Sulli Deals: Mwanamke wa India 'auzwa mtandaoni kwa kuwa Muislamu'

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wiki moja iliyopita makumi ya wanawake wa Kiislamu nchini India walijikuta wanauzwa mtandaoni.

Hana Khan, rubani wa ndege aliyekuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa kwenye orodha hiyo, aliiambia BBC kwamba alifahamishwa juu ya suala hilo na rafiki yake alipomtumia ujumbe wa Twitter ulioambatanishwa na tangazo hilo.

Ujumbe huo ulimpeleka "Sulli Deals", progamu tumishi na tovuti ambayo ilikuwa imechukua picha za wanawake zilizo mtandaoni na kuziambatanisha na maelezo kuwa wanawake hao ni "dili ya siku".

Ukurasa wa kwanza wa App hiyo ina picha za mwanawake asiyejulikana. Katika kurasa mbili zilizofuata Bi Khan aliona picha za rafiki yake. Baada ya ukurasa huo aliona picha yake.

"Nilihesabu majina 83. Huenda kuna mengine zaidi," aliiambia BBC. "Walichukua picha yangu kutoka Twitter na ilikuwa na utambulisho wangu. Hii app imekuwa ikiendelea kufanya kazi kwa siku 20 na hatukuwa na habari. Imenishtua sana."

Ijidai kuwapa nafasi watumiaji wake kununua "Sulli" - neno linalotumiwa na Wahindu wa mrengo wa kulia kuwanyanyasa mtandaoni wanawake wa Kiislamu. Hakukua na mnda wa aina hiyo - lengo la app hiyo lilikuwa kuwadhalilisha.

Bi Khan anasema alilengwa kwa sababu ya dini yake. "Mini ni mwanamke wa Kiislamu anayeonekana na kusikika," alisema. "Na wanataka kutunyamazisha."

GitHub - mtandoa uliotumiwa kama mwenyeji wa app hiyo - ilifungwa baada ya malalmishi kuibuka. "Tulisimamisha akaunti za watumiaji kufuatia uchunguzi wa ripoti za shughuli kama hizo, ambazo zote zinakiuka sera zetu," kampuni hiyo ilisema katika taarifa.

Lakini kisa hicho kimewaogofya wanawake. Wale walioangaziwa katika app hiyo ni wanawake wote walio na ushawishi, wakiwemo waandishi wa habari, wanaharakati, wasanii na watafiti. Baadhi yao wamefuta akaunti zao za mitandao ya kijamii na wengine zaidi wanasemakana kuwa na wasiwasi huenda wakaendelea kunyanyaswa.

"Hata ukiwa mkakamavu kiasi gani, picha na maelezo yako ya kibinafsi yakiwekwa mtandaoni bila shaka utaingiwa na hofu, na utapata usumbufu wa kiakili,"mwanamke mwingine aliiambia BBC Idhaa ya Kihindi.

Lakini wanawake wengine ambao maelezo yao yaliwekwa mtandaoni waliwakaripia waliohusika, na kuapa kukabilian nao vilivyo. A Makumi wao wamesambaza ujumbe katika makundi ya WhatsApp kuomba msaada na wengine kama Bi Khan wamewasilisha taarifa kwa polisi.

Watu mashuhuri, wanaharakati na viongozi pia wamelaani kitendo hicho. Polisi imesema kuwa imeanzisha uchunguzi lakini haijataja ni nani anaendesha app hiyo.

Watu waliounda app hiyo walitumia utambulisho feki,lakini Hasiba Amin, mshirikishi wa mitandao ya kijamii ya chama cha upinzani cha Congress, amelaumu akaunti kadhaa ambazo mara kwa mara huwashambulia Waislamu hususan wanawake wa Kiislamu na kudai wanaunga mkono siasa za mrengo wa kulia.

Hii si mara ya kwanza, Bi Amin alisema, kwamba wanawake wa Kiislamu wamelengwa kwa njia hiyo. Mei 13, wakati Waislamu walikuwa wakiadhimisha sherehe za Eid, chaneli moja ya YouTube ilionesha mnada wa "Eid Special" - "mnada" wa moja kwa moja wa wanawake wa Kiislamu kutoka India na Pakistan.

"watu walikuwa wakiweka dau la rupee tano na rupee 10, walikuwa wakiwaorodhesha wanawake kulingana na sehemu zao za mwili wakitumia vitendo vya kingono na kutishia kuwabaka," Bi Khan alisema.

Anaamini wale waliojaribu kumnadi kwenye Twitter ndio waliohusika na app ya Sulli Deals na chaneli y a YouTubel -ambayo imefutwa na mtandao huo.

Katika wiki kadhaa zilizopita, Twitter iliziwekea marufuku ya muda akaunti zilizodai kuhusika na app hiyo na huenda ikarudishwa tena hivi karibuni.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema unyanyasaji wa mtandaoni unaweza "kudhalilisha, kutisha na mwishowe kuwanyamazisha wanawake".

Wiki iliyopita, zaidi ya waigizaji mashuhuri 200, wasanii, wanahabari na maafisa wa serikali kutoka maeno mbali mbali duniani waliwaandikia barua ya wazi maafisa wa kuu watendaji wa Facebook, Google, TikTok na Twitter kupatia ''kipaumbele'' usalama wa wanawake.

"Intaneti ni mji wa karne ya 21. Ni mahali ambapo mijadala inafanyika, jamii zinajengwa, bidhaa zinauzwa na sifa kutengezwa. Lakini kiwango cha unyanyasaji mitandaoni kwa wanawake wengi kinashiria, ulimwengu wa kidijitali sio salama. Hali hii ni tishio kwa upatikanaji wa usawa wa kijinsia."

Ripoti ya Amnesty International kuhusu unyanyasaji mitandaoni mwaka jana ilionesha kuwa wanawake walio na ushawishi mkubwa wanashambuliwa zaidi.

Bi Amin anasema wanyanyasaji hawakuwa na "hofu kwa sababu wanajua hawatapatikana.''

Aliangazia visa kadhaa vya hivi karibuni vya udhalimu dhidi ya Waislamu vinavyoendekezwa na wafuasi wa chama tawala cha BJP, ama cha waziri wa serikali kuwapongeza wanaume wa Kihindu wanane walioshtakiwa kwa kumshambulia Muislamu.

Kwa wanawake ambao utambulisho wao ulichukuliwa na kutumiwa na app ya "Sulli Deals", mapambano ya kupigania haki huenda yakawa magumu. Lakini wamejitolea kupigania haki.

"Polisi wakifanikiwa kuwanasa wale waliotuuza mtandaoni,Nitaenda mahakamani," Bi Khan alisema. "Nitafuatilia suala hili hadi mwisho."