ni wazi yanalenga Wakristo.

"Kile tunachofanyiwa na serikali Si jambo jema," alisema.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na Meja Jenerali mstaafu SG Vombatkere alisema kuwa watu hawafai kuchukua sheria mkononi.

"Ikiwa nina malalamiko dhidi yako, siwezi kuja na kukupiga," alisema. "Sina haki ya kukushambulia, kwa lolote. Lakini jambo lisilo la kawaida limegeuzwa kuwa la kawaida siku hizi."