Waridi wa BBC: Everlyne, mwanamke anayehangaika na ugonjwa wa jasho kwa miaka 32

Kuanzia baba mzazi na hata kaka zake Everlyne walikuwa wanatokwa jasho jingi mwilini

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Maelezo ya picha, Kuanzia baba mzazi na hata kaka zake Everlyne walikuwa wanatokwa jasho jingi mwilini
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Kwa umbali, anaonekana kama mwanamke wa kawaida kwa umbo na urembo , ila anapokaribia unagundua kuwa ameloa jasho karibu mwili mzima kuanzia usoni, miguu na kwapa zake . Ndio hali ya maisha yake ya kila siku.

Everlyne Juma , anaishi na ugonjwa wa kutokwa jasho jingi kupita kiasi katika mwili wake ujulikanao kwa lugha ya kitaalam kama (hyperhydrosis).

Everlyne anasema kuwa ni hali aliyozaliwa nayo, na alivyokuwa anaendelea kukua, familia yake iliona hali yake kama ni jambo tu la kawaida. Kwani kuanzia baba mzazi na hata kaka zake walikuwa wanatokwa jasho jingi mwilini:

"Nilizaliwa Kaunti ya Kakamega ,Magharibi mwa Kenya, baada ya muda wazazi wangu walituhamisha hadi mtaa wa mabanda wa Kibera mjini Nairobi, nikiwa bado mdogo ...Suala la kutokwa na jasho kila dakika halikunisumbua' anasema Everlyne.

Akiwa shule ya msingi mtaa wa Kibera, aligundua kuwa kalamu yake kila wakati ilikuwa inateleza na kitabu chake kililoa kutokana na jasho lake lililoendelea kutiririka muda wote alipokuwa darasani.

Kando na haya ilikuwa changamoto kubwa kwake kuvaa viatu vya kawaida vya shule mara kadhaa alipojaribu, ilikuwa kama aliyevivaa viatu vilivyoloa maji, lakini lilikuwa ni jasho lake.

Everlyne Juma

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Maelezo ya picha, Akiwa shuleni wazazi wa Everlyne hawakuwa na uwezo wa kumnunulia viatu zaidi ya kimoja, ilibidi aishi na hali yake

Aliamua kuvalia viatu vya wazi (sandals) patipati, changamoto ya viatu vya wazi kwake ilikuwa sio kubwa mno , lakini kilichomkera ni pale jasho lilipochanganyikana na mchanga.Hilo lilimlazimisha aoshe miguu yake kila anapowasili shuleni.

Baada ya Shule ya msingi, ilibidi aingie shule ya sekondari ya bweni. Hapo ndipo mambo yalianza kubadilika, kwa sababu alilazimika kuvaa viatu vya kawaida vya sare ya shule ambavyo vilikuwa vinafunga miguu.

Wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumnunulia viatu zaidi ya jozi moja na ilibidi aishi na hali yake .

Baada ya mwezi mmoja katika shule ya sekondari tayari viatu vyake vilianza kutoa harufu mbaya.

Lakini anasema alikuwa na mbinu tosha za kuwaficha wenzake wasijue uvundo uliomo ndani ya viatu vyake.

Hatahivyo haikuchukua muda tetesi zikaanza kusambaa kuwa alikuwa anatoka jasho jingi kama maji mwilini mwake.

"Wakati mmoja nakumbuka, ni wakati tulikuwa tunajitayarisha na mazoezi katika klabu ya utumbuizaji, pale sisi sote hatukuwa tumevaa viatu, kila zamu yangu ilipowadia niliponyanyua miguu nyayo zangu zilichora unyevunyevu, baadhi ya wenzangu pale walinong'onezana huyu ana nini anamwaga maji ovyo ovyo? Maneno hayo yaliniumiza sana, yalinifanya nichukue uamuzi wa kuondoka katika klabu hiyo ya burudani , ile siku ilikuwa ya kwanza na ya mwisho niliachia pale ... "Anakumbuka Everlyne.

Baada ya hapo ndipo alipoanza kugundua kuwa haikuwa hali ya kawaida bali ilikuwa tatizo, kwa kuwa hata kuwasalimia watu kwa mikono, ilikuwa shida. Wakati mwingi mikono yake ilikuwa imeloa jasho jingi kupindukia.

Everlyne alimua kutowasalimu watu kwa mikono kutokana na kwamba mikono yake ilikuwa inatoka jasho jingi

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Maelezo ya picha, Everlyne alimua kutowasalimu watu kwa mikono kutokana na kwamba mikono yake ilikuwa inatoka jasho jingi
Jasho

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Matukio kama haya yalimfanya kuamua kuacha kumsalimia mtu yeyote kwa kumpa mkono.

"Nilielewa fika jinsi mila na desturi za waafrika zilivyo kuhusu umuhimu wa kumsalimia mtu kwa kumpa mkono, ilikuwa changamoto kubwa sana kwangu. Wengi walinioana kama binti asiye na nidhamu, wengi walinitazama tu kwa kunikejeli "Anasema Everlyne

''Je, unadhani kuishi na hali ya kutoa jasho kila wakati ni rahisi?'', Everlyne alijiuliza na kuongeza kuwa "Kila kukicha huwa ninapanga jinsi nitakabiliana na hali hiyo pindi jasho likianza kutoka... hakuna saa maalum ambayo ninaweza kusema jasho litatoka . Jasho linaweza kutoka asubuhi usiku au mchana na wakati mwingine hata mchana kutwa", Everlyne anasema.

Kuishi na hali hii daima

Hali ya wasi wasi na uoga alioyoishi nayo katika wakati akiwa shule ya msingi alienda nayo hadi alipojiunga na taasisi ya mafunzo ya mawasiliano , ila akiwa pale alihisi kana kwamba changamoto zingekuwepo wakati wa kuajiriwa, kulingana na mwanamke huyu kutamani kuwa mwanahabari ila kutokana na hali yake ya jasho alihisi kukata tamaa na hatimaye kuachana na ndoto hiyo.

Mahangaiko ya kupata ajira yalikuwepo, ila wakati mmoja aliamua kufanya kazi ya kuajiriwa kama mhudumu wa mapokezi. Kama ilivyo kawaida na urembo aliokuwa nao, alikutana na wanaume waliomuhitaji kuwa nao kwenye mahusiano. Ila wale wanaume walipomkaribia na kugundua hali yake walionekana kukata tamaa na wengine kumkimbia.

Lakini kama waswahili wasemavyo Mungu si Athuman, hatimaye alipata mume aliyempenda. Alikua ni mtu walifahamiana naye mtaani na hatimaye waliamua kufunga pingu za maisha.

"Baba wa watoto wangu wawili na ambaye ni mume wangu hakuonekana kushtushwa na jasho langu yeye alisimama nami wakati wote wa uchumba wetu na hadi sasa miaka mingi baadaye ndoa yetu ingali imara'' anasema Everlyne.

Everlyne anasema kuwa amepata ujasiri wa kuzungumzia hali yake bila ya uoga

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Maelezo ya picha, Everlyne anasema kuwa amepata ujasiri wa kuzungumzia hali yake bila ya uoga

Everlyne anasema kuwa amepata ujasiri wa kuzungumzia hali yake hii aliyoishi nayo kwa miaka 32 bila uoga na anajikubali alivyo, Ila hofu yake kuu imekuwa kwa bintiye mmoja ambaye pia tayari ameanza kuonyesha dalili za kuwa na tatizo hilo.

''Ninapomtazama binti wangu ninaona haja ya kujitokeza kwa umma kuzungumzia ugonjwa huu wa kutoa jasho jingi kila wakati , kwani nimepita changamoto nyingi hadi nilipo hivi sasa . Ni katika harakati hizi mimi na baadhi ya Wakenya wanaoishi na hali hii tuliunda muungano wetu ambao ungetupa fursa ya kusaidiana na pia kupeana nguvu .'', anasema Everlyne .

Na je wataalam wa ngozi wanasema nini kuhusu hali hii

Jasho la kupindukia linalohusiana na hyperhidrosis kawaida hutokea mikono, miguu, kwapani, na sehemu zilizonenepa zaidi za mwili kwa sababu ya viwango vyake vya tezi za jasho.

Hyperhidrosis inaweza kuwepo tangu kuzaliwa au inaweza kujitokeza baadaye maishani. Ila, mara nyingi hali ya mtu kutokwa na jasho kupita kiasi huwa inaanza wakati mtu anapofikia umri wa ujana.

Hali hiyo inaweza kuwa kwa sababu ya hali ya kiafya, au haina sababu dhahiri, wataalam pia wanaihusisha na mtu kurithi kutoka wa ukoo wake.

Dalili

  • Kutokwa na jasho jingi linalotiririka mikononi
  • Kutokwa na jasho jingi kwenye nyayo za miguu
  • Kutoka jasho jingi na la mara kwa mara mwilini
  • Kutokwa na Jasho jingi linaloweza kulowesha mavazi na kuonekana wazi
Everlyne alimua kutowasalimu watu kwa mikono kutokana na kwamba mikono yake ilikuwa inatoka jasho jingi

Chanzo cha picha, Everlyne Juma

Maelezo ya picha, Uchunguzi unaonesha kuwa jeni fulani zinahusika katika hali ya hyperhidrosis aliyonayo Everlyne

Watu walikuwa wakidhani kwamba hyperhidrosis ya msingi ilikuwa imeunganishwa na hali ya akili na joto la mgonjwa, kwamba hali hiyo ilikuwa ya kisaikolojia na iliathiri tu watu wenye msongo, wasiwasi, au woga.

Lakini , utafiti wa hivi karibuni umeonesha kuwa watu walio na hyperhidrosis hawana tena hisia za wasiwasi, woga, au mafadhaiko kuliko watu wengine wanapopatikana na vichocheo vivyo hivyo.

Uchunguzi pia umeonesha kuwa vinasaba fulani mwilini vinahusika katika kuchangia hali hiyo, na kuifanya iweze kuonekana kuwa inaweza kurithiwa. Wengi wa wagonjwa walio na hyperhidrosis ya msingi wana ndugu au mzazi aliye na hali hiyo, ama aliyewahi kuwa na hali hiyo.

Tiba asilia

Mabadiliko kadhaa katika shughuli za kila siku na mtindo wa maisha yanaweza kusaidia kuboresha dalili, ukifanya haya kunaweza kusaidia hilo:

  • Vitambaa - Vitambaa maalumu au hata Pedi zikivaliwa kwenye makwapa vinaweza kunyonya jasho na kulinda nguo kulowa.
  • Mavazi - Vaa mavazi yenye nyuzi fulani za sintetiki, kama nylon, yanaweza kudhoofisha dalili. Mavazi huru ni bora.
  • Viatu - Vipo viatu vyenye sintetiki vina uwezekano wa kuzidisha dalili. Viatu vya asili, kama vya ngozi, vinapendekezwa.
  • Soksi - Vaa Soksi ambazo ni bora na husaidia kufyonza unyevunyevu, hasa soksi nene na laini zilizotengenezwa na nyuzi za asili.

Ikiwa hatua hizi hazina ufanisi na hazijakusaidia, yapo matibabu ya tatizo hili yanayoweza kukusaidia.

Matibabu

Waone madaktari au wataalam wa ngozi, hawa wanaweza kushauri na kupendekeza zaidi kuhusu matibabu yanayofaa kwa tatizo hili, kulingana na hali ya mgonjwa.