Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Saad Al-Jabri: Mwanamfalme Mohammad bin Salman alituma watu waje kuniua Canada
Saad al-Jabri, afisa wa zamani wa masuala ya usalama nchini Saudi Arabia, alimlaumu mwanamfalme Mohammed bin Salman kwa kutuma kundi la wauaji kumuua nchini Canada, siku chache baada ya kuuawa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul, wakati wa mahojiano na kipindi cha televisheni ya CBS America, 60 Minutes.
Al-Jabri alikuwa ameandikisha kesi kwenye mahakama nchini Marekani mwaka 2020 inayojumuisha makaratasi 106 ambayo hayajathibitishwa na yanayochunguzwa na mahakama katika mji mkuu wa Marekani Washington ambapo anamlaumu mwanamfalme kwa kujaribu kumuua ili kumnyamazisha.
Jabri anasema ana habari za siri kubwa. Nyaraka hizo zinafichua habari kuhusu madai ya ufisadi na usimamizi wa kundi la mamluki linalojulikana kama Tiger Team lililoshiriki kwenye mauaji ya Khashoggi.
Saad Al-Jabri ni nani?
Saad al-Jabri hakuwa afisa wa usalama au afisa wa jeshi kimasomo au kuhitimu. Alisomea uhandisi wa kompyuta katika chuo cha Uskochi cha Edinburgh kabla ya kujiunga na wizara ya mambo ya ndani.
Alifanya kazi huko kwa miongo minne na kupanda vyeo hadi kufikia cheo cha meja jenerali akiwa karibu sana na waziri wa mambo ya ndani na mwanamfalme Muhammad bin Nayef, ambaye sasa yuko gerezani.
Mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya kompyuta
Mkurungezi wa gazeti la New York Times mjini Beirut, Ben Hubbard alimtaja kama mmoja wa maafisa muhimu zaidi wa wa ujasusi nchini Saudi Arabia na mtaalamu katika masuala ya teknolojia ya kompyuta na alitoa mchango mkubwa katika jitihada za Saudi Arabia kupambana Al-Qaeda na ushirikiano wa masuala ya usalama na idara za ujasusi za nchi za magharibi.
Kulinga na maafisa nchini Marekani, al-Jabri alikuwa na jukumu muhimu kwenye faili nyingi za siri za eneo hilo ikiwemo vita dhidi ya al-Qaeda na ulinzi kwa vituo vya mafuta vya Saudi Arabia na alikuwa akiwasiliana na CIA kuhusu Iraq, Syria, Iran na Yemen.
Al-Jabri amekuwa kimya tangu ahamie Canada mwaka 2017 lakini baada ya kukamatwa mtoto wake wa kiume na bintiye, alivunja kimya chake na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masaibu yake.
Mtoto wake wa kiume Dr. Khaled, ambaye pia anaishi Canada anasema baba yake anahofia maisha yake na yuko chini ya shinikizo kali kutoka kwa mwanamfalme Mohammed bin Salman kurudi nchini Saudi Arabia.
Shinikizo zinazoongezeka
Shikikizo dhidi ya Al-Jabri ziliingia awamu mpya baada ya kukamatwa kwa mwanae Omar na bintiye Sarah pamoja na ndugu yake Abdel Rahman Machi 2020 na mawasiliano yao nao yamekatwa tangu wakati huo.
Hubbard alimnukuu Khaled na waliokuwa maafisa nchini Marekani waliokuwa na uhusiano wa kikazi na Al-Jabri kuwa Mohammed bin Salman anamshinikiza Saad Al-Jabri arudi Saudi Arabia kwa sababu ya hofu kuwa mtu kama yeye ana siri kubwa na habari ambazo ziko nje ya uwezo wake.
Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Yemen, Gerald Feierstein, ambaye alikuwa akiwasiliana na Al-Jabri kwa sababu ya kazi yake, anasema bin Salman ana wasi wasi kuwa yeyote yuko nje ya udhibiti wake. Anaongeza kuwa Al-Jabri amekuwa akishughulikia nyaraka za siri wakati akifanya kazi nchini Saudi Arabia kwa miongo kadhaa na ana habari nyingi zikiwemo habari kumhusu Mohammed bin Salman.
