Covid 19: Mbwa wa kunusa kuimarisha uchunguzi katika viwanja vya ndege

Mbwa wa kunusa kuimarisha uchunguzi katika viwanja vya ndege

Chanzo cha picha, JOHN AKEHURST

Maelezo ya picha, Mbwa wa kunusa kuimarisha uchunguzi katika viwanja vya ndege

Mbwa wa kunusa wanaweza kuchangia katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa corona katika jamii wakati ambao shughuli zinaanza kurejea katika hali ya kawaida, kulingana na wanasayansi.

Kama sehemu ya majaribio, mbwa wamepewa mafunzo kutambua harufu ya watu waliopata maambukizi ya virusi vya corona ambayo haiwezi kubainika kupitia pua ya mwanadamu.

Na hatua hii huenda ikawa na umuhimu mkubwa katika maeneo ya viwanja vya ndege au matukio ya watu wengi.

Lakini matokeo ya mbwa yatathibitishwa kwa vipimo vya maabara, watafiti wamesema.

Ingawa mbwa hao walifanilikiwa kubaini asilimia 88 ya maambukizi ya virusi vya corona, pia ilibaini asilimia 14 ya watu kimakosa ambao hawakuwa na virusi vya corona.

Mbwa wanaweza kuwa na uwezo wa hadi mara 100,000 wa kunusa zaidi ya mwanadamu na kipindi kirefu wamekuwa wakitumiwa kwa shughuli za kunusa kubaini dawa za kulevya na vilipuzi.

Utafiti wa hivi karibuni umeonesha kuwa mbwa - wanaweza kubaini harufu za kipekee za magonjwa ikiwemo saratani, ugonjwa wa kutetemeka wa Parkinson na malaria.

Kama sehemu ya majaribio ya sasa hivi, mbwa sita walipewa mafunzo kubaini harufu ya mwanadamu waliopata maambukizi ya virusi vya corona kwa kutumia soksi, barakoa na fulana za vitambaa mbali.

Baadhi ya watu ambao hawakuwa na virusi walibainika kuwa na homa ana kuhakikisha kwamba mbwa hao wamefanikiwa kubaini tofauti iliyopo kati ya ugonjwa wa Covid-19 na maambukizi mengine ya kupumua.

Mbwa hao walifanikiwa kunusa na kubaini magonjwa hata kama yalikuwa ni maambukizi mengine wakati mtu hakuwa na dalili au kiwango cha chini cha virusi katika mifumo yao ya mwili.

Dkt. Claire afisa mkuu wa Sayansi katika kituo cha mbwa wa kunusa kinachotoa mafunzo kwa walimu, alisema matokeo yalikuwa ushahidi zaidi kwamba mbwa wanaweza kutegemewa zaidi katika kubaini harufu ya magonjwa katika mwili wa mwanadamu.

Walibaini takriban asilimia 88 ya waliokuwa na maambukizi ya corona - ikimaamisha kuwa katika maambukizi 100, mbwa hao walishindwa kubaini watu 12 tu waliokuwa na maambukizi.

Lakini kati ya watu 100 ambao hawakuwa na maambukizi ya Covid-19, mbwa hao kimakosa walionesha kupitia njia ya majaribio ya kunusa - kwamba 14 kati yao walipata maambukizi.

Kwahiyo, ikiwa mtu mmoja kati ya watu 300 abiria kwenye ndege ndio mwenye maambukizi ya virusi vya corona, mbwa hao wana uwezo wa kubaini mtu huyo, lakini pia wanaweza kubaini kimakosa kuwa wengine 42 wamepata maambukizi.

Kupitia njia hii, wengi watabainiwa kuwa na maambukizi ingawa baadhi yao watakuwa hawana ikilinganishwa na njia ya upimaji ya pua.

Kwa hiyo timu ya watafiti inasema haipendekezi utumiaji wa mbwa pekee kubaini maambukizi ya virusi vya corona.

Dkt Claire anaishi na Asher , mmoja ya mbwa wanaohusishwa katika majaribio hayo

Chanzo cha picha, MDD

Maelezo ya picha, Dkt Claire anaishi na Asher , mmoja ya mbwa wanaohusishwa katika majaribio hayo

Lakini wanaamini kuwa mbwa wataweza kuwa kiungo muhimu katika upimaji wa virusi vya corona. Wanasema kuwa utumiaji wa mbwa, kisha kukafuatiwa na utumiaji wa vipimo vya pua kutafanikiwa kubaini asilimia 91 ya maambukizi ya virusi vya corona.

Pia kingine cha muhimu ni matokeo kujulikana kwa haraka kwasababu hata matokeo ya haraka zaidi sio chini ya dakika 15, huku mbwa wenye uwezo wa kunusa, inawachukua sekunde tu kubaini mgonjwa.

Pia mbwa wawili wanaweza kunusa watu 300 kwa nusu saa, watafiti wanasema.

Kiuhalisia ni kwamba, watu wanawea kunuswa wakiwa kwenye foleni wakielekea uwanja wa ndege au wakitaka kuingia katika tukio fulani na yeyote ambaye atabainiwa na mbwa, atafanyiwa majaribio ya kimaabara na bila shaka matokeo sahihi yatajulikana.

Na hili linaweza kupunguza idadi ya watu wanaotakiwa kuwa karantini.

Mbwa pia wanaweza kutumiwa katika maeneo ambayo hakuna uchunguzi wa kina kama vile kwenye vituo vya treni vyenye shughuli nyingi kusaidia kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.