Bilionea Richard Branson na kampuni yake Virgin Galactic kuanzisha utalii wa anga za mbali mwakani

Sir Richard Branson

Chanzo cha picha, Getty Images

Kampuni ya Virgin Galactic inasema itauza hisa zake zenye thamani ya dola za kimarekani $500m baada ya kufanikiwa kukamilisha safari yake ya anga za mbali jumapili.

Kampuni hiyo inasema inapanga kutumia fedha zitakazopatikana kuendeleza miundombinu yake.

Jumapili hii, Sir Richard Branson, bilionea na mwanzilishi wa kampuni hiyo ya Virgin Galactic, amefanikiwa kufikia anga ya mbali kabisa nje ya sayari ya dunia akitumia moja ya ndege zilizotengenezwa kwa miaka 17.

Ameiita safari hiyo kama "safari ya uzoefu" baada ya kurejea kwenye sayari ya dunia akitumia zaidi ya lisaa limoja.

Safari hiyo imemfanya mfanyabiashara huyo kuwa mtalii wa mwanzo mwanzo kutalii anga za mbali kwa kutumia usafiri wa kampuni yake akiwapiku mabilionea wenzake kama Jeff Bezos wa Amazon na Elon Musk wa SpaceX, ambao ni manguli pia kwenye teknolojia

Hisa kwenye kampuni ya Virgin Galactic zilipanda kwa asilimia 8% kabla ya soko la hisa kufunguliwa Marekani siku ya Jumatatu. Lakini zilishuka vibaya kwa 17% kufikia jioni ya siku hiyo, baada ya kutangazwa kuwa hisa zake zinauzwa.

Sir Richard anamiliki karibu robo ya hisa zote za kampuni hiyo.

'Ujionee mwenyewe'

Virgin
Maelezo ya picha, Ndege ya kampuni ya Virgin, iliyombeba Bilionea Branson

Sir Richard aliambatana na marubani mawili kwenye ndege hiyo na wafanyakazi watatu wa kampuni hiyo- ikiwa ni jaribio la kutalii kwenye anga za mbali akitaka kuanza kufanya biashara hiyo ya kupeleka watalii kwenye anga hizo.

"Nilikuwa na kijitabu kidogo na kuandika karibu vitu 30 mpaka 40 vitakavyomsaidia yeyote atakayekwenda huko kufurahia zaidi," alisema. "Njia pekee ya kuvijua vitu hivi vidogovidogo ni kusafiri na kwenda huko na kujione amwenyewe."

Karibu watu 600 wameshalipia tikieti zao zitakazowagharimu mpaka dola $250,000 - miongoni mwa waliolipia tiketi ni bilionea na mmiliki wa makampuni ya Space X na Tesla, Elon Musk, kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Wall Street Journal.

Kwa mara ya kwanza Sir Richard alitangaza nia yake hiyo ya kutengeneza ndege itakayosafiri kwenye anga za mbali mwaka 2004, akiamini kwamba angeweza kuanzisha biashara ya utalii wa anga za mbali kufikia mwaka 2007.

Licha ya changamoto za kiufundi na ajali ya mwaka 2014, hisa za kampuni hiyo ziliongezeka maradufu mwaka huu, wakati huu ambapo biashara hiyo anayotaka kuianzisha ya utalii wa anga za mbali ikikaribia kuanza.

Ken Herbert, mchambuzi wa masuala ya anga, alisema kampuni hiyo inaweza kuanza kuuza kwa matajiri hivi karibuni tiketi za kwenda huko.

"Tunaona mafanikio ya Branson kama mapinduzi makubwa ya soko kwa Virgin Galactic ambayo ni ngumu kwa jamii kuyapuuza," alisema kwa kifupi.