Firstein alimsifu Al-Jabri: Yeye ni mtu mzuri, bila ya kutilia shaka. Ninafikiri yeyote ambaye amefanya kazi naye ana mawazo sawa na hayo. Ana akili, mchapa kazi na mshirika mzuri wa Marekani.
Saad Al-Jabri alijipata muathirika kwenye mzozo ndani ya familia tawala nchini Saudi Arabia. Alikuwa mshirika wa karibu wa mtu aliyekuwa na ushawishi na waziri wa mambo ya ndani Prince Muhammad bin Nayef, ambaye kwa msaada wa watu wapya na waliokuwa wamesoma kama Jabri walifanikiwa kuwashinda al-Qaeda nchini Saudi Arabia.
Kabla ya Muhammad bin Salman kumpindua binamu yake na mwanamufalme Mohammad bin Nayef mwaka 2017 na kumweka chini ya kifungo cha nyumbani, alikuwa amedhoofisha nafasi yake kwa kuwandoa wale waliokuwa karibu naye wakiongozwa na Saad al-Jabri.
Baadhi ya vyombo vya habari vinaripoti kuwa makabiliano kati ya al-Jabri na Muhammad bin Salman yalianza wakati wa kifo cha mfalme Abdullah na kuingia mamlakani kwa Mfalme Salman mwaka 2015.
Baada ya muda mfupi Muhammad bin Salman ambaye alikuwa waziri wa ulinzi akaanzisha vita dhidi ya Yemen.
Al-Jabri alipinga hatua ya Saudi Arabia kuingia vitani nchini Yemen, kwa sababu aliamini kuwa vilikuwa vya gharama kubwa na matokeo hayakutarajiwa, msimamo ambao umekuja kuwa wa ukweli.
Mateka
Baada ya Muhammad bin Nayef kuwa mwanamfalme mwaka 2015, mvutano uliibuka kuhusu ni nani angesimamia wizara ya mambo ya ndani ambayo ilikuwa chini ya usimamizi wa bin Nayef kwa muda mrefu.
Pande mbili kwenye mzozo huo ndani ya wizara ya mambo ya ndani zilikuwa kati ya al-Jabri na Meja Jenerali Abdulaziz al-Huwairini, ambaye ana uhusiano wa karibu na Muhammad bin Salman na matokeo ya mzozo huo yalipendelea mrengo wa bin Salman, na al-huwairini akapewa jukumu la mkuu wa usalama wa taifa nchini Saudi Arabia mwaka 2017.
Kulingana na Washington Post ni kuwa kutimuliwa kwa Jabri kulijiri baada ya yeye kukutana na aliyekuwa mkurugenzi wa CIA John Brennan mjini Washington bila ufahamu wa Mohammed bin Salman.
Al-Jabri na bosi wake wa zamani walishangazwa mwishoni mwa mwaka 2015 wakati televisheni nchini Saudi Arabia ilitangaza habari za kufutwa kwake. Baada kurejea uamuzi ulitolewa afutwe kupitia amri ya kifalme, ambapo baadaye alisafiri na watu wengi wa familia yake nchini Ujerumani na Marekani.
Baada ya Nayef kupinduliwa na mali yake kutwaliwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwaka 2017, Al-Jabri aliogopa kuwa anaweza kukutana na hatma kama hiyo, kwa hivyo aliamua kubaki ng'ambo na hakurudi tena nchini Saudi Arabia.
Katika taarifa ya Mei 24 2020, Human rights Watch walinukuu taarifa zilizosema kuwa Saad al-Jabri aliondoka Saudi Arabia mwaka 2017 kabla ya kuondolewa kwa Muhammad bin Nayef na kuapiswa kwa Muhammad bin Salman kama mwanamfalme Juni 21, 2017.
Wakati wa kuondolewa kwake Mohammad bin Nayef, na watoto wawili tu wa al-Jabri, Omar na Sarah ambao wakati huo walikuwa na umri wa miaka 18 na 17 mtawalia ndio walikuwa nchini Saudi Arabia.
Wote walijaribu kukimbia nchi siku hiyo lakini walisimamishwa na maafisa kwenye uwanja wa ndege na kuambiwa kuwa walikuwa wamepigwa marufuku ya kusafiri ng'ambo.