Paul Rusesabagina: Mfahamu mkosoaji mkuu wa rais wa Rwanda Paul Kagame

Paul Rosesabagina

Chanzo cha picha, RIB

Maelezo ya picha, Paul Rosesabagina

Mtu ambaye alioneshwa katika filamu ya ''Hotel Rwanda'' kama shujaa aliyeokoa maisha ya watu wengi wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda amepatikana na hatia ya ugaidi katika mahakama nchini Rwanda.

Paul Rusesabagina alipatikana na hatia ya kulifadhili kundi moja la waasi akiwa mafichoni ambalo liliwauawa raia katika shambulio la 2018.

Familia yake imedai kwamba alichukuliwa na kupelekwa nchini Rwanda kwa nguvu.

Lakini Je Paul Rusesabagina ni nani haswa?

Paul Rusesabagina ni raia wa Rwanda aliyezaliwa tarehe 15 mwezi Juni 1954) .

Alikuwa mmoja kati ya watoto tisa waliozaliwa kutoka kwa baba Mhutu , mzee aliyeheshimika sana na jamii kwa jina Thomas Rupfure na mama Mtutsi kwa jina Murama nchini Rwanda.

Ijapokuwa amekuwa akisema kwamba alilelewa katika maisha ya umasikini, Rusesabagina ameelezea maisha yake ya utotoni kama yale ya wastani kwa viwango vya Afrika miaka ya hamsini.

Wazazi wa Rusesabagina walimpeleka katika shule moja iliokuwepo mjini karibu na Gitwe iliokuwa ikifadhiliwa na kanisa la Seventh-day Adventist Church.

Akiwa na umri wa miaka 13 , alikuwa anaweza kuongea Kiingereza na Kifaransa pamoja na lugha ya mama ya Kinyarwanda.

Ni kwanini Rusesabagina alikamatwa?

Paul Rusesabagina, ni kiongozi wa muungano wa kisasa MRCD-Ubumwe ambao Rwanda inauhusisha na mashambulio ya ugaidi yaliyowauwa Wanyarwanda katika kituo cha polisi cha mjini Kigali.

Rusesabagina alipata umaarufu baada ya kucheza filamu ya Hollywood kwa jina Hotel Rwanda iliyotolewa mnamo mwaka 2004.

Katika filamu hiyo , Paul Rusesabagina aliangaziwa kama mtu aliyetumia ushawishi wake - na rushwa- kuwashawishi maafisa wa kijeshi kuwapa njia salama ya kuwatorosha karibu watu1,200 ambao walitafuta maficho katika Hôtel des Mille Collines, ambayo alikuwa meneja wake wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Baada ya filamu hiyo kutolewa Bw. Rusesabagina alitunukiwa medali ya Rais wa Marekani ya Uhuru 2005,George Bush.

Hata hivyo kundi la manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Ibuka lilisema kuwa alitilia chumvi jukumu lake la kuwasaidia wakimbizi kujificha hotelini katika siku 100-za mauaji ya kikatili mwaka 1994.

Jina la Rusesabagina hivi karibuni lilikuwa katika kesi ya ugaidi nchini Rwada. Mahakama ilisikiliza madai kwamba kundi la waasi wa the National Liberation Front (FLN), lilipokea msaada kutoka kwa rais wa Zambia Edgar Lungu kwasababu ya urafiki wake wa karibu na Bwana Rusesabagina. Msemaji wa Bwana Lungu alikana madai hayo katika mahojiano na BBC.

Mwaka 2011, Bwana Rusesabagina alishutumiwa kudhamini kundi na muungano wa makundi ya ugaidi yenye silaha na itikadi kali.

Rusesabagina amekuwa naibu kiongozi wa muungano wa vyama vya kisasa vinavyoipinga serikari ya Kigali wenye makundi ya kijeshi -FLN -unaoendesha harakati zake mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mwaka 2018, kundi la FLN lilidai kufanya mashambulizi kwenye ardhi ya Rwanda kwenye maeneo ya msitu wa Nyungwe ambapo watu wengi waliuawa..

