Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku 100 za Rais Samia Suluhu: Fahamu changamoto za Rais Samia katika kufanya mabadiliko ya kijinsia
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Hata kama namba na takwimu hazitazungumza kwa kushawishi kuhusu nini hasa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania umekifanya kwa wanawake walau katika siku zake 100 za kwanza, jambo kubwa kuliko yote ambalo amefanikiwa na lina athari chanya kwenye jamii ni moja - kuwa Rais mwanamke wa kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.
Kwa bahati mbaya, hili ni jambo ambalo halipimiki kwa namba. Katika mojawapo ya mahojiano ya kusisimua yaliyofanywa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakati wa ziara ya Rais Samia nchini Kenya, mmoja wa wanawake wa Mombasa alisema hivi wakat huo;
" Sisi wanawake tumefurahi kwa sababu tu ya kuona kwamba mmoja wetu - mwenzetu, amefanikiwa kushika wadhifa wa juu kabisa wa uongozi katika nchi. Hilo peke yake linatosha kutupa matumaini makubwa sisi na watoto wetu kuhusu hatua ambazo mwanamke anaweza kupiga.
" Na kwa wanawake wa pwani ya Kenya ambao wanajulikana kwa kuvaa hijabu kama Rais Samia, jambo hilo lina maana ya ziada kwetu. Kwa muda mrefu jamii ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, haikuwa ikiwaangalia kwa heshima wanawake wanaovaa hijabu kichwani. Urais wa Samia utatuheshimisha," alizungumza mwanamke yule.
Nakumbuka siku moja, mimi binafsi nikiwa na mke wangu nyumbani, nilijaribu kukosoa mojawapo ya hotuba alizotoa Rais Samia. Haikuchukua hata dakika moja nikaambiwa; " Ndiyo tatizo la wanaume, yaani kwa sababu Rais ni mwanamke, mnatafuta hata tatizo dogo tu ili mkosoe".
Hicho ndicho urais wa Samia aliyeingia madarakani Machi 17 mwaka huu kufuatia kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, John Magufuli, ulichokifanya kwa wanawake wa Tanzania. Umewapa nguvu na ari ya kuweza kuvunja vikwazo vyote vilivyowekwa na mfumo dume katika jamii ya Watanzania.
Swali pekee ambalo watu wengi watakuwa wanajiuliza kufikia sasa ni moja; je, urais wa Samia ni mwanzo wa zama mpya za maendeleo ya wanawake katika Tanzania na eneo zima la Afrika Mashariki? Mahali pazuri pa kuanzia ni kwa kutazama nini hasa kimetokea katika siku zake 100 za kwanza madarakani.
Wanawake katika nafasi za juu za uongozi
Katika duru za kisiasa za Tanzania, kuna minong'ono kwamba Rais Samia amepanga kuwateua wanawake wengi zaidi katika nafasi za juu za uongozi ambazo hazijawahi kushikiliwa na watu wa jinsia hiyo tangu taifa hilo lipate Uhuru.
Tayari amefanya uteuzi wa Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi, kushika wadhifa huo akiwa mwanamke wa kwanza. Kwa wafuatiliaji wa siasa za Bunge, Nenelwa alistahili kupewa wadhifa huo kabla hata Samia hajawa rais lakini pengine jinsia yake au kutojihusisha kwake na makundi ya kisiasa ndani ya chama ilikuwa kikwazo kwake.
Katika mkutano alioufanya na wawakilishi wa wanawake nchini Tanzania mnamo Juni 8, mwaka huu mjini Dodoma, Samia alisema kwamba katika utawala amedhamiria kuongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya juu vya maamuzi ili washiriki katika michakato ya haki na maendeleo.
Akitoa mifano, alisema kwamba katika orodha ya Makatibu Tawala Mikoa 26 aliyowateua tangu aingie madarakani, ameweza kuwapa wanawake 12 nafasi ambayo ni sawa na asilimia 46 ya wateule wote.
Pia alisema kwamba katika Majaji 28 wa Mahakama Kuu aliyowateua, majaji 13 - sawa na asilimia 43 walikuwa ni wanawake. Kwa sababu hiyo, katika majaji wote 86 wa Mahakama Kuu, wanawake sasa wamefika 40.
Eneo pekee ambalo alisema lina changamoto kubwa ni kwenye ajira rasmi ambako alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017, katika ajira rasmi milioni tatu (3,014,106), wanawake waliopata nafasi ni milioni moja (1,107,900) tu sawa na asilimia 36.7.
