Thomas Lubanga: Aliyekuwa mkuu wa waasi ataka uchunguzi kufanywa kuhusu mauaji ya Ituri

Chanzo cha picha, AFP
Aliyekuwa kiongozi wa waasi wa Union of Congolese Patriots, UPC, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Thomas Lubanga, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati mzozo unaoendelea mashariki mwa Congo, akitaja mauaji yanayoendela kama mauaji ya kimbari.
Akiongea na BBC, Lubanga aliyeachiliwa huru na mahakama ya kimataifa ya ICC baada ya kufungwa jela kwa miaka 14 , amesema mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo yanachochewa na ushindani wa mali asili na madini.
Uhusiano wa mapigano na maliasili
Lubanga amedai kwamba kuna wanasiasa wanaowatumia vijana katika eneo hilo ili kusababisha machafuko kwa lengo la kulinda maslahi yao na kuiba maliasili kama vile dhahabu na mafuta katika eneo hilo . Amesema serikali ya Congo na Jamii ya kimatafa zinafaa kuingilia kati ili kuzuia mauaji zaidi na mateso ya raia mashariki mwa nchi hiyo .
Kiongozi huyo wa zamani wa waasi aliyeshtakiwa ICC kwa kuwatumia watoto kama wanajeshi katika vita vilivyosababisha mauaji ya watu wapatao 60,000 miaka ya 2002 na 2003 alidai kwamba wakati wa harakati zake za vita hakuwahi kutekeleza mauaji na uhalifu unaofanyika sasa na iwapo angetekeleza uhalifu huo hangetaka kuachiliwa huru na mahakama .
Alipoulizwa kuhusu historia yake ya kuwa kiongozi wa waasi hapo awali na mauaji yaliyotekelezwa na kundi lake, Lubanga alisema;
'Tulipokuwa msituni hakukuwa na serikali na tulifanya uwezekano ili kuepusha mauaji' .
Lubanga amesema wanaoendeleza machafuko mashariki wanaandika historia ya Ituri kutumia damu ya watu na kamwe hawataishinda serikali kuu na Umoja wa Mataifa .
Historia ya vita
Eneo hilo la Ituri limekuwa likishuhudia mapigano yanayohusisha makundi mbali mbali yaliyojihami dhidi ya wanajeshi wa serikali na mapigano makubwa mapema mwezi huu watu 30 wakiwemo raia 11 waliuawa baada ya mapigano ya siku mbili katika eneo hilo .
Mojawapo ya makundi yanayohusika na mashambulizi katika eneo hilo ni kundi la CODECO(Cooperation for the Development of Congo) ambalo limeshtumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kuchimba madini ya eneo hilo kinyume cha sheria .
Kundi la CODECO limehusishwa na mauaji ya Zaidi ya raia 1000 tangu disemba mwaka wa 2017 .
Zaidi ya makundi 120 yaliyojihami yanaendesha oparesheni zake mashariki mwa DRC na mengi yana historia ya kuhusika na vita vilivyohusisha nchi mbali mbali za eneo hilo miaka ya 90.
'Muasi hadi mwanaharakati wa amani'
Lubanga aliongoza kundi la Union of Congolese Patriots, wapiganaji wa kabila lake la Hema, katika vita vilivyoanza eneo la Ituri na mji mkubwa wa eneo hilo wa Bunia mwaka wa 1999.
Mzozo huo ulikuwa wa ndani ya DRC na watu takriban milioni 5 waliaga dunia kwa ajili ya njaa na magonjwa .Wakati wa kesi dhidi yake, mahakama ilisikiza kuhusu jinsi Lubanga alivyokuwa akienda katika maboma ya watu kuwataka watoe Michango ya kusaidia jitihada zake za kivita . Aliitisha pesa,ng'ombe au mtoto wa kutumiwa kama mwanajeshi katika kundi la waasi .
Alikamatwa Machi mwaka wa 2005 na walinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa pamoja na wapiganaji wengine .Hakuonyesha hisia zozote alipohukumiwa kifungo cha miaka 14 jela .Alibubujikwa machozi wakati alipohamishwa hadi mahakama ya The Hague Machi mwaka wa 2006













