Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afya: Jinsi kupata watoto kunavyoathiri ubongo wa wanawake
Sote tunajua kwamba mwili wa mwanamke hupitia mabadiliko mengi ya kimwili wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
Lakini jambo lisilojulikana sana ni kwamba kuwa na mtoto pia hurekebisha muundo wa ubongo.
Imegundulika hata wale ambao ni mama au baba bila ujauzito hupata mabadiliko katika akili zao kutokana na kuwatunza watoto wao.
Hivi ndivyo uchunguzi wa mwandishi wa habari wa BBC wa sayansi Melissa Hogenboom umefichua, ambaye alihoji kundi la wataalamu ambao wamejitolea kutafiti jinsi kuwa na watoto huathiri ubongo.
"Mabadiliko makubwa yanayotokea katika viwango vya homoni wakati wa ujauzito huathiri ubongo wa mwanamke, na kumtayarisha kwa ajili ya uzazi," aeleza Pilyoung Kim, profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Denver, nchini Marekani.
"Tuligundua kuwa katika miezi ya kwanza ya kipindi cha baada ya kujifungua, akili za mama zilikuzwa," anasema.
"Hilo linaonekana kupingana moja kwa moja na dhana iliyozoeleka iliyopo ya 'ubongo mjamzito'," anasema, kuhusiana na imani kwamba wajawazito ni wasahaulifu na ni vigumu kuzingatia.
Hata hivyo, mwanasayansi wa neva Ann-Marie De Lange, kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Lausanne, Uswisi, anasema kwamba si imani tu:
"Wanawake wengi huhisi kwamba utendaji wao wa akili si mzuri sana katika kipindi hiki, na kwamba wana uwezo mdogo wa kukumbuka", anasema.
De Lange ana nadharia kwa nini wanaweza kuhisi hivi wakati ubongo wao unakua.
"Inaweza kuwa katika kipindi hiki ubongo unajirekebisha na kuanza kuzingatia kitu kingine," anaeleza.
"Kuna tafiti zinazoonesha kuwa mabadiliko haya yanahusishwa na tabia za uzazi kama vile kushikamana na mtoto," anabainisha.
Mabadiliko ya ubongo
Wanasayansi na wataalam wengine wameweza kutambua ni maeneo gani ya ubongo ukuaji wa muundo unaohusiana na uzazi hutokea.
Moja ni katika maeneo ambayo yanahusiana na kinachojulikana kama reward circuit, ambayo inahusisha gamba la mbele na sehemu nyingine ndogo katikati ya ubongo.
Mabadiliko haya huwafanya wanawake kujisikia kuhamasishwa sana kuitikia mwito wa watoto wao, na kwamba wanahisi furaha wakati watoto wao wadogo wanatabasamu.
Pia kuna marekebisho katika maeneo ya ubongo yanayohusiana na udhibiti wa kihisia, kama vile amygdala na gamba la mbele la singulate, ambayo huruhusu mama kudhibiti wasiwasi wake mwenyewe wakati wa kilio cha mtoto.
Na kuna mabadiliko mengine katika eneo la gamba la mbele ambayo huathiri uwezo wa kujifunza na kufanya maamuzi, na ambayo husaidia mama kuchagua jibu linalofaa zaidi.
Kwa upande mwingine, kuna marekebisho katika maeneo sita tofauti yanayohusiana na huruma, ambayo huwasaidia akina mama kuelewa ni nini watoto wao wanahisi.
Na hatimaye, maeneo yote ya ubongo yanayohusiana na hisia huimarishwa - harufu, ladha, kugusa, kusikia na kuona - kusaidia mama kujuana na kuzoeana na watoto wao wachanga.
"Tukitafakari kwa mtazamo wa mageuzi ni mantiki kuwa mabadiliko yoyote yanayokuza malezi na ulinzi wa mtoto yana manufaa si kwa watoto pekee bali pia kwa mafanikio ya uzazi kwa mama," anasema De Lange.
