Ghasia Afrika Kusini: Taarifa ghushi zinazosambazwa mtandaoni

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Na Peter Mwai na Christopher Giles
- Nafasi, BBC Reality Check
Kadiri ghasia zilivyoenea Afrika Kusini kutokana na kufungwa jela kwa rais mstaafu Jacob Zuma, watu mitandao ya kijamii wamekuwa wakisambaza baadhi ya video na picha ambazo ni za kupotosha.
Rais wa sasa Cyril Ramaphosa tayari amewahimiza raia wa Afrika Kusini "kujizuia kuchapisha na kusambaza jumbe za uchochezi kwenye mitandao ya kijamii, na kutosambaza taarifa za uvumi na za kupotosha..."
Tumechunguza baadhi ya picha na video za kupotosha zilizosambazwa sana.
Picha hii haimuonyeshi Zuma akiwa jela

Chanzo cha picha, EPA
Picha iliyohaririwa kuifanya ionekane kana kwamba inaonyesha Jacob Zuma akiwa na sare za wafungwa za rangi ya chungwa imesambazwa sana.
Ilisambazwa mara elfu kadha ilipochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook unaojiita "Jacob Zuma deluxe", huku mamia ya watu wakichangia maoni yao, wengi wakimuonea huruma Bw Zuma na wengine wakisema alistahiki kufungwa jela.
Hata hivyo, baadhi walishuku uhalisi wa picha hiyo. Ukitazama kwa makini, picha hiyo ina jina la akaunti ya Twitter ambapo ilichapishwa mara ya kwanza mnamo 8 Julai.
Na ukiitazama kwa makini tena utaona kwamba kuna mstari unaoonekana kana kwamba unazunguka kichwa chake, hasa juu kichwani jambo ambalo linatilia shaka uhalisi wake.
Ukitafuta picha hiyo mtandaoni, inatokea picha nyingine ambayo inafanana sana na hiyo, ila haina kichwa cha Zuma.
Imekuwepo mtandaoni kwa miaka mingi.
Tumebaini chanzo chake kuwa hifadhi ya picha za AFP, ambayo inaonyesha wazi kwamba ilipigwa mwaka 2002, katika gereza la Pollsmoor, Cape Town.
Ni vyema kusisitiza kwamba ingawa rais huyo wa zamani yumo gerezani, chini ya kanuni za Covid za sasa nchini humo, bado hajaruhusiwa kutangamana na wafungwa wengine.
Binti wa Zuma alitumia picha za zamani
Akaunti ya Twitter ya binti wa Zuma, Dudu Zuma-Sambudla, ilichapisha picha ya watu wakiwa wamejilaza chini kwenye moja ya barabara kuu za jiji la Durban.

Ilikuwa na ujumbe: "Jiji la Durban, Twawaona! Amandla," na ilikuwa na kitambulisha mada #FreeJacobZuma. "Amandla" - maana yake ni nguvu - na ni kauli mbiu iliyotumiwa wakati wa maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi.
Hata hivyo, picha hiyo haihusiani na matukio ya sasa.
Inatokana na maandamano mengine yaliyofanyika mwaka jana.
Tumeipata picha inayokaribia sana kufanana na picha hiyo ambayo ilichapishwa 25 Septemba 2020 ambapo watu wale wale na magari yayo hayo yanaonekana barabarani.
Ilipigwa wakati wa maandamano ya wapiganaji wa zamani waliotaka malalamiko yao ya kijamii na kiuchumi kuangaziwa.
Ingawa picha hiyo ni tofauti kidogo, ukizingatia yalipo magari na walipo watu na mavazi yao, ni dhahiri kwamba ilipigwa wakati mmoja na hiyo iliyochapishwa na Dudu Zuma-Sambudla.
Video ya zamani inayodaiwa kuonyesha matukio ya sasa
Video inayoonyesha makabiliano kati ya watu weusi na wazungu imetazamwa zaidi ya mara 300,000 kwenye Twitter, na aliyeichapisha anadai inaonyesha makabiliano yaliyotokea kipindi hiki.
Ujumbe huo wa Twitter uliochapishwa 13 Julai, unasema: "Wakuliwa wazungu Afrika Kusini wakichapwa kwa mijeledi na magari yao kuibiwa baada ya taifa hilo kutumbukia kwenye uporaji".

Akaunti hiyo ya Twitter iliyochapisha video hiyo mwenyewe anatokea Poland, na imekuwa ikichapisha ujumbe wenye mantiki ya nadharia za kupotosha na chuki dhidi ya wahamiaji pamoja na kuendeleza ubabe wa wazungu.
Video hiyo si ya wakati huu bali ilikuwa ikisambazwa kabla ya ghasia za sasa kuzuka 9 Julai.
Zipo taarifa mtandaoni zilizochapishwa 25 Juni zikiangazia video hiyo, ambapo zinasema mgogoro huo ulitokana na malipo ya mshahara. Hatujaweza kubaini kikamilifu ukweli halisi kuhusu mzozo huo ingawa ni wazi haihusiani na matukio ya sasa.
Simba hawajaachiliwa kutoka kwenye hifadhi

Video moja iliyosambazwa sana ilidai kwamba waandamanaji walikuwa wameubomoa ua kwenye hifadhi ya Hluhluwe katika mkoa wa KwaZulu-Natal, na kuwaachilia wanyama wakiwemo simba.
Akaunti hiyo iliwatahadharisha watu wajichunge dhidi ya simba na ujumbe huo ulitolewa maoni sana na watu na kusambazwa sana.
Lakini unapotosha kwani video hiyo ni ya zamani.
Ezemvelo KZN Wildlife, shirika la serikali linalosimamia hifadhi hiyo ya wanyama, linasema video hiyo ilichukuliwa katikati ya mwezi Mei wakati wa maandamano tofauti na ya sasa.
Wenyeji walikuwa wameandamana wakitaka kuajiriwa.
"Kwa sasa hatujashuhudiwa uharibifu wowote kwenye mali yetu," hifadhi hiyo ilisema kwenye Twitter 12 Julai.















