Kutunguliwa kwa ndege isiyo na rubani yakoleza utamu wa mchezo wa Chile dhidi ya Argentina

Drone

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukizungumzia uhamasa kwenye soka, uhasama ulipo kati ya Chile na Argentina ni uhasama wa hali ya juu kabisa.

Kutokana na uhasama huo, haikushangaza kuona timu ya taifa ya Chile, ikidai inachunguzwa na mahasimu wao Argentina baada ya kuona ndege ndogo isiyokuwa na rubani (drone), ikirandaranda juu wakati kikosi cha timu hiyo ya taifa kikiwa mazoezini, kujiandaa na mchezo wa kufuzu kombe la dunia, unaopigwa Alhamis hii.

Chile ikaamua kutuma ndege ndogo kama hiyo kuiangusha ndege inayodaiwa kuja kuwapeleleza.

Chile's coach Martin Lasarte gestures during the friendly football match against Bolivia at the El Teniente stadium in Rancagua, Chile, on March 26, 2021.

Chanzo cha picha, AFP

Hata hivyo, ndege hiyo baadaye ilibainika kuwa haikuwa ya mahasimu wao Argentina bali ni ya Kampuni moja ya nishati ya nchi hiyo ya Chile.

line

Tukio hilo limetokea ikiwa siku chache kabla ya mahasimu hao kukutana alhamis hii katika mchezo wa kufuzu kombe la dunia.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Chile, waliiona ndege hiyo ndogo wakati timu hiyo ikifanya mazoezi katika uwanja wa Juan Pinto Durán, uliopo katika makao makuu ya nchi hiyo, huko Santiago..

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeripoti kwamba, Kocha wa Chile, Martín Lasarte, ndiye aliyeamua kutumwa kwa ndege ingine isiyokuwa na rubani iliyo chini ya timu hiyo ili kuchunguza kuhusu ndege iliyokuwa inarandaranda kwenye mazoezi ya timu hiyo na iliyodhaniwa kuwa ni ya mahasimu wao Argentina.

Ndege hizo mbili baadae ziligongana, katika kile ambacho chama cha Soka nchini Chile kinaeleza ilikuwa ni tukio la bahati mbaya, huku waandishi walioshuhudia tukio hilo wakieleza kwamba lilikuwa tukio la kudhamiria.

Hata hivyo badala ya kuiangusha ndege ya mahasimu wao, ikaiangusha ndege ya kampuni ya nishati ya, Enel, ambayo kwa mujibu wa kampuni hiyo, ndege hiyo ilitumwa kuangalia taa za barabarani.

Mmoja wa waandishi wa habari, Cristian Alvarado aliweka kipande cha video kwenye mtandao wake, kuonyesha tukio zima.

Taarifa zakutumia kwa ndege hizo zisizokuwa na rubani kutumika kuchunguza mbinu za wapinzania zimewahi kulalamikiwa huko nyuma na makocha mbalimbali. Mwaka 2014, kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps aliliomba Shirikisho la soka duniani (FIFA) kufanya uchunguzi baada ya kuonekana kwa ndege isiyokuwa na rubani ikirandaranda kwenye kambi ya timu hiyo ya taifa nchini Brazil, ikijiandaa na mchezi wa ufunguzi wa kombe la dunia dhidi ya Honduras.

Mwaka 2017, Honduras iliituhumu Australia kutumia ndege isiyokuwa na rubani kuichunguza timu hiyo, ikijiandaa na michezo ya kufuzu kombe la dunia. Timu hiyo iliweka kwenye mtandao wa twitter video kuonyesha tukipo hilo.

1px transparent line

Zipo taarifa za ndege kama hizo kuchunguza pia vilabu vikubwa. Mwaka 2018 timu ya Werder Bremen ya Ujerumani ilikiri kutuma ndege kwenye kambi ya mazoezi ya Hoffenheim na kuomba radhi kwa tukio hilo.

Wakati tuhuma hizo za matumizi ya ndege ndogo zisizokuwa rubani kuchunguza na kupeleleza timu pinzani zikishamiri na kuonekana za kawaida, baadhi ya makocha wamekuwa wakiendelea kutumia nja za zamani kuchunguza wapinzani wao.

Mwaka 2019, Leeds United iliomba radhi baada ya kocha wake, Marcelo Bielsa, kukiri kwamba alituma baadhi ya maafisa kwenye benchi lake la ufundi kwenda kuchunguza mazoezi ya timu pinzani ya Derby Country.