George Bush akimtuza Rosesabagina kwa jukumu lake alilochukuwa la kuwahifadhi wakaazi katika hoteli

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, George Bush akimtuza Rosesabagina kwa jukumu lake alilochukuwa la kuwahifadhi wakaazi katika hoteli

Je alifika vipi nchini Rwanda na kufunguliwa mashtaka

Akizungumza na BBC mtoto wa kike wa Bwana Rusesabagina -Anaïse Kanimba alisema :''alitekwa nyara alipokuwa safarini Dubai ", katika Muungano wa nchi za kiarabu (UAE).''

"Alifika Dubai, ikiwa ndio mara ya mwisho tulipozungumza nae akituambia kuwa amefika salama, hatukumsikia tena hadi tulipoona kuwa amekamatwa na utawala wa Rwanda.

"Hatujui alifikaje huko na kilichotokea, ndio maana tunafikiria kuwa alitekwa kwasababu asingeenda Rwanda kwa hiari yake."

Hatahivyo kulingana na televishini ya Al Jazeera, Waziri wa sheria wa Rwanda Johnston Busingye alikubali kuwa Rwanda iliilipa ndege ya kumsafirisha mshukiwa huyo.

Wakati alipofikishwa Kigali, wachunguzi wa Rwanda walisema alikamatwa na ushirikiano wa polisi wa kimataifa.

Amekuwa akiishi uhamishoni Marekani na ni raia wa ubelgiji , aliongeza.

Je alikuwa anakabiliwa na mashtaka yapi?

Raia huyo mwenye umri wa miaka 66 alikamatwa mwezi Agosti 2020 na kufunguliwa mashtaka 9 dhidi yake ikiwemo kufadhili ugaidi, mauaji kwa njia ya ugaidi, kuanzisha kundi la wapiganaji kinyume na sheria na kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi miongoni mwa mashtaka mengine.

Wakati wa kesi hiyo - ambayo ilisikilizwa nchini Rwanda, mkosoaji huyo mkubwa wa rais Paul Kagame aliambia mahakama kwamba alitaka kutambuliwa kama raia wa Ubelgiji na kusema kwamba alitekwa nyara na serikali ya Rwanda ambayo haina haki ya kumfungulia mashtaka.

Serikali ya Rwanda inasema nini?

Kwa upande wa serikali ya Rwanda, inasema kwa muda mrefu jina la Bwana Rusesabagina lilikua miongoni mwa majina yaliyopo kwenye waranti ya kimataifa, kwa ajili ya kukamatwa na kuwasilishwa katika mahakama za Rwanda.

Ofisi ya Rwanda ya upelelezi (RIB) ilisema kuwa amekamatwa kwa ushirikiano wa kimataifa.

Waziri wa sheria wa Rwanda Johnson Busingye alipongeza ushirikiano wa kimataifa katika kumkamata Bwana Rusesabagina

Chanzo cha picha, MINIJUST/RWANDA

'' Rusesabagina alikuwa anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikiwa ni pamoja na ugaidi, utekaji, kuchoma moto mali na mauaji'' , alisema kaimu msemaji wa Ofisi ya Rwanda ya upelelezi (RIB) Dkt Thierry Murangira .

Bwana Murangira aliwaambia waandishi wa habari kuwa uhalifu anaodaiwa kuufanya aliutekeleza dhidi ya Wanyarwanda ambao hawakuwa na silaha, wasio na hatia kwenye ardhi ya Rwanda ikiwa ni pamoja na mashambulizi yaliyotekelezwa katika wilaya ya Nyaruguru Juni 2018, Nyungwe, na Wilaya ya Nyamagabe Disemba 2018.

Waziri wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda , Johnston Busingye alisema kuwa kukamatwa kwa Rusesabagina ni ujumbe wa wazi kwa yeyote anayeua au kufanya ugaidi dhidi ya Rwanda atakamatwa.

"Wale wanaoshukiwa kuua na kufanya ugaidi dhidi ya Wanyarwanda , wale wanaopanga, kudhamini kwa pesa ugaidi dhidi ya Wanyarwanda wataletwa mbele ya sheria," alisema.

Waziri Busingye alipongeza ushirikiano wa kimataifa na juhudi zilizofanyika katika kumkamata Bwana Rusesabagina.