Billionea Mackenzie Scott agawa dola zingine bilioni 2.7 kwa wanaohitaji misaada

Mackenzie Scott

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mackenzie Scott ni mmoja wa wanawake tajiri zaidi duniani

Billionea MacKenzie Scott, mke wa zamani wa mwanzilishi wa Amazon, bilionea Jeff Bezos, amechangia tena dola bilioni 2.7 kwenye mashirika mbalimbali yanayosaidia jamii.Bi. Scott alisema kupitia mtandao kwamba anataka kutoa sehemu kubwa ya fedha zake kwa watu ambao kihistoria wamekuwa hawapati misaada ya kifedha na wamekuwa wakitelekezwa.

Kwenye kutekeleza nia yake hiyo, Scott ameandika kwenye mtandao kwamba ameamua kuchagua mashirika 286 yanayoshughulikia masuala ya ubaguzi wa rangi, sanaa na elimu. Bi. Scott ni mmoja kati ya matajiri wakubwa wanake duniani.

Mali zake nyingi amezipata kutokana na talaka aliyopewa mwaka 2019 na Bezos, ambaye anaongozas kwa utajiri duniani. Mbali na mpango huo, Bi Scott alipatiwa asilimia nne za hisa za Amazon, hakiwa amemsaidia mumewe huyo wa zamani Bezos kuanzisha kampuni hiyo kubwa ya teknolojia ya Amazon mwaka 1994.

Tangu apewe talaka, mwanamama huyo amekuwa akiandika sana kuhusu hatua yake ya kusaidia jamii, kwa mfano mwezi desemba mwaka jana, alieleza kuchangia zaidi ya dola billioni 4 kwa kipindi cha miezi minne tu kwa mashirika yanayoopngozwa na wanawake, hifadhi za chakula na vyuo vya wanafunzi weusi wenye asili ya afrika.

Licha ya kutoa kiwango hicho cha mchango, bado anashikilia nafasi ya 24 kwa utajiri duniani, akiwa na utajiri wenye thamani ya dola bilioni 59.5, kwa mujibu wa Forbes.

MacKenzie Scott na Dan Jewett.

Chanzo cha picha, Giving Pledge

Maelezo ya picha, MacKenzie Scott na mumewe mpya Dan Jewett.

Katika chapisho lake la hivi karibuni la kwenye mtandao, siku ya Jumanne, mtalaka huyo wa Jeff Bezo alisema anania ya kugawa utajiri wake na kwamba anafanya kazi na timu yenye watafiti pamoja na mumewe mpya, Dan Jewett kuchagua wanaostahili kupewa mgao huo.

" Katika jitihada hizi, tunaongozwa na imani kwamba mali hizi zisiwafikie kundi la watu wachache tu, kwa hivyo kuna watu wameandaa namna bora na inafanyiwa kazi."

Mwaka 2019, alisaini 'Giving Pledge', akihaidi kugawa sehemu kubwa ya mali zake.

Giving Pledge ni kama mpango wa ahadi ya kujitolea unahowahusisha watu matajiri zaidi duniani na familia zilizoamua kuwa sehmu kubwa ya mali zao ziende kwa jamii. Ulianzishwa mwaka 2010 na familia ya kitajiri ya Bill Gates kupitia Bill and Melinda Gates pamoja na Warren Buffett, wako matajiri wengine waliojitoa kama George Lucas.

Bezos hajajiunga na mpango huo wala kutia saini , lakini mume wa sasa wa Scott, Bwana Jewett, yeye alijiunga na mpango huo mwezi Machi, mwaka huu.