Kulingana na mtaalamu, "baadhi ya mabadiliko yanaweza kuisha baada ya kujifungua, lakini wengine wanaweza kuendelea na mabadiliko hayo wakati wa kipindi cha baada ya kujifungua na hata kwa miaka."
Mabadiliko kutokana na uzoefu
Kile ambacho wataalam hawajui kwa uhakika ni ikiwa mabadiliko haya ambayo hudumu kwa miaka kadhaa ni matokeo ya kuzaa mtoto na mabadiliko yake ya homoni, au ikiwa kwa kweli ni kile kinachojulikana kama "plastiki ya ubongo": mabadiliko yanayoletwa sio kutokana na ujauzito lakini kutoka kwa uzoefu wa malezi.
neuroplasticity ni mchakato ambao ubongo wetu hupanga upya na kurekebisha mtandao wake wa neva kwa kukabiliana na mabadiliko ya nje au ya ndani.
Hadi si muda mrefu uliopita iliaminika kuwa watoto pekee wana uwezo huu wa kuunda akili zao, lakini sasa inajulikana kuwa maeneo mengi ya ubongo yanabaki "plastiki" - au kubadilishwa - hata wakati wa watu wazima.
Na kuna ushahidi kuonesha kwamba kulea mtoto husababisha mabadiliko katika ubongo.
"Kadiri mama anavyopata uzoefu zaidi, ndivyo miunganisho tunayoona kati ya niuroni katika maeneo ya ubongo ambayo ni muhimu kwa uzazi," anasema Kim.
Mabadiliko haya yanaweza pia kutokea katika ubongo wa mzazi. Kim anataja uchunguzi uliofanywa nchini Israel na wanandoa wa kiume ambao walipata watoto hivi karibuni.
"Inapendeza sana," anasema. "Sio tu kwamba wazazi wote wawili walionekana kuwa na mwitikio mkubwa wa ubongo kwa mtoto wao, lakini mzazi ambaye ndiye mlezi mkuu alionesha usikivu zaidi wa ubongo kuliko mpenzi wake."
Kwa Hogenboom hii inaonysha kuwa kupata watoto hurekebisha ubongo wa mama au baba zaidi ya ujauzito. Na pia inathibitisha kuwa "wanawake hawajakusudiwa kibaiolojia kuwa walezi wa msingi wa watoto."
"Ujauzito kwa hakika hutayarisha mwili, lakini ni wazi kuwa ni wakati na nguvu ya mahusiano ya kihisia ambayo yanahusiana na jinsi ubongo unavyobadilika," anasema.
Kusoma mabadiliko ya muda mrefu ambayo uzazi huacha katika akili za wanawake ilisababisha ugunduzi ambao haukutarajiwa.
Utafiti wa Dk De Lange na timu yake katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Lausanne ulionesha kuwa wanawake ambao walikuwa wamejifungua watoto wengi walikuwa na akili ambazo zilionekana "za ujana" kuliko za wenzao wa rika moja.
"Wanawake ambao walikuwa wamezaa watoto wengi walionesha mabadiliko machache ya ubongo kuliko tunavyoona kawaida tunapozeeka.
"Hii inaweza kuonesha kuwa, kuwa na watoto katika umri mdogo kunaweza kuwa na athari ya kinga kwenye ubongo tunapozeeka," anasema.
Hata hivyo, anafafanua kuwa manufaa waliyopata yalikuwa "ya wastani sana", na kwamba kuwa na watoto wachanga ni mojawapo tu ya mambo mengi yanayoathiri jinsi tunavyozeeka.
Kwa maana hii, inaangazia kuwa uzazi pia unahusishwa na viwango vya juu vya msongo wa mawazo - kutokana na ukosefu wa usingizi na kupungua kwa mwingiliano wa kijamii, kwa mfano - ambao hauathiri tu mchakato wa kuzeeka lakini pia unaweza kuathiri afya ya akili ya baadhi ya wanawake.