Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uganda-Tanzania:Jinsi Idi Amin alivyotoroka Uganda baada ya mji mkuu Kampala kutekwa na majeshi ya Tanzania
Vita vya Uganda-Tanzania, vinavyojulikana nchini Tanzania kama Vita vya Kagera na nchini Uganda kama vita vya Ukombozi vilihusisha Uganda na Tanzania kati ya Oktoba 1978 hadi Juni 1979. Matokeo yake yalikuwa kutimuliwa kwa Idi Amin madarakani na mwezi kama huu wa Juni 1979 ambapo vita viliisha tunakupakulia kumbukumbu za chanzo na matokeo ya vita hivyo . Leo katika sehemu ya nne na ya mwisho ya makala zetu tunaangazia jinsi Amin alivyotoroka kutoka Uganda baada ya majeshi ya Tanzania kuuteka mji wa Kampala .
Wanajeshi wa Tanzania walipoingia Uganda na vita kupamba moto, Idi Amin aliahidi kuwafurusha ama kufariki akiwa mstari wa mbele
Lakini kusema ni rahisi kuliko kutenda. Wakati jeshi la Tanzania likianza mashambulizi ya kuuteka mji wa Entebbe Amin alikuwa Ikulu.
Hakuilinda mpaka mwisho Ikulu yake, badala yake makombora yalipotua kwenye viwanja vya Ikulu alipanda helikopta ya jeshi na kutimkia Kampala.
Kampala nayo iliangukia mikononi mwa jeshi la Tanzania na washirika wake. Idi Amin alikimbia tena.
Safari hii alitumia mwanya aliopewa Muammar Gaddafi na Mwalimu Julius Nyerere.
Mwalimu hakutaka kuwashambulia askari wa Libya baada ya wengi wao kuuawa Entebbe.
Kufuatia kushindwa vibaya katika vita vya Lukaya, sehemu ya vikosi vya Jeshi la Uganda viliripotiwa kumhimiza Amin aondoke madarakani .
Alikataa kwa hasira, na akasema: "Ikiwa hamtaki kupigana, nitafanya mwenyewe." Kwa hivyo alimfuta kazi mkuu wa jeshi Yusuf Gowon.
Walakini, Amin alilazimika kukimbia mji mkuu wa Uganda kwa helikopta mnamo 11 Aprili 1979, wakati Kampala ilipotekwa. Baada ya jaribio la muda mfupi la kukusanya wanajeshi waliobaki wa Uganda mashariki mwa Uganda ambapo inasemekana Amin alitangaza jiji la Jinja kuwa mji mkuu mpya wa nchi yake, alikimbilia uhamishoni.
Amin alitoroka kwa mara ya kwanza kwenda Libya, ambako alikaa hadi 1980, na mwishowe alikwenda Saudi Arabia, ambapo familia ya kifalme ya Saudi ilimruhusu kuishi na kumlipa ruzuku kubwa ili kumzuia asijiunge na siasa.
Amin aliishi kwa miaka kadhaa kwenye ghorofa mbili za juu za Hoteli ya Novotel kwenye Barabara ya Palestina huko Jeddah. Brian Barron, ambaye aliripotia BBC wakati wa Vita vya Uganda na Tanzania kwa kama mwandishi mkuu wa Afrika, pamoja na mpiga picha Mohamed Amin (hakuna uhusiano) wa Visnews jijini Nairobi, walifaulu kumpata Amin mnamo 1980, na kuwapa mahojiano ya kwanza naye tangu aondolewe madarakani .
Akiwa uhamishoni, Amin alifadhili mabaki ya jeshi lake ambalo lilipigana katika vita vya kichakani nchini Uganda.
Ingawa aliendelea kuwa mtu wa kutatanisha, baadhi ya wafuasi wake wa zamani na vile vile vikundi kadhaa vya waasi waliendelea kupigana kwa jina lake kwa miongo kadhaa na mara kwa mara walitetea apewe msamaha na hata kurudishwa kwake kwa Urais wa Uganda.
Wakati wa mahojiano aliyotoa akiwa uhamishoni huko Saudi Arabia, Amin alishikilia kuwa Uganda inamuhitaji, na kamwe hakuonyesha kujuta kwa hali ya kikatili ya utawala wake.
Amin ajaribu kurejea Uganda kupitia Zaire
Mnamo 1989, Amin aliondoka uhamishoni bila idhini ya serikali ya Saudi Arabia, na akasafiri kwa ndege pamoja na mmoja wa wanawe kwenda Zaire. Huko, alikusudia kukusanya jeshi la waasi kuiteka tena Uganda ambayo ilikuwa imezongwa na vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe wakati huo.
Watu wengine wa familia yake walibaki Jeddah. Licha ya kutumia pasipoti ya uwongo ya Zaire, Amin alitambuliwa kwa urahisi alipofika na Air Zaïre katika Uwanja wa ndege wa N'djili, na kukamatwa mara moja na vikosi vya usalama vya Zaire.
Serikali ya Zairea ilichukulia vibaya kuwasili kwa Amin, na kujaribu kumfukuza nchini humo. Mwanzoni, Saudi Arabia ilikataa kumruhusu arudi, kwani serikali yake ilikerwa sana kwamba "alitumia vibaya ukarimu wao" kwa kuondoka bila ruhusa.
Serikali ya Zairea haikutaka kumrudisha Amin nchini Uganda ambapo rais huyo wa zamani alikabiliwa na mashtaka ya mauaji wala kumweka Zaire, na hivyo kudhoofisha uhusiano wa nchi hiyo kimataifa.Baadaye, Amin hapo awali alifukuzwa kwenda Senegal ambapo alipaswa kupelekwa Saudi Arabia, lakini serikali ya Senegal ilimrudisha Zaire wakati Saudi Arabia ilipomnyima Amin visa
Kufuatia kuingilia kati kwa Mfalme wa Morocco, Hassan II, mwishowe uongozi wa Saudi Arabia ulimruhusu Amin arudi. Kwa kurudi, Amin alilazimika kuahidi kutoshiriki tena katika shughuli zozote za kisiasa au za kijeshi au kutoa mahojiano.
Kwa hivyo alitumia muda wake uliosalia kwa njia ya utulivu huko Saudi Arabia.
Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, Amin aliripotiwa kula lishe ya matunda. Chakula chake cha kila siku kilisheheni machungwa mengi hatua iliyomfanya kupewa jina la utani "Dk Jaffa" miongoni mwa raia wa Saudi Arabia
Kuugua na kifo
Mnamo Julai 19, 2003, mke wa nne wa Amin, Nalongo Madina, aliripoti kwamba alikuwa katika hali ya kukosa fahamu na alikaribia kufa katika Hospitali ya wataalam ya King Faisal na Kituo cha Utafiti huko Jeddah, Saudi Arabia, kutokana na kufeli kwa figo. Alimsihi rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amruhusu arudi Uganda kwa kipindi kilichosalia cha maisha yake.
Museveni alijibu kwamba Amin lazima "ajibu dhambi zake wakati atakaporejeshwa". Familia ya Amin mwishowe iliamua kuzima mashine zilizokuwa zikimsaidia kupumua na Amin alifariki katika hospitali ya Jeddah mnamo tarehe 16 Agosti 2003. Alizikwa katika Makaburi ya Ruwais huko Jeddah katika kaburi la kawaida bila shughuli kuba zinazoambatana na hafla kama za marais wa zamani .
Baada ya kifo cha Amin, David Owen alifichua kwamba wakati wa kipindi chake kama waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza (1977 hadi 1979), alikuwa amependekeza Amin auawe. Alitetea mpango wake huo akisema: "Sioni aibu nilizingatia chaguo hilo, kwa sababu utawala wake upo katika kiwango cha Pol Pot kama moja ya serikali mbaya zaidi za Kiafrika