Oli London: Atumia dola 200,000 kufanya upasuaji mara 18 afanane na Jimin, msanii maarufu wa Korea

Muimbaji Oli London ametumia miaka na miaka na gharama kubwa ya maelfu ya dola akijaribu kujibadilisha muonekano afanane na msanii anayempenda sana.

Jamaa huyu raia wa Uingereza mwenye miaka 31, anataka kufanana na mwimbaji maarufu wa bendi ya BTS ya Korea Kusini, Park Ji-min almaarufu kama Jimin.

Ili kufikia lengo hilo, ameshafanya upasuaji mara 18 hasa wa sura yake, ili aonekane sawa na msanii huyo anayemzimia kupita kiasi.

Aliwahi kujitokeza kwenye kipindi kimoja cha Televisheni kilichomjumuisha Dokta Phil, kuzungumzia upasuaji wake ili afanane na nyota huyo wa BTS, Jimin.

Hata hivyo uamuzi huo wa kufanya upasuaji kubadili muonekano wake, umeleta maneno mitandaoni na kuanza kushambuliwa.

"Kwangu sijali najisikia vyema sasa kuwa mkorea, baada ya miaka mingi ya kuwa kwenye mwili tofauti na utamaduni tofauti," aliandika Oli katika mtandao wake tweeter wiki iliyopita.

Hata hivyo Oli ambaye ana ushawishi mkubwa kwenye mtandao wa Instagram amejibu mapigo ya kushambuliwa kwa kuleta ubaguzi wa taifa.

"Mimi ni Mkorea, watu wakubali ama wasikubali, hivyo ndivyo natambulika sasa, hili linanifanya kuwa na furaha. Hivyo ndivyo nilivyo, ndio vinasaba vyangu", alisema Oli.

Kubadilisha sura na kufanana sana na watu wa Korea

Oli mwenye wafuasi 245,000 kwenye mtandao wake wa Instagram, alianza kufanya upasuaji mwaka 2019, alipokuwa nchini Korea.

Alikutana na Oli na kufanya nae kazi kwa muda kadhaa, ndipo mahaba dhidi yake yalipoanza na kuamua kufanya upasuaji afanane na msanii huyo.

Mpaka kufikia mwaka 2019 Oli alikuwa ameshatumia zaidi ya dola 200,000 kwa ajili ya kurekebisha pua yake, kupandikizwa kidevu na kurekebisha nyusi na kuweka sura, kidevu na nyusi za kufanana na Jimin.

Toka mwaka 2019, anachoma sindano za kurekebisha ngozi yake ili iwe sawa na ngozi za wakorea, na anatumia dola zaidi ya dola 6,000 kwa sindano moja.

"Jimin ni mtu ninayevutiwa naye sana. Nimetumia pesa nyingi kufanya upasuaji ili nifanane nae na kwa hakika sasa kama ni mweza wangu."

Matusi na lawama

Kwa sasa Oli anakumbaa na shutuma nyingi kupitia mitandao akionekana ni mbaguzi kwa ama kupuuza nchi yake au utaifa wake.

"Mkorea ni utaifa sio suala la jinsia, huwezi kujitambulisha kama mkorea kisa tu unampenda mkorea, huko ni kudhalilisha utaifa wako, aliandika kwa hasira mmoja wa watu wanaompinga Oli na uamuzi wake wa ujibadilisha muonekano.

Mwenyewe anasema hajali kutukanwa ama kupewa maneno makali, anachoangalia sasa ni furaha yake tu. Na furaha hiyo ni kufanana na Msanii Jimin.

Maisha yake ya sanaa

Oli aliyeanza kupata umaarufu kama mshawishi tu wa mtandaoni kwa kuchapisha video zenye mahadhi na jumbe tata, baadae akajiingiza kwenye muziki February 2019. Aliachia wimbo wake unaoitwa Perfection, ambao ulitizamwa na watu milioni 1.9 ambao wengine waliuponda, wengine waliusifia. Baadaye akatoa nyibo zingine kama Butterfly, Heart of Korea na Mirror Mirror , ambazo zote pamoja na Perfection zilipata watazamaji milioni 6. Ingawa umaarufu wake hautokani zaidi na nyimbo zake, ila ameendelea kujijenga midomoni mwa watu kwa uamuzi wake wa kubadilisha muonekano kutoka mzungu mpaka kuwa mkorea, ili afanane na mtu ampendaye zaidi duniani.