Samia alisema takwimu zinaonyesha Tanzania ina wanawake wengi zaidi kuliko wanaume na hilo lingetakiwa kuakisiwa katika takwimu muhimu za kimaendeleo kama ajira lakini wengi wa wanawake wamejiajiajiri katika sekta binafsi na isiyo rasmi ambako vipato vyake si vya uhakika.
Changamoto ya Samia katika kufanya mabadiliko
Urais wa Samia Suluhu Hassan haukuwa umepangwa na ulitokea kwa sababu ya bahati mbaya iliyomkuta Magufuli. Kwa sababu hiyo, katika siku yake ya kwanza tu madarakani alikuwa na changamoto ya kwanza ya kujizatiti madarakani.
Katika nchi ambayo Rais kikatiba ndiye Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, jambo hilo si dogo. Zaidi ya majukumu hayo, Rais wa Tanzania - kwa utamaduni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachotoka Samia, ndiye pia hutakiwa kuwa Mwenyekiti wa chama.
Kwa sababu hiyo, hata kabla ya kufikiria namna ya kuwawezesha na kuwanyanyua wanawake, Samia kwanza amejikuta katika jukumu la kujenga msingi wa urais wake ndani ya CCM, Serikali na kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Karibu katika teuzi zake zote kubwa alizofanya kuanzia kwenye mawaziri hadi kwenye taasisi za umma, Samia ameonekana kuzingatia makundi tofauti ndani ya chama chake, serikalini na pia kuzingatia nafasi ya Zanzibar ndani ya Muungano.
Baada ya kuwa amemaliza mchakato huo wa kujikita katika urais, inatarajiwa kwamba pengine Samia ndiyo atakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa nafasi zaidi kwa wanawake na kufungua zama mpya kwao. Lakini kwa sasa, kazi kubwa mkononi mwake ni kukamata madaraka.
Wanasiasa, wenye ushawishi na wanaharakati wanamuonaje?
Katika siku zake 100 za urais, Samia amekuwa - kwa wastani, akipata maoni mazuri kutoka kwa wanasiasa wenzake, wanaharakati na taasisi zinazojihusisha na masuala ya wanawake kwa ujumla.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira, amemweleza Samia kama aina ya kiongozi ambaye wanawake wote wanamtazama kama alama ya kuwaonyesha wapi wanaweza kwenda kama watatimiza wajibu wao ipasavyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Tanzania Legal Services Facilities (LSF), Lulu Ng'wanakilala, alisema urais wa Samia umefungua fursa nyingi kwa wanawake kuweza kuona hatua kubwa wanayoweza kupiga kwenye maisha yao.
Katika mitandao ya kijamii hususani twitter ambao umekuwa kipenzi cha wasomi na watu wa daraja la kati, Samia amekuwa akipongezwa na kukosolewa kwa kila linaloonekana zuri au baya kwa jicho la wachambuzi.
Kulinganisha na utawala wa mtangulizi hususani katika siku za mwisho za utawala wake, Rais Samia ana ahueni kutoka kwa wanaharakati kama Fatuma Karume, ambao hawaoni taabu kumpongeza na kumkosoa kila inapobidi.
Zama mpya
Rais Samia ni mwanasiasa anayefahamu vizuri nini hasa jamii ya Tanzania inakitarajia kwa kiongozi mwanamke. Takribani miaka 11 iliyopita wakati alipoamua kwa mara ya kwanza kuwania ubunge kwao, Makunduchi, Zanzibar, alitakiwa kubadili kuanzia aina ya mavazi aliyokuwa akipenda kuvaa na mwonekano wake ili aweze kukubalika na kupigiwa kura.
Mafanikio yake kisiasa kufika alipo sasa - katika nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa nchi, yametokana zaidi na uwezo wake wa kucheza karata za kisiasa na kufahamu lipi ni jambo sahihi kufanywa na katika wakati sahihi.
Pasi na kufanya mambo makubwa, urais wa Samia tayari umeiingiza Tanzania katika zama mpya hata bila ya kusemwa chochote. Mawazo yake, hisia zake, utambuzi wake wa changamoto na namna yake ya kufikia suluhisho la matatizo haitafanana na marais wanaume waliomtangulia ingawa urais ni taasisi na si mtu mmoja.
Makubwa zaidi katika uwezeshaji wa wanawake yanatarajiwa kufanywa na Samia pale atakapoona kwamba amejikita ipasavyo madarakani na amefanya mambo yatakayompa uhalali wa kutekeleza yaliyo moyoni